94.-(1) Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani
endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa
masharti ya Ibara hii.
(2) Bila kuathiri masharti mengineyo ya Ibara hii, hoja yoyote ya
kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama itadaiwa kwamba Rais ametenda
mojawapo ya makosa yafuatayo:
(a) ukiukwaji mkubwa wa masharti ya Katiba hii;
(b) makosa makubwa ya jinai;
(c) kuzuia kwa namna yoyote ile yeye kuchunguzwa kwa mujibu wa
Ibara hii;
(d) rushwa;
(e) amekuwa na mwenendo unaodhalilisha nafasi ya madaraka ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano;
33
(f) kupuuza au kukataa kutekeleza uamuzi au amri halali ya Mahakama;
au
(g) amefanya kitendo ambacho kinakiuka kanuni za maadili au miiko ya
uongozi.
(3) Bunge halitapitisha hoja ya kumshtaki Rais isipokuwa tu kama-
(a) hoja ya namna hiyo itatolewa baada ya miezi kumi na mbili tangu
hoja kama hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge; na
(b) taarifa ya maandishi, iliyotiwa saini na kuungwa mkono na
Wabunge wasiopungua asilimia ishirini na tano ya Wabunge wote
itawasilishwa kwa Spika siku kumi na nne kabla ya kikao ambapo
hoja hiyo inakusudiwa kutolewa Bungeni.
(4) Taarifa itakayowasilishwa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (3)(b)
itafafanua makosa aliyoyatenda Rais, na itapendekeza kuwa Kamati Maalum ya
Uchunguzi iundwe ili ichunguze tuhuma zilizotolewa dhidi ya Rais.
(5) Wakati wowote baada ya kupokea taarifa iliyotiwa saini na Wabunge
na kujiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuwasilisha hoja
yametimizwa, Spika atamruhusu mtoa hoja kuiwasilisha mbele ya Bunge na
kisha Spika atalitaka Bunge, bila ya kufanya majadiliano, lipige kura juu ya hoja
ya kuunda Kamati Maalum ya Uchunguzi.
(6) Endapo hoja ya kuunda Kamati Maalum ya Uchunguzi itaungwa
mkono na Wabunge wasiopungua asilimia sabini na tano ya Wabunge wote,
Spika atatangaza majina ya wajumbe wa Kamati Maalum ya Uchunguzi.
(7) Kamati Maalum ya Uchunguzi, kwa madhumuni ya Ibara hii, itakuwa
na wajumbe wafuatao:
(a) Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, ambaye atakuwa Mwenyekiti
wa Kamati;
(b) Jaji Mkuu wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti; na
(c) Wabunge watano kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano,
watakaoteuliwa na Spika kwa kuzingatia uwakilishi wa kila upande
wa Muungano.
(8) Ndani ya siku saba baada ya Kamati Maalum ya Uchunguzi
kuundwa, itachunguza na kuchambua mashtaka dhidi ya Rais, pamoja na
kumpatia Rais fursa ya kujieleza, kwa kufuata utaratibu utakaowekwa na kanuni
za kudumu za Bunge.
(9) Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile katika muda usiozidi
siku tisini, Kamati Maalum ya Uchunguzi itatoa taarifa yake kwa Spika.
(10) Baada ya Spika kupokea taarifa ya Kamati Maalum ya Uchunguzi,
taarifa hiyo itawasilishwa Bungeni kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni
za kudumu za Bunge.
(11) Baada ya taarifa ya Kamati Maalum ya Uchunguzi kuwasilishwa,
Bunge litaijadili taarifa hiyo na kutoa fursa kwa Rais kujieleza, na kisha, kwa
kura za Wabunge wasiopungua asilimia sabini na tano ya Wabunge wote, Bunge
litapitisha azimio kuwa mashtaka dhidi ya Rais ama yamethibitika au
hayakuthibitika.
(12) Endapo Bunge litapitisha azimio kuwa mashtaka dhidi ya Rais
yamethibitika na kwamba hastahili kuendelea kushika madaraka ya Rais, Spika
34
atamfahamisha Rais juu ya Azimio la Bunge na Rais atakuwa ameondolewa
madarakani na Makamu wa Rais ataapishwa mara moja kushika madaraka ya
Rais.
(13) Endapo Rais ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na
mashtaka dhidi yake kuthibitika, hatakuwa na haki ya:
(a) kushika nafasi yoyote ya madaraka nchini; na
(b) kupata malipo yoyote ya uzeeni, posho wala kupata haki au nafuu
nyingine anazopewa Rais au mtu aliyekuwa Rais kwa mujibu wa
Katiba au sheria.