Hussein Massanza
JF-Expert Member
- Dec 26, 2012
- 918
- 1,994
Ukiona elimu ni ghali jaribu ujinga! Ni msemo maarufu sana, kwamba ukiona elimu ni bei mbaya, basi baki upande wa pili ukutane na gharama za ujinga zilivyo kubwa. Hii ina maana pia kuwa ukiona kinga zinagharimu sana, jaribu maradhi uone.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, yupo nchini Marekani kwa matibabu. Amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostate) katika Hospitali ya Johns Hopkins, iliyopo Baltimore, Jimbo la Maryland.
Kwa kitendo cha Mkuu wa Nchi kutibiwa Marekani, baadhi ya wana wa taifa la lawama (Tanzania), wanalalamika, eti kwa nini wakubwa wanatibiwa nje ilhali hali za hospitali hapa nchini ni mbaya. Hawa wanaona gharama za kumtibu rais wa nchi ni kubwa, wanahitaji kuona matokeo ya upande wa pili.
Wapo wanasiasa (sishangai, ni kawiada yao), kuna watu mbalimbali pia wanakosoa Rais Kikwete kutibiwa Marekani. Kichekesho; eti wanataka atibiwe Amana, Mwananyamala au Temeke kisha apewe rufaa kwenda Muhimbili. Anayejadiliwa hivi ni mkuu wa nchi!
Kabla ya kuwaza ubora wa matibabu, tufikirie tu mazingira halisi. Mathalan; Rais Kikwete angetibiwa Muhimbili, je, wakosoaji wanajua gharama ambazo wananchi watazipata kwa kitendo cha mkuu huyo wa nchi kulazwa hospitali hiyo ya taifa?
Hivi, wanadhani JK akilazwa Muhimbili, wananchi watakuwa wanaweza kuingia na kutoka pale hospitali kwa uhuru kama ilivyo sasa? Wakosoaji wanajua mfumo wa kumlinda Rais wa Nchi ulivyo? Hawa nao wanataka kujaribu ujinga.
Wakosoaji hawajui kuwa JK kulazwa muhimbili, ingeweza kusababisha vifo vya wananchi wasio na hatia kutokana na kucheleweshwa kuanzishiwa tiba. Muda ambao mgonjwa mahututi angeshughulikiwa matibabu Kitengo cha Dharura (Emergency Unit) kuokoa maisha yake, angekuwa anapitishwa kwenye mashine za ukaguzi wa kiusalama. Hawatakufa watu hapo?
Hata hivyo, najua kuwa JK angetibiwa Muhimbili bado malalamiko yasingekosekana. Kuna ambao wangelaumu kwa sababu upatikanaji wa matibabu ungekuwa wa shida kutokana na mfumo wa ulinzi ambao ungeboreshwa hospitalini hapo. Ulinzi kwa Mkuu wa Nchi haukwepeki. lazima alindwe sana.
Walalamikaji hao, si ajabu ndiyo haohao wakosoao JK kufanyiwa upasuaji Marekani, wangetamka: "Kwa nini hajapelekwa nje akatibiwe?" Wangesonya na kuzungumza kwa jazba kwamba anasababisha foleni kubwa ya kupata matibabu Muhimbili.
Wengine wangebeza; je, taifa limefikia hali ya kutojiweza kiuchumi kiasi cha kushindwa kumpatia Mkuu wa Nchi matibabu ya uhakika katika mataifa yaliyopiga hatua kubwa kwenye nyanja ya utoaji wa huduma za afya? Kila eneo litakosolewa!
Vilevile JK angetibiwa hapa nchini, wapo ambao wasingeacha kuibuka na hoja kuwa "anajikosha kwa wananchi", aonekane anaishi maisha ya kawaida wakati siyo kweli hata kidogo. Unaweza kumzuia mwana wa lawama? Anayekuwinda hakosi sababu ya kukusema!
SHANGAA WATANZANIA:
Mwaka jana, Rais Marekani, Barack Obama, aliwasili nchi kwa ziara ya siku mbili. Tulikuwa mashuhuda jinsi ambavyo Marekani ilivyotumia mamilioni ya dola (mabilioni ya shilingi), kuhakikisha kiongozi wao huyo hapatwi na janga lolote akiwa nchini.
Tena Watanzania tulishangilia kweli; "Dah, Marekani kiboko, rais wao analindwa si mchezo", magazeti ya Tanzania yakaandika "ulinzi wa Obama balaa", mengine "Obama anavyolindwa ni funga kazi", yaani tunakuwa mashabiki wa jinsi Marekani wanavyomlinda rais wao, sisi wa kwetu hatutaki apate huduma bora za afya! Sisi Watanzania ni watumwa?
Utumwa si mpaka uchukuliwe mateka au ununuliwe kwenda kufanya kazi za watu bila uhuru binafsi. Upo utumwa wa fikra ambao Watanzania tunaamua kuupokea na kuufanya ni utaratibu wetu. Swali; Kifo cha Obama au JK, kipi kina gharama kubwa kwa Watanzania?
Marekani wanatambua gharama ambayo wanaweza kuipata kwa kumpoteza kiongozi wao ndiyo maana wanamlinda hivyo. Nasi tunageuka mashabiki wa huo ulinzi ambao rais wa taifa hilo anapewa. Ila tunanung'unika rais wetu akipelekwa Marekani kutibiwa.
Yaliandikwa madege ya kijeshi ambayo yalitua Tanzania, likasifiwa lile manowari la kivita ambalo liliweka doria majini na rada zake kumulika anga lote. Walizungumziwa makomandoo wa FBI na utitiri wa majasusi CIA, yalizunguzwa magari bila kusahau lile Cadillac DTS Limousine (Cadillac One) linalombeba Obama.
Aliyekuwa Rais wa China, Hu Jintao, alitembelea Tanzania mwaka 2009. Japo ulinzi wake si wenye mbwembwe nyingi kama Marekani lakini tuliona jinsi ambavyo Wachina wanamlinda kiongozi wao. Ulinzi ni mkubwa sana kuhakikisha taifa lao haliingii hasara ya kumpoteza kiongozi wao.
Hata kiongozi wa China wa sasa, Rais Xi Jinping, mwaka jana baada tu ya kuchaguliwa na kabla hajaapishwa kulitumikia taifa hilo, alizuru Tanzania na tuliona ulinzi ambao Wachina waliutoa kwake. Yaani sisi tunapenda watoto wa nyumba jirani wanavyomlinda baba yao, ila sisi kumlinda baba yetu inakuwa nongwa.
Ilishatolewa taarifa rasmi kuwa inakuja zamu ya Urusi, lile taifa namba mbili kwa mbwembwe za Kijeshi duniani baada ya Barekani. Rais wao, Vladimir Putin atawasili nchini Februari mwakani. Kwa mara nyingine tutashangilia ulinzi ambao Warusi wanautoa kwa rais wao.
Sababu ya mataifa hayo kutumia gharama kubwa kulinda viongozi wao hata wanapokuwa nje ya mipaka ya nchi zao, si kwamba hawana imani na vyombo vya ulinzi na usalama katika mataifa ambayo wakuu wao wanatembelea, isipokuwa wanajua kuwa jukumu la kuwalinda wakuu wao ni lao wenyewe.
Yaani Marekani wampandishe Obama ndege halafu wampigie simu JK kumtaarifu kuwa yupo njiani na wanategemea ulinzi wa uhakika uliopo Tanzania, thubutu! Tena hiyo siyo Tanzania tu, hata anapokwenda Uingereza ambalo ni taifa swahiba damu na Marekani, bado ulinzi ni uleule. Anapokwenda Israel ni vilevile. Kwa kifupi ni kwamba dunia nzima, ulinzi ni huohuo.
Hata Obama anapozunguka ndani ya Marekani yenyewe, ulinzi unaboreshwa kwa kiwango cha juu sana. Tukumbuke pia Rais wa 43 wa nchi hiyo, George Bush alipotembelea Tanzania mwaka 2008, tuliona ulinzi wake. Vilevile Rais wa 42, Bill Clinton alipofika Arusha kwa mwaliko wa marehemu Mzee Nelson Mandela wakati wa kutia sahihi makubaliano ya kumaliza mgogoro wa kivita Burundi.
Kwa kifupi ni kwamba Marekani hutumia wastani wa dola milioni 50 (zaidi ya shilingi bilioni 80) katika ziara moja ya rais wao nje ya nchi. Ziara ya Rais Obama barani Afrika mwaka jana, iliigharimu Marekani dola milioni 100 (zaidi ya shilingi bilioni 160). Pesa zote hizo zinateketezwa kwa sababu moja kuu, lazima kiongozi wao alindwe.
Uingereza siyo tu kwamba inamlinda kwa nguvu zote Waziri Mkuu wao (sasa hivi David Cameron), bali inatumia fedha nyingi kumhudumia Malkia Elizabeth II pamoja na ukoo wote wa Kifalme, wao huo ni utamaduni wao na haulalamikiwi.
Kila mwaka Serikali ya Uingereza inatumia wastani wa pauni milioni 40, sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 109 kuhudumia ukoo wa Kifalme (The Civil List). Vilevile Malkia Elizabeth II anapewa pauni milioni 8 (shilingi bilioni 22) kila mwaka, kwa ajili ya matumizi yake tu. Fedha hizo zinaidhinishwa pia na Bunge la Uingereza (House of Commons).
Hapa ni kuweka hoja sawa kwamba suala la kumhudumia Rais wa Nchi ni utamaduni wa mataifa yote ulimwenguni. Hata Wamarekani au Waingereza wakisikia Watanzania wanalalamika rais wao kutibiwa Marekani watashangaa!
Jambo baya ni matumizi mabaya ya fedha za umma, ila kama imeonekana JK akitibiwa Marekani ndiyo anapata huduma bora kabisa kwa nini asipelekwe? Kwa hali ambayo tayari nimeshaieleza, angetibiwa Tanzania gharama zake ni kubwa kuliko alipo Marekani.
ILA NYUMA YAKE KUNA HOJA YA MSINGI
Kwa upande wa pili, kuna hoja kuhusu hospitali zetu. Hali ni mbaya. Hili ndilo la kuwekewa mkazo. Kwa nini wagonjwa waendelee kulala chini mpaka leo tukielekea miaka 53 baada ya uhuru?
Ni kweli kwamba serikali imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya. Hata hivyo, kasi yake ni ndogo na haiendani na mahitaji halisi ya wagonjwa ambao wamekuwa wakikabiliana na mazingira magumu ya huduma.
Tanzania haina uhaba wa madaktari, hilo halina ubishi. Tatizo kubwa ni vifaa vya utoaji huduma za afya. Matokeo yake kuna madaktari wapo nchini na hawana kazi kwa sababu aina ya magonjwa ambayo wamebobea kuyatibu, vifaa vyake vya ugunduzi na tiba havipo nchini. (Hii ni mada ambayo siku yake ikifika nitaichambua na kutaja majina ya madaktari ambao imebidi watibu magonjwa mengine na kuacha yale waliyobobea.)
Kutokana na ukosefu wa vifaa, serikali kupitia wizara ya afya na hata Mfuko wa Bima ya Afya ya Tifa, imekuwa ikilazimika kutumia fedha nyingi kuwadhamini wagonjwa kwenda kutibiwa India na nchi nyinginezo, ikiwemo Afrika Kusini.
Kadhalika, serikali imekuwa ikilazimika kupeleka viongozi mbalimbali kutibiwa nje, hata katika magonjwa ambayo ingewezekana kabisa kuwatibu nchini. Hii yote ni kwa sababu ya mazingira ya utoaji wa huduma za afya nchini bado ni duni.
Serikali iboreshe huduma. Hata hivyo, kilio hicho hakipaswi kufikia hatua ya kutaka na Rais Kikwete naye atibiwe hapahapa. Hapo tunazungumzia habari nyingine. Hata kama vifaa na wataalamu wa kutosha wangekuwepo Muhimbili, ukweli ni kwamba angelazwa pale ingekuwa shida juu ya shida kwa wagonjwa wengine. Ulinzi wa rais ni kero kwa wananchi wa kawaida.
Mazingira ya Muhimbili kwa sasa na muundo wake kwa jumla, hautoshi kumlaza Rais wa Nchi pasipo kusababisha bughudha kwa wananchi wengine watakaokuwa wanakwenda kupata tiba, wagonjwa waliolazwa na ndugu zao wanaowahudumia au wanaokwenda kuwatembelea.
Tusiwe na ndoto kama za yule mbunge (nimemsahau jina), aliyetoa hoja bungeni Dodoma miaka 1990, kwamba Tanzania imefikia hatua iwe na treni ya umeme! Yaani umeme wetu wenyewe shida, tunawaza treni ya umeme. Ndiyo haya ya kutaka JK atibiwe Muhimbili. Je, tunataka kujaribu ujinga? Maana elimu tunaona ni ghali sana.
Luqman Maloto