TANZIA Prof. Nkunya wa TCU afariki dunia

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,582
6,627
Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Prof. Mayunga Habibu Hemedi Nkunya amefariki dunia leo Julai 20, 2021 katika Hosp ya Taifa, Muhimbili.

Marehemu Prof. Nkunya alikuwa Profesa Emerita katika Idara ya Kemia, Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi. Alianza kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama Mkufunzi Msaidizi mwaka 1976. Alipandishwa vyeo vya kitaaluma hadi kufikia ngazi yaya mwisho kitaaluma ya Profesa, cheo alichokuwa nacho hadi alipostaafu utumishi wa umma mwaka 2012. Baada ya kustaafu Prof. Nkunya aliendelea na utumishi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajira ya mkataba. Mwaka 2020 aliteuliwa kuwa Profesa Emerita kwa kuthamini na kutambua mchango wake mkubwa kitaaluma.

Prof. Nkunya alikuwa msomi na mwanataaluma mbobezi aliyetafiti, kuchapisha na kushauri katika maeneo ya kemia ya onaniki (organic chemistry) hususani katika kemia ya dawa asilia(chemistry of natural products).

Prof. Nkunya alitoa zaidi ya machapisho 100 katika majarida yanayoheshimika duniani na katika vitabu. Alishiriki katika kazi mbalimbali za ushauri ndani na nje ya nchi. Aidha alikuwa mwenyekiti/mjumbe katika kamati nyingi za kitaaluma na za ushauri.

Prof. Nkunya alishika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwemo Afisa Taaluma Mkuu cheo (sawa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma sasa) (1999-2006) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(2007-2010); na Katibu Mtendaji wa Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki(2011-2015).

Mpaka anafariki alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania wadhifa aliokuwa nao kuanzia mwaka 2019 na Mwenyekiti wa Baraza la Ujenzi la Taifa kuanzia mwaka 2016. Mipango ya mazishi ya Prof. Nkunya inafanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na familia.

Mwili wa marehemu unatarajia kusafirishwa siku ya Jumatano tarehe 21 Julai 2021 kuelekea Tabora kwa Mazishi.

Roho ya Marehemu Ipumzike kwa Amani!


9aaa506c-7dca-4d9e-b955-304c9c7bdf17.jpg
 
Back
Top Bottom