SIMULIZI; BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA THEMANINI MBILI
Tano alijilegeza kidogo ikawa laini kama mlenda kisha akaanguka kwenye bodi ya gari. Askari wote walipatwa na mshangao mkuu, waliacha kumuelekezea ile midomo hatari ya bunduki, walimsogelea huku bunduki zao zikining'inia mabegani.
Lilikuwa kosa la mwaka!
Tano akiwa kajilegeza vilevile alijirusha nje ya ile gari na kushuka katika barabara ya lami.
Balaa!
Tano alifikia vibaya sana katika barabara ya lami, kumbuka gari lilikuwa linatembea kwa kasi kubwa sana. Pia Tano alikuwa amefungwa pingu mikononi. Lakini Tano hakujari hilo hata chembe.
Wale Askari walibaki midomo wazi, na bunduki zao mkononi zikiwa zinawashangaa. Hawakuwa na ujanja wa kuruka kwa kasi ile, ilikuwa ni zaidi ya hatari. Askari walipigapiga bodi ya gari ile ili kumuamrisha dereva apunguze mwendo, maskini dereva hakusikia chochote, mwendo ule ukichanganya na kelele za king'ora, ilikuwa ni kama kumpigia mbuzi gitaa. Walimuacha Mhalifu hataru sana njiani, wao wakiendelea na kasi yao ya kutisha kuelekea gerezani!
Tano, kwa sasa alikuwa ametapakaa damu mwili mzima, akiwa na maumivu kila sehemu ya mwili wake, maumivu ya kupewa kichapo na Daniel Mwaseba, maumivu ya kuruka katika barabara ya wakati gari ikiwa kasi, tena na kuangukia kwenye lami. Tano alikuwa na roho ya paka! Kwa kutambaa ingawa kwa shida sana alijisogeza pembeni ya barabara, alikuwa na maumivu makali sana, kiasi kwamba alikuwa anashindwa kunyanyuka. Nasema ilimpasa ashindwe kunyanyuka lakini Tano wa Six Killers alijitahidi kunyanyuka, maana kuendelea kukaa mahala pale ilikuwa ni hatari sana kwake. Jamaa alijitahidi kunyanyuka, aliweza, Tano alinyanyuka kwa mwendo wa kusuasua alijisogeza pembeni zaidi ya barabara.
Gari ya polisi ilikuwa inaingia katika viwanja vya gereza la Kilwa. Dereva alipiga kona kwa mbwembwe nyingi huku akifunga breki kali sana. Laiti angejua kama mhalifu Tano hakuwepo kule nyuma ya gari....
ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA