"Peter Colmore na Masengo na Mimi Bosco" Mwenda Jean Bosco Katika Nyimbo Yake: "Shangwe Mkubwa" (1960)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,261
PETER COLMORE, MWENDA JEAN BOSCO NA EDUARDO MASSENGO, KENYA 1959


View: https://youtu.be/1LH7T6hbKto?si=j8ZNHvlOpbzEOdX4

Majina haya matatu: Peter Colmore, Eduardo Masengo na Mwenda Jean Bosco yana sehemu maalum katika maisha yangu.

Nilianza kumsikia Mwenda Jean Bosco, Eduardo Masengo kisha Peter Colmore nikiwa mtoto mdogo.

Hawa wote watatu walikuwa watu maarufu Afrika ya Mashariki utangazaji kupitia radio ulipoanza mwanzoni mwa miaka ya 1950.

Tanganyika Sauti ya Dar es Salaam ilianza mwaka wa 1952.

Huu ndiyo mwaka muziki wa Mwenda Jean Bosco uliponza kusikika Tanganyika na ndiyo mwaka mimi nimezaliwa.

Muziki wangu wa kwanza kuusikia katika radio na gramaphone ulikuwa muziki wa Bosco, muziki wa Septeto Habanero kutoka Cuba na baadae muziki wa Salum Abdallah na Cuban Marimba.

Kumbukumbu hizi hazijapotea katika kichwa changu na zimekuwa sehemu ya uandishi wangu.

Kwa ajabu kabisa nimekuja kuunganishwa na watu hawa kwa karibu sana kupitia kwanza kwa baba yangu Salum Abdallah kisha kupitia Ally Sykes na Peter Colmore.

Kwa hakika ni historia ya kuvutia sana na kuleta kumbukumbu ya maisha yalivyokuwa wakati wa ukoloni mimi bado mtoto mdogo sana dunia yangu ikizunguka kati ya Mtaa wa Kipata na Mtaa wa Livingstone alipokuwa akiishi mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha Mohamed.

Bi. Mwanaisha alikuwa na gramaphone na santuri za wanamuziki hizi nikizisikiliza kwake.

Nakumbukuka kumuona Peter Colmore nikiwa mdogo kwa kuwa nyumba yetu Mtaa wa Lindi Street (Zamani Kirk Street) ilikuwa jirani na ofisi yake ambayo kwa upande wa Tanganyika ndiyo ilikuwa ofisi ikiendeshwa na Ally Sykes.

Peter Colmore alikuwa kila akija Dar es Salaam kwa shughuli zake za kazi alikuwa anakaa International Hotel, Annex nyumba ambayo ilikuwa ya tatu kutoka kwetu.

Alikuwa akiishi hapo hotelini na mlango wa chumba chake ulikuwa na jina lake limeandikwa kwa ''brass.''

Hii iliwekwa makhsusi kuitambulisha nguvu ya Peter Colmore ambae miaka ile alikuwa na ndege yake binafsi na Rolls Royce.

Mtu tajiri.

Ukivuka barabara ndiyo unaipita International Hotel yenyewe na nyuma yake ndiyo ilipokuwa ofisi yake ya High Fidelity Production alipokuwa Ally Sykes.

Nyumba hii baadae mambo yalipowachafukia Peter Colmore alimwachia Ally Sykes biashara ya Tanganyika na akamuuzia nyuma ile Ally Sykes.

Nyumba hii ikaja kutaifishwa na serikali mwaka wa 1971.

Yote haya ni mikasa kuanzia Colmore kuondoka Tanzania hadi ofisi aliyomuuzia Ally Sykes kutaifishwa.

Makao Makuu ya kampuni ya Peter Colmore, High Fidelity Productions yalikuwa Delemere Avenue, Nairobi.

Nimemjua Ally Sykes katika ofisi hii lakini kabla baba yangu hajaamia mtaa ule.

Fast Forward.

Sasa mimi ni mtu mzima nimemaliza kuandika kitabu cha Abdul Sykes baada ya kufunguliwa Nyaraka za Sykes.

Huu ulikuwa mwaka wa 1991 mswada ulipokamilika.

Katika nyaraza hizi ndipo nilipokutana na Peter Colmore, Eduardo Masengo
na Hugh Tracey Mzungu kutoka Southern Rhodesia ''aliyemvumbua,'' Bosco Congo akipiga gitaa lake mtaani kujiburudisha na kuwaburudisha rafiki zake.

Kwa hakika ziwezi nikaleza kila kitu kwani hatutatoka hapa.

Itoshe kusema tu Hugh Tracey ndiye akamfanya Bosco afahamike kwa kurekodi muziki wake akaupeleka Johannesburg kampuni ya Gallatone zikatengenezwa santuri na kuanza kusambazwa na hivi ndivyo musiki wa Mwenda Jean Bosco ulipofika Tanganyika na Afrika ya Mashariki yote.

Mwaka ni 1995 niko nyumbani kwa Peter Colmore, Muthaiga sehemu wanakoishi matajiri wakubwa wa Kenya.

Mimeweza kumashawishi Ally Sykes kukubali tukae kitako tuandike kumbukumbu zake, ''Under The Shadow of British Colonialism in Tanganyika.''

Tumefika mwaka wa 1942 Ally Sykes kijana mdogo wa miaka 16 ametoroka nyumbani kujunga na KAR, Jeshi la Waingereza ili awe sehemu ya Burma Infantry akapigane Burma Vita Vya Pili Vya Dunia.

Hiki ni kisa kinachoweza kumtoa kila mzazi machozi.

Historia hii kanihadithia Bi. Bahia Lumelezi nyumbani kwa Ally Sykes mbele yake na mbele ya mkewe, Bi. Zainab.

Bi. Bahia anasema mama yao alikuwa analia anajitupa chini akigaragara na wakati mwingin akizimia.

Ally kamfuata kaka yake vitani.

Turudi kwa Ally Sykes keshajiunga na KAR Burma Infantry.

Tulipofika hapa Bwana Ally akanyanyua simu akampigia Peter Colmore Nairobi na kumwambia kuwa anamleta mwanae kwake anaandika kitabu cha maisha yake.

Akamwambia Colmore kuwa anataka yeye amueleza historia ya maisha yao na vipi walikutana Nairobi wote wakiwa katika unifomu ya jeshi la Kiingereza lililokuwa likipambana na Wajerumani, Wataliani na Wajapani.

Hivi ndivyo nilivyojikuta niko nyumbani kwa Peter Colmore.

Peter Colmore akanieleza historia yake na Ally Sykes na ndiyo pia akanieleza historia yake na Eduardo Masengo na Mwanda Jean Bosco.

Peter Colmore ndiye ''aliyemvumbua,'' Eduardo Masengo siku moja machana River Road, Nairobi katika kilabu cha pombe za kienyeji akipiwapigia gitaa walevi na yeye kaka chini walevi wale wamemzunguka.

Mara moja alipomsikiliza Masengo alikigundua kipaji cha huyu kijana.
Kuanzia siku ile Masengo maisha yake yakabadilika.

Akaingizwa studio na Peter Colmore kurekodi muziki wake na kupitia Masengo ndipo Colmore akajuana na Mwenda John Bosco.

Bosco na Masengo walikuwa binamu.

Peter Colmore akamchukua Edward Masengo hadi Elizabethville kumfuata Bosco ili aje Kenya kuitangaza Aspro.

January 1959 Peter Colmore na Edward Masengo wakapanda ndege hadi Elizabethville kumchukua Bosco kujanae Nairobi.

Bosco tayari alikuwa mwanamuziki maarufu Afrika ya Mashariki lakini hakuna hata mtu mmoja aliyepata kuona hata picha yake huyu Bosco anafananaje.

Serikali ya Wabelgiji wakaweka sharti Peter Colmore alipe Franca 30,000 kama dhamana kuhakikisha kuwa Bosco atarejeshwa Congo.

Bosco wakati huo kama nilivyoeleza hapo mwanzo alikuwa akirekodi muziki wake na kampuni ya Gallatone kutoka Johannesburg.

Bosco alikaa Nairobi kwa miezi sita.

Peter Colmore alimtembeza Bosco Kenya nzima akiitangaza Aspro kwa muziki wake kama dawa mujarab kwa mafua, kuumwa kichwa na homa.

Mauzo ya Aspro yalipanda sana.
Bosco wakati ule alikuwa kijana wa miaka 29.

Alipokamilisha mkataba wake anarejea kwao Elizabethville Bosco alimtungia Peter Colmore nyimbo, ''Shangwe Mkubwa,'' na wakairekodi hapo Nairobi.

Siku zote nikiisikiliza nyimbo hii huwa nawakumbuka watu hawa ambao wote sasa ni marehemu.
1703479285708.jpeg

1703479336028.jpeg

1703479395311.jpeg

1703479442484.jpeg

 
Back
Top Bottom