Riwaya - Balaa

Pole but til now no mfadhili itaendelea kurushwa hapa mpk mwisho....na kila cku ntaeka labda dharula itokee
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA THELATHINI NA TATU

Wote wawili Tano na Mwanasheria walipelekwa kituo cha afya Masoko, chini ya ulinzi mkali sana wa askari Polisi.

Kama ilivyo kawaida katika hospitali nyingi Tanzania, wahalifu huwa hawapati huduma nzuri pindi wanapoumwa. Labda kwa kuwa wanakuwa hawana wauguzi wa kuwapa pesa wagonjwa
( hongo).
Hali hiyo iliwakuta Tano na Mwanasheria pale kituo cha afya Masoko. Waliachwa wamelala katika kitanda vyao wakiwa na pingu zao mikononi.

Saa kumi na mbili jioni, Mwanasheria alizinduka, ni kudra za Mungu tu ndizo zilimuasha. Mwanasheria hakupata huduma yoyote ile pale kituo cha afya. Mwanasheria aliamka na maneno yake, Mwanasheria aliamka na lawama za kutosha, lawama kwa Polisi, lawama kwa Serikali, lawama kwa mfumo mzima wa nchi, lakini lawama hazikusaidia, ukweli ulibaki palepale, Mwanasheria alikuwa amelala kitandani akiwa hoi bin taaban na pingu zake kitandani !

Tano wa Six killers naye alikuwa katika wakati mgumu sana, mguu wake ulikuwa umeumia vibaya sana, alikuwa anagugumia kwa maumivu. Lakini hakuwa na jinsi, alikuwa amelala katika kitanda kidogo cha kituo cha kituo cha afya akiwa dhooful hali, huku akiwa hana namna ya kuwapigia wenzie ili awataarifu kwamba alikuwa mahali pale, kwa kuwa simu yake ilikuwa katika kituo cha Polisi.

Kundi la six killers walikutana kwa kikao cha dharura. Kikao kilichokuwa kinaoongozwa na Don Genge mwenyewe, kikiwa na ajenda kuu mbili.
Ajenda ya kwanza ilikuwa ni makabidhiano ya mioyo kumi na tano iliyipatikana kwa siku ile ya pili. Mambo yalienda sawa, na Dokta Sharifa alikabidhi deli kubwa jekundu lenye mioyo kumi na tano.
Ajenda ya pili, ilikuwa inahusu kutoonekana kwa Tano. Masaa zaidi ya kumi na tatu Tano alikuwa hajaonekana, na siku yake ilikuwa haipatikani!

"Hii ni siku ya tatu ya Mpango huu, kwa asilimia 90 mpango wetu umeenda sawa, lakini Kwa bahati mbaya sisi hatufanyi kazi kwa asilimia 90. Huwa tunafanya kazi kwa asilimia 100, au zaidi ya hizo ikiwezekana. Tano hajulikani alipo, na hizo ndio asilimia 10 tulizozipoteza. Natoa masaa mawili, Tano akiwa hai au mwili wake uwe hapa!.
Baada ya masaa hayo mawili, tutaenda kutoa mioyo tukiwa na Tano kama atabahatika kuwa hai, mmebaki wa tano, hakikisheni mnarudi na Tano! Mnaweza kwenda..."

Six killers walitoka mle ndani kwa lengo kuu moja, kwenda kumtafuta muuaji aliyepewa namba Tano....

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA THELATHINI NA NNE.

Mbili alitoka nje, na kukutana na Sita. Walijipanga vizuri kwenda kumtoa Tano katikati ya maaskari wawili wenye bunduki!

Askari hawakuwa kizuizi kabisa kwa Mbili, bunduki hazikuwa tishio kabisa kwa Mbili. Alipewa namba mbili katika kundi la Six killer's kwa kuwa alikuwa mahiri kuliko wanakikundi wanne waliobakia. Wakiwa na Sita, walijiandaa kwa uvamizi.

Kule ndani Mwanasheria alikuwa anaendelea kuongea kama ilivyo ada yake. Askari Polisi walijaribu kumnyamazisha bila mafanikio yoyote. Kilabu sasa kilihamia katika kituo cha afya. Makelele yale yale ya Mwanasheria yalichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umakini kwa askari wale wawili. Wote walikuwa wanajitahidi kumnyamazisha Mwanasheria na kusahau kabisa suala la ulinzi.

Mbili na Sita walikuwa nje ya wodi ile. Walisikia kila kitu kilichokuwa kinaendelea kule ndani. Walijipanga vizuri.

Moja, mbili taaaaa.....wote kwa pamoja waliukumba ule mlango wa wodi kwa kutumia miili yao ya kimazoezi na wote kujikuta wako ndani. Kila mmoja kwa namna yake na bastola zao mkononi.

E bwana weee!

Mbili alijiviringisha kwa mtindo wa sarakasi na kujificha nyuma ya kitanda alicholala Tano huku akibonyea kidogo ili kile kitanda kimfiche, Sita nae alijiviringisha kwa kasi na kumfikia moja kwa moja askari mmoja na kumkaba shingoni, huku akimtumia kama ngao!
Huku bastola yake ikimtazama yule askari mwengine. Askari wote wawili waliwahiwa vizuri sana. Yule askari aliyepigwa kabali ilinasa kisawasawa, alijaribu kujitoa bila kutegemea, huku yule askari mwengine aliyeoneshwa bastola hakuwa na lolote la kufanya, alibaki ameganda kama sanamu. Six Killers walihamishia balaa wodini...

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA THELATHINI NA TANO.

Ghafla! Yule askari aliyesimama alijishika kifuani, kulikuwa na majimaji mekundu, damu! Bastola ya Mbili yenye kiwambo cha kuzuia sauti ilikuwa imefanya kazi iliyotumwa. Yule askari aliyesimama alikuwa amepigwa risasi takatifu ya kifua. Aliyumba kidogo huku akipiga kelele, na kudondoka chini mzimamzima kisogo kikitangulia kufika chini !
Askari alikuwa mfu zamani sana kabla hata hajaigusa sakafu ya hospitali.

Sita naye aliongeza nguvu katika ile kabari, yule askari alikosa pumzi, nguvu zikamuishia, alilegea. Sita alimuachia yule askari, akadondoka chini. Vitendo vyote vilivyokuwa vinatokea Mwanasheria mlevi na Tano walikuwa wanashuhudia kila kitu, kimyakimya.

Wakati Tano akiufurahia ujio wa watu wale wawili aliokuwa anawafahamu vizuri sana, Mwanasheria mlevi alikuwa katika mshangao mkuu, hakutegemea wala kuelewa kinachotokea mle ndani wodini.

Mbili na Sita walikisogelea kitanda alicholala Tano. Waliliangalia lile jeraha kubwa la Tano pale mguuni, wote walimuonea huruma. Walimbeba na kutokomea nae kusikojulikana!

Baada ya robo saa kutokea kwa tukio lile, mganga wa kituo cha afya Masoko aliingia katika wodi ile.
Mganga alikutana na Balaa !
Miili ya askari wawili ilikuwa imelala chini, ikiwa haina uhai. Na mwili wa mgonjwa mmoja ukiwa haupo huku mwili wa Mwanasheria mlevi ukiwa juu ya kitanda, ukiwa umeloa jasho, hakika Mwanasheria aliyaona matukio ambayo hakutegemea kuyaona katika maisha yake. Alikuwa anatetemeka huku anatoa jasho!

Daktari hakuamini kabisa madhara yaliyotokea mle wodini. Alijishika kichwa huku akipiga kelele za kuomba msaada. Ndani ya dakika chache manesi na baadhi ya watu waliokuja pale hospitali walijaa katika wodi ile. Kila mmoja alistaajabu kilichotokea mle ndani, ilikuwa ni balaa !

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA THELATHINI NA SITA

Nesi mmoja alipiga simu kituo cha Polisi kuwataarifu juu ya mauaji yale.
Askari waliwasiri baada ya muda mfupi sana, na kushuhudia unyama mkubwa waliofanyiwa askari wenzao. Huku Mwanasheria mlevi akiwa ni shuhuda pekee aliyeshuhudia kila kitu.

Nusu saa baadae, kundi la Six Killers walikutana tena na bosi wao. Ilikuwa ni furaha kubwa sana kwao, kuitekeleza kazi ya masaa mawili kwa nusu saa tu.

"Hongereni sana vijana wangu, mmefanya kazi kwa haraka sana, ila sina uhakika kama mmeifanya kwa umakini ninaouhitaji" Don Genge alikuwa anaongea huku akiwaangalia Mbili na Sita usoni.
"Tumefanya kazi kwa umakini mkubwa mno Bosi" Mbili alijibu kwa kujiamini.
"Mmeuwa watu wote waliowashuhudia? Kuanzia huyo askari aliyekupeni siri alipo Tano, Mganga mkuu pamoja na huyo mgonjwa aliyelazwa pamoja na Tano?"
Mbili na Sita waliangaliana usoni, waligundua kuwa walikuwa wamefanya kosa!
"Tumefanya kosa, dakika kumi" Mbili alijibu kibabe.
"Naongeza kumi na tano"
"Sawa mkuu"

Walikuwa wamepewa dakika kumi na tano kuhakikisha yule askari aliyewapa siri, Mganga mkuu na Mwanasheria mlevi wanauwawa!
Kundi zima sasa kasoro Tano walinyanyuka na kuingia kazini.

Dakika kumi baadae kundi zima la Six killers lilikuwa limerejea tena. Wakiwa wamefanikisha kuwauwa watu wawili kati ya wale watatu. Askari na mganga mkuu walikuwa wameelekea kuzimu kwa mtindo tofauti, wakati yule askari aliuwawa kwa bastola nyumbani kwake, Mganga mkuu wa hospitali aliuwawa kwa kisu ofisini kwake. Wote wakiwa hawajawahi kutumia hata senti tano katika zile laki moja walizokuwa wamepewa.

Tatizo lilikuwa kwa Mwanasheria mlevi, walienda mle wodini hawakumkuta yule mgonjwa, na kwa bahati mbaya hawakuwa wameshika kabisa sura yake. Lilikuwa kosa la kubwa sana walilolifanya wauaji hawa wazoefu.

Askari polisi sasa walikuwa wanamlinda Mwanasheria mlevi kupita kiasi. Jeshi la Polisi hawakuwa wanajua kabisa kama kuna watumishi walihusika katika kutoa siri, na kupokea hongo kutoka kundi la Six killers...

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA THELATHINI NA SABA.

Nusu saa baadae taarifa mbaya zikalifikia jeshi la Polisi.
Taarifa mbaya za vifo !
Kifo cha Sajenti Alex Omolo wa kituo cha Polisi Masoko, na kifo cha daktari Mosha Gabriel, Mganga mkuu wa kituo cha afya Masoko. Askari walitapakaa mtaani kuwasaka watu waliowauwa Afande Alex Omolo na Dokta Mosha Gabriel. Askari walifanya msako kimyakimya. Lakini ilikuwa kama wanawatafuta watu ambao hawakuwahi kuwepo duniani. Msako wao haukuwasogeza kabisa karibu ya Muuaji.

Wakati askari wakimwagika kama njugu huko Kilwa Masoko kuwatafuta watu waliowauwa Afande Alex na Dokta Mosha, Kundi hatari la Six Killers walikuwa wapo njiani kwenye gari wakielekea hospitali ya wilaya Kilwa Kivinje huku wakilaumiwa vibaya mno na Don Genge kushindwa kumuua mgonjwa aliyewashuhudia wakati wanafanya mauaji. Ilikuwa ni lawama nyingi sana, kundi zima walikuwa kimya wakati Don Genge akifoka!

"Six killers huwa hatufanyi makosa. Kosa lolote inamaanisha kujiweka katika hali ya hatari, na mipango yetu kukwama. Ona sasa, yule Dokta mpumbavu bado anaishi, yule mgonjwa mpumbavu bado anaishi. Ni makosa haya, Dokta mpumbavu anamfahamu Tano, Mgonjwa mpumbavu anawajua Mbili na Sita. Ni makosa makubwa sana, lazima wafe!"

Kundi la Six Killers walimwacha Tano katika nyumba yao iliyokuwa kama kambi ya muda mfupi huko Ngome, akipatiwa matibabu na daktari waliomkodi. Wao walikuwa wanaenda Kilwa Kivinje kufanya kazi yao hatari! Ya kutoa mioyo ya wagonjwa kumi na tano kama ilivyo ada.

Ingawa askari Polisi walimtaka Dokta Yusha akae pale kituo cha Polisi kwa usalama wake. Lakini Dokta Yusha hakukubali kabisa, Dokta Yusha alipinga katakata. Alikuwa anataka kutoka ili akamzike rafiki yake Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, pia alikuwa anataka arudi hospitali Kilwa Kivinje kuwaona wagonjwa wake. Polisi hawakuwa na jinsi, walimruhusu Dokta Yusha atoke pale kituo cha Polisi.

Katika mtaa wa National, katika nyumba aliyokuwa anaishi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa kulikuwa na umati wa watu mkubwa sana. Watu wengi wakilia kwa uchungu mkubwa mno, msiba huu ulikuwa msiba mkubwa sana ndani ya Kilwa Masoko.

Alivyotoka kituo cha Polisi, Dokta Yusha alienda moja kwa moja msibani. Alishiriki vizuri kwenye shughuli za mazishi. Hadi Mwanasheria alivyopumzishwa katika makazi yake ya milele katika makaburi ya Sanga.

Baada ya mazishi, Dokta Yusha alielekea hospitali Kilwa Kivinje ambako kundi la Six killers na Don Genge walielekea huko. Huko wakiwa na mikakati ya kumuua yeye na Mwanasheria mlevi.....

ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…