PENDEKEZO LA WASTANI: Tusiishie kutengana kwenye kuchinja; tutengane kwa kila kitu...

Status
Not open for further replies.

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,478
40,000
KAMA TUMEAMUA KUWA WADINI TUSIISHIE NJIANI –TWENDE HADI MWISHO Na. M. M. Mwanakijiji


539433_10151398986191156_154230423_n.jpg

Hatujali tena kama sisi sote ni Watanzania. Hatujali tena kuwa kama taifa moja hatima yetu ni moja – tukifanikiwa tunafanikiwa sote, tukianguka tunaanguka sote. Yale maneno tuliyoimba utotoni (ujanani kwa wengine) kuwa "Binadamu wote ni ndugu zangu" hayana maana tena. Leo hii tumeamua kujitenga kwa kutumia kiwango cha chini kinachotuunganisha – dini. Kwamba leo kama jamii ya watu tumeingia kwenye ule mtego ambao wengine tumeonya sana na kwa machozi wa kuamua kujitenga kwa kuangalia dini zetu.

Mwaka 2009 niliandika makala moja ambayo ilikuwa na kichwa cha habari "Huu Uenzetu Huu". Katika makala ile nililiangaliza taifa kuwa tumefika mahali tunaangalia nani anafanya uhalifu na tukiona ni mwenzetu wa aina fulani basi ndivyo tunavyoamua kuitikia. Tukikuta ni mtu wa dini yetu basi tunaangalia mara mbili tatu kabla hatujaanza kupiga kelele. Nikatolea mfano wa suala la Mkapa na Kikwete na jinsi gani wote wawili inaonekana wanapendwa sana na watu wa dini zao na watu wa dini zao hawajawa na uthubutu wa kuwakemea.

Matukio ya siku za karibuni yamezidi ni kunithibitisha kuwa tulipofika siyo tu ni pabaya lakini kwa kweli ni pagumu sana kurudi. Inawezekana tumefika mahali ambapo hatuwezi kurudi tena na hivyo ni lazima twende mbele ya pale tulipofika hadi tuone mwisho wake. Makala yangu hii basi inaenda mbali zaidi kutoka kwenye makala ile ya 2009. Katika makala hii nimetafakari sana hasa baada ya matukio ya Mwanza kuhusu kuchinja wanyama kwa ajili ya kuuza na hadi tukio la mauaji ya Padre Mushi huko Zanzibar.

Tumeamua kutukuza dini zetu? Tukio la Mwanza na mwitikio wa kwanza wa serikali kupitia Waziri Wassira umetuhakikishia kuwa tofauti ambayo tulijua ipo ni kubwa kuliko tulivyodhania. Waislamu wameamua kudai pasi ya shaka kuwa wanataka wao waachiwe kuchinja wanyama kwa sababu hawataki kulishwa kibudu na Wakristu na kuwa kuna kanuni za uchinjaji wa Kiislamu ambao unapaswa kuzingatiwa. Kwa kukosa hekima Wassira akakubali pendekezo hilo bila kufikiria matokeo yake.

Matokeo yake Wakristu wakiongozwa na maaskofu wao wakakuali pendekezo hilo lakini wakaenda mbali. Wakasema na wao hawataki waumini wao wale nyama iliyochinjwa katika ibada wa Waislamu kwani maandiko yao yanakataza kula vilivyotolewa katika ibada ambazo wao hawaziamini. Lakini hawauishia hapo Wakristu sasa wamefika mahali – kama kule Geita – kutangaza kuwa sasa kutakuwa na mabucha ya Wakristu ambapo watachinja wanavyopenda wao na Wakristu wakanunua huko.

Cha kusikitisha sana ni kuwa waumini Wakiislamu wako nyuma ya viongozi wao na waumini wa Kikristu wako nyuma ya viongozi wao. Waislamu wachinje wanavyotaka na kuuziana wenyewe na Wakristu wachinje wanayvotaka na kuuziana wenyewe na kila mmoja atakuwa na furaha. Mkristu akiamua kuchinja nguruwe, mbuzi au sungura hataki aulizwe na Muislamu na Muislamu akichinja anavyochinja anataka wengine wale kwa sababu yeye ndiyo halali kuchinja.

Yote hii ni kwa sababu tumeamua kutukuza dini zetu kuliko undugu wetu, ujamaa wetu, familia zetu na kwa hakika umoja wetu wa asili. Tumeamua kukumbatia udini wa kijinga niliouzungumza miaka michache nyuma na hapa tulipofika hatuna budi twende hadi mwisho wake.

Kujitenga katika jumuiya Sasa tumefika mahali – na sitaki kurudia kwanini kwani nimeandikwa kirefu juu ya hili tangu 2006 – kwamba jamii yetu imeanza kukubali kutengana. Swali la kuchinja nyama ni suala moja na wala siyo kubwa kivile. Lakini limekuwa kubwa zaidi kwa sababu wapoo baadhi ya Waislamu ambao wanaamini katika jamii ya Watanzania ni wao peke yao wanatakiwa kuchinja wanyama wa biashara (labda hata binafsi) ili kwamba wasilishwe kibudu. Na wanadai kuwa wanafanya hivi kwa sababu mnyama lazima achinjwe Kiislamu na hivyo awe ‘halal'. Kutokikidhi hilo ni kutojali hisia zao za kidini (religious sentiments).

Sasa wametaka wao wawe wachinjaji katika mabucha na wengine wanatakahata kwenye sherehe wao ndio wachinjaji. Sasa yote hayo si tatizo kwani kuna njia nyingi tu za kuweza kukubaliana. Lakini walioharibu ni watu wa serikali kuingilia kati kwa namna walivyoingilia. Wassira – sababu ya uzembe au woga – hakujali hisia za kidini za Wakristu hivyo akaamua kutangaza tu kuwa Waislamu ndio wachinje. Hakufikiria wala kujali je Wakristu wako tayari kula wanyama waliochinjwa na Waislamu? Hasa kama inasemwa kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya "ibada"?

Matokeo yake utengano ukatokea – Wakristu wakaamua wa mara ya kwanza kukataza waumini wao kula nyama iliyochinjwa katika ibada ya Waislamu. Lakini hawakuishia hapo tu wakasea basi kuanzia sasa watakuwa namabucha yao yatakayouza nyama waliochinja wao (bila ya shaka hata nyama ambayo wengine hawaruhusiwi kula kutokana na imani yao). Mkristu "bila kuuliza uliza" anaweza kwenda kununua nyama kwenye bucha la Waislamu kwani anaamini "ufalme wa Mungu si katika kula na kunywa bali katika haki, amani na furaha ya Roho Mtakatifu" (Rum 14:17)

Matokeo ya maamuzi ya makundi haya ya Waislamu na Wakristu ni kuwa vijana wetu wameanza kutengana. Nimekuwa kwenye mitandao ya kijamii toka mwanzo wake na labda ni miongoni mwa Watanzania wachache ambao tumekuwa kwenye mitandao ya aina hii kwa karibu miaka kumi na nne sasa lakini sijawahi kuona Watanzania Wakristu na Waislamu wakitofautiana, kuitana majina, kudharauliana na kusutana kwa sababu ya dini. Kwa kweli ni aibu!
Lakini tumeamua kuufuata ujinga basi tuufuate hadi mwisho wake. Waislamu si wanakereka na Wakristu na Wakristu wanakereka na Waislamu nakuwa haiwezekani tukarudi na kuishi pamoja na kushirikiana, kuheshimiana, kuinuana pamoja basi twende mbele katika ujinga wetu hadi tufike mwisho. Si viongozi wetu na wenyewe wamekuwa sehemu ya ujinga huu huu? Basi na wao na sisi tuufuate hadi tuone hitimisho lake la kimantiki. Kama tumeamua kutengana tusitengane kwenye kuchinja tu twende mbele zaidi? Si udini umekuwa dini; twendeni tuabudu kwa pamoja!

Tutengane katika elimu Waislamu wanadai kuwa mfumo Kristu unawakandamiza na kuwa unawafelisha watoto wao katika elimu. Matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka juzi yamethibitisha kuwa kashfa kubwa zaidi nchini ni ile katika elimu. Kwamba asilimia 60 ya watoto wetu waliofanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne wamefeli. Katika shule ishirini bora zilizofanya vizuri 13 ni za Kikristu na katika shule kumi zilizofanya vibaya zote kumi ziko kwenye maeneo yenye Waislamu wengi. Nina uhakika watu wakipitia matokeo hayo na kuangalia watoto waliofaulu sitoshangaa wapo watakaoona watoto wa Kiislamu wakiwa wengi wamefeli (bila kujali kama wapo wakristu wengi pia wamefeli) na kuendelea na hoja ya kuwa elimu inawatenga.

Sassa kwa vile tumeamua kuufuata ujinga tusiwawajibishe kina Kawambwa, tusizibeze sera mbovu za elimu za CCM, tusitake kuiondoa madarakani tutengane! Waislamu wawe na shule zao – kuanzia za chekechea hadi sekondari na Wakristu vile vile. Na tusiishie huko tu twende hadi vyuoni! Maana katika shule zinazochanganyika sasa hivi, Waislamu wanaweza kuona wanaonewa au mahitaji yao ya kidini hayatimizwi (si tumeona Bagamoyo mwaka jana? Sasa kwanini tugombane?

Si Nyerere ambaye wapo wanamuita "dhalim" aliamua kutaifisha shule hadi za kidini ili watoto wa Kikristu, Kiislamu na Wapagani wasome kwa pamoja? Si leo watu wanamuita "amelaaniwa" huku viongozi wakuu wakifuta hadhi yake ya Baba wa Taifa na kumuita "Mzee Nyerere" si kwa sababu ya heshima bali kufuta upekee wa mchango wake katika historia yetu? Sasa tuufuate ujinga hadi mwisho wake! Kama Wakristu na Waislamu hawawezi kusoma pamoja, kwa heshima na kujaliana hakuna jinsi isipokuwa kila jamii iwe na shule zake – si tumeanzia kwenye mabucha?

Tutengane katika makazi Mmojawapo wa wachochezi wa udini Ustaadh Illunga ambaye amepata umaarufu sana siku za karibuni katika video yake moja ameitisha kisasi dhidi ya Wakristu. Huyu bwana akitumia theolojia iliyopotoka amejaribu kujenga hoja kuwa akiuawa Muislamu (bila kujali kauawa na nani na kwanini) basi waislamu wana haki ya kulipiza kisasi dhidiya Mkristu yeyote. Kasema akiuawa shehe basi auawe padre, askofu, kardinali au mtu yeyote mwingine – hata mlei wa kawaida. Akifanya mkutano hadharani na akichochea faraka bila kujificha (huku watawala wakiendelea kula wavivyopanda) Bw. Illunga kawaambia wasikilizaji wake kuwa likitokea jambo kama hilo basi mlei yeyote mtaani kwao ni haki yao.

Sasa kwa vile tumeamua kuufuata ujinga tuufuate hadi mwisho! Kwanini Wakristu na Waislamu waishi kwa kuogopana? Kwanini kusiwe na mitaa ya Wakristu na Mitaa ya Waislamu? Wakristu wataishi kwenye maisha yao, wanywe pombe zao, wavae nguo zao wanavyopenda bila kujisikia wanalazimishwa kuwa wasivyo na Waislamu wakifuata mafundisho ya dini na wenyewe waishi katika mitaa inayoongozwa kwa maadili ya Kiislamu. Si wakoloni ndivyo walivyoigaa Dar - kukawa na Muslim Quarters na Christian Quarters? Kama Wakoloni walikuwa na akili ya kututenganisha tukatukuza kwanini leo tusijitenganisha wenyewe tukajitukuza? Ili kuhakikisha anayekuja mtaani kwenu ni mwenzenu basi mnaweza kuweka ‘check points' na vitambulisho! Utajuaje sasa kama ni Mkristu mwenzio au Muislamu mwenzio!

Tutengane katika kazi Kwa vile ujinga tulioamua kuufuata wa kutukuza dini zetu na kusahau umoja na udugu wetu kiasi cha kutishiana maisha basi tusiachie njiani. Tuufuate hadi mwisho wake. Leo hii Wakristu na Waislamu wanafanya kazi pamoja na wengi wamekuwa wakifanya kazi pamoja katika nafasi mbalimbali kwa miaka na miaka. Hakukuwa na tatizo watu walifanya kazi vuziri tu. Leo hii watu wanaogopa kujadiliana masuala mbalimbali kwani watu wataleta hoja za udini. Kwanini hawa wanakuwa na mti wa Krismasi mbona sisi hatuna, kwanini wanaenda kusali Ijumaa wakati wengine tunafanya kazi, n.k

Sasa kwanini tufike mahali watu waishi kwa woga? Huko Zanzibar siku hizi baadhi ya wafanyakazi wanaitishana roll call kila giza likiingia na mtu akikosekana kujibu simu au radio call watu wanaanza kumtafuta! Sasa kwanini kila mmoja asifanye kazi na watu wa dini yake ambako atavaa nguo anazotaka atakula anachotaka bila kujihisi anawakwaza wengine au yeye kukwazwa.

Tutengane na kwenye miji Sasa kwa vile ujinga wa udini ndio tumeamua kuufuata basi tusiishie njiani. Twende mbele zaidi. Tukishaamua kugawana makazi, elimu, na kazi tutajikuta kwamba bado tunaishi kwenye miji iliyochanganyika. Sasa hili haliwezi kuwa zuri kwa wadini kama sisi. Tutaweza vipi kuchanganyika na watu wa dini nyingine, tuwaone wanavyovaa, wanavyosali, na kuishi? Njia pekee ni kuamua kugawana miji! Sijui tutatumia kanuni gani lakini miji ya Wakristu iwepo na miji ya Waislamu (wengine tunaweza kuwaweka katikati kama mpaka! Sasa sijui kama wilaya tu inatosha bali itabidi tutenge mikoa kabisa; ile yenye WAislamu wengi iwe ya Waislamu na ile yenye Wakristu wengi iwe ya Kikristu!

Unaweza ukasema mwanakijiji kachanganyikiwa lakini ukifikiria sana utaona hakuna namna. Waislamu wanataka kuishi Kiislamu na kufuata ibada wanayotaka bila kukwaza na Wakristu nao Wakristu wanataka kuishi wanavyoishi wao wenyewe. Sasa kwanini tusirahisishe tu. Mikoa kama Tanga, Lindi, Mtwara, Tabora, Kigoma, Pwani, iwe ni mikoa ya Waislamu watupu halafu mikoa kama Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Shinyanga iwe ya Wakristu na mikoa mingine tunaweza kufikiria namna ya kuifanya! Hivyo, Wakristu wataishi kwenye mikoa yao na Waislamau vile vile. Tukiufuata ujinga tusiishie njiani!

Tugawane uongozi wa kisiasa Sasa mojawapo ya malalamiko makubwa ambayo yametokea siku hizi ni kuwa wapo Waislamu ambao wanakejeli kabisa mchango wa Nyerere na kumuona ndiye chanzo cha matatizo yao; hawa wamewarithisha watoto wao simulizi kuwa Nyerere ndiye aliyesababisha matatizo yao yote na wao hawana lolote katika hili. Hivvyo, kwao uongozi wa Kikristu ndio umetengeneza mfumo "kristu". Hawa wanachukia siyo kanisa tu, bali dhana nzima ya Ukristu kwao ni adui na kiongozi wa KIkristu hawako tayari.

Na kuna uwezekano wataanza kudai kuwa kutawaliwa na Muislamu ni bada na hivyo wanataka watawaliwe na Muislamu mwenzao tu. Wakristu nao wanapoona kuwa matukio fulani fulani yanatokea chini ya utawala wa Muislamu nao wanaanza kuwa nawasiwasi kama wanaweza kuishi kwa amani chini ya uongozi wa Kiislamu. Sasa isiwe shida; baada ya kugawana mitaa na miji ni wazi kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kuchagua viongozi kwa kuangalia dini zao. Sasa kama tutabakia kwenye nchi moja itabidi tuwe na wagombea wawili kila mwaka wa uchaguzi; Waislamu wachague Rais wao Muislamu na Wakristu wachague Rais wao Mkristu na yeyote atakayepata kura nyingi kuliko mwingine anakuwa Rais wa wote na anayefuatia anakuwa makamu! Wakiingia Magogoni, mmoja anashughulikia mambo ya watu wa dini yake na mwingine watu wa dini yake na watu wote wawe na furaha!
Labda itabidi tuwe pia na mabunge mawili, mabaraza mawili, wizara mbilimbili ilimradi tuondoe manung'uniko!
Tukiufuata ujinga, tuufuate hadi mwisho wake!

Tugawane nchi Lakini tuigawana mitaa na miji, kazi, na shule tutakuwa kweli tumetatua tatizo la kutotaka kuishi pamoja, kuheshimiana kama ndugu na kuinuana pamoja basi sidhani kama kuna njia nyingine nzuri ya kuhakikisha watu wa dini mbalimbali wanaishi vizuri katika dini zao bila kujisikia wana lazimika kukaa katika nchi moja.

Sasa hili si jipya na siyo kwamba halijawahi kujaribiwa. Kuelekea uhuru wa India miaka sitini iliyopita, Wahindu na Waislamu waliamua mataifa mawili yatakayozaliwa yaende kwa kufuata mgawanyo wa kidini. Waliweza kuishi pamoja kwa kulazimisha na Waingereza lakini baada ya Mwingereza kuondoka wakajigundua kuwa wao ni "Wahindu" na wengine ni "Waislamu". Matokeo yake wakaamua kugawanyika; lakini baada ya vita mbaya sana baina ya pande mbili matokeo yake ni mataifa ya Pakistani na India.

Sasa na sisi tukifuata ujinga wetu tunaweza kugawa nchi sehemu mbili; ya Wakristu na ya Waislamu. Nigeria walijaribu na ikauzka vita vya Biafra; lakini leo hii kuna majimbo yamekubali kutawaliwa kwa sheria za Kiislamu (majimbo a Kaskazini) na majimbo mengi ya Wakristu (Kusini) yakiishi bila sharia. Na Wakristu wengi waliondoka Kaskazini kurudi Kusini na Waislamu wengine walitoka KUsini kwenda Kaskazini kwani hawakuweza kuishi pamoja. Je wote wanafuraha leo hii? Labda! Kwanini na sisi tusiwafuate vile vile! Tuigawe nchi ikibidi ziwe nchi mbili! Msiniulize tutaigawaje nitawaachia wajinga wenzangu wengine wenye kuufuata udini waamue au waulize wale ambao wanaamini hatuwezi kuishi pamoja katika nchi moja.

Kwenye hizo nchi Wakristu wataendelea kuwa na Ubalozi wa Vatican bila kuulizwa na mtu, kuimba nyimbo za injili huku Waislamu wakiunganisha nchi yao kwenye OIC bila kulalamikiwa na wabunge Wakristu na wanawe kupiga Qasida usiku kucha!

Pendekezo langu hili ni la wastani (a modest proposal) na nina uhakika baada ya watu kulitafakari kwa makini na kuona mantiki yake wengi watalikubali na kuhakikisha linaanza utekelezaji wake mara moja. Kwa vilet umeamua kuufuata ujinga tusiachie njiani. Kama tumeweza kuwavumilia wachochezi wa kidini, na kukubali waendelee kufanya kazi tukijua wanachofanya ni kuhasamisha jamii basi tusiishie njiani! Kama magazeti yenye mada za kichochezi yanaachiliwa yakipandikiza chuki, vituo vya radio na luninga vikichochea uhasama baina yetu basi tusiishie njiani!

Kama viongozi wetu katika woga wao wanaendelea kuvumilia uongozi mbovvu wa jesh la POlisi na Usalama wa taifa kwa sababu wenye kuongoza ni jamaa zao na hawawezi kuwafukuza huku watu wanachinjana na kuuana na watu hao hao wanarudia hotuba zile zile zilizopauka za "tunajipanga, tumeunda tume, tutahakikisha halitokei tena" basi nasema tusiishie njiani!

Na tukishatengana kabisa (complete separation) basi huko walikotengana waanze tena kuangalia ni nani ambaye hawapatani naye kwa sababu yoyote na waendelee na kutengana. Kama wengi ni Sunni (kwenye hilo taifa jipya) basi waangalia kama Shia, Ismailiya, Ahmadiya, Sufi na wengine nao wanafaa kuwemo vinginevyo na wenyewe waanze kujitenga kwa kanuni hii hii niliyoipendekeza. Hili nalo liwe kweli kwenye zile jamii za Kikristu - Wakatoliki, Walutheri, Waanglikana nao wajitenge. Haitakuwa mara ya kwanza jamii za Kikristu kujitenga kwa madhehebu - ilishatokea Ireland ya Kaskazini.

Na tukifika mwisho kabisa tuangalie kwenye familia zetu zile vile, tuendelee kujitenga hadi abakie mmoja tu na dini yake, imani yake, elimu yake, kazi yake, maisha yake, Biblia au Qurani yake. Awe na nyumba yake ya ibada, awe na shule yake atakakosomesha watoto wake n.k Kwa kadiri ya kwamba tofauti zetu hizi ni kubwa kiasi kwamba hatuwezi kuishi pamoja basi ni lazima tutengane na tukitengana tusiishie kwenye mabucha tu, mabasi na shule.

Tukiufuata ujinga tuufuate hadi mwisho.

THE END

* Kujifunza zaidi kuhusu uandishi wa 'straight up satire - kejeli ya wazi' BONYEZA HAPA
 
Tukishamaliza, kwa kuwa hewa tunayovuta inakuwa imechanganyika na hewa chafu inayotoka kwa wengine, pasi shaka kila mtu achukue mkebe wake wa hewa avute, na kutoa hewa yake, ili asipate bugudha kutoka kwa wengine, vivyo hivyo kwa maji.

wewe umenisoma.... tusiishie njiani...
 
BE SITTED, god be with you! also with ya spirit! I can iquet your brain with that of king solomon but dont revere nyerere's oration too much to forget he was an orator!

Moslem will never love christians, and they never will. tumewapenda waislamu kwa kiwango cha kuwaona ni kaka na dada zetu mpaka tulifikia kuwaunga mkono kususia kitabu cha Aya za shetani. lakini ona wao wanavyofanya kwetu. kukashifu dini yetu hadharani mpaka kutunga cds na DVDs na kuzisambaza mitaani!

ni ukweli gani wanaotaka kutuambia sisi wakristu na dini yetu ikiwa ukweli walioambiwa na muislamu mwenzao Salman Rushdi katika kitabu cha Aya za shetani,hawataki kuusikia na wanataka kumuua?
 
Mimi sijaona mantiki yoyote,zaid zaid nakuonan ni mchochezi tu unaeuma na kupuliza.,napozisoma hisia zako kwenye hili bandiko lako reeefu,naziona wazi wazi hisia za mihemko mikali ya chuki moyon mwako,nakufuatilia sana kauli zako,una lako jambo tuh..

Nadhani huja muelewa, unahitaji kulisoma tena hili bandiko, hii ni aina nyingine ya kuwasiliasha ujumbe, si lazima aeleze moja kwa moja. Soma utafakari.
 
Nadhani huja muelewa, unahitaji kulisoma tena hili bandiko, hii ni aina nyingine ya kuwasiliasha ujumbe, si lazima aeleze moja kwa moja. Soma utafakari.


Mustafa wewe humjui vyema huyu mzee,me nakuhakikishia nikimuangalia kwa jicho la undani sana sion tofauti kati ya Shekhe Ilunga na MWANAKIJIJI..
Wote nawaona ni wachichezi tuh,sema wanatofautiana approach,Ilunga anachochea wazi wazi,MWANAKIJIJI anachochea kichini chini na kujificha,waerevu tunalifaham hili..
 
Hongera kwa pendekezo lako,nisaidie kitu kimoja,unadhani Wassira alitakiwa kutoa uamuzi gani kuhusiana na swala la nani achinje?
 
wasi wasi wangu ni kuwa huo ndio ulikuwa ni mtego wa kundi fulani. Na kwa maelezo haya inaonyesha Mm umenasa.Na lengo la kutengana ni pamoja na urahisi wa kumtambua adui na hivyo kuwa rahisi kumshambulia.
 
wasi wasi wangu ni kuwa huo ndio ulikuwa ni mtego wa kundi fulani. Na kkwa maelezo haya inaonyesha mm umenasa.na lengo la kutengana ni ppamoja na urahisi wa kumtambua adui na hivyo kuwa rahisi kumshambulia

Kwa kuwa ni maamuzi ya kijinga, hatutaishia hapo, lazima tutaohoji kila tofauti baina yetu ilimradi tubaguane, maamuzi ya kijinga huzaa ujinga na kuendeleza ujinga. Ubaguzi ni tunda la ujinga
 
wasi wasi wangu ni kuwa huo ndio ulikuwa ni mtego wa kundi fulani. Na kkwa maelezo haya inaonyesha Mm umenasa.Na lengo la kutengana ni ppamoja na urahisi wa kumtambua adui na hivyo kuwa rahisi kumshambulia

Duh.. kweli tuna kazi sana; mtu kaweka na nyota kabisa lakini bado haijaeleweka...kadizooo!!! wala sifafanui..
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom