Riadha Tanzania | Special thread

MamaSamia2025

JF-Expert Member
Mar 29, 2012
10,223
22,303
Wakuu nimeona nianzishe huu uzi uwe kama kijiwe chetu cha kujadili na kushauriana mambo mbalimbali kama familia ya riadha. Mwenye maoni, kero, dukuduku na jambo lolote la riadha tutatumia huu uzi. Nina uhakika riadha ndo mchezo pekee hapa nchini uliowahi kuweka alama zisizofutika duniani.

Lakini kwa bahati mbaya hadi leo hii wananchi wengi wanadhani riadha ilianza na Filbert Bayi na kuishia na Filbert Bayi. Wanasiasa mara nyingi wakiwa wanaongea utasikia "tunataka nchi itengeneze kina Bayi wengine"... sio mbaya lakini ni kama kuaminisha watu kwamba hakukuwahi kuwa na wanariadha wakali kama Bayi. Tukiangalia riadha tokea kizazi cha kina Bayi hadi sasa kina Simbu, tutaona kumekuwa na vizazi kama vinne na vyote vilitoa nyota kadhaa. Nitachambua kizazi kimoja baada ya kingine na kuwaongelea nyota wake kadhaa.

Kizazi cha kina Bayi (1970 hadi miaka ya 80 mwishoni) naweza sema ndo kilikuwa na wanamichezo bora zaidi kuanzia riadha, Ndondi na mpira wa miguu. Ndo enzi za kina Leodger Tenga. Bayi alikuwa wa moto kwelikweli huko duniani. Kinachomtofautisha Bayi na wanariadha wengine nchini ni kuvunja rekodi za dunia na pia kushinda mbio nyingi sana za kuanzia 800m hadi Marathon (42km). Aliweka rekodi za dunia za mita 1500 mwaka 1974 na maili mwaka 1975. Rekodi yake ya dunia katika mita 1500 pia ilikuwa rekodi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola hadi 2022.

Rekodi za Bayi pia zinakumbukwa sana duniani kwa sababu ziliambatana na maajabu. Kwenye rekodi yake ya dunia ya 1500m kwa dakika 3:32:16 huko Christchurch, New Zealand ni kwamba hata mshindi wa pili raia wa New Zealand, John Walker, aliweza kuvunja rekodi wa dunia iliyokuwepo. Na pia mshindi wa 3 hadi 7 waliweza kuweka rekodi za nchi zao. Ni mbio ya 1500m inayotajwa kuwa bora ya wakati wote. Ikumbukwe rekodi iliyokuwepo ilikuwa ya dakika 3:33:1 ya mmarekani Jim Ryun. Hata rekodi yake ya pili aliyoweka huko Kingston, Jamaica huwa inaitwa "Miracle Mile" kwa kuwa Bayi aliongoza tangu mwanzo wa mbio hadi mwisho. Kuna beberu kaelezea kwenye kitabu chake kwa kuiita hizo mbio "Catch me if you can".

Isitoshe Bayi ni miongoni mwa wanariadha wachache walioweza kushiriki mbio za kuruka viunzi za 3000m (steeplechase) na kufanya vizuri. Huwa haiongelewi sana ila kwenye mbio za 5k mzee wetu alikichafua mno. Yaani rekodi zake zimefikiwa na wanariadha wachache hapa nchini hadi leo.

Kabla ya kustaafu mwaka 1989, Mzee Bayi alishiriki mbio ndefu za Marathon ingawa matokeo yake huko hayakuwa ya kuridhisha. Honolulu Marathon ya mwaka 1986 ndo inatambulika kama marathon ambayo Bayi alifanya vizuri kwa kuwa mtu wa nne nyuma ya mkenya Ibrahim Hussein na watanzania Suleiman Nyambui na Gidamis Shahanga. Bayi anatajwa kama mmoja wa wanariadha wenye nidhamu, wanaojituma na pia mwanamichezo bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania.

Lakini enzi za Bayi kulikuwa na wanariadha wengine waliokuwa wanafanya vizuri sana kimataifa. Mzee Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa na Gidamis Shahanga ni miongoni mwa wanariadha tishio kwa wakati huo.

Mzee Suleiman Nyambui, mjita kutoka Musoma Mara, msomi wa Chuo Kikuu cha Texas kwa ngazi ya Bachelor na Master's degree ana alama nyingi kwenye riadha duniani. Kwenye rekodi ya dunia aliyoweka Bayi mwaka 1974 kwenye 1500m hata Suleiman Nyambui alishiriki na alikuwa mtu wa nane akitumia muda wa dakika 3:39.62, ikumbukwe mbio hizo zinatajwa kama miongoni mwa mbio bora za muda wote kwenye 1500m. Nyambui alishinda medali ya shaba katika Michezo ya All-Africa 1978, medali ya fedha katika mita 5000 kwenye Olimpiki ya 1980, na alimaliza wa kwanza katika mbio za marathoni tatu mfululizo kati ya 1987 na 1988.

Anashikilia rekodi nyingi za kitaifa za Tanzania katika riadha. Kuna kitu ambacho hakisemwi sana kuhusu Nyambui. Ni kuwa naye alivunja rekodi ya dunia za mita 5000 kwa mbio za ndani (indoor games) kwenye Millrose Games huko New York mnamo Februari 1981, kwa dakika 13:20.4. Kimsingi Mzee Nyambui alikichafua zaidi kwenye full marathon kwa kushinda mara mbili Berlin Marathon.

Mzee Juma Ikangaa ambaye ni mzaliwa wa Dodoma naye kama ilivyo Nyambui alifanya makubwa kwenye mbio ndefu. Alishinda mbio za New York City Marathon za 1989 katika muda wa rekodi wa saa 2:08:01. Ikangaa pia alikuwa kipenzi cha watu wengi katika mbio za Boston Marathon baada ya kumaliza wa pili miaka mitatu mfululizo kuanzia 1988-1990. Medali za dhahabu alizo nazo Mzee Ikangaa ni kwenye mashindano ya ubingwa wa Afrika (1982), Melbourne Marathon (1983, 1984), Tokyo Marathon (1984, 1986), Fukuoka Marathon (1986), Beijing Marathon (1987) na New York City marathon (1989). Medali za fedha na shaba nazo pia anazo nyingi. Kimsingi mzee wetu alifanya makubwa sana kwenye marathon.

Mzee Gidamis Shahanga naye ni nyota wa kwenye kizazi cha kina Bayi. Mzee huyu ambaye ni mzaliwa wa Katesh, Manyara aliweka muda wake bora kabisa wa marathon wa masaa 2:08:32 kwenye Berlin Marathon ya 1990. Medali za dhahabu alizo nazo ni za kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola (1978, 1982), Los Angeles Marathon (1984), Rotterdam Marathon (1984), mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (1988), Vienna Marathon (1990) na Munich Marathon (1993, 1994). Ni mwanariadha bora wa muda wote upande wa Marathon.

Walikuwepo pia wanariadha wengine wazuri ila hao wanne walifanya makubwa zaidi kimataifa. Waliiheshimisha Tanzania. Baada ya kina Bayi kiliibuka kizazi kingine miaka ya 80 mwishoni hadi 2000 mwanzoni. Nitarudi tujikumbushe enzi za kina Simon Robert Naali, Morris Okinda, Maxmillian Matle, Faustin Baha, Zebedayo Bayo, na wakali wengine wa miaka ya 90.

KAA HAPA NITARUDI....
 
Kizazi cha pili baada ya kina Bayi kinaanzia miaka ya 89 hadi mwanzoni mwa 2000. Kizazi hiki kilikuwa kizuri lakini ukweli ni kwamba hawakuweza kufikia rekodi za kina Bayi na Nyambui. Kina Bayi, Nyambui, Shahanga na Ikangaa walikuwa ni tishio dunia nzima. Kwa kizazi hiki cha pili tutawatazama nyota kadhaa ili kuweka kumbukumbu sawa. Tumtazame Hayati Simon Robert Naali.
 
Back
Top Bottom