Rais Samia, peleka muswada Bunge lifute adhabu ya kifo

KooZito

JF-Expert Member
Dec 14, 2020
396
1,377
SIKU zote ninaamini kuwa jamii inayojadiliana mambo yao kwa uwazi bila hofu ya kuhojiwa na dola ni jamii hai. Utamaduni wa mijadala na malumbano ya hoja huzaa maendeleo. Hii ni kwa sababu sisi binadamu ni tofauti na wanyama hayawani wanaoongozwa na hisia-silika. Hawana utashi ndio maana hawajadiliani zaidi ya kula na kujamiiana. Je, tusijadiliane? Hapana, tutakuwa wanyama.

Naam! Nchi yetu Tanzania inaongozwa kwa Katiba kama Sheria mama, Sheria za Kibunge, Kanuni, Sera na Tamaduni anuai. Katika makala haya nitatalii katika eneo la Sheria. Na katika Sheria nitajikita katika inayotoa Hukumu ya Kifo (death penalty) inayoangukia kwenye makosa ya jinai ya mwaka 1950 (Penal Code Act 1950). Kwa haraka tu unaweza kugundua kuwa ni miongoni mwa Sheria zilizotungwa na wakoloni nasi tukairithi.

Hii Sheria utekelezwa kwa agizo la Rais wa nchi baada ya kuamuliwa na Jaji wa Mahakama Kuu ndio huitwa, "State-Sanctioned Killing of a Person as a purnishment for a crime). Kwamba ni Hukumu ya Kifo inayotolewa na Mamlaka ya Ikulu kwa mtu kama adhabu kwa muuaji (tafsiri ni yangu).

Maana yake ni kwamba mtu anaweza kuhukumiwa kifo ambapo kwa Tanzania ni kunyongwa hadi kufa lakini kama Rais hajatia saini hati ya Kifo (Hukumu) hakuna Askari Magereza anayeweza kuthubutu kumnyonga mhukumiwa.

Hukumu ya Kifo ipo katika nchi mbalimbali duniani. Tofauti ni namna ya utekelezaji wa kifo ambapo sisi tukinyonga hadi kufa wengine hupiga risasi, wengine hulisha watu sumu, wengine hutumia umeme nakadhalika.

Ripoti ya Armnest International ya siku za karibuni inaonesha kuwa Kati ya mwaka 2018/20 Hukumu ya Kifo zimetolewa zaidi 207 huku watu zaidi ya 57 tayari wameuawa.

Wakati huo shirika la habari la CNN baada ya kufanya uchunguzi limeripo kuwa 71% ya Waprotestanti wa Ulaya wanaunga mkono Hukumu ya Kifo huku chini ya 27% ya waumini wa Roman Catholic ndio wanaamini katika Hukumu hiyo. Ripoti hiyo haisemi kuhusu Uislamu, Hindu, Budha, Orthodox, Uzayuni wala Walokole wa kisasa.

Miaka minne iliyopita Papa Francis alianzisha kampeni duniani akitoa wito kwa Serikali za kiulimwengu kufuta Sheria hiyo Kwani inakwenda kinyume na Ulinzi wa uhai wa binadamu sawa na utoaji mimba na matumizi ya kondom.

Kwa hapa Tanzania Sheria hii ilikoma kutumika toka 1994 ambapo mtu wa mwisho Deogratias Mushi aliponyongwa. Hii ni baada ya ujio wa mfumo wa vyama vingi ulioambatana na haki za binadamu. Toka wakati huo wote waliohukumiwa kunyongwa hawajanyongwa. Rais Magufuli (Mkatoliki) aliweka hadharani kwamba hatosaini hati ya Kifo. Maana yake ni kwamba kama JPM angeongoza hadi 2025 hakuna mtu angenyongwa. Je, alitii kampeni ya Papa Francis?

Sasa ameingia Rais Samia Suluhu Hassan, je, atasaini hati ya Hukumu ya vifo kwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ambao idadi yao inaongezeka gerezani? Rais Samia Suluhu Hassan hajatoa msimamo wake ambao sidhani kama utatofautiana na mtangulizi wake baada ya kusema, "Mimi na Hayati Magufuli letu ni moja".

Kama naye hatosaini wafungwa hao wanyongwe Kuna haja gani ya kuendelea na Sheria hii katili? Hawa watu watasubiri kunyongwa hadi lini?

Niharakishe kusema kwamba binafsi ni mpinzani wa Hukumu ya Kifo maana haitoi majawabu chanya ya lengo la adhabu.

Adhabu yoyote huwa na shabaha mbili: Mosi ni kumfanya mkosaji kujirekebisha kutorudia kutenda kosa. Adhabu ya Kifo inamuondoa mkosaji duniani. Pili, hulenga kuwaogofya wengine wasitende kosa kama hilo. Yaani iwe fundisho. Lakini hakuna utafiti wa kisayansi uliothibitisha kuwa adhabu ya Kifo imezuia watu kuua. Bado tunakutana na matukio ya mauaji kila uchao kwa maana kwamba lengo la pili nalo halikufanikiwa.

Mimi ninaamini elimu ya utu wema kwa jamii pana pekee inaweza kuondoa au kupunguza mauaji yanayopelekea kutolewa kwa Hukumu ya Kifo. Viongozi wa dini na wazee wa kimila wanayo nafasi kubwa ya kuwaelekeza wanajamii kumuogopa Mungu/Allah ili Sheria hii ya kikoloni iondolewe. Kama jamii tunaweza kutafuta adhabu mbadala wa adhabu ya Kifo ili kulinda uhai. Vinginevyo Sheria hii ifutwe na iwe moja ya kumbukumbu maridhawa (legacy) kama zawadi kwa Watanzania.

Nawasilisha kwenu kwa tahadhima!
 
Back
Top Bottom