kitabu hiki na vingine vingi vinapatikana ndani ya maktaba app(by pictuss). Inapatikana playstore.
Sehemu I
ONYESHO I
Kijiji cha Ngarambe (Rufiji)
Njia inakwenda mtoni. Bibi Kitunda na mtoto wake, Chausiku, wanatoka kuchota maji.
CHAUSIKU: Mama tazama-nyumba ya Kinjeketile! Moshi!
BI KITUNDA: Pengine anapika. Ebu chungulia.
(Mtoto anakwenda. Hajafika mbali) Ludi, Chausiku! Ludi, anakuja ntu.
(Mtoto anarudi, anachukua mtungi wake).
BI KITUNDA: Habali, Bi Kinjeketile?
BI KINJEKETILE: Nzuli, nzuli. Salama?
BI ·KITUNDA: Salama tu. Leo watu hawajaludi mpaka sasa. Wamechelewa.
BIKINJEKETILE: Shamba la Bwana Kinoo limezidishwa ukubwa sasa. Kila ntu, nasikia, kapata mahali pakubwa zaidi.
BI KITUNDA: Bule tu. Hata huyo mume wangu akiludi sina cha kumpa. Nimetafuta walau muhogo, hata sikupata; na mizizi inatisha. Ntoto wa Bi Bobali amekufa—kwa hiyo hiyo mizizi.
BI KINJEKETILE: Kweli Bi Kitunda. Hata mimi naona taabu kupata chakula. Njaa.
BI KITUNDA: Isiwe njaa nanna gani, wanaume wenyewe wote wanalima shambani kwa Bwana Kinoo? Njaa itakosa wapi?
BI KINJEKETILE: Kweli unayosema.
BI KITUNDA: Mwenzangu huna hata kisamvu au kihogo unigaiye?
BI KINJEKETILE: Sina, babu.
BI KITUNDA: Basi sisi tulipoona moshi tukafikili unapika.
BI KINJEKETILE: Moshi ule ... Kinjeketile huyo anafanya kafala. Kajifungia ndani leo siku ya ngapi sijui.
BI KITUNDA: Kweli mimi simuoni. Lakini nanna gani yeye anaweza kukaa ndani bila kwenda shambani?
BI KINJEKETILE: Sijui, pengine amekwenda. Mimi sendi kuntazamatazama.
BI KITUNDA: Siku moja nikankuta ntoni peke yake. Mimi nilikwenda kalibu akuniona. Alikuwa anafata nto unakotokea. Anatazama maji kama hajayaona.
BI KINJEKETILE: Kabadilika sana. Analosema mimi silisikii. Aya kwa heli.
BI KITUNDA: Kwa heli.
(Wanaachana. Kimya. Bi Kitunda na mtoto wake wamebaki peke yao. Wanatazama moshi unaotoka kwa Kinjeketile. Mama mtu anamwambia mtoto) Katazame wanapika nini. (
Chausiku anakwenda nyumbani kwa Kinjeketile huku ananyema. Amefika akitaka kuchungulia-mara mbio. Mama yake anamkamata.)
BI KITUNDA: Nini
?
CHAUSIKU: Nyoka! Nnafukuzwa na nyoka.
BI KITUNDA: Yuko wapi?
CHAUSIKU: Nyuma yangu.
BI KITUNDA: Wapi?
CHAUSIKU: Nyuma yangu.
BI KITUNDA: Akuna nyoka,
Akuna nyoka.
Tazama!
Yuko nyoka?
Akuna nyoka.
CHAUSIKU: Alikuwepo-nmemuona.
(Kimya. Wanatazama moshi)
BI KITUNDA: Kinjekitile.
(Kimya)
Watu wengi wanarudi kutoka shambani wamechoka, wana msaidia Kitunda. Bi Kitunda anakwenda kwa mumewe.
BI KITUNDA: Nini kimetokea?
BWANA WA KWANZA: Kitunda aliinuka kunyosha mgongo. Mnyapala akampiga viboko. Kitunda hakukubali; alikikamata kiboko. Pale pale Jumbe akaja, akaamrisha akamatwe atandikwe.
MNYAPALA: Pale akuna maongozi juu yaliyopita shambani. Itakuwa taabu.
KITUNDA: Niache nimtoe! Oho ...
(Anataka kupigana. Anafungwa mdomo na bwana wapili. Anamnong'oneza.)
BWANA WA PILI: Kumbuka kuna mkutano leo, watu wamekwisha kuja. Imani. Imani. Basi, Bwana Mnyapala. Yamekwisha. Basi.
MNYAPALA: Asifanye taabu. Kesho mapema kazini.
(Mnyapala anaondoka. Watu wengine wanakwenda mtoni. Kitunda na Bi Kitunda wanakwenda kwao. Chausiku angali anautazama moshi.)
KITUNDA: Unatazama nini?
BI KITUNDA: Chausiku alikwenda kalibu na nyumba ya Kinjeketile, akafukuzwa na nyoka.
KITUNDA: Nilitaka sana kuonana na Kinjeketile lakini, Ieo alipata mahali mbali na mimi.
BI KITUNDA: Alikuwa shambani?
KITUNDA: Nimemuona mtu kama yeye ... Yeye hasa, lakini kwa mbali.
BI KITUNDA: Mkewe kasema yuko ndani anafanya kafala.
KITUNDA: Mimi nimemuona leo!
BI KITUNDA: Ajabu hii.
(Wanatazama moshi huku wanaondoka.)