Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
PENZI JINI HATARI.
1.Penzi ni jini hatari, wa kutesa na kuua,
Huzibeba zote shari, za kiangazi na mvua,
Nina kuomba Qahari, miye asije niua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
2.Penzi mganga mzuri, huponya wanougua,
Hukusanya nyingi heri, za mwezi hata za jua,
Kwa idhini Ya Jabari, aponye changu kifua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
3.Mapenzi istiimari, hakika nimetambua
Baridi naona hari, meli mwenzenu mashua,
Asali kwangu shubiri, ninajuta kuyajua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
4.Mapenzi ni zingifuri, kwa mja anayejua,
Narauka Alfajiri, naswali naomba dua,
Yarabi penzi la siri, lisije kuniumbua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
5.Penzi si kama johari, huwezi kulinunua,
Si mchanga wa bahari, bure ukalichukua,
Thamaniye si mahari, mkaja hata jazua.
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
6.Penzi halina jabari, si chuma la kuinua,
Uwe bondia hodari, pia laweza sumbua,
Huba zataka sukari, moyo upate kutua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
7.Mapenzi jua qadari, uwaze na kuwazua
Alo lipanga Ghafuri, hakuna wa kupangua,
Hivyo hatuna hiyari, hata kama twaamua
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
8.Mapenzi si kibatari, ni mshumaa tambua,
Nyonda apate fahari, mwenyewe unaungua,
Yengekuwa samsuri, wallahi ningeyavua,
Mahaba yanizuzua, mtima wata ghururi.
Dotto Rangimoto Chamchua (Njano5)
0622845394