Ripoti ya Uwajibikaji Utoaji wa Huduma kwa Jamii 2021/22

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,462
Taasisi ya WAJIBU imetumia ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2021/22 kukuletea taarifa rahisi ili kukuwezesha mdau wa uwajibikaji kuzielewa ripoti hizo na kudai uwajibikaji pale unapokosekana. Ripoti hii inategemea ukamilifu na usahihi wa ripoti na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vilivyotumika kutengeneza ripoti hii.

Serikali ina wajibu kisheria kutoa huduma za kijamii kwa Wananchi wake, ambao ndio walioikasimisha madaraka, pale ambapo Serikali haiwezi kutoa huduma hizo kikamilifu, hushirikiana na wananchi, taasisi za dini, asasi za kiraia na sekta binafsi kwa kuzingatia misingi ya uwazi, usawa na haki.

Kwa mujibu wa mkataba wa Jamii (social contract) baina ya Wananchi na Serikali, Wananchi wanayo haki ya kushirikishwa katika maamuzi na masuala yanayohusu maisha yao, nao pia wanajukumu la kushiriki kwenye shughuli za jamii na kudai uwajibikaji kwa watoa huduma kwa kuzingatia dhana ya uwazi na uwajibikaji.
Sio sawa kutumia Walimu kusimamia na kukagua miradi.jpg

Utendaji kazi wa Serikali kwa uwazi unaimarisha imani ya wananchi
Ibara ya 146 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa #Tanzania, inampa nafasi Mwananchi kushiriki na kushikirishwa na Serikali za Mitaa katika kupanga mipango na utekelezwaji wa shughuli za maendeleo katika sehemu wanazoishi.

Uwazi husaidia Wananchi kupata taarifa muhimu kuhusu #HudumaZaJamii zinazotolewa na Serikali ili waweze kuzipata pamoja na kufuatilia utendaji wa Serikali ili kuona kama uwajibikaji unakuwepo.
Serikali_inawajibika_kutoa_Ufafanuzi_pale_Wananchi_wanapohoji_kuhusu.jpg

Serikali inawajibika kufafanua Wananchi wanapohoji utoaji Huduma kwa Jamii
Uwajibikaji ni hali ya Serikali kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu na kubeba dhamana ya kutoa ufafanuzi na uthibitisho pale Wananchi wanapohoji utoaji wa huduma kwa jamii.

Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 “Serikali (viongozi na watendaji) itawajibika kwa Wananchi”, hivyo Serikali inawajibika kwa Wananchi na Wananchi wana wajibu wa kuiwajibisha Serikali yao

Serikali kuwa na ufanisi katika utoaji wa #HudumaZaJamii ni lazima dhana ya uwazi na Uwajibikaji iwepo na itekelezwe kwa ukamilifu.

Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 132(5)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Kifungu cha 5(2)(c) cha Sheria Na.6 ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 (kama ilivyorekebishwa mara kwa mara)
Sio sawa kutumia Walimu kusimamia na kukagua miradi.jpg

Sio sawa kutumia Walimu kusimamia na kukagua miradi
Utaratibu huo kutumika katika miradi ya ujenzi inayotekelezwa kwenye Sekta ya Elimu ni kinyume na mwongozo wa Kutekeleza Kazi za Ujenzi kwa Njia ya Kutumia Uwezo wa Ndani Katika Utekelezaji wa Miradi “Force Account” wa Mei 2020.

Muongozo unamtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kutumia wataalamu wa Halmashauri kusimamia utekelezaji wa mradi husika.

Pia, Mhandisi wa Halmashauri ana jukumu la kusimamia shughuli za ujenzi za kila siku, kushindwa kutekeleza hilo kumesababisha miradi kusimamiwa na Walimu na wanajamii wasio na utaalamu wa masuala ya ujenzi, hivyo kuathiri ufanisi na ubora wa majengo hayo.

50% ya ujenzi wa shule mpya haukukamilika licha ya fedha zilizotengwa kutumika zote
Ripoti ya CAG ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 2021/22 inaonesha kuwa ujenzi wa shule mpya za Sekondari 59 sawa na 50% ya shule zilizotengewa fedha za #UVIKO19 hazikuwa zimekamilika licha ya kuwa fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo kuwa zimetumika zote.

Changamoto hizi katika ujenzi wa miradi ya elimu kwenye baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zimesababisha mapungufu kwenye miradi ya elimu katika Shule za Msingi na Sekondari.


Miradi ya Elimu ya mamilioni yakamilika lakini haitumiki
RipotiYaUwajibikaji ni kuwa miradi hiyo inapatikana Wilaya ya #Chamwino; Ujenzi wa maabara Shule ya Sekondari Mvumi (thamani Tsh. Milioni 75), Ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Dabalo (Tsh. Milioni 40).

Nyingine ni katika Mji wa #Kasulu; Ujenzi wa Shule ya Msingi Nyansha (Tsh. Milioni 400) na Jiji la #Mwanza; Ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkolani (Tsh. Milioni 470).

Miradi ya Elimu iliyotekelezwa bila vibali vya lazima na vyeti vya ujenzi
#RipotiYaUwajibikaji imebainika kuwa miradi hiyo ipo Wilaya #Tunduru ambapo kuna ujenzi wa Shule ya Sekondari Nakayaya (thamani Tsh. Milioni 470), ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukumbule (Tsh. Milioni 470) na ujenzi wa Shule ya Sekondari Majimaji (Tsh. Milioni 470).

Kwingine ni Wilaya ya Songea; ujenzi wa Shule ya Sekondari Dr. Joseph Kizito Mhagama (Tsh. Milioni 470), ujenzi wa Shule ya Sekondari Jenister Mhagama katika Kijiji cha Parangu (Tsh. Milioni 820).

Mji Kasulu; Shule mpya ya Sekondari ya Nyumbigwa (Tsh. Milioni 993), Shule ya Sekondari Mwilamvya (Tsh. Milioni 452), Shule ya Sekondari wa Kimobwa (Tsh. Milioni 402), madarasa mawili Shule ya Msingi Msivyi (Tsh. Milioni 60), Shule ya Msingi Nyasha (Tsh. Milioni 400) na Shule ya Sekondari Nyumbigwa (Tsh. Milioni 100).

Wilaya Kigoma; bweni Shule ya Sekondari Bitale (Tsh. Milioni 160), bweni Shule ya Sekondari Nyarubanda (Tsh. Milioni 160), bweni Shule ya Sekondari Mwandiga (Tsh. Milioni 80) na majengo mbalimbali ya Shule ya Sekondari Kigalye (Tsh. Milioni 470).

Miradi ya Elimu iliyotelekezwa
Wilaya Nanyumbu Ujenzi wa Shule ya Msingi Kilimanihewa inayojengwa na LANES II tangu Mwaka 2019 (thamani Tsh. Milioni 400), Wilaya ya Kibiti; bwalo la Shule ya Sekondari Mahege tagu Mwaka 2008 (Tsh. Milioni 120).

Wilaya ya Sikonge; nyumba ya mwalimu Shule ya Sekondari Pangale inayojengwa kwa mapato ya ndani imetelekezwa toka Mwaka 2018 (Tsh Milioni 50), Wilaya ya Monduli; nyumba za Waalimu Shule ya Msingi Eluwai zinazojengwa kwa michango ya jamii zimetelekezwa toka Mwaka 2015 (Tsh. Milioni 30), bwalo Shule ya Sekondari ya Irkisongo inayojengwa kwa michango ya jamii limetelekezwa toka Mwaka 2013 (Tsh Milioni 300).

Wilaya ya Mkinga; bweni Shule ya Sekondari ya Mkingaleo inayojengwa kwa EP4R limetelekezwa toka Mwaka 2016/17 (Tsh Milioni 105).

Mji wa Babati; nyumba za watumishi Shule ya Sekondari Kwaangw’ zinazojengwa kwa michango ya jamii zimetelekezwa toka Mwaka 2019/20 (Tsh. Milioni 100).


Changamoto utekelezaji wa Miradi ya Elimu husababisha mazingira duni ya kufundishia na kujifunza
Changamoto katika utekelezaji wa miradi ya elimu husababisha mazingira duni ya kufundishia na kujifunza, hivyo kuwa na athari katika Ufaulu usioridhisha kwenye baadhi ya Shule za Serikali.

Athari nyingine ni kukatisha masomo kwa baadhi ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari na Miundombinu isiyojitosheleza kwa shule za Msingi na Sekondari.
CHANGAMOTO_UTEKELEZAJI_WA_MIRADI_YA_ELIMU_HUSABABISHA_MAZINGIRA.jpg

Mamlaka za Serikali zilivyoathiriwa na Mazingira duni ya Elimu Mwaka 2021/22
Mwaka 2021/22 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 96, Wanafunzi 158,185 sawa na 66% ya waliofanya mtihani wa Taifa wa kidato cha 4 Mwaka wa masomo 2021/22 walipata daraja la 4 au 0.

Mamlaka za Serikali za Mitaa 11, Wanafunzi 19,945 sawa na 25% ya Wanafunzi waliosajiliwa Mwaka 2015, hawakumaliza darasa la 7 Mwaka 2021/22, pia katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 19, Wanafunzi 22,039 sawa na 28%, waliojiunga na kidato cha kwanza Mwaka 2018/19 hawakufanikiwa kukamilisha elimu ya kidato cha 4.

Mwaka 2021/22, Mamlaka za Serikali za Mitaa 45 zilikuwa na upungufu wa miundombinu kama vyoo vya Wanafunzi, nyumba za Waalimu, mabweni, maktaba, vyumba vya kompyuta, majengo ya utawala na maabara.

Upungufu mkubwa wa miundombinu kwenye Shule za Msingi umeonekana zaidi kwenye nyumba za Walimu (78%) na vyoo vya Wanafunzi (56%), upungufu wa miundombinu katika Shule za Sekondari umeonekana zaidi katika nyumba za Walimu (81%), maktaba (84%), vyumba vya chakula (84%) na vyumba vya kompyuta (80%).

Kamati za Shule na Bodi za Usimamizi wa Shule zishirikiane na Serikali ya Kijiji
Mapendekezo ya WAJIBU kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa Kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; Kuacha kutumia Walimu kwenye kusimamia ujenzi wa miundombinu shuleni kwa kuwa hawana utaalamu na ujuzi kwenye shughuli hizo ambazo ni za kitaalamu.

Kuhakikisha Kamati za Shule na Bodi za Usimamizi wa shule zinaendelea kupewa mafunzo juu ya majukumu yao, pia zishirikiane na uongozi wa Serikali ya Kijiji katika kusimamia na uangalizi wa ujenzi wa miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari.

Kuhuisha makadirio ya gharama za ujenzi ili kuzingatia uhalisia wa maeneo husika na muda wa ujenzi. Kwani pamekuwepo na utoaji wa fedha za ujenzi wa shule/madarasa/maabara kwa kiwango kinacholingana kwa shule zote Nchini.

Serikali yashauriwa kutenga 20% ya bajeti ya nchi au 6% ya pato Ghafi la Taifa kwenda kwenye Sekta ya Elimu
#RipotiYaUwajibikaji inapendekeza katika kuhimiza utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bunge limeshauriwa liitake Serikali kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Miongozo na Matakwa ya Kimataifa Kuhusu Ugharamiaji wa Elimu kwa kutenga 20% ya Bajeti ya Nchi au 6% ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) kwenda kwenye Sekta ya Elimu.

Pia Serikali iongeze ufanisi na tija kwenye kusimamia mapato na matumizi yake kwa kupunguza upotevu wa mapato na matumizi yasiyo na tija, kufanya hivyo Serikali itaongeza uwezo wake wa kutoa fedha kulingana na Bajeti iliyoidhinishwa katika Sekta ya Elimu.

Afya: Miradi ya Tsh. Bilioni 4.93 ilikamilika lakini haikutumika
Miradi ya Afya iliyokamilika yenye thamani ya Tsh. Bilioni 4.93 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 16 haikutumika kwa muda wa miezi mitatu hadi miaka mitatu

#RipotiYaUwajibikaji kuhusu Ripoti ya CAG ya 2021/22 ambapo miradi hiyo inahusisha Zahanati, jengo la wagonjwa wa nje, maabara na Kituo cha Afya ambapo changamoto hii ilisababishwa na ukosefu wa vifaa tiba, ukosefu wa Wafanyakazi na miundombinu rafiki

Baadhi ya miradi ni; Kituo cha Afya Olorien (Arusha, Tsh Milioni 450), Maabara na jengo la wagonjwa wa nje Kituo cha Afya Nyansha, ujenzi wa Zahanati ya Msambara, Zahanati ya Kumnyika na wodi ya wazazi zahanati ya Kigondo (Kasulu, Tsh. Milioni 400), Kituo cha Afya Malezi (Handeni Tsh. Milioni 500), Kituo cha Afya Kadashi (Kwimba Tsh. Milioni 500), Wodi ya Watoto, Wanaume na Wanawake Hospitali ya Mpitimbi (Songea, Tsh. Milioni 500).
Miradi ya Tsh. Bilioni 4.93 ilikamilika lakini haikutumika.jpg

Menejimenti ya Wizara imeshindwa kumsimamia Mkandarasi kuwepo eneo la ujenzi
Ili kuboresha kilimo Nchini, RipotiYaUwajibikaji inapendekeza yafuatayo; Wizara ya Kilimo kupitia menejimenti ya ufuatiliaji na tathmini miradi, isimamie kwa makini vipengele vya mikataba vinavyomtaka mkandarasi kuwepo eneo la ujenzi au kutoa taarifa ya kutokuwepo kwake

Pia, Wizara ihakikishe hatua za kisheria zinachuliwa dhidi ya Wakandarasi wote waliotelekeza miradi ya ujenzi pamoja na Watumishi wa Wizara ya Kilimo wanaohusika katika usimamizi wa miradi iliyotelekezwa wachukuliwe hatua za kinidhamu

Hatua za kisheria zinachuliwa dhidi ya Wakandarasi wote waliotelekeza miradi ya ujenzi
Ili kuboresha kilimo Nchini, #RipotiYaUwajibikaji inapendekeza yafuatayo; Wizara ya Kilimo kupitia menejimenti ya ufuatiliaji na tathmini miradi, isimamie kwa makini vipengele vya mikataba vinavyomtaka mkandarasi kuwepo eneo la ujenzi au kutoa taarifa ya kutokuwepo kwake.

Pia, Wizara ihakikishe hatua za kisheria zinachuliwa dhidi ya Wakandarasi wote waliotelekeza miradi ya ujenzi pamoja na Watumishi wa Wizara ya Kilimo wanaohusika katika usimamizi wa miradi iliyotelekezwa wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Hatua za kisheria zichuliwe dhidi ya Wakandarasi.jpg

Kuhifadhi dawa zilizokwisha muda wa matumizi bila kuziteketeza kunaweza sababisha madhara ya Afya kwa umma
RipotiYaUwajibikaji imebainisha matumizi ya Dawa na Vifaa vilivyozidi muda yanaweza kusababisha kuongezeka kwa idadi ya vifo vya Wajawazito.

Ripoti ya #CAG ya Mwaka 2021/22 imeonesha ongezeko la idadi ya vifo vya Wajawazito zaidi ya lengo la vifo 100 kwa kila vizazi hai 100,000 katika Mamlaka 20 za Serikali za Mitaa.

Dawa hizo zikifika mikononi mwa watu wasio waaminifu zinaweza kuuzwa kwa Wananchi na kuleta madhara kwa Afya za watumiaji.
DAWA ZILIZOISHA MUDA.jpg

Chanzo: Ripoti ya Uwajibikaji 2023 - Huduma kwa Jamii
 
Back
Top Bottom