Nyuma yako - Riwaya ya SteveMollel

*NYUMA YAKO – 24*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA
Nikatembea kuvuka barabara. Ila hamaki, gari likaja kwa upesi mno likilenga kunizoa! Nikalikwepa upesi ila likanisukumia kando kwanguvu mno! Sijajikusanya, risasi zikatupwa kwa fujo kunifuata! Moja ikajeruhi paja langu la kushoto!
Nikajitahidi kunyanyuka, nikipuuzia maumivu, nikakimbia kidogo, ila napo kabla sijafika popote, nikadungwa risasi ya mgongo. Nikapoteza nguvu na kuanguka.
ENDELEA
Sikufahamu nini kiliendelea baada ya hapo, wala sikujua nilikuwa siko fahamuni kwa muda gani, nilikuja kuamka nikiwa eneo la giza! Sikuwa naona mbele wala nyuma yangu, kushoto wala kulia!
Nikiwa nahema kwanguvu, nikakodoa lakini haikusaidia. Nilikuwa nimefungiwa kitini nisiweze kunyanyuka wala kujitetea. Na kiti chenyewe kilikuwa kimesimikwa chini kiasi cha kutoweza kukinyanyua!
Nikajaribu kukumbuka nini kilitokea mara ya mwisho, sikuambulia kitu bali maumivu ya kichwa. Sikuwa nakumbuka jambo lolote. Kitu pekee nilichoambulia ni kuhisi maumivu kwenye paja langu la kushoto. Nilikuwa na jeraha hapo, nilihisi hilo, lakini sikuweza kugusa sababu ya mikono yangu kufungwa. Na pia, nilikuwa nahisi maumivu mgongoni.
Mengine hayo sikuwa naweza ku … mara mlango ukafunguliwa na kusababisha mwanga mkali kuzama ndani na kunichapa usoni. Haraka nikafunga macho yangu na kuyaminya kwanguvu kujitetea na mwanga ule mkali hivyo sikupata kumwona aliyeingia. Lakini nikajua muda ule ulikuwa ni mchana.
Mlango ulipofungwa, taa zikawashwa kufukuza kiza kile ndani. Hapo ndipo nikamwona mtu yule aliyekuja kunisabahi. Alikuwa mwanaume mrefu mwenye mwili mpana. Alivalia suruali ya jeans, koti la ngozi jeusi, na tisheti ya bluu kwa ndani ikiwa imeandikwa maneno ya njano – “GO **** YOURSELF!”
Mwanaume huyo akasonga karibu yangu akivuta kiti alichokitwaa konani. Akakigeuza kiti hicho na kuketi akin’tazama. Alikuwa ni mwanaume mwenye miba ya ndevu mashavuni na kidevuni. Nyusi zake pana na lips zake nyembamba, kidogo zikiwa zimemezwa na hii miba ya ndevu.
Hapa kabla mwanaume huyo hajasema jambo, nikafahamu kinachoenda kutokea. Mazingira haya hayakuwa mageni kwangu. Nimeshapitia mazingira kama haya maishani mwangu, kama si mara nne basi tano. Angalau nikaanza kuvuta kumbukumbu. Na kumbukumbu zangu hizo zikanambia kuwa mazingira hayo huwa hatarishi.
Huwa yanaambatana na maumivu ya mateso kumlazimisha mtu kuongea kitu ambacho aidha anakijua ama hakijui. Anachohusika nacho ama lah! Lakini sasa mimi nitaeleza nini na kumbukumbu zangu bado hazikuwa zimenijia kichwani?
Si hicho kilichokuwa kinanipa hofu, bali pia hali ile nlokuwamo ilikuwa ni tishio kwa usalama wangu kwani naweza jikuta nikitoa taarifa ambazo hazitakiwi kutolewa kwa adui!
Unajua kabla ya kutumia ujuzi wa kudanganya na kulaghai lazima kwanza uwe unaujua ukweli ili ufahamu namna gani ya kuumba katika njia nyingine ya tofauti ambayo inafanana nayo. Sasa mimi sikuwa naujua huo ukweli. Nilitaraji bwana huyu angenitesa sana kuutoa mwilini mwangu, lakini angeambulia damu tu.
Ila … mawazo haya yalikuwa kinyume. Bwana yule baada ya kunitazama, akaniuliza, “Unanikumbuka?”
Nikatikisa kichwa, “Hapana.” Akatabasamu kisha akapitisha ulimi wake kusafisha meno. Ungepata kuuona ulimi huo kwenye lips zake ukiwa unatembea.
Akaniuliza tena, “Unakumbuka mara yako ya mwisho ulikuwa wapi?”
“Hapana,” nikamjibu.
“Nini unakumbuka?” akaniuliza.
“Mazingira haya,” nikamjibu. “Nadhani sio mageni.”
“Yapi?”
“Haya ya kufungwa kamba kitini, na mtu kukaa mbele yangu.”
Akan’tazama kidogo alafu akanyanyuka aende zake. Nikamwita, “Tafadhali niambie hapa nipo wapi na nafanya nini?”
Akan’tazama asiseme kitu alafu akaenda zake. Akaufungua ule mlango na kupotea ila saa hii akiwa ameacha taa zinawaka. Nikaangaza huku na huko ndani ya mahali nilipo. Hakukuwa na kitu isipokuwa meza na kiti upande wangu wa kulia, tena kwa mbali.
Chumba kilikuwa cheusi na kisicho na dirisha. Ila kulikuwa na na viyoyozi ambavyo vilikuwa vinamwaga kipupwe cha baridi. Nikajiuliza hapa ni wapi? Kabla sijapata majibu, tena hata sijachukua sekunde tano, mlango ukafunguliwa akaingia mwanaume mwenye kimo cha kati akiwa anaongozana na mijibaba miwili kwa nyuma.
Mwanaume huyo alikuwa na mustachi mweupe kama nywele zake za kichwani. Amevalia miwani ya jua na mkononi mwake ameshikilia sigara kubwa. Suruali nyeusi na buti kubwa huko chini.
Akasimama karibu yangu, kiti na ile meza vikasogezwa karibu naye. Hapa ndiyo nikajua kumbe vitu vile vilikuwa vimetengwa kwa ajili yake. Lakini mbona hakuja yeye mwanzoni na badala yake akaja yule mwanaume mwingine?
Akili yangu ikaniaminisha kuwa bwana yule alikuwa ametumwa aje kun’tazama kwanza kama najua jambo lolote, kama nakumbuka kitu, na alipoona hilo limefaulu ndipo akaja huyu.
Kwahiyo hawa ndiyo watakuwa wanahusika na kupotea kwangu kwa kumbukunbu, nikaamini hilo. Nikamtazama bwana yule, naye akintazama akaketi. Akanyonya sigara yake kubwa alafu akantemea moshi pasipo adabu!
Akaita, “Kijana!” nami nikamtazama pasipo kumsemesha.
“Najua haukumbuki jambo, nami nipo hapa kukupatia machaguzi mawili ambayo ni juu yako kuchagua.” Aliposema hayo akavuta tena sigara, na tena pasipo adabu, akanipulizia usoni mwangu. Nilimtazama kwa hasira sana na kama ningekuwa na uwezo ningemdaka na kumfunda nidhamu!
“Moja, ufanye kazi na sisi ukapate nyumba ya kukaa, ama mbili, tukuache ukarande mtaani ukiwindwa kama swala!”
Nikashangazwa na hiyo kauli. Kwani wanadhani sina pa kwenda? Nikajiuliza. Wanadhani mimi ni mzururaji au? Wanadhani sina makazi wala kazi ya kufanya?
Nikawauliza, “ninyi ni wakina nani na kwanini mmenikamata?”
Bwana yule akaniambia, “Sipo hapa kwa ajili ya kuulizwa maswali na wewe. Nipo hapa kukupatia nafasi ya pili, kama uko tayari, sema, na pia kama haupo tayari.”
“Nitakubalije kitu nisichokifahamu?” nikawauliza. Yule bwana hakujali swali langu, akanyanyuka na kwenda zake kuufuata mlango. Nikapaza sauti, “Ngoja!” akasimama pasipo kunitazama akiendelea kuvuta sigara yake.
“Nimekubali,” nikamjibu. “Nimekubali kufanya kazi nanyi!” basi bwana huyo akarejea pale kitini kisha akazamisha mkono wake ndani ya mfuko wa koti na kutoa kikopo kidogo chenye tembe nyeupe, akasema, “Unaona hiki?” akitikisa hiko kikopo. “Ni dawa ya kurejesha kumbukumbu zako, na ukifanya kazi yetu kwa takribani juma moja tu, kazi moja tu, utapewa tembe hizi ukaendelee na maisha yako na pesa nyingi mkononi.”
Aliposema hayo akavua miwani yake, hapo ndipo N jicho moja lililobovu, la kulia, na pia tattoo ya chozi jicho la kushoto.
“Deal?” akaniuliza.
Mimi nikamjibu kwa kumtikisia kichwa.

**

Leo nilikuwa najua ni siku gani na muda gani tofauti na ile jana yake. Nilipewa chai nzuri na muda wa kupumzika kwenye chumba ambacho ni ‘luxury’ chenye kila kitu akitakacho binadamu. Na pia jeraha langu lilipewa dawa na kufungwa bandeji.
Sasa ningeweza kutembea, na nadhani hata kukimbia, kwani nilihisi maumivu kwa mbali, na nilitambua kuwa jeraha hilo halikuwa lililonichimba sana. Kama ndani ya majuma mawili ama matatu laweza likawa limepona kabisa.
Nikiwa hapa sebuleni, baada ya kunywa chai, nikaendelea kuwazia kitu ambacho bado sikuwa nakipatia majibu. Hapa nipo wapi? Hawa watu ni wakina nani? Wanataka nini kwangu?
Na kubwa zaidi MIMI NI NANI?
Nikaja tu kuamini kuwa kujiuliza maswali hayo ni kupoteza muda tu maana nisingepata majibu abadani. Inabidi nipate zile tembe. Tembe za kumbukumbu. Lakini sasa nita ….
Ngo! Ngo! Ngo! Sijajibu, mlango ukafunguliwa, akaingia yule mwanaume aliyekuja kunipa chaguzi jana yake kwenye kile chumba. Kama kawaida alikuwa anaongozana na wanaume wawili waliojaza misuli, akaketi kwenye kochi litazamanalo na langu kisha akaniuliza, “Unaendeleaje?”
“Naendelea vizuri,” nikamjibu pasipo kutia neno lingine.
“Sasa upo tayari kwa kazi yetu?” akaniuliza.
“Kazi gani hiyo?” nami nikamuuliza. Akan’tazama kwanza kabla hajavua miwani yake.

***
Nyuma ni nyuma eenh.
 
*NYUMA YAKO – 25*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA
“Naendelea vizuri,” nikamjibu pasipo kutia neno lingine.
“Sasa upo tayari kwa kazi yetu?” akaniuliza.
“Kazi gani hiyo?” nami nikamuuliza. Akan’tazama kwanza kabla hajavua miwani yake.
ENDELEA
“Kumuua balozi!” akaniambia kwa sauti kavu. Nikatoa macho, “balozi gani?”
“Balozi wa Marekani!” akanijibu kana kwamba ni kazi ya kumuua kuku kisha akanipatia na muda, “ndani ya siku tatu kazi hiyo inabidi iwe imeshakwisha kufanyika.”
Mimi nikatikisa kichwa. “sitaweza.”
“Unasema?”
“Sitaweza!” nikarudia kauli yangu. Basi bwana yule akazamisha mkono wake ndani ya koti na kutoa kile kijichupa cha tembe na kunambia, “Ni uchaguzi wako, kufanya kazi yetu ama kwenda ukawe mbwa huko mtaani!”
“Ni sawa!” nikawajibu kwa kiburi. “Niachieni huru ila siwezi kwenda kumuua mtu ambaye sijui sababu yake ya kifo!”
Basi bwana yule akan’tazama kwa kukunja ndita alafu akawatazama wale wenzake wawili. Akanyanyuka akitaka kwenda zake.
“Niambie mimi ni nani!” nikamwomba.
Akanitazama pasipo kunisemesha kitu, akaondoka akiniacha na wale wanaume wawili waliojaza miili. Wanaume hao wakanisomba na kwenda kunitupia nje ya nyumba, huko barabarani, alafu kabla hawajaondoka mmoja wao akanambia, “akili itakapokukaa kichwani, unajua pa kurudi!”
Sikumjali nikaenda zangu.
Nikatembea ndani ya jiji la Berlin likiwa jipya kabisa machoni mwangu, sijui wapi pa kwenda wala pa kuelekea. Nikazunguka kwa kama masaa matatu kabla sijajikuta ufukweni nikiwa nimechoka.
Sikuwa nakumbuka kitu! Nilidhani nitakumbuka lolote kwa kutazama watu na majengo lakini haikuwa kama nilivyowaza. Sikukumbuka hata tone ya jambo. Nikawaza niende hospitali na kuwaelezea shida yangu pengine watanisaidia lakini mfukoni sikuwa na pesa. Ni vipi watanielewa?
Hapo ndipo nikakumbuka hata pesa ya chakula sikuwa nayo. Na nilipokumbuka hayo tu, nalo tumbo likanguruma! Nikaona nifanye stara kutafuta kazi yoyote ile ambayo itanipatia hata vijisenti kabla jua halijazama na kiza kutawala.
Nikatafuta kwa kupita huku na huko, ila sikufanikiwa kupata kitu, kila nilipoenda hata kuomba kusafisha vyombo, waliniambia hawahitaji watu. Mpaka giza linaingia, sijapata kitu. Tumbo likawa linadai haswa.
Sikuwa na namna bali kulala vivyo hivyo huko ufukweni. Nilitafuta mahali ambapo pangenikinga kidogo na upepo mkali wa bahari, kakibanda, nikajiegesha hapo nikijikunyata.
Nikawaza sana sana pasipo mafanikio. Mwishowe usingizi ukanibeba, ila ukiwa ni wa kukatakata. Nadhani sababu ya njaa na kuhisi sipo eneo salama.
Ukiwa ni usiku mzito, kama majira ya saa saba hivi, nikiwa nimefumba macho yangu, nikasikia sauti ya mwanamke ikipiga kelele. Nikashtuka na kuketi kitako upesi. Nikatazama kushoto na kulia, sikuona kitu!
Sauti hiyo ikaendelea kulia na kunifanya ninyanyuke kuangaza maana ilikuwa inaomba msaada. Niliposkiza vizuri nikatambua inatokea upande wangu wa mashariki, upesi nikakimbilia huko, kidogo nikawaona wanaume wawili, mmoja alibebelea rungu la baseball na mwingine ana kisu wakiwa wanamkimbiza mwanamke fulani mnene.
Kidogo wakamkamata mwanamke huyo na kumtupia chini! Mmoja akampokonya mkoba wake kwanguvu na kumwamuru anyamaze kimya.
Hapo ndipo nikaona kuna haja ya kwenda kumsaidia mwanamke yule. Nikasonga pasipo kujiuliza mara mbilimbili mpaka karibia na eneo ambalo wapo. Nikapaza sauti, “Hey! Mwachieni mwanamke huyo huru!” nilikuwa natumia lugha ya kijerumani. Hicho sikuwa nimekisahau. Basi wanaume wale wakanitazama na kushtuana kwa mmoja kumgusa mwengine bega kisha wakajiandaa kwa kukamatia silaha zao.
Mmoja, yule mwenye kisu, akanifuata kwa pupa. Akatupa mkono wake wenye kisu, nikaukamata na kuuvunja alafu nikamviringita na kumpatia teke kali la tumbo, akarukia huko!
Mweziwe kuona hivyo basi naye kurupu akanifuata na rungu lake, naye nikamkabili kwa wepesi kabla sijampokonya rungu lake na kumwadhibu nalo kwanguvu mara tatu, akabaki hapo chini akilalamia maumivu. Kwanguvu nikampokonya mkoba wa yule mwanamke na kumfuata mhanga kumjulia hali.
Mwanamke huyo kanambia yupo sawa, ni maumivu kidogo ya mgongo ndiyo alikuwa nayo. Nikampatia mkoba wake na kumtakia usiku mwema lakini kabla sijaenda akanishukuru sana na akaniuliza,
“Mtu mwema kama wewe wafanya nini usiku huu hapa?”
Nikatabasamu kidogo kabla sijamwambia jibu ambalo kwa namna moja lilimshangaza, “Sina makazi.”
Akan’tazama kwa huruma.
“Kweli?”
“Ndio, nalikuwa nimelala kule ufukweni kabla ya kusikia sauti yako ikiomba msaada.”
Akan’kagua upesi kabla hajatabasamu usoni mwangu.

**

“Hapa ni kwangu!” alisema akinifungulia mlango. Ilikuwa ni nyumba ya ukubwa wa wastani ikiwa imefumbwa na uzio mwepesi wa nondo zilizojenga mistari. Tokea eneo lile ambapo tukio la kukabwa lilitokea mpaka hapa ni kama umbali wa nusu maili.
“Karibu sana, jisikie huru!” akanambia akionyesha meno yake madogo.
“Ahsante!”
Nikaketi kochini na kuangaza kidogo sebule yake ndogo iliyopambwa vema. Nikamuuliza, “Waishi mwenyewe hapa?”
“Hapana, nipo na wanangu. Watakuwa wameshalala.”
Akaketi na kuvua viatu vyake. Akanishukuru tena na kisha akanambia, “kama isingalikuwa gari langu kuharibikia huko mbali nisingekuwepo pale kwa miguu. Lakini Mungu wa ajabu, alimtuma malaika wake kuniokoa.”
Nikatabasamu nisiseme kitu. Akan’tazama na kuniuliza, “Imekuaje hauna makazi?”
“Hata nikikueleza sijui kama utaamini,” nikasema kabla sijatazama chini. Akan’toa hofu,
“Usijali, ntakusikiliza.”
“Sijui kwanini sina makazi,” nikamjibu. “Sijui kwanini nipo kwenye hali hii. Sikumbuki kitu chochote!” nikamweleza kisha kukawa kimya kidogo.
“Nashukuru maana unenisaidia,” nikamweleza nikimtazama. “Sikuwa na pa kulala. Naomba unisaidie kwa kipindi kifupi, natumai kumbukumbu zangu zitarejea na kila kitu kitakuwa sawa.”
“Usijali,” akaniambia akinitikisia kichwa. “Utapumzika hapa na tutaangalia cha kufanya.”
Basi hatukukaa hapo sana maana ulikuwa ni usiku mkubwa na alitaka kupumzika. Akaniacha mimi pale sebuleni yeye akienda chumbani. Nikalala hapo mpaka asubuhi ambapo niliamshwa na makelele ya watoto.
Nilipofumbua macho nikamwona mtoto wa kiume na wa kike. Walikuwa wa makamo sawa, kama miaka mitano hivi. Walinitazama kwa mashaka kabla hawajaendelea na mbio zao kuelekea nje.
Kidogo akaja msichana wa miaka kumi na, akanisalimu na kisha akaenda zake. Alikuwa amevalia begi mgongoni. Nadhani alikuwa anaenda shule ama chuo. Naye alinitazama kwa maulizo kabla hajapotelea zake.
Nilipokaa hapo kwa muda kidogo, ikiwa ni majira ya saa tatu asubuhi kwa mujibu wa saa ya ukutani, mwanamke yule mwenye nyumba akanijia. Alikuwa ana tabasamu usoni mwake japo machoni bado usingizi ulikuwa umemjalia.
“Umemkaje?”
“Salama. Vipi wewe?”
“Salama tu. Ule pale ni mlango wa bafuni na choo. Waweza kwenda kuoga kisha upate kifungua kinywa.”
“Ahsante.”
Nikafuata maelekezo yake kwenda huko. Nikiwa bafuni nakoga, kama baada ya dakika tano tu, nikasikia mlango wa bafu ukigongwa kwa nguvu. Sijaitikia, yule mwanamke akafungua na kunisihi kwa sauti ya woga. “Usitoke humu ndani ya bafu. Tafadhali!”
Hakuwa ananitazama, bali akirushia macho yake pembeni asinione uchi. Kabla sijamuuliza chochote, akawa ameshatoka na kuufunga mlango akiniacha na maswali.
Sikuendelea kuoga tena.
 
*NYUMA YAKO -- 26*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA
Nikafuata maelekezo yake kwenda huko. Nikiwa bafuni nakoga, kama baada ya dakika tano tu, nikasikia mlango wa bafu ukigongwa kwa nguvu. Sijaitikia, yule mwanamke akafungua na kunisihi kwa sauti ya woga. “Usitoke humu ndani ya bafu. Tafadhali!”
Hakuwa ananitazama, bali akirushia macho yake pembeni asinione uchi. Kabla sijamuuliza chochote, akawa ameshatoka na kuufunga mlango akiniacha na maswali.
Sikuendelea kuoga tena.
ENDELEA
Nilitega masikio yangu nipate kusikia kinachojiri. Nilisonga karibu na mlango nikiwa nimejiveka taulo kwa dharura ya lolote litakalotokea basi lisinikute uchi. Niliposkiza kwa ufupi nikajua kuna magombano, watu wawili walikuwa wanazoza kwa kutumia lugha ya kijerumani, mmoja mwanaume ambaye sikumtambua kwa sauti yake na mwingine mwanamke ambaye ni wazi alikuwa ni yule mwanamke mwenyeji wangu.
Kama haitoshi magombezano hayo yaliambatana na kuvunjwa kwa vitu kadhaa.
“Yuko wapi?” Mwanaume alifoka. “Nasema yuko wapi? Sema kabla sijakuua!” Baada ya hapo nikasikia sauti ya kofi na yowe toka kwa mwanamke. Kidogo nikasikia sauti ya kishindo cha mtu na mara mlango wa bafuni nilimo ukafunguliwa kwanguvu! Uso kwa uso nikakutana na mwanaume mpana mrefu aliyekuwa amefura haswa.
Alinikodolea na kusema akininyooshea kidole, “Umekwisha!” Akazama ndani ya bafu na kujaribu kunishambulia. Nilimsihi aniskize lakini hakuwa tayari, alidhamiria kuniumiza ama tuseme kuniua kabisa, hivyo ikanipasa nitetee uhai wangu.
Sikuhangaika naye sana, alikuwa ni mtu mwenye ‘maguvu’ mengi na mzito. Nilifanikiwa kumkabili kwa mapigo matatu akawa yu chini hoi. Nikatoka bafuni na kwenda kukutana na yule mwanamke mwenyeji wangu, yeye alikuwa amelala chini akiwa analia.
Nikamnyanyua na kumtazama, uso wake ulikuwa unavuja damu, alikuwa amjeruhiwa vibaya. Nikamsihi nimpeleke hospitali lakini hakuwa tayari kabisa badala yake akawa ananishauri niondoke upesi kwa usalama wangu.
“Nenda, nitakuwa salama usijali!” Aliniambia akinisukuma, lakini ningemwachaje vile? Nilimwomba aende hospitali basi hata pale nitakapoondoka, bado akaendelea kunisisitiza niende na saa hii akinipa vitisho, “atakumaliza yule! Si mtu mzuri kabisa!”
Akiwa analia akanambia kuwa watoto wake walikutana na baba yao huyo na kumwambia kuwa yupo na mwanaume nyumbani. Alikiri mume wake ni mhalifu na mkatili, ni mtu ambaye hafikirii mara mbilimbili kummaliza mtu.
“Nisingependa nikuweke matatizoni, tafadhali nenda.” kauli yake hiyo ilinisababishia maumivu makali kwani niliona mimi ndiye nilimsababishia matatizo. Nilitamani sana kumsaidia, roho yangu haikuwa radhi kabisa kumwacha hapo. Lakini kwasababu ya shinikizo lake nikaona nitimize agizo lake. Nikanyanyuka na kujongea mlango, nikajiendea.
Nilipiga hatua kumi na mbili, kama nipo sahihi, mbali na eneo lile. Ghafla nikasikia makelele ya mwanamke toka kwenye nyumba ile, hapo nikasita nikisimama na kuwekeza jitihada kwenye masikio yangu. Alikuwa ni yule mwanamke anapigwa, halikuhitaji elimu kulibaini hilo. Sikuweza kuvumilia, basi nikarejea kumsaidia.
Nilifungua mlango kwa pupa na kuangaza. Nilichokiona ni yule mwanaume akiwa amemshika mwanamke yule nywele zake, mkono wake ukiwa unachuruza damu. Nikamwamuru, “Mwachie huyo mwanamke upesi!” nikamwamuru nikiwa namkodolea haswa. Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanaenda mbio kwa hasira. Nilimwona mwanaume huyu ni mnyama kabisa.
Kwa kiburi, akaniambia, “Utanifanya nini nisipomwacha?” kabla sijajibu nilimwona mwanamke yule akipambana kunusuru nywele zake. Alikuwa anahisi maumivu, ungeliona hilo kwa namna alivyokuwa amekunja sura yake akiugulia na kugugumia.
“Usipomwacha nitakuadhibu kwa kipigo ambacho hujawahi pewa tangu uzaliwe!” nikamwambia nikimnyooshea kidole. Basi akamtupia kando yule mwanamke na kunifuata. Laiti angelijua niliyokuwa nimempangia kichwani mwangu basi asingediriki kupiga hata hatua moja karibu yangu. Niling’ata meno na kukunja ngumi, nikamwona akichomoa kisu nyuma ya mgongo wake.
“Nitakuua na kukufukia nyuma ya bustani. Na hamna mtu atakayekuja kuniuliza chochote!” alibwatuka, nami nisiseme kitu bali nikimngoja nimfundishe adabu.
Alipokaribia, naam, nikampa kitu roho inapenda. Nilimsubiri arushe kisu chake, nikaudaka huo mkono na kuutegua uache silaha kisha nikamvuta na kumwadhibu kwa kumtwanga ngumi nzito chini ya kidevu chake. Akiwa anapepesuka, nikamzika na teke zito lililonyanyua mwili wake mzito kwa kiasi chake na kisha kumbwagia chini. Alikuwa hoi asiyejiweza.
“Twende!” nikamwambia mwanamke yule nikimsogelea. Nikamnyanyua na kutoka naye ndani kwenda nje. Moja kwa moja nikamwongoza mpaka hospitali ambapo aliingia ndani kupata huduma mara moja. Uzuri alikuwa na kadi yake ya afya akiambatana nayo. Kumbe wakati mwanaume huyo anamdaka alikuwa yu njiani kujiondokea zake.
“Sasa kwanini haukutaka kwenda na mimi?” nikamuuliza. Alikuwa tayari amehudumiwa, kwa kiasi uso wake umefunikwa na bandeji.
“Nimeshakuambia, sitaki kukuingiza kwenye matatizo,” akaniambia akiwa ananitia huruma haswa. Nilikuwa naona hastahili yale anayopitia. Kila alipokuwa anateta neno moyo wangu ukawa unapiga kwa kunigusa.
“Matatizo yapi?” nikamuuliza. “Mume wako naweza kummudu, hawezi kunipa shida kabisa.”
Akan’tazama. Jicho lake la kushoto lilikuwa limefunikwa kiasi na bandeji.
“Unaweza kupambana naye lakini vipi kuhusu kundi lake? Hayupo mwenyewe!” aliposema hayo akapangusa pua yake kwa mgongo wa kiganja kisha akasema kwa sauti inayotikiswa na kilio.
“Watakusaka na kukuua kisha wakakutupie baharini. Nami sitaishi kwa amani tangu leo.”
Nikampa moyo, hatokumbwa na lolote mimi nikiwa hai. Ila kitu kilichokuwa kinanifikirisha ni namna gani atarudi kule kwake kwa yule mwanaume katili.
“Inabidi utafute mahali pengine pa kukaa, sawa?” nikamshauri. “Kuhusu watoto wako nadhani wataelewa maamuzi yako.” alipofuta makamasi mepesi yalokuwa yanamchuruza, akasema akiwa anatazama chini, “Wale si watoto wangu bali wa mume wangu.”
Hapa nikaona basi ni rahisi kwake yeye kuwa salama, lakini pia nikapata picha kwanini watoto wale waliweza kwenda kumpandikiza maneno baba yao huko walipokutana naye.
“Kwanini usiwe mwenyewe? Kwanini unaishi na mwanaume katili kama yule?”
Hapo ndipo nikajifunza kuwa mwanamke huyo hayupo kimapenzi na yule jamaa, bali kwa hofu. Yapata miaka mitatu iliyopita ndipo mahusiano yao yalianzia baada ya mwanaume huyo kumpoteza mke wake kwenye mazingira ya kutatanisha. Kwa muda wote huo alikuwa akiishi akijua mke wa mwanaume huyo alipata ajali, lakini siku moja alikuja kuubaini ukweli baada ya mwanaume huyo kumwadhibu na kumtamkia kuwa akiendelea kuwa mkaidi basi atammaliza kama alivyofanya kwa mkewe na kisha akamtupia baharini!
“Nisingeweza kumtoroka, mtandao wake ni mkubwa hapa Berlin. Ningejifichia wapi?” alimalizia kwa kauli hiyo akiwa anadondosha machozi.
Tuliondoka hapo hospitali tukaenda mahali pa kupumzikia alipopalipia kwa kutumia pesa yake mwenyewe. Huko tukakaa kwa siku mbili kwa amani kabisa, yeye akiwa kwenye chumba chake na mimi changu. Nilijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kumjali lakini bado nikajiona napwaya. Nilihisi nahitaji kufanya kazi niingize kipato. Nisingeweza kumtegemea mwanamke huyo siku zote hizo.
Usiku wa siku ya tatu, pasipo kuaga, nikatoka na kwenda kwenye moja ya klabu ya usiku. Huko nikajitahidi kukutana na wafanyakazi wa klabu hiyo na kujinasibu nahitaji kazi ya kulinda eneo hilo.
“Wewe?” aliuliza mmojawao, jamaa mwenye mwili mpana na uso mwekundu. Sikio lake la kulia alikuwa amelitoboatoboa na hereni kadhaa. Mdomo wake mdogo ulikuwa umefichwa na ndevu nyingi mithili ya beberu asiye na matunzo.
“Ndio, mimi!” nikamjibu nikimtazama usoni pasi na kupepesa mboni. Basi akanitazama kwa sekunde kadhaa kisha akanipa ishara ya kichwa kuelekea upande wake wa kulia. Nikaongozana naye na punde nikajikuta ndani ya ofisi ndogo alimokuwa amekaa jamaa mwembamba ndani ya suti. Jamaa huyo hakuwa anaonekana vema kutokana na kuchezacheza kwa mwanga. Alikuwa anavuta sigara kubwa na amezungukwa na wanawake takribani saba ambao vifua vyao vilikuwa wazi.
“Vipi?” akamuuliza yule mwanaume aliyenileta, yule jamaa akajieleza kunihusu na kisha akakaa kando akiwa amefumbata mikono yake.
“Sogea karibu kijana!” yule jamaa akaniamuru. Niliposonga karibu zaidi ndipo nikamgundua bwana huyo, si kwa jina, lah! Bali umri wake. Alikuwa makamo sawa na mimi. Haikunishangaza kwa namna anavyoheshimika, alikuwa ni ‘mkuu’. Nadhani ndivyo ilivyo popote pale.
“Kipi kinachokufanya udhani unaweza kazi hii?” akaniuliza akinitazama. Niliona macho yake mara kadhaa mwanga ulipopita na kujiendea.
“Kwasababu naweza kupambana,” nikamjibu. Hiko ndicho kitu pekee ambacho nalikuwa na uhakika nacho kuwa naweza. Uzuri nilijithibitishia hilo mara mbili ama tatu hapo nyuma baada ya kupoteza kumbukumbu zangu zote.
Lakini bwana yule alionyesha wazi hakuniamini. Alimtazama jamaa yule aliyenileta na kisha akampa ishara ya kichwa, nikashangaa bwana huyo ananifuata.

**
 
It's been a while hatujaonana wakuu. Najua 'tumemissiana' sana au sio wandugu? Haya sasa nimerudi tena na Riwaya ya NYUMA YAKO yenye mahadhu ya Kijasusi na kiitelijensia kama tulivyofanya kwenye riwaya kadhaa zilizopita.

Riwaya hii mpaka sasa inakaribia ukingoni hivyo kwa mtu atakeyihitaji basi asisite kunijuza kwa namba 0685 758 123 - whatsapp.
Habari,hii story naweza kuipata yote nikikutumia hiyo 2,000/=?
 
Nitakutumia kesho maana nahitaji kuisoma yote kwakuwa kuanzia keshokutwa nitakuwa safarini kwenda dsm itanifariji sana
Story hii ipo mpaka mwisho. Kama waihitaji tuma 2000 tu kwenda 0685 758 123 kwa story nzima
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom