Polisi waua watano Mwanza

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Sheilla Sezzy, Mwanza na Suzy Butondo, Shinyanga,

JESHI la Polisi mkoani Mwanza limewaua watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika majibizano ya risasi yaliyotokea jana asubuhi katika Mtaa wa Pamba.

Mapambano hayo ya risasi yalizua mtafaruku katika maeneo mengi ya katikati ya Jiji la Mwanza na kusababisha watu kukimbia ovyo huku wengine wakiacha shughuli zao. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alisema jana kwamba watuhumiwa hao wa ujambazi walivamia Duka la Mukesh Ganatra na kuwaamuru watumishi wote kulala chini. Alisema watu hao walitoa amri hiyo huku wakiwaelekezea wafanyakazi hao mitutu ya bunduki na mapanga na kuwataka waeleze fedha ziliko.

Kamanda Barlow alisema baada ya kupata taarifa, walielekea katika eneo la tukio na kuwakuta watuhumiwa hao wa majambazi. Alisema walitoa amri kuwataka wajisalimishe lakini badala yake wakaanza kupambana na polisi.

Alidai kuwa majambazi hao waliwashambulia polisi lakini kwa kuwa walikuwa wamejiandaa vyema kukabili tukio hilo walifanikiwa kuwazidi nguvu na kuwaua wote watano na kuokoa mali ambazo zingeibwa ambazo hata hivyo, thamani yake bado haijafahamika. baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walipongeza jeshi la Polisi kuwahi katika eneo la tukio na kufanikiwa kuzima ujambazi huo wakisema ni tofauti na walivyozoea kuona.

“Hii ndiyo kazi ya polisi, katika tukio la leo wamewahi sana kufika, walichukua kama dakika tano hivi kufika, ndiyo maana majibizano yalikuwa makali,” alisema mmoja wa wananchi waliokuwa katika eneo la tukio.

Mtafaruku Shinyanga
Ajali bandia ya ndege ambayo ilikuwa sehemu ya kubaini uelewa wa umma katika kukabiliana na majanga Shinyanga, jana ilizua hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha shughuli nyingi katika mji huo kusimama huku wananchi wengi wakikimbilia lililokuwa tukio hilo. baadhi ya walioshuhudia zoezi hilo walisema liliwashutua na kuwafanya wengine waache kazi zao na kukimbia kuelekea Uwanja wa Ndege wa Shinyanga ili kushuhudia ‘ajali ya ndege’ iliyotokea.

“Kwa kweli zoezi hili limetushtua sana, baada ya kusikia ajali imetokea tumefunga biashara zetu ili kwenda kuwaokoa wenzetu waliopata ajali. Tulipofika uwanja wa ndege ingawa kweli tumekuta kukiwa na pilika kama za uokoaji, lakini tulipojiunga nao tukabaini si tukio la kweli ni feki,” alisema Patrick Richard.

Shuhuda mwingine alisema baada ya kusikia ajali hiyo alishtuka na kuamua kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alikuta wananchi wakiwa wamejazana huku wakisukumana na wengine wakilia wakiwataja ndugu zao waliokuwa wakitarajiwa kuabiri ndege jana.

“Niliposikia ajali imetokea, kweli nilishtuka na kidogo nizimie kwa sababu nilikuwa na kaka yangu ambaye aliniaga kuwa anasafiri kwa ndege kuelekea Dar es Salaam. Niliposikia kuna maiti wanane na wengine wamejeruhiwa, nilihisi kaka yangu amekufa ndiyo maana nilichanganyikiwa ghafla,” alisema Daudi Joseph. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Costa Mniko alisema tukio hilo lilikuwa zoezi lililoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ili kuona jinsi wananchi wa mkoa huo watakavyojitokeza katika kuokoa au kusaidia ajali ikitokea.

“Zoezi hili lilikuwa limepangwa lifanyike. Wananchi wote hawakuwa na taarifa. Hata wahudumu (hospitali) wote hawakuwa na taarifa. Lakini walipoona tukio hilo walihudumia vizuri na wananchi walijitokeza kwa wingi, lakini kwa sasa mimi siwezi kutoa taarifa zozote, mnatakiwa kumuona RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga),” alisema Mniko.

Hata hivyo, RPC Diwani Athumani hakupatikana kuzungumzia tukio hilo ikielezwa kuwa, alikuwa katika kikao cha tathmini ya tukio hilo.

chanzo: http://mwananchi.sekenke.com/
 
Back
Top Bottom