52...
Kwa Smith, hicho ndicho kilikuwa kipindi maalumu cha kuionyesha dunia kwamba msichana yule aliyekuwa bora kwa kuimba duniani, alikuwa mpenzi wake. Pasipo kujiuliza chochote kile, pasipo kuogopa kamera wala kujua kwamba watu wawili waliokuwa wakimpenda sana Tatiana walikuwa wakilifuatilia shindano lile kwenye televisheni, hapohapo akamkumbatia Tatiana kwa nguvu kisha kuanza kubadilishana mate kitu kilichoshangiliwa sana na watu waliokuwa pale ukumbini.
*****
Ilikuwa ni zaidi na kupigiliwa msubali wenye ncha kali moyoni mwake au kuteketezwa na moto huku akijiona, maumivu aliyokuwa ameyapata Peter yalikuwa makubwa yalioufanya mwili wake kuanza kutetemeka na kijasho chembamba kuanza kumtoka.
Hakuamini kile alichokuwa akikiona mahali pale, msichana aliyekuwa akimpenda, aliyempa nafasi kubwa moyoni mwake, alikuwa amesimama jukwaani na mwanaume mwingine kisha kubadilishana mate naye.
Alihisi wivu mkali ukiuchoma moyo wake, hasira zake zikawaka, pasipo kutarajia, machozi yakaanza kububujika mashavuni mwake. Hakuendelea kuangalia kwani kadiri alivyokuwa akiangalia na ndivyo alivyozidi kuumia zaidi, akajikuta akiizima televisheni na kukimbilia chumbani.
Huko hakunyamaza, akaanza kulia kwa sauti ya juu kama mtoto. Wafanyakazi wa nyumba ile wakaogopa kwa kuhisi kwamba inawezekana kulikuwa na msiba, hivyo wakaanza kuelekea chumbani kwa Peter lakini mlango ulifungwa kwa ndani.
Walijaribu kuugonga lakini haukufunguliwa, bado kilio cha Peter kiliendelea kusikika ndani ya chumba kile, kilio kilichochanganyikana na maumivu makali ya moyo wake.
“Peter...fungua mlango,” alisema mfanyakazi mmoja, alikuwa mama mtu mzima.
Peter hakutaka kufungua mlango, bado aliendelea kubaki ndani huku akilia tu. Alishinda ndani asubuhi mpaka mchana.Mchungaji Lazaro aliporudi kutoka kanisani, akaambiwa kile kilichokuwa kimetokea.
“Kisa nini?” aliuliza.
“Hata sisi hatufahamu, tulisikia tu akilia,” alijibu mfanyakazi yule.
Mchungaji Lazario akaelekea chumbani kwa Peter, akajaribu kuufungua mlango lakini ulikuwa umefungwa kwa ndani. Mama Peter akawa na wasiwasi kwamba inawezekana kulikuwa na jambo baya lilikuwa limetokea, hivyo kuendelea kuuliza zaidi.