SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA HAMSINI NA SITA
Kweli Dokta Yusha alitembea kwa miguu, ilikuwa safari ngumu sana, lakini hakukuwa na namna nyingine. Ilikuwa ni lazima atembee.
Alipofika hospitali ya Kivinje breki yake ya kwanza ilikuwa ni wodi aliyowaacha kina Nasra. Alipofika mlangoni tu na kuangalia katika kitanda alipokuwa amelazwa mkewe, Nasra.
Alipingwa na butwaa!
Kitanda cha Nasra kilikuwa tupu. Hakukuwa na mtu. Akiwa kasimama palepale mlangoni chozi la uchungu liligusa sakafu ya hospitali. Dokta Yusha alikuwa analia. Kutumuona Nasra pale kitandani alijua kuna mawili, kama mkewe kipenzi hajafariki na kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti basi kundi lile la wanaharamu itakuwa wamemteka. Lakini Dokta Yusha yote hayo mawili hakutaka kabisa yatokee. Alikuwa anampenda sana Nasra, na alikuwa anatamani sana kumuona Nasra anakuwa na siha njema kama zamani.
Dokta Yusha alipiga hatua za taratibu kuingia ndani ya hospitali, huku akifuta machozi kwa kutumia kiganja chake, alikipita kitanda cha mkewe, Nasra akiwa anakiangalia sana, alifika katika kitanda alicholala Hasina, alipofika tu pale kitandani kilitokea kitu cha ajabu sana! Hasina alifungua macho!
Dokta Yusha hakuamini alichokuwa anakitazama, ulikuwa ni ukweli ambao hakukubaliana nao.
"Umeamka Hasina, niambie mke wangu Nasra yuko wapi, naomba uniambie hata kama wamemchukua wale washenzi, wewe nambie tu"
Dokta Yusha alikuwa anaongea na Hasina lakini ilikuwa ni kama anaongea na sanamu, Hasina alimwangalia tu, bila kusema chochote.
Maneno yale ya Dokta Yusha yalimuamsha Mzee Mpaukha toka usingizini. Naye alishangaa sana kumuona Dokta Yusha pale. Kwa sauti dhaifu aliongea.
"Ulikuwa wapi Dokta, umeacha watu wanateseka sana hapa, hii sio hospitali kabisa, hapa ni wakala wa kifo!"
Dokta Yusha alimwacha Hasina, alisogea taratibu kuelekea katika kitanda alicholala Mzee Mpaukha huku akiyasikiliza kwa umakini sana maneno akiyoyaongea Mzee yule. Yalimuingia kabisa akilini.
"Nimekuelewa Mzee wangu"
Dokta Yusha aliongea kwa huzuni alipofika pale kitandani. Huku akijificha ili asijulikane kama alikuwa analia.
"Katafute gari sasahivi Dokta, katafute gari kama unatujari, utuhamishe katika hospitali hii"
"Nasra yupo wapi baba?"
"Nasra yupo ICU"
"Tutaondoka vipi sasa baba na mke wangu yupo ICU?"
"Ni kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, hata huko ICU unafikiri anapewa huduma gani, amelazwa tu kama alivyolazwa hapa! Tuhamishe Dokta hii siyo hospitali!"
******
Don Genge alikaa pale sofani muda mrefu kidogo. Baada ya kutafakari sana akapata wazo kichwani kwake, na akalifanyia kazi wazo lake muda huo huo. Aliitoa simu yake katika mfuko wa suruali yake, akatafuta mamba fulani na kuzipiga.
"Hallo Dokta Zaidi Kilumba"
"Nambie Don"
"Huyu jamaa katoroka huku, lakini kwa vyovyote vile lazima aje hospitali kuviangalia hivyo vikaragosi vyake, weka mtu makini wodini atuambie pindi tu atakapotia mguu wake hapo hospitali"
"Sawa Don, natekeleza hilo sasahivi"
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA