Pemba: Kisiwa kilichotengwa tangu 1652

TIGOPESA

Senior Member
Apr 2, 2014
190
62
Pemba ni kisiwa kinachojulikana kwa umaarufu kama "al'jazeera al'khadra", yaani "kisiwa cha kijani" kwa lugha ya Kiarabu; ni kisiwa kinachoelea mashariki ya pwani ya Afrika kwenye Bahari ya Hindi – ni takriban kilometa hamsini kaskazini ya kisiwa cha Unguja; na kilometa hamsini mashariki ya Tanganyika. Pemba, kama "kisiwa" kimetokea kuwa maarufu kwa zao la karafuu na hata kupewa jina la "kisiwa cha marashi".

Kisiwa hiki kina historia ndefu ya ukaaji wa bin'adam wenye ustaarabu wa kipekee wanaojishughulisha na ukulima mdogomdogo wa mazao ya mpunga, minazi, migomba (ndizi), muhogo, maharagwe-mekundu; pamoja na uvuvi wa asili kwa utumizi wa mashua na ngarawa (kwa mishipi, madema, ndoana na mitego). Pemba inasifika sana kwa kuwa na maeneo mazuri ya kupiga-mbizi, matumbawe yasiyoharibiwa na maisha mororo ya bahari kwa viumbe na/au mimea wa/ya baharini (samaki, kasa, majongoo, makonokono, matumbawe, na mwani).

Mji Mkuu wa Kisiwa cha Pemba ni Chake-Chake uliyopo juu ya ‘kilima' ilhali magharibi yake kuna kisiwa kidogo cha Misali ambapo mawimbi-bahari hutoa fursa ya wakati gani ngalawa na/au mashua zinaweza kuingia ghatini. Magharibi mwa Chake-Chake kuna mkono-bahari maarufu wa Mkumbuu uliyosheheni magofu (mabaki ya majengo) ya Ndagoni yanayokadiriwa kujengwa karne ya 14. Mashariki mwa Mji wa Chake-Chake kuna magofu ya Mkama Ndume yanayopatikana kwenye kijiji cha Pujini (kusini ya uwanja wa ndege). Magofu ya "Ngome ya Mkama Ndume", kama yanavyojulikana, yanakadiriwa kuwa ya kwanza katika pwani yote ya Afrika Mashariki yanayokadiriwa kujengwa na Wareno mnamo karne ya 15.

Kisiwa cha Pemba kinasifika kwa maeneo tajiri ya uvuvi wa samaki wa baharini. Kati ya kisiwa hicho na mwambao wa mkoa wa Tanga kuna upana wa kama kilometa 32 za Mkondo wa Pemba wenye utajiri mkubwa kwa uvuvi katika pwani ya Afrika ya Mashariki. Wakati wa "enzi za karafuu", mapato ya Zanzibar (Pemba na Unguja) yalitegemea sana zao la karafuu kwa uchumi; na sehemu kubwa ya kilimo cha karafuu (mashamba ya mikarafuu) yalikuwapo/yangalipo kisiwani Pemba (kama mikarafuu milioni 3.5 hivi) kwa vile hali ya mazingira (udongo, mvua, jotoridi na mwinuko) ya kisiwa hicho inaruhusu ukulima na ustawishaji wa zao la karafuu.

Pamoja na uzuri wa mandhari ya kisiwa cha Pemba kijiografia na kimeteorolojia, makala haya yamekuja si kuonesha uzuri wa harufu ya marashi ya karafuu, hasha! Makala haya yanajaribu kwa muhtasari kuonesha kutengwa kwa kisiwa cha Pemba tangu zama za historia ya kabla ya yale yanaoitwa leo "mapinduzi matukufu" ya tarehe 12 Januari 1964.

Pemba ni kisiwa; wala si ule Mji Mkuu wa Jimbo la Cabo Delgado (Msumbiji) au ule Mji Mdogo uliyopo nchini Zambia! Pemba ni kisiwa wanachoishi wale leo wanaoitwa Wapemba – watu wanaopatikana kisiwani, wenye asili ya kisiwani na waliyostaarabika na Uswahili wa Pemba. Wanahistoria wengi waliyoandika historia ya kisiwa cha Pemba wanakinasibisha kisiwa hicho na mchanganyiko wa watu wenye asili ya Uarabu na Uswahili (mchanyato wa Uarabu na Ubantu).

Wareno walikuwa wa kwanza kukikalia kisiwa hicho na watu wake (Wapemba wa kale) kwa mabavu hadi pale walipotimuliwa na Imam Sultan bin Seif mwaka 1652. Na kuanzia hapo, yaani mwaka 1652, visiwa hivyo, yaani Pemba na Unguja vikawa chini ya "Milki ya Sultan wa Oman". Waarabu walipofika maeneo ya visiwa hivyo waliwakuta wenyeji wa huko (weusiweusi) na ndipo walipoliita eneo hilo la visiwa kama Zinji-bar (kwa Kiarabu) au Zang-bar (kwa Kifursi).

Baada ya kuwashinda Wareno, Imam Sultan bin Seif hakuanzisha maskani yake visiwani humo bali aliondoka kurejea Oman (Maskati) na alimuweka mtu kutoka kwa ukoo wa Al'hath ili aangalie ‘milki' yake mpya! Alipofariki Imam Sultan bin Seif, mamlaka ya kuendesha shughuli za dola aliyashika mwanawe wa kiume, Seif bin Sultan ambaye alikuwa mtawala mwenye makeke na anayependa sifa za kutawala; naye ndiye aliyekuwa Mwarabu wa kwanza aliyeweza kuzuiwiya "mauwaji holela" yaliyokuwa yanafanywa na Wareno dhidi ya watu weusi wa Afrika ya Mashariki.
Mwaka 1711, mjukuu wa Seif bin Sultan aliachia ngazi baada ya kupoteza udhibiti wa kuendesha dola na mahala pake kuchukuliwa na ukoo wa Al'Busaid na hawa masultan wa ukoo wa Al'Busaid ndio waliyokuja kuwa masultan wa Zanzibar kwa muda mrefu katika historia.

Seyyid Said bin Sultan bin Ahmed (aliyetawala kati ya 1804 na 1856) alikuwa ni mjukuu wa Ahmed bin Said, kiongozi wa kwanza wa ukoo wa Al'Busaid aliyechukuwa usultan baada ya kumuuwa ami ya baba yake (Badar bin Seif) mwaka 1804 aliyetawala baada ya kifo cha Seyyid Sultan. Mnamo mwaka 1832, Seyyid Said alifanya maamuzi ya kuhamisha makao makuu ya ‘milki' yake kutoka Maskati (Oman) na kuufanya Mji Mkongwe (Unguja) kuwa ndiyo Mji Mkuu wa Milki ya Usultan wa Oman. Uamuzi huu uliigeuza Zanzibar (Unguja) katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii
Dhamira ya Seyyid Said ilikuwa ni kuubadilisha Mji wa Zanzibar (Unguja) kuwa mji wa kibiashara mashariki ya duniya. Uamuzi huo unatokana na ukweli uliyokuwapo wakati huo kwamba Unguja (Mji wa Zanzibar) ulikuwa na ulinzi asilia wa matumbawe uliyozuwiya mashambulizi ya adui kutokea baharini; pamoja na kuwa na kina (kilindi) kirefu cha bahari kinachotoa fursa kwa meli kubwa kutia nanga, vilevile ugavi muruwa wa maji safi (baridi) ya kunywa kwa min'ajili ya wafanyabiashara na meli zinazotia nanga Mjini Zanzibar.

Seyyid Said aliubadilisha Mji wa Zanzibar (Unguja) kutoka nyumba za udongo zilizoezekwa makuti (ya mnazi) hadi kuwa wa maghorofa (na maroshani) yaliyojengwa kwa mawe, chokaa na zege. Ujenzi wa nyumba ulifanywa na mafundi stadi na makini kutoka Uarabuni na kusaidiwa na vibarua wa kizalendo. Maendeleo haya ya haraka ya Mji wa Zanzibar yaliwashajihisha Waomani wengi kuhama kutoka Oman na kuja kuishi Mjini Zanzibar.

Seyyid Said alianzisha "Biashara ya Kubadilishana" na Wazungu waliyowekeza kwenye fukwe za Zanzibar. Katika kufikia malengo yake, Seyyid Said aliwashajihisha wageni (Wazungu) (kama wanavyofanya sasa watawala wa kimamboleo) kufungua vituo vya biashara kisiwani Unguja (Zanzibar), na mwaka 1833 alisaini "Mkataba wa Biashara" na Wamerekani kuanzisha biashara katika ‘milki' yake. Waomani walibadilishana bidhaa kama nazi, magamba ya kobe (kasa), pilipili nyekundu, nta na bidhaa nyengine zilizopatikana wakati huo na kwa upande wa Wamerekani waliwaletea vifaa vya ujenzi, pamba, sufi na nyuzinyuzi za nguo.

Kutokana na "Mkataba wa Biashara" uliyosainiwa, Wamerikani walianzisha wakala wa biashara Zanzibar (Unguja Mjini) aliyejulikana kama John Berthram & Co (kutoka Salem Massachusetts) na baadaye mwaka 1837 Marekani ilifungua rasmi ubalozi wa kwanza visiwani Zanzibar – makao ya ofisi za ubalozi yalikuwa Mjini Zanzibar! Kutokana na kupanuka na kunawiri kwa biashara, kampuni lingine la kibiashara la Arnold Hines & Co (kutoka New York) likafungua ofisi Mjini Zanzibar. Kana kwamba si Wamarekani peke yao, bali pia mwaka 1841 Uingereza ikafungua ofisi ya kampuni ya kibiashara iliyofuatiwa na kuweka ofisi ya ubalozi (consulate) Mjini Zanzibar. Baadaye, nchi za utaliano, Ujerumani, Ubeleji, Ufaransa, na Austria zilituma "ujumbe" wao Zanzibar ili kuangalia fursa zilizopo na kuweka vituo vyao. Zanzibar (Unguja) ilianza kuingizwa kwenye mawanda ya diplomasia ya kimataifa kutokea Mji Mkongwe (Unguja) ilhali Pemba (kisiwa) kikiachwa solemba!

Utashi wa Seyyid Said katika kukuza kilimo cha kibiashara kulipelekea kuvumbua matumizi ya ardhi yenye rutuba ya visiwa vya Pemba na Unguja. Seyyid Said alianza "utafiti" wa kutafuta zao (mmea) litakolopewa thamani na Wazanzibari na kuvuta soko la ulimwengu. Jibu la "utafiti" wake likawa ni mmea (au zao) wa karafuu uliyopatikana kutoka visiwa vya Moluccus ambao maua yake yakikauka huwa na harufu ya viungo kwa jina karafuu.

Seyyid Said alinunua miche kwa maelfu kutoka Moluccus na kuwashajihisha wakulima (wengi wakiwa Waarabu kwa wakati huo) kupanda miti ya karafuu kwa wingi! Karafuu ya Zanzibar ilikuwa bora sana kwa vile ililimwa kwenye ardhi yenye rutuba na hali-bora ya hewa. Ukulima mkubwa wa zao (mmea) hilo ulikuwa zaidi kisiwani Pemba – kwa hiyo Pemba kukawa mashamba zaidi ilhali Unguja (mjini) kukawa mjini zaidi kwa shughuli za kiserikali, kidiplomasia, kiuchumi na kijamii.

Wakati wa utawala wake Seyyid Said alikienda mara kwa mara "nyumbani kwao – Oman" kutatua mizozo ya kisiasa ya ndani; na mwaka 1856 wakati akirejea kutoka Oman alipatwa na maradhi yaliyopelekea kifo chake akiwa "chomboni" tarehe 19 Oktoba 1856 nje kidogo ya visiwa vya Ushelisheli. Baada ya kifo cha Seyyid Said alitawala mtoto wake mdogo wa kiume, Seyyid Majid Said bin Sultan (aliyetawala kati ya mwaka 1856 hadi 1870) alichukuwa usultan badala ya kaka yake Thuwain. Thuwain alijaribu kutaka nafasi ya usultan (wa Zanzibar) hata hivyo Uingereza ambayo ilikuwa "mlinzi" iliteuwa Tume ya Canning kutatua mzozo huo.

Uingereza ilimpendelea Majid na wakati huohuo iliweza kumpoza Thuwain. Uamuzi ulikuwa kwamba Thuwain atawale Oman na maeneo ya pembe ya Afrika (Djibuti, Eritrea na Somaliland) na Majid atawale Zanzibar. Uamuzi huu ulianzisha tawala mbili ndogo chini ya "Milki ya Usultan wa Oman" na kuweka mifumo ya utawala na mahakama ilipofika mwaka 1861.

Mfumo huu wa utawala ulisababisha mizozo kati ya Majid na kaka yake Bargash; na Uingereza kama kawaida yake iliingilia kati na kumpeleka Bargash Mumbai (Bombay) nchini India kwa masomo zaidi. Baada ya kifo cha Majid, Barghash alirejea Zanzibar akiwa na uchu, hamu na ghamu ya kuchukuwa utawala ili kuonesha utashi wake wa kuyaenzi maisha ya kimagharibi na kifahari aliyoyapata alipokuwa masomoni nchini India. Kwa mtaji huo, Seyyid Barghash alitumia fedha nyingi kwa maendeleo ya usultan wake – aliwezesha kusambaza maji ya bomba (mfereji) kutoka kwa chechem ya asili hadi Mjini Zanzibar!

Mwaka 1872, Seyyid Barghash alilishawishi kampuni la meli la India la British India Steam Navigation Company kuanza huduma za kila mwezi za usafiri wa meli kati ya miji ya Aden na Zanzibar. Huduma hii iliiwezesha Zanzibar kusafirisha barua na vifurushi sehemu mbalimbali za dunia. Baada ya kufunguliwa kwa Mfereji wa Suez (mwaka 1869), Seyyid Barghash aliingia mkataba na kampuni la Eastern Telegraphic Company kutandaza mkonga wa mawasiliano ya simu chini ya bahari kati ya Aden na Zanzibar! Kazi ya kutandaza mkonga huo wa chini ya bahari ilimalizika mwaka 1879 na ofisi ya mawasiliano ya simu ilifuguliwa kukiwa na wataalamu na mafundi sanifu kutoka Uingereza, Goa na Mumbai (Bombay) – India.

Inasemekana kwamba Seyyid Said alikuwa kinara wa kuzuiya biashara haramu ya utumwa pale alipotiliana saini na Uingereza wa kuizuwiya biashara hiyo mwaka 1870; hii ilifuatiwa na kuzuwiya biashara hiyo kwenye ‘milki' ya Zanzibar na kulifunga "Soko la Watumwa" lililokuwapo Mkunazini (mahala palipojengwa Kanisa la Kiingereza – Anglican Church). Seyyid Barghash alikufa mwaka 1888 kutokana na utu uzima na msongo wa kuongoza ‘milki' yake.

Kifo cha Seyyid Barghash kilimleta kwenye kiti cha usultan Seyyid Khalifa aliyeendeleza yale ya Barghash hususan kuzuia biashara haramu ya utumwa na yeye (Khalifa) alitoa amri kwamba "watumwa wote watakaoingia kwenye milki yake wataachwa huru". Seyyid Khalifa alikufa kwa "homa" akiwa na umri wa miaka 36 tarehe 13 Februari 1890 akitawala miaka miwili tu!

Baada ya Seyyid Khalifa alifuatia Seyyid Ali bin Said. Seyyid Ali bin Said aliiweka Zanzibar na Pemba chini ya "Ulinzi wa Uingereza" mnamo tarehe 1 Novemba 1890. Katika kipindi hichohicho kifupi alichotawala Seyyid Ali bin Said alitawala vilevile Seyyid Hemed bin Thuwein (yaani kati ya mwaka 1890 hadi 1893). Wote hawa walikuwa na maskani yao Mjini Zanzibar!

Seyyid Khalid bin Barghash alichukuwa utawala wa Zanzibar kwa "nguvu" mnamo tarehe 25 Agosti 1896 kinyume na utashi wa Uingereza waliyomtaka Seyyid Hamoud. Khalid bin Barghash alipewa muda maalumu wa kujisalimisha kwa Uingereza, aliposhindwa meli za kivita za Uingereza zilizokuwa chini ya amri ya Rear Admiral Rawson zililishambulia "Jumba la Kisultan" kwa mizinga; na kuhofia usalama wake Khalid bin Barghash alikimbilia Dar es Salaam na kuomba hifadhi kwa serikali ya Ujerumani iliyokuwa inatawala Tanganyika wakati ule.

Baada ya kukimbia kwa Khalid bin Barghash Uingereza harakaharaka ikamuapisha Seyyid Hamoud kuwa Sultan wa Zanzibar. Seyyid Hamoud alikuwa na mtoto mmoja wa kiume aliyekiitwa Ali aliyesomeshwa Uingereza katika Chuo Kikuu cha Harrow. Seyyid Hamoud alikufa tarehe 18 Juni 1902 akiwa na umri wa miaka 51 baada ya kifo cha rafiki yake mpenzi na msiri wake mkuu, Sir Lyod Mathews aliyekufa mwaka 1901.

Wakati wa kifo cha Seyyid Hamoud, Ali alikuwa mtoto (kijana) mdogo. Alipopewa kiti cha usultan aliishi maisha ya kimagharibi kama alivyozoweya alipokuwa akisoma Uingereza. Mwaka 1911 alikaribishwa kuhudhuria "Sherehe za Kuwekwa Wakfu wa Ufalme" Mfalme George wa IV. Alipokuwa Ulaya aliamua kukitelekeza kiti cha usultan na kubaki Ulaya! Katika mazingira ya kutatanisha alifariki akiwa Ufaransa katika mwaka huohuo (wa 1911). Watoto wake waliyobaki Zanzibar hawakuhitaji kiti cha usultan alichokiacha baba yao!

Nafasi iliyoachwa wazi na Seyyid Hamoud ilichukuliwa na Seyyid Khalifa bin Haroub na "Ulinzi wa Uingereza" uliondolewa kutoka Ofisi ya Mambo ya Nje na kupelekwa kwenye "Ofisi ya Makoloni" mwaka 1925. Ofisi ya Ubalozi na Wakala wa Ufalme (Consulate and Majesty Agency) ilibadilishwa na nafasi ya Balozi wa Uingereza Mkazi iliundwa. Katika kipindi hiki bandari ya Zanzibar ilipanuliwa na kuwekwa zana na vifaa; barabara za lami zilijengwa kuzunguka maeneo muhimu ili kurahisha biashara. Vilevile, elimu na huduma za afya zilibuniwa na kupanuliwa hadi mashambani! Mfumo wa sheria uliboreshwa kwa kuweka mabaraza ya wenyeji (native councils) na mahakama za mudir zilianzishwa. Seyyid Khalifa bin Haroub alifariki Oktoba 1960. hata wakati wa kifo cha Sultan Seyyid Khalifa bin Haroub alikuwa akiishi Mjini Zanzibar!

Nafasi ya Khalifa bin Haroub ikachuliwa na Seyyid Abdullah bin Haroub. Hata hivyo utawala wake ulikatishwa na kifo kilichotokana na hali mbaya ya afya yake. Alikiugua "kisukari" kwa muda mrefu hali iliyopelekea kuvimba kwa "gangrene" na kusababisha miguu yake ikatwe. Seyyid Abdullah bin Haroub alifariki mwaka 1963 alipokuwa anafanyiwa upasuaji wa kukata miguu yake!

Na wa mwisho katika silsila ya usultan wa Zanzibar alikuwa Seyyid Jamsheed bin Abdullah. Jamsheed bin Abdullah alikuwa mtoto wa Seyyid Abdullah bin Haroub; alipata elimu yake kwenye Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Naval Academy, Uingereza kama wanavyosoma watoto wengi wa familia za kifalme na/au kisultani. Seyyid Jamsheed bin Abdullah alimrithi baba yake tarehe 1 Julai 1963. Kama baba yake, utawala wake haukuwa mrefu na aliondolewa na "mapinduzi" yanayoitwa matukufu ya tarehe 12 Januari 1964! Jamsheed bin Abdullah alifanikiwa kutoroka kwa kutumia mashua binafsi (Al Hathira) hadi Dar es Salaam na alipewa "hadhi" ya ukimbizi wa kisiasa nchini Uingereza.

Masultan wote tuliowasoma na kuwaelezea hapa walielekeza nguvu zao kiuchumi, kisiasa na kijamii katika kuijenga Zanzibar Mjini (Unguja) na kuiacha Pemba pembeni. Hata yale mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 yaliyoandaliwa na "Field Marshal" John Okello (Messiah Mjinga) yaliendeleza hali hiyo ya kukitenga kisiwa cha Pemba na Wapemba sawiya!

Upembuzi na udondozi wa kihistoria wa kutengwa kwa kisiwa cha Pemba ndio chimbuko la "mpasuko" wa kisiasa unaoendelea leo visiwani humo. Historia inaonesha kwamba: palikuwapo na ZPPP (Zanzibar and Pemba Peoples Party) na ZNP (Zanzibar Nationalist Party) vilivyoungana mwaka 1961 na kuunda umoja wa Waafrika weusi (wengi) na Waarabu (wachache) waliyokilazimisha chama cha ASP (Afro-Shirazi Party) kuwa chama cha upinzani! Ngome ya ZNP ilikuwa Pemba – na hili ndilo chimbuko la kuendeleza "chuki" inayotokana na "mapinduzi daima" yaliyoasisiwa na "mhandisi, mhunzi, fundi-mchundo" wa mapinduzi aliyeshirikiana na baadhi ya mamluki waliyokodiwa kuendesha mauwaji ya watu kati ya 15,000 na 25,000 wengi wakiwa wenye asili ya Kiarabu, Kihindi na Kifursi.

John Okello alipanda mbegu ya chuki kati ya Wapemba na Waunguja na kutengeneza "upogo" uliyojengwa kwenye misingi ya ubaguzi wa rangi (na dini); japokuwa wapo watu wa Unguja wanaojiita Waislam ilhali vitendo vyao ni kinyume navyo. Kuundwa kwa CCM (kulikotokana na kuunganishwa kwa ASP na TANU) ilikuwa njama mahsusi ya kuviingiza visiwa vya Pemba na Unguja katika mfumo wa Kimarekani na kuondoa satwa ya Waingereza waliyokuwa nayo kabla ya tarehe 10 Desemba 1963 siku ya Uhuru wa Zanzibar na kufuatiwa na mapinduzi yaliyofanywa kwa madai ya kuondoa usultani wa ki-Oman na kuweka usultani wa tabaka la wanaojiita "wanamapinduzi" – wenye uchu na tamaa ya kuendeleza kumwaga damu za watu wasiyo na hatia.

Kama Wapemba (na kisiwa cha Pemba) walitengwa kijamii, kiuchumi na kisiasa tangu mwaka 1652, sioni sababu kwa nini Pemba isijitenge!

Hii inatosha kuonesha utengano uliyopo – ni ufa gani unaotakiwa uzibwe kama hali ni hii kwa zaidi ya miaka 350? Matokeo ya songombingo na/au sintofahamu ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa kipindi cha miaka kati ya 1652 na 2014 inatosha kuonesha kutengwa kwa kisiwa cha Pemba. Na kama ipo nia ya dhati kwa yeyote anayejifanya mkombozi (na/au mtatuzi) wa kutafuta tiba mujarabu ya mpasuko wa kisiasa visiwani Unguja na Pemba; basi na aitazame upya historia ya mpasuko huo na nini chanzo chake kisha aelekeze "nguvu" za ziada katika kulivunja "genge" la wahafidhina wenye ubaguzi ndani ya CCM-Zanzibar. Inawezekana, ni uamuzi makini unaohitajika kuukubali ukweli wa "Mpasuko wa Zanzibar" na utashi wa kisiasa kuutatua unaohitajika. Viongozi wa CCM (Bara na Zanzibar) waache unafiki, unazi, uzabizabina, uzuvendi, undava, na undumilakuwili wakubali ukweli juu ya suluhisho la kudumu.
 
Naomba kujua haya:

Hao wapemba wa kale wakoje?....maana umesema wareno ndy wa kwanza kuukalia huo mji kimabavu dhidi ya wapemba wa kale....


Mreno aliondolewaje pemba?...kwa mazungumzo au kimapinduzi?...

Katika safu ya masultan wote waliotawala pemba...je kuna hata mmoja alikuwa 'mpemba wa kale'?,,,' mchanyato wa kibantu na kiarabu'?...

Kabla ya kuingia wareno na waarabu katika pemba...walikuwa na mfumo gani wa utawala?...


Tafadhali.
 
Kabla ya wageni wapemba asili walikuwa na uongozi was aina gani? Na kama walikuwa wabantu waliongea lugha gani
 
Back
Top Bottom