SEHEMU YA 20...
Ilikuwa ni barua ndefu, baada ya bi Frida kumaliza kuisoma, uso wa Tatiana ulijawa na tabasamu pana, maneno matamu yaliyoandikwa ndani ya barua ile yakaufanya moyo wake kufarijika mno.
Hakujali kama mbele yake alikuwepo mama yake, barua ile iliugusa moyo wake kupita kawaida. Mama yake aliyekuwa mbele yake, akamsogelea na kumkumbatia, bi Frida akashindwa kujizuia, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
Tatiana alikata tamaa, hakuamini kama kwenye maisha yake angetokea mwanaume ambaye angetamka kwamba alikuwa akimpenda mno. Mbali na uzuri aliokuwa nao, alikuwa msichana kipofu ambaye angeshindwa kufanya kitu chochote katika maisha yake, kitendo cha kusikia kwamba Peter alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, kwake ikaonekana kuwa faraja kubwa.
Hicho ndicho kilichokuwepo hata kwa mama yake, hakutegemea kama ingetokea siku ambayo angekuja mwanaume na kumwambia kwamba anampenda na alitaka kumuoa na hatimaye waishi milele.
Hata kama walimpenda Mungu, hawakutaka kufanya dhambi lakini barua ya Peter ikawafanya wabubujike na machozi muda wote. “Mama! Ninapendwa....” alisema Tatiana huku akilia kama mtoto.
“Unapendwa mwanangu, Mungu amekuletea mwanaume atakayekuwa bora katika maisha yako,” alisema bi Frida huku akijitahidi kuyafuta machozi yake.
Barua ile, ikaifanya mioyo yao kubadilika na kufurahi sana, ila pamoja na hayo, hawakutaka mzee Sangiwa afahamu chochote kile.
“Nimwambieje?”
“Mwambie umekubaliana naye.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Huyu mwanaume ameletwa na Mungu! Hii ni baraka,” alisema bi Frida.
Tatiana akaanza kuandika barua ya majibu. Japokuwa alikuwa kipofu, ila alikuwa na uwezo wa kunyoosha mwandiko, hasa kwenye karatasi.
Ila mbali na hayo, alijua kwamba kulikuwa na mapenzi pasipo maumivu, yaani angependa na kupendwa siku zote, asingeumizwa kitu ambacho hakikuwa kweli, kwa kuwa alikubali kuingia kwenye mapenzi, basi ilimpasa kukubaliana na maumivu pia kitu ambacho hakuwa akikielewa kwa wakati huo.
Itaendelea.