Penzi jini hatari

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
12919686_1284996248181877_7933896011048899692_n.jpg

PENZI JINI HATARI.
1
Penzi ni jini hatari, wa kutesa na kuua,
Huzibeba zote shari, za kiangazi na mvua,
Nina kuomba Qahari, miye asije niua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
2
Penzi mganga mzuri, huponya wanougua,
Hukusanya nyingi heri, za mwezi hata za jua,
Kwa idhini Ya Jabari, aponye changu kifua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
3
Mapenzi istiimari, hakika nimetambua
Baridi naona hari, meli mwenzenu mashua,
Asali kwangu shubiri, ninajuta kuyajua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
4
Mapenzi ni zingifuri, kwa mja anayejua,
Narauka Alfajiri, naswali naomba dua,
Yarabi penzi la siri, lisije kuniumbua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
5
Penzi si kama johari, huwezi kulinunua,
Si mchanga wa bahari, bure ukalichukua,
Thamaniye si mahari, mkaja hata jazua.
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
6
Penzi halina jabari, si chuma la kuinua,
Uwe bondia hodari, pia laweza sumbua,
Huba zataka sukari, moyo upate kutua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
7
Mapenzi jua qadari, uwaze na kuwazua
Alo lipanga Ghafuri, hakuna wa kupangua,
Hivyo hatuna hiyari, hata kama twaamua
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
8
Mapenzi si kibatari, ni mshumaa tambua,
Nyonda apate fahari, mwenyewe unaungua,
Yengekuwa samsuri, wallahi ningeyavua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0622845394
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom