Operation Kataa Ndoa - SAWA, vipi kuhusu child support, nayo utakataa? Jifunze hapa kuhusu malezi na matunzo ya Mtoto (Sheria ya Mtoto) ujipange!!

sajo

JF-Expert Member
Nov 8, 2010
3,026
5,258
Operation imepamba moto, vijana wanahimizana kukataa ndoa kwa kutokuoa ila hakuna anayepinga kuhusu suala la kujaza ulimwengu. Mizagamuano na misuguano inaleta sio tu raha na burudani kwa wafanyaji bali pia inaleta watoto kwenye dunia. Wakishakuja sasa wapenzi wanaanza kukimbiana na wengine kufikishana polisi kwenye madawati ya jinsia. Sasa basi kam yamekukuta ua hayakukuta, usiondoke bure hapa, kaa ujifunze kuhusu sheria ya mtoto na namna ya kuitumia.

SHERIA YA MTOTO YA MWAKA 2009

Tunaendelea na masomo yetu ya Sheria kila mwezi. Somo la leo linahusu malezi, uangalizi na matunzo ya mtoto pale wazazi wake wanapokuwa hawapo pamoja kimahusiano. Wazazi wa mtoto wanaweza kumaliza mahusiano yao kwa talaka, kutengana au mapenzi kufa (ikiwa hawakuwa wanandoa) lakini kama walifanikiwa kuwa na watoto bado wana wajibu wa kuwatunza na kuwalea. Jambo hilo limekuwa gumu kufanyika (practical) kwani wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kukomoana na matokeo ni madhara kwa watoto wao. Ndipo katika Mazingira haya, Serikali ikatunga sheria ya mtoto ya mwaka 2009 (imerejewa mwaka 2019) ili kuweza kuweka utaratibu wa kufuatwa kuhakikisha mtoto anapata matunzo na malezi vile ipasavyo.

Naitwa Lusajo W. Mwakasege, ni Mwanasheria, namba yangu ya simu ni 0713-368153 (inapatikana whatsapp In WhatsApp teilen na telegram) na telegram) na barua pepe yangu ni mwakasege@gmail.com. Tuanze somo letu:

MTOTO NI NANI?
Mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane (18).
👉Kwa sheria ya mtoto ya Tanzania, mtoto anaweza kutambulika tangu akiwa tumboni mwa mama yake (yaani kutambulika kabla hata hajazaliwa).


MALEZI, UANGALIZI, KUMTEMBELEA MTOTO NA MATUNZO

A: NI WATU GANI WANAOWEZA KUOMBA ULEZI (PARENTAGE) WA MTOTO?


Sheria ya mtoto inaeleza kuwa watu wafuatao wanaweza kuiomba Mahakama kutoa amri ya kumthibitisha kupewa malezi ya mtoto -

(a) mtoto mwenyewe;

(b) mzazi wa mtoto;

(c) mlezi wa mtoto;

(d) Afisa Ustawi wa Jamii; au

(e) mtu mwingine yeyote, ikiwa mahakama itatoa amri maalum.


B: JE, NI MUDA GANI MTU ANAWEZA KUFANYA MAOMBI YA ULEZI WA MTOTO?

👉 Kabla ya mtoto kuzaliwa;

👉 Baada ya kifo cha baba au mama wa mtoto;

👉 Kabla mtoto hajatimiza umri wa miaka kumi na nane; au

👉 kwa kibali maalum cha mahakama baada ya mtoto kutimiza miaka kumi na nane.


C: JE, MAHAKAMA INATUMIA VIGEZO VIPI KAMA USHAHIDI KATIKA KUTOA AMRI YA MALEZI YA MTOTO?
  • Ndoa yoyote iliyofungwa kwa kuzingatia Sheria ya Ndoa;​
  • Jina la mzazi lililoingizwa kwenye Rejesta ya vizazi na kutunzwa na Msajili Mkuu wa Vizazi;​
  • Taratibu za kiasili (adoption) zilizofanywa na baba wa mtoto;​
  • Kutambuliwa na jamii kama mzazi wa mtoto; au​
  • Majibu ya Vinasaba vya Binadamu (Human DNA).​

D: JE, NINI KIFANYIKE IKIWA BABA MZAZI WA MTOTO ANAKATAA UBABA WAKE KWA KUDAI YEYE SIO BABA WA MTOTO?

Mama wa mtoto anaweza kuiomba mahakama itoe amri ya kumlazimisha mtu anayehisiwa kuwa ni baba mzazi wa mtoto kufanyiwa kipimo cha DNA katika maabara ya ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali;

▪️Pia ikiwa ushahidi wa mama haujitoshelezi na haujairidhisha mahakama kuhusu ubaba wa mtu, mahakama yenyewe bila hata ya ombi la mama inaweza kuamua vipimo vya kinasaba (DNA) kifanyike ili kumthibitisha baba wa mtoto.

JE, KATIKA MAZINGIRA HAYO NI NANI ATALIPIA GHARAMA ZA KIPIMO CHA DNA?

Mahakama itaamua yenyewe kuwa nani kati ya mama au baba alipie gharama za kipimo cha DNA.

👉 Kwa sasa, Gharama za kipimo cha DNA ni Tshs. 100,000/= kwa mtu mmoja. Hivyo kwa uchunguzi wa baba, mama na mtoto jumla ya gharama ni Tshs. 300,000/=.

Zingatia:
Maombi ya kipimo cha DNA hayafanywi moja kwa moja na wahusika bali hutakiwa kuombwa na maafisa ustawi wa jamii, mawakili wa kujitegemea, mahakama, jeshi la polisi, madaktari, Wakuu wa Wilaya au taasisi za tafiti zinazotambuliwa kisheria.


E: NINI KITATOKEA IWAPO KIPIMO CHA DNA KITATHIBITISHA UBABA MZAZI?

Ikiwa kipimo cha DNA kitamthibitisha mtu kuwa baba mzazi wa mtoto, Mahakama itatoa amri kwa baba mzazi kuchukua jukumu la kumtunza na kumlea mtoto huyo kama vile mtoto huyo amezaliwa ndani ya ndoa,

Mtoto aliyepata ulezi baada ya baba yake kupimwa DNA na kuthibitishwa juu ya uzazi wake atakuwa na haki zote kutoka kwa baba yake huyo ikiwa ni pamoja na haki ya kurithi mali za baba yake (Lakini hii itategemea imani ya dini ya baba yake).


F: JE, NI KOSA KUKATAA UBABA NA ULEZI WA MTOTO BAADA YA KIPIMO CHA DNA?

NDIYO
, Sheria inaeleza kuwa mtu atayekataa amri ya mahakama kwenda kupimwa DNA, au kukataa kumlea mtoto baada ya kipimo cha DNA kufanyika na kumthibitisha kuwa ni baba mzazi wa mtoto, anatenda KOSA LA JINAI.

Mtu huyo atakapotiwa hatiani, adhabu yake ni kulipa FAINI isiyopungua Tshs. 500,000/= au kifungo cha miezi mitatu (3) jela au vyote viwili kwa pamoja, FAINI na KIFUNGO jela.

G: MAOMBI YA ULEZI YANAKUWA DHIDI YA NANI?

▪️ Mtu anayesadikiwa kuwa baba mzazi wa mtoto;

▪️Mwangalizi wa mtoto nk📌

mtoto africa 2.jpeg
 
UANGALIZI WA MTOTO (CUSTODY)

H: NI WATU GANI WANAOWEZA KUOMBA UANGALIZI WA MTOTO?
👉 Mzazi, mlezi au ndugu anayemlea mtoto anaweza kuiomba mahakama impe uangalizi wa mtoto;

👉 Pia, wakati mwingine mahakama inaweza kutoa amri ya uangalizi wa mtoto kwa mwombaji wakati wa utoaji wa amri ya malezi tuliyoiona awali na wakati mwingine amri hii huweza kutolewa na mahakama wakati wa utoaji wa talaka.

📍Utoaji wa amri ya uangalizi wa mtoto huzingatia kwanza MASLAHI YA MTOTO na sio ya wazazi au mwombaji.

▪️Hata hivyo, amri ya uangalizi wa mtoto inaweza kutenguliwa na mahakama muda wowote na uangalizi kupewa mtu mwingine au taasisi maalumu ikiwa kutakuwa na ulazima.


I: MAMBO YANAYOWEZA KUPELEKA UTENGUZI WA AMRI YA UANGALIZI

👉Tabia mbaya ya mwangalizi (mzazi au mlezi) ikiwa ni pamoja na :-
▪️ulevi uliopitiliza,

▪️utumiaji wa mihadarati,

▪️ukahaba nk

▪️Kifo cha mwangalizi

▪️Hali ya kiafya ya mwangalizi (hii ni pamoja na afya ya akili)

▪️ Maslahi (maoni) ya mtoto


J: KUMTEMBELEA MTOTO (ACCESS)

Mzazi, mlezi au ndugu aliyekuwa anamlea mtoto kabla ya Mahakama kuamuru mtoto huyo alelewe na mtu mwingine, anaweza kuiomba mahakama imruhusu kumtembelea mtoto katika vipindi fulani.


K: JE, ZIPI NI HAKI ZA MTOTO PALE WAZAZI WAKE WANAPOTENGANA (SEPARATION) AU KUTALIKIANA (DIVORCE) KISHERIA?

Mtoto atakuwa na haki ya;

👉Kupata matunzo na elimu yenye ubora ule ule aliyokuwa anaupata kabla wazazi wake hawajatengana au kutalikiana;

👉 Kuishi na mzazi ambaye, kwa maoni ya mahakama, ana uwezo wa kumlea mtoto kwa kuzingatia maslahi ya mtoto; na

👉 Kutembelea na kukaa na mzazi mwingine wakati wowote mtoto atakapotaka isipokuwa kama mpango huo hautaingilia na programu ya masomo au mafunzo.


L: JE, MTOTO ANAWEZA KUPANGIWA KUISHI NA MTU MWINGINE BILA KUJALI UMRI WA MTOTO?

NDIYO
, bila ya kujali umri wake, mtoto anaweza kupangiwa kuishi na mtu yeyote yule ikiwa jambo hilo litakuwa na maslahi kwa mtoto husika.

🔘Lakini ikiwa mtoto ana umri wa chini ya miaka 7, kutakuwa na dhana isiyopingika kuwa ni maslahi ya mtoto huyo kuishi na mama yake mzazi, isipokuwa kama kutoa amri hiyo kutaathiri maisha ya mtoto kwa kuhamisha makazi yake.

ANGALIZO:
Dhana isiyopingika maana yake ni kuwa, ikiwa kutaletwa uthibitisho wa kupinga dhana hiyo, basi dhana husika itafutika mara moja.

Kwa muktadha huu maana yake ni KUWA sio lazima mtoto aliye chini ya umri wa Miaka 7 kuishi na mama yake.


M: MAMBO YAZINGATIWAYO NA MAHAKAMA WAKATI WA KUTOA AMRI ZA ULEZI NA UANGALIZI

🔷 Haki ya mtoto kuhusu makazi yake (makazi ya mtoto);

🔷 Umri na jinsia ya mtoto;

🔷 Kuzingatia kuwa na wazazi wake isipokuwa tu kama haki zake zinavunjwa mara kwa mara na wazazi wake;

🔷 Maoni ya mtoto kama maoni hayo yametolewa huru;

🔷 Kuwa ni muhimu kuwaweka watoto pamoja;

🔷 Kuzingatia umuhimu wa mwendelezo wa malezi na usimamizi wa mtoto; na

🔷 Sababu nyingine yoyote ambayo mahakama itaona inafaa.​


N: JE, NI KOSA KUMTOROSHA MTOTO AU KUMNYANG'ANYA KUTOKA KWA MTU ANAYEISHI NAE?

Ikiwa amri ya kuishi na uangalizi wa mtoto ulitolewa kwa amri ya mahakama, Mtu yeyote atakayemtoa kwa nguvu mtoto na kumtorosha ili aishi naye yeye badala ya aliyeamriwa na mahakama, atakuwa ametenda KOSA LA JINAI.​
 
MATUNZO YA MTOTO
O: JE, NI NANI ANA WAJIBU WA KUTOA MATUNZO (MAINTANACE) YA MTOTO?

Mzazi ambaye amri ya malezi imetolewa kwake atakuwa na wajibu wa kuchangia ustawi na matunzo ya mtoto na kutoa mahitaji muhimu kwa uhai na maendeleo ya mtoto.

P: NI WATU GANI WANAOWEZA KUOMBA AMRI YA MATUNZO YA MTOTO?

👉 Mzazi wa mtoto;

👉 Mlezi wa mtoto;

👉 Mtoto, mwenyewe kupitia mwangalizi wake;

👉 Afisa Ustawi wa Jamii; au

👉 Ndugu wa mtoto.


Q: JE, MAOMBI YA MATUNZO YA MTOTO YANAFANYWA DHIDI YA NANI?

Maombi ya kumtunza mtoto yanaweza kufanywa dhidi ya mtu yeyote mwenye uwezo wa kumtunza mtoto au kuchangia katika ustawi na matunzo ya mtoto huyo.

Lakini mtu huyo ni lazima awe mwenye uhusiano na mtoto.


R: JE, MAHAKAMA INAWEZA KUTAFUTA TAARIFA ZAIDI MBALI YA USHAHIDI ULIOWASILISHWA NA MWOMBAJI?

NDIYO
, Mahakama yaweza kumuamuru Afisa Ustawi wa Jamii katika mazingira husika kuandaa taarifa ya uchunguzi wa kijamii kabla ya kutoa uamuzi juu ya maombi ya amri ya matunzo, uangalizi na kumtembelea mtoto.

Mahakama katika kutoa amri hizo itazingatia taarifa ya uchunguzi wa kijamii iliyoandaliwa na Afisa Ustawi wa Jamii.


S: JE, MAOMBI YA MATUNZO YA MTOTO YANAWEZA KUFANYWA DHIDI YA MTU ANAYESADIKIWA KUWA BABA MZAZI WA MTOTO?

NDIYO
, Maombi yanaweza kufanywa mahakamani dhidi ya mtu anayehisiwa kuwa baba wa mtoto.

Maombi hayo yanaweza kufanywa:


▪️ Na mama mtarajiwa, wakati wowote kabla ya mtoto kuzaliwa;

▪️ Wakati wowote ndani ya masaa ishirini na nne tangu mtoto alipozaliwa;

▪️ Wakati wowote baada ya mtoto kuzaliwa pakiwa na uthibitisho kwamba mtu anayesadikiwa kuwa ni baba mzazi wa mtoto aliwahi kutoa fedha za matunzo ya mtoto ndani ya miezi ishirini na nne baada ya mtoto kuzaliwa;

▪️ Katika muda wowote ndani ya miezi ishirini na nne (24) baada ya mtu anayesadikiwa kuwa ni baba mzazi wa mtoto kurudi Tanzania Bara, baada ya kuthibitisha kwamba aliacha kuishi Tanzania Bara kabla au baada ya mtoto kuzaliwa; au

▪️ Na mtu ambaye amri ya kuwa mzazi imetolewa na mahakama dhidi yake kulingana na kifungu cha 34 cha Sheria ya Mtoto.

T: MAHAKAMA ITATOA AMRI YA MATUNZO A MTOTO DHIDI YA BABA MZAZI IWAPO ITARIDHIKA KUWA:

👉 Kuna sababu za msingi za kuamini kwamba mtu anayesadikiwa kuwa ni baba wa mtoto ni baba wa mtoto kweli na kwamba maombi ya amri ya matunzo yamefanywa kwa nia njema na si kwa lengo lolote la kudhalilisha au kumrubuni ; na

👉 Mtu anayesadikiwa kuwa ni baba wa mtoto alishaombwa na mwombaji au mtu mwingine kwa niaba yake, kutoa matunzo ya mtoto na amekuwa akikataa kutoa mtunzo au amekuwa akitoa matunzo yasiyotosheleza.


U: MAMBO YAZINGATIWAYO NA MAHAKAMA WAKATI WA KUTOA AMRI YA MATUNZO YA MTOTO

(a) Kipato na utajiri wa wazazi wote wa mtoto na wa mtu ambaye anawajibika kumtunza mtoto kisheria;

(b) Upungufu wowote wa uwezo wa kutafuta kipato wa mtu mwenye jukumu la kumtunza mtoto;

(c) Majukumu ya kifedha ya mtu anayehusika na matunzo kwa watoto wengine;


V: NI NAMNA GANI MAOMBI YANAFANYIKA?

Kuna fomu maalumu za kufanya maombi husika. Ni vizuri kutumia huduma ya wanasheria ili kuandaliwa fomu zilizokamilika.


W: JE, NI MAHAKAMA GANI MAOMBI HAYA YANAPELEKWA KUSIKILIZWA?


Ni katika Mahakama maalumu za watoto (Juvenile Court) ambapo maombi husikilizwa kwenye mahakama isiyo ya wazi (in camera, not in open court)

Juvenile Court Inaweza kuwa mahakama ya wilaya au mahakama ya mwanzo lakini wakati wa kusikiliza kesi itakuwa ni mahakama maalumu ya watoto, haitaruhusu watu wasiouhusika kuingia kusikiliza maombi hayo.

▪️Mahakama hiyo inatakiwa iwepo eneo ambalo wazazi wote wanaishi; AU

👉 Mahakama iwe eneo ambalo mjibu maombi (mshtakiwa) anaishi.


MUHIMU:

📌 Maombi yote yahusuyo watoto ni muhimu na nyeti sana, wakati mwingine ni lazima yahusishe maafisa ustawi wa jamii. Maafisa Ustawi ndio wanaofanya maombi kwa niaba ya Serikali na pia ndio wanaotoa mahakamani taarifa ya uchunguzi juu ya maisha ya mtoto, watu anaoishi nao na mazingira anayoishi ili kuisaidia mahakama kufikia uamuzi.

Maafisa ustawi wa jamii wanapatikana katika ofisi za Kata na Makao Makuu ya Halmashauri au Manispaa.

Wakati mwingine watu huchanganya kati ya maafisa ustawi wa jamii na maofisa wa polisi waliopo katika dawati maalumu la Jinsia na watoto.


Ahsanteni.​
 
Hapa ndo pabaya sana....... Tena ukiwa na tusenti wadada wanapigia vizinga humohumo kwenye child support...... Samtaimu bora kuoa, utasikia mtoto anaumwa jino kung'oa laki 5😐😐, sijawahi kukutana na Msela anaetoa child support bila kulialia
Ni kweli mkuu, wanawake wengi wanatumia ujinga wa wanaume zao kuwanyoosha kupitia Child support. Wanaume wengi hawajui wachomokaje kuhusu hilo. Naamini wengi watajifunza kitu kupitia somo hili, hawatapigwa tena!
 
Nimejifunza mengi

Swali je gharama gani utatakiwa lipa kama matunzo ya mtoto?

Sent from my M2006C3LG using JamiiForums mobile app
Ahsante kwa kujifunza mkuu. Kuhusu gharama, ukisoma hapo kwenye aya U nimeeleza mambo yazingatiwayo na mahakama kutoa matunzo ya mtoto.

Hakuna Gharama uniform, itategemea kati ya mtu na mtu kulingana na mazingira ya kifedha na utetezi atakaoutoa mahakamani wa majukumu ya kifedha aliyonayo. Kipato kikiwa kikubwa basi uwezekano wa kutoa kiwango kikubwa ni mkubwa pia, mtoto anaishi maisha ya hadhi sawa na ya mzazi wake.
 
Damu nzito kuliko maji, Vijana tubadilike maana tunapenda ngono zembe kavu kavu lakini kutekeleza majukumu tunakwepa, wanaoathirika ni Watoto wetu wenyewe wasio na hatia zozote kimaisha.
 
Back
Top Bottom