Copy & Paste from Setfree
Wapendwa, leo kuna tukio la kustaajabisha lililotokea katika nchi fulani. Tukio hilo linafanana sana na kile ambacho Biblia inatufundisha kuhusu kuja kwa Bwana Yesu Kristo. Katika nchi hiyo, kuna mwanasiasa mwenye utata, anayeitwa Lopelope. Alitangaza kwamba leo saa mbili atalihutubia taifa hilo "live." Watu walijiandaa kumsikiliza tangu asubuhi, wakakaa tayari mbele ya simu zao na kompyuta, wakitarajia kumuona "online" saa mbili kamili. Lakini kilichotokea ni tofauti kabisa – saa mbili ikapita, saa tatu ikapita, bado hajatokea. Hatimaye mitandao iliyokuwa imepanga kurusha "live" hotuba yake ikakata matangazo. Watu wakaingiwa na hasira na kuanza kulalamika: “Kwanini Lopelope hajatokea?”
Ndugu zangu, tukio hilo ni mfano halisi wa fundisho la Bwana Yesu. Biblia inasema:
“Kesheni basi kwa maana hamjui siku wala saa atakapokuja Mwana wa Adamu.” (Mathayo 25:13)
“Basi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.” (Luka 12:40)
Yesu hajasema ni lini atarudi. Watu wengi wanataka kujua tarehe na saa, lakini hakuna anayeijua isipokuwa Baba wa Mbinguni (Mathayo 24:36). Kazi yetu siyo kujua tarehe, bali ni kukesha na kujiandaa kila wakati.
Fikiria waliokuwa wanamngojea Lopelope: walikuwa macho, walijiandaa mapema, lakini wakachoka, wakavunjika moyo kwa sababu hakutokea kwa muda walioutarajia. Vivyo hivyo, watu wengi leo wamepunguza bidii ya kumngojea Yesu kwa sababu wanaona kana kwamba amekawia.
Yesu atakuja ghafla, kwa siku na saa wasiyoitarajia watu, kisha kufumba na kufumbua atawanyakua wote waliotubu dhambi zao na kumwamini, na kuwapeleka mbinguni.
Kwa mantiki hiyo, Yesu anaweza kuja hata leo usiku. Hivyo tujiweke tayari kama wale wanawali wenye busara (Mathayo 25). Itakuwa kilio na kusaga meno kwa watu wasiokesha, maana wataachwa duniani; na dunia yote itapatwa na dhiki kuu ambayo haijawahi kutokea tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
Copy & Paste from Setfree