J_Okay
JF-Expert Member
- Nov 22, 2010
- 318
- 196
Umewahi kujiuliza kama iwapo matakwa ya ndugu Humphrey Polepole yangetekelezwa angesema anayoyasema sasa mitandaoni kupambana na Rais Samia?
Siamini hilo. Haijalishi kama ni kweli au ya uongo, nina hakika tusingeyajua yote haya nina hakika maana asingekuwa na haja ya kulipa kisasi. Falsafa ya Polepole ni aidha njia yangu au hamna njia. Ni kajitu kama DNA ya udikteta na ndio maana kalinawiri na kupendwa na bwana yule aliyepita.
Inatisha kuona kuwa mtu kama Polepole yuko tayari kufanya lolote lake liwe – hata kutoa siri alizozijua kwa kuamniwa kwenye chama chake na Serikalini na akala kiapo. Ukimsikiliza, haini tabu kutumia vitisho (blackmail): Msipofanya hivi, nitafanya hivi. Sitashangaa siku akitokea hata rekodi za afya za rais, siri za maisha binafsi – alimradi lake liwe.
Cha ajabu ni kuwa Polepole hana huo usafi wa kuwa wa kwanza kumlenga jiwe Rais Samia. Mpaka hivi majuzi alikuwa ni shetani ambaye sasa anapambana kujigeuzi kuwa malaika.
Mwenyewe amesikika akiomba radhi kwa ushiriki wake katika mambo maovu ya kuunda mifumo ya wizi wa kura, lakini sasa kwa sababu mambo hayaendi anavyotamani yawe, yeye kajivua ushetani na kuvaa umalaika... mpaka itakampofalia tena kurejea ushetanini.
Na nimaminini kuwa atarejea ushetanini kwa sababu hajawahi kujuta kuwa msaidizi wa Mwenda zake na kiuhalisia huyo ndie Mwenda Zake ndiye kiigizo chake. Ukimsoma Polepole vema anatamani kusimika utawala utawala wa ndoto zake unaofanana na uliopita wa awamu ya tano. Lakini wote tunajua giza la haki na uhuru lililogubika enzi zile.
Ajabu ajabu ajabu Polepole hadi amekuwa mtetezi wa Tundu Lissu akisahau wakati akiwa shetani alishiriki katika njama za kumuangamiza, aidha kwa moja kwa moja au kwa vinginevyo, wakati huo akiwa msaidizi mkuu na wa bwana mkubwa aliyeenda zake. Hii ni mbinu ya kutafuta uungwaji mkono, hapo hatujazungumzia wahanga wengine. Kilele cha unafiki.
Kuna na huyo Askofu Josephat Gwajima, shetani mwingine aliye mbioni kujibadili kuwa Malaika!, kiumbe anayejulikana kwa chuki yake dhidi ya dini nyingine akitamani hadi zitoweke kwenye uso wa dunia na ambaye aliingia bungeni kwa kupitia uporaji wa kura. Maajabu! Maajabu!
Nini hasa kinatokea?
Kinachotokea hapa ni Polepole na hata Askofu Gwajima kushindwa kukubaliana na ukweli kuwa mzee wao wa awamu ya tano alifariki. Kutokubaliana huko kunapelekea watamani nchi ingeendeshwa kama alivyoendesha bwana mkubwa.
Lakini hilo halijawahi kuwezekana, haliwezekani, na halitawezekana. Kiukweli ni kuwa kila urais ni tofauti. Kila urais una vipaumbele tofauti, mitindo yake ya kuongoza na hata vipaumbele havifananani. Hiyo inafanya kila urais uwe na uzuri na udhaifu wake.
Urais sio sayansi, kwamba, kuna namna moja ya kutawala, kama ambavyo moja jumlisha moja jawabu haliwezi kuwa jingine zaidi ya mbili! Kwa nini basi Polepole adhani kuwa urais wa Samia yafaa uwe rudufu ya Magufuli? Huko nyuma kuna waliofanana? Au Magufuli ndio rejea ya urais bora?
Kimkakati kabisa, Polepole kaamua azingatie ubaya wa Kikwete na Samia, lakini vipi kuhusu wengine? Huna ya kukumbushia kuhusu ufisadi wao na makosa yao makubwa yaliyogharimu nchi na kupoka haki za watu?
Unadhani tukianza kumpekua Kikwete, tutaacha pia kumchunguza Magufuli aliyeirejesha nchi maili 10,000 nyuma katika safari yake ya ujenzi wa demokrasia, na bila kumsahau Nyerere na madudu yake mengi.
Polepole anazungumzia kuhusu genge la wahuni, lakini lilikuwepo pia genge la wasukuma wala halizungumzii utadhani halikuwepo, genge ambalo katika nyakati zake za umaarufu harufu ya ukuu wa kisukuma ilitawala kila ofisi?
Kuna jambo jingine lililojificha katika haya yote. Hisia kuwa ukristo unakandamizwa. Lakini yuko wapi kiongozi mmoja tu wa dini ya Kikristo aliyekaa mahabusu miaka 10 bila kesi kusikilizwa? Ntakuonesha dazeni ya kama hao Waislamu. Wapigania haki Polepole na Gwajima mbona hamuwasemei hao? Bado wanadhani wanaonelewa zaidi?
Wanazijuia hawa kesi za ugaidi ambazo zimewafundisha ndugu zetu Waislamu kujifunza kuacha hata kulalamikia mambo ya msingi kabisa katika haki zao? Hivi kama, kwa mfano, Polepole na Gwajima, wangekuwa Waislamu wakinukuu aya za Qur’an na visa vya Muhamadi wanajua kingewatokea nini?
Polepole anazungumzia sana mila lakini natamani angeanza na mila ya taifa kabla ya hiyo ya CCM. Mila ya taifa hili, iliyohubiriwa mno, ni kutenganisha dini na siasa, ya kutotumia hisia za udini kujenga hoja za kisiasa ambazo hatimaye zinaamsha hisia za watu kuchukiana kidini na taifa kugawika. Huu moto unachochewa utaliunguza taifa na wawili hawa na wanaowasaidia watabeba msalaba huo. Na bahati mbaya, haya mambo hayanaga ‘reverse gear’ yakianza ni mwendo mdundo.
Hili linalinipeleka kwenye nadharia ya ‘greater good’. Mnapambana na ufisadi lakini mtakapokuwa mmemaliza huo ufisadi, kwa hiyo njia mnayotumia ya ‘kibiblia’ huku mkiwalenga watu wa dini moja (kana kwamba marais wengine waliopita wote ni watakatifu), hakuna namna watu hawatasoma udini ndani yenu.
Mwishowe, mtaamsha hisia za kali za udini katika mchakato wenu, hasa kwa namna mnavyoonesha ukuu wa kanisa dhidi ya imani nyingine - kwamba nyinyi ndio mnaamua lipi liwe na lipi lisiwe Tanzania.
Nikirudi kwenye mila, hivi Polepole ulipomshawishi Warioba agombee urais ulisahau mila unayoitataja ma kuitetea kila mara, ya kuwa aliyewahi kuwa waziri mkuu hafai kugombea urais? Hakujua mila ya kuzuia magenge kula njama nje ya mchakato rasmi kusimamisha mgombea?
Nina mengi ya kusema lakini nihitimishe hapa kwa leo kwa kusisitiza aliyejibadili kuwa malaika kwa muda mfupi kutimiza malengo maovu... hebu tuache kaka. Tumechoka.
Kwenu Watanzania, mwajua kuwa hatuna taifa jingine zaidi ya hili. Maoni yangu ni kuwa hakuna jema litakalotokana na huu mwenendo zaidi ya kuligawa taifa. Mimi sijali kuhusu mnaenda kupiga kura au hamuendi, mnamchagua tena Rais Samia au la, lakini natamani Polepole na Gwajima, kwa kulipenda taifa lao wawe makini na kujizuia kwa yale wasemayo.