Unapenda movies? Pitia hapa kidogo

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
5,793
2,000
Kutokana na mlipuko na kusambaa kwa homa kali ya mapafu – Corona (COVID -19) ni muda sasa wa kupunguza rapsha za hapa na pale tujitulize nyumbani muda wote ama muda mwingi zaidi. Ni kweli ni kadhia kubwa, huchosha sana, lakini hatuna budi kwa ajili ya usalama wetu binafsi na familia zetu.

Basi katika muda huo wa kujiweka zaidi nyumbani, tunaweza kuchangamsha siku zetu kwa kutazama baadhi ya Movies ambazo kwa namna moja ama nyingine zitakusisimua, kukufurahisha na kukufikirisha. Movies hizi kwa uhondo wake maridhawa zitakufanya uone masaa yanatiririka na kuyoyoma kwa kasi sana huku zikikuacha aidha na mafumbo, furaha, makisio na hata mishangao muda mwingine.

Kwa upande wangu, binafsi, mimi ni mpenzi sana wa Horror Movies japo si kwamba sitazami aina zingine, lah! Napenda sana movies ambazo hufikirisha lakini pia zenye stories kali na za kipekee. Hizi ni baadhi ya nilizozitazama, na pengine naweza kukushawishi nawe ukazitazama kwa muda wako:

NB: Huwa siamini sana rates za IMDb, Rotten Tomatoes, Metacritic na platform zingine juu ya movies maana mara nyingi tu washawahi niingiza chaka kwa kutoa marks za juu kwenye movies ambazo binafsi niliziona za hovyo, na wakizipa marks ndogo zile ambazo kwa namna fulani zilinikonga. Naamini macho na akili yangu tu.


EXAM (Mtihani)Filamu ya mwaka 2009.

Tangu nimetazama filamu hii, bado haijatoka kichwani mwangu kama kovu la ajali kubwa katika mwili wa binadamu. Kweli niliwaza sana juu ya kile alichokifikiria mtunzi (story writer) kwenye kuandika kitu kama hichi ambacho ‘setting’ yake ni chumba kimoja tu kwa masaa yote ya filamu lakini bado unaitazama mpaka unasahau kumeza mate.

Vipi ushawahi kwenda kwenye usahili wa kupata kazi fulani muhimu sana kwako? Yani unaihitaji kinomanoma kiasi kwamba unajiandaa kwa kila njia uipate, kuanzia mavazi na tafiti za kutosha alafu matokeo yake unaenda kwenye usahili na kuona yale yote uliyoyafanya yalikuwa bure? Yani hukuti vitu relevant kabisa? Basi bora ya wewe kuliko mchezo wa akili waliofanyiwa ‘candidates’ hawa.

IPO HIVI: Watu takribani nane ambao wameshapita kwenye hatua za awali za usahili wa kupata kazi kwenye kampuni kubwa ya madawa wanakutanishwa kwa ajili ya zoezi la mwisho ili kumpata atakayefuzu kuwa C.E.O wa kampuni husika.

Wakiwa ndani ya chumba ambacho hata madirisha hakina, wanapatiwa makaratasi na kupewa maelekezo muhimu sana na msimamizi (invigilator) ya kwamba jaribio lililopo mezani mwao ndo’ litakaloamua nani atapewa mkataba wa kazi na ni nani atakayepewa nauli ya kurudi nyumbani. Swali ni moja tu, na jibu ni moja vilevile, na muda ni dakika themanini (80) maelekezo yakiwa haya: mosi, hawatakiwi kuwasiliana na msimamizi kwa namna yoyote ile, pili, hawaruhusiwi kuharibu/kuchafua makaratasi waliyopewa, na mwisho, hawaruhusiwi kutoka ndani ya chumba. Endapo yeyote angelifanya lolote kati ya hilo basi angekuwa ameshajitoa kwenye kinyang’anyiro mara moja.

Baada ya kusema hayo, msimamizi akauliza: KUNA SWALI LOLOTE? Kisha akaenda zake. Shida ikaja pale wahusika walipotupia macho kwenye makaratasi waliyopewa wasione swali lolote! Makaratasi ni meupe pe yakiwa yameandikwa namba tu! Si mbele wala nyuma ya karatasi. Hakuna neno.

Muda wa saa unayoyoma. Mtihani unageuka nyuma mbele, mbele nyuma, badala ya watu kutafuta majibu wakawa wanatafuta maswali! Je, nani atafuzu? Swali ni nini? Swali liko wapi?

Ni kijasho chembamba ndani ya chumba. Mambo yanakuwa tafrani haswa kila mtu akionyesha njaa yake ya kupata ajira hii adhimu. Akili yote hutumika mpaka yako wewe mtazamaji. Mwisho wa siku mmoja ndiye anang’amua swali ni nini … utajishangaa ukija tambua swali hilo waweza kujiona mjinga katafuta utazame.

Screenshot_20200403-004851.jpg

TRIANGLE ya 2009.

Moja ya kitu kikubwa sana ambacho nimejifunza katika hii filamu ni kwamba kwenye maisha haya hutakiwi kabisa kupuuza mambo unayoyaona ama kuyachukulia madogomadogo kwani muda mwingine hayo ndo’ hupelekea vikubwa vya kushangaza. Kila kitu ni muhimu. Muda mwingine tunapewa dondoo lakini tunapuuzia kwa kuziona ni ndogo zisizohitaji umakini wetu.

Hii ni aina ile ya filamu ambayo huwezi tazama mara moja, tena huku kutazama kwetu ukiwa unambembeleza mtoto ama una mboga jikoni, utaishia kuona maruweruwe tu na kuchukia filamu hii tamu kabisa kupata kutokea. Bali utakapoirudia kwa mara ya pili na ya tatu, utabaini mambo mapya ambayo hukuyaona hapo nyuma, mambo madogomadogo ambayo ndiyo hutengeneza na kuelezea makubwa ambayo inawezekana hukuyaelewa.

IPO HIVI: Mwanamke anayeitwa Jessie ni mama mwenye kulelea mtoto mdogo wa kiume mwenye matatizo ya akili, lakini Jessie anaonyeshwa ni mama mkali mwenye ufinyu wa kuonyesha mahaba kwa mtoto wake kama vile inavyotakiwa.

Basi ingali akiwa na mwanaye nyumbani anajikuta akikasirishwa sana na kitendo cha mtoto kuchafua mazingira. Akiwa anafanya usafi, anasikia hodi mlangoni lakini alipoenda kutazama hakumkuta mtu. Anapaki vitu pamoja na mtoto, lakini pia na mzigo Fulani ambao hatuuoni ni nini, kisha anaendesha zake gari na kutokomea.

Hatuonyeshwi nini kilitokea ila baadae tunamwona mwanamke huyu akiwa mpweke, hana mtoto, anashushwa na dereva taxi anayemuahidi amngoje kwani atarejea kisha anaungana na wenzake na kwenda safari baharini. Huko wanapata mushkeli na boti inazama kabla ya kuja kujiokoa na kujitunza kwenye meli kubwa na pweke iliyoandikwa AEOLUS ubavuni.

Kwa wakati wote huu Jess anahisi kuna kitu hakipo sawa. Anahisi kama vile anapajua mahali hapo lakini hakumbuki haswa. Zaidi ya hapo wanaanza kuwindwa na mtu ndani ya meli. Ajabu ni kwamba, mmoja wa watu waliokuwa pamoja na Jess anajeruhiwa vibaya mno na kuanza kumtuhumu Jess kuwa ndiye muuaji ambaye anawawinda ndani ya meli! Jess na wengine wanaduwazwa na kauli hii!

Lakini Jess anakuja kulibaini hilo ni kweli baada ya kukutana uso kwa uso na muuaji. Alikuwa ni yeye kabisa. Kila kitu kuanzia kidoleni mpaka mguuni. SI MCHEZO! Anamkabili mwanamke huyo na kumuua hivyo anabaki peke yake ndani ya meli, lakini baada ya muda kidogo anasikia sauti za watu wakiomba msaada. Anapoenda kutazama ni wakina nani, LA HAULA! Anawashuhudia wenzake tena pamoja na yeye wakiwa wamesimama juu ya boti iliyopinduka kwa kuzama majini, wanapunga mikono kuomba msaada! Vilevile kama alivyokuwa ameketi awali pamoja na wenzake (ambao sasa hivi wameshakufa) wakiipungia mkono meli ile AEOLUS! ni kisanga na nusu, hapo ndo Jess anajitambua yupo kwenye mzunguko usiokuwa na kikomo.

Atatokaje?

Anafanikiwa kuwamaliza tena wenzake na kurejea nyumbani kwake. Anachungulia dirishani na kukutana macho kwa macho na mtoto wake wa kiume. Mtoto anashtuka na kumwaga uchafu (kumbe ndo maana mtoto alifanya uchafuzi huu mwanzoni mwa movie) mara mama anatokea na kumfokea, na hapo Jess anajiona yeye kabisa mbele ya macho yake!

Anagonga kengele ya mlangoni, Jess ambaye yuko na mtoto anaenda kufungua lakini hamwoni mtu (kumbe aliyegonga muda ule mwanzoni alikuwa ni Jess huyu!). baadae Jess aliyetoka kwenye meli anamuua Jess huyu aliye na mtoto kisha anamweka kwenye mfuko na kumpakia kwenye gari (Kumbe ule mzigo tuliouona mwanzoni ukipakiwa ni mwili wa Jess aliyekuwa na mtoto!), gari linatimka.

So kwa ufupi Jess yupo kwenye mzunguko wa kifo na maisha ambao hawezi kujitoa. Ni kwanini haswa? Wapi kisa kilianzia? Nini Jess afanye kujikwamua? Nini chanzo cha yote haya? Haya katazame. Hapo ndo utajua “everything counts”. Jina la Meli na Dereva Taxi ndo funguo wa kuelewa kinachoendelea..

Screenshot_20200403-004458.jpg

SCARY STORIES TO TELL IN THE DARK ya 2019.

Kilichonifanya nikaipenda filamu hii ni wazo lake la kiubunifu na la kipekee. Ndio ni movie ya kutisha lakini story yake ipoje? Sio tu watu wanaibukaibuka na kutokea watu ama familia fulani sababu ya kukaa nyumba yao – NO! Lazima kuwe na kitu interesting cha kufanya utazame filamu na kusema wow! Interesting.

IPO HIVI: Kikundi cha ‘ma-teenagers’ wanavutiwa kwenda kwenye nyumba fulani ambayo imetelekezwa na kugeuka kuwa ghofu. Wakiwa huko msichana anayeitwa Stella anapata kuona kitabu kilichotelekezwa, na ndani ya kitabu hicho kuna hadithi mbalimbali za kutisha na kusisimua.

Stella, kwa kuvutiwa na kitabu na hadithi hizo, anakibeba kwenda nacho nyumbani akapate kujisomea na kufurahia hadithi za kale lakini kwa kutotambua anakuwa amefanya kosa kubwa sana ambalo si tu linamgharimu yeye bali pia na marafiki zake wote alofunga nao safari.

Anasoma hadithi moja baada ya nyingine akiamini ni tungo makini, namna watu walivyokufa na kutokewa na ‘mavitu’ ya ajabu huko zamani, lakini cha ajabu baada ya kumaliza hadithi hizo anastaajabu kuona hadithi zingine zinaendelea kuandikwa ndani ya kitabu ingali anayeandika haonekani!

Na kama haitoshi, wahusika anawaona kwenye hizi hadithi mpya si wageni tena machoni mwake bali ni majina ya marafiki zake kabisa, wale aloenda nao katika ile nyumba kuukuu! Stella anastaajabu sana lakini anakuja kustaajabu zaidi baada ya kugundua kuwa zile si hadithi tu, bali ni uhalisia unaotokea.

Sasa anahaha kupambana na hadithi, sasa anahaha kupambana kuokoa wenzake na nafsi yake pia dhidi ya hadithi anazoziona zikiwa zimeandikwa kugusia mauaji ya kikatili kuwahusu.

Je, nani anayeziandika hadithi hizo? Ni nini haswa Stella na wenziwe walifanya kustahili adhabu hiyo? Ni nini wafanye kujinasua dhidi ya yanayotabiriwa kuhusu wao? Tafuta popcorn!

Screenshot_20200403-005038.jpg

ESCAPE ROOM ya 2019.

Kama unataka filamu ambazo zitakunyima usingizi ukabaki ukikodoa kujua nini kinafuata ama kinaendelea, basi kwenye hii umefika. Hii ni filamu ambayo itakufanya uone haja kamili ya kutumia akili yako nzima, maana ni aidha uitumie akili yako uendelee kusurvive, ama ukishindwa basi ufutikie mbali kwenye huu ulimwengu usipatikane hata mzoga!

Hii filamu ni maana halisi ya nadharia ile ya mwanasayansi wa kiingereza, Bwana Charles Darwin ya ‘Theory of Evolution’ (Nadharia ya Mabadiliko) haswa kwenye kategoria ya ‘Survival of the Fittest’ – kwamba yule mwenye/chenye nguvu ndicho kitakachodumu kwa ‘expenses’ za yule mdhaifu. Sasa humu kwenye hii filamu kinachofanya udumu na uhai wako ni uwezo wako wa kutumia werevu kwenye kung’amua changamoto mbalimbali kupata suluhisho, na ubaya unakuja pale ambapo suluhisho likikosekana, unachopoteza ni kitu chenye thamani kuliko chochote kile – UHAI.

IPO HIVI: Watu sita wanapewa mwaliko wa kuhudhuria jaribio la kuwapo ndani ya chumba na yule atayefanikiwa kusuluhisha majaribio atakayopewa basi ataondoka na donge nono la dola za kimarekani alfu kumi! Lakini shida ni kwamba, hawajui atakayeshindwa basi atapata kifo.

Basi wakaona pesa laini hii, usikatae wito bali ujumbe, wakafika walipotakiwa kufika na kungoja wakutane na mtu atakayewapa maelekezo. Ajabu ni kuwa, hakukuwa na mtu yeyote wa kuja kuwapa maelezo, na hapohapo walipokuwa wameketi kungoja , jaribio ndo’ likaanzia! Joto linapanda taratibu kuwa kubwa kupita kiasi, muda unatangazwa, na hivyo basi wanatakiwa kutoka katika chumba hicho ndani ya muda kabla wote hawajaokwa kuwa mkate!

Ni matumizi makubwa ya akili yanahitajika kujikomboa, na kila unapofuzu kimojawapo basi unaenda kwenda chumba kingine ambacho nacho kina mtihani wake wa kipekee. JE, AKILI YAKO ITAKUOKOA MARA NGAPI?

Kilichonifurahisha zaidi ni kuona mtoto mdogo zaidi kati ya hao nane waliopo kwenye usahili huu wa ajabu, ndiye mwenye akili inayofikiri kwa upesi na ufanisi zaidi kuliko watu wazima kiasi kwamba kuna mitihani ikija wanamtazama wasikie anasema nini.

Jaribio jipya la kila chumba ndo’ inafanya filamu hii kuwa ya kipekee na kiubunifu kabisa. Unaona namna mwandishi alivyoketi chini na kutumia asilimia zake kadhaa za ubongo inavyotakiwa.

Screenshot_20200403-004342.jpg

PHONE BOOTH ya 2002.

Hivi mtu akikutafuta, tena usiyemjua kabisa – hujawahi kuonana naye wala kumsikia – akataka umpe sababu nzito za yeye kukubakizia uhai, utampa sababu gani? Nina watoto na familia? Hahaha au zipi haswa? Alafu ukizingatia mtu huyo anakujua nje na ndani kiasi kwamba huwezi kumdanganya chochote kile katika maisha yako?

Japo filamu hii nilipata kuitazama muda mrefu ulopita lakini imebakia kuwa moja ya filamu bora zaidi kwangu. Itakuchukua dakika themanini tu (80 Minutes) kuimaliza mwanzo mpaka mwisho wake lakini hautazijutia. Kitendo cha ‘setting’ yake kuwa kibanda cha simu tu karibia filamu nzima lakini bado kitu kikawa cha kusisimua na kueleweka, kulinifanya niiweke hii katika kumbukumbu zangu.

IPO HIVI: Bwana anayeitwa Stu, mwanaume mjivuni na mkorofi, anaenda kwenye kakibanda cha kupigia simu (phone booth) ili apate kufanya maongezi na moja ya mtu muhimu kwake. Na kinachomfanya atumie njia ya kibanda cha simu ni kuongea na kimada wake sababu kutumia simu ya nyumbani ingemfanya mkewe apate walakini juu ya ‘bill’ ya simu kwa mwezi.

Alipoingia humo kibandani anaongea na kimada wake na anapomaliza tu mara simu inaita, anapokea na kusikia sauti nzito ya mtu ambaye anajieleza kuwa anamjua na amejiweka mahali akitumia risasi ya masafa marefu ambayo tayari rada zake zimeshamweka vema ndani ya ‘tageti’, akibofya tu ni kiza cha kifo ndo’ kitammeza pasipo hiyana!

Mtu huyo anayeongea ndani ya simu sio tu kwamba anatishia, la hasha! Yuko ‘serious’ na anachokisema, na kwa kuthibithsha hilo anafyatulia risasi toy iliyopo kwenye kibanda fulani karibu na kibanda cha simu ili kuthibitisha uwepo wake. Lakini pia kama haitoshi anamtajia Bwana Stu jina la kimada wake, bibie Pam, na jina la mkewe, bibie Kelly, akiwa anatambua mpaka wanapoishi.

Mdunguaji anampa maelekezo Bwana Stu, ya kwamba hatakiwi kutoka bandani hapo wala kukata simu mpaka atakapoagizwa afanye hivyo. Anamtaka Bwana Stu akiri ayafanyo kwa mkewe na pia amjuze kumhusu kimada wake. Mosi, mdunguaji akampigia simu Pam na kumweka on, Bwana Stu akamweleza ukweli kuwa ana mke, baada ya hapo, Mdunguaji anamtaka Bwana Stu ampigie mwenyewe mkewe amwambie kuwa ana kimada anayempenda.

Kabla hajafanya hivyo, wanakuja wateja wengine, wanawake, wakitaka kuongea na simu. Wanamhenyesha haswa bwana Stu mpaka bwana wao anakuja hapo kumchachafya Bwana Stu kwa kung’ang’ania simu kama ya kwake ingali wengine wanataka huduma, watu hawa pasipo kujua kuwa Bwana Stu si kwamba anang’ang’ania simu bali anang’ang’ania uhai wake.

Hapa ndo Bwana Stu akabaini kuwa mdunguaji hakuwa hana masikhara hata kidogo kwani alimdungua bwana huyo aliyekuwa anamsumbua na kusababisha kizaizai haswa baada ya hapo kwani ni Bwana Stu ndiye aliyedhaniwa kuwa muuaji akitumia bunduki aliyoificha mwilini!

Je, Bwana huyu atajinasuaje na kisanga hiki cha dangamanya Mdunguaji? Movie hii imetumia kiasi cha dola milioni 13 tu mwanzo mpaka mwisho wake, lakini kilichopatikana kwenye mauzo tu ya tiketi (Box Office) ni dola milioni 97! Katazame kwanini ilipiga mkwanja kiasi hiko.

Screenshot_20200403-005342.jpg

INSIDOUS (Chapter 1) ya 2011.

‘How far can you go for your family?’ ni swali zito ambalo kadiri unavyotazama hii filamu yakupasa ujiulize – ni kwa kiasi gani unaweza kutenda kwa ajili ya familia yako? Ni namna gani wewe kama mzazi unaweza kubeba ‘risk’ ya aina yoyote ile kuwahakikishia usalama wa watoto wako – wewe kama mama, wewe kama baba?

Lakini zaidi cha kujifunza si tu kwamba kuna magonjwa ya kurithi ambayo yanazunguka ndani ya familia na koo fulani fulani, bali kuna vya zaidi ya hapo. Kujua kwamba vinasaba vyetu haviishii kubeba tabia, maumbo, hulka na afya zetu bali vinabeba hata historia, laana na vifungo kadha wa kadha ambavyo tunarithi na kurithisha mpaka pale mnyororo wa kuzima utakapovunjwa.

UHONDO UPO HIVI: Familia ya Bwana Josh na Bibi Renai iliyobarikiwa watoto watatu wanahamia kwenye makazi yao mapya pasipo kuonyeshwa wametokea wapi haswa, lakini kuna kitu hakipo sawa katika familia hii, miongoni mwa picha za familia, picha ya baba ingali akiwa mtoto haipo, kitu ambacho si kawaida. Mtoto wa kiume, Dalton, anamuuliza mama yake kuhusu hili lakini anadanganywa (Hapa kulikuwa na siri nzito inayobeba filamu nzima).

Basi siku moja, Dalton, akiwa katika michezo yake, anapata kusikia sauti kwenye moja ya chumba cha juu, hivyo anaenda kutazama nini kinaendelea. Akiwa anapanda ngazi inakatika anadondoka chini. Kesho yake Dalton haamki toka usingizini, wazazi wanamkimbizia hospitali ambapo huko daktari anakosa cha kuwasaidia kwa kuwaambia hajawahi kutana na ‘case’ kama hiyo.

Baada ya kukosa msaada Dalton anarejeshwa nyumbani akiwa bado katika hali yake ya kutojitambua. Hapo ndo’ mambo yanazidi kuwa tafarani nyumbani haswa kwa mama ambaye mara nyingi anashuhudia mambo ambayo akimweleza mume wake hapati kuamini.

Lakini zaidi ni kwamba, mtoto mdogo kabisa wa familia hii, Foster, anawaambia wazazi wake kuwa Dalton huwa anazungukazunguka chumbani nyakati za usiku hivyo anaogopa! – kumbuka Dalton ni yule mbaye yuko kwenye hali ya kutojitambua (coma).

Mama kwa kuona vitimbi na vitu asivyoweza kuvumilia, akamsihi mume wake watafute nyumba nyingine akidhania ni nyumba ndo’ yenye shida lakini hata baada ya kuhama mambo yanaendelea kama kawaida, tena yanapamba moto kadiri na siku zinavyoenda!

Hapa sasa ikabidi watafutwe ‘wataalamu’ haraka iwezekanavyo kuja kuokoa jahazi. Wataalamu walipofika, wakiongozwa na mwanamke makamo ya uzee, wakafanya mambo yao na kubaini ya kwamba mtoto Dalton alisafiri nje ya mwili wake (astral projection – hii ni sayansi/Sanaa ya kujitoa nje ya mwili wako ingali mwili huu halisi wa nyama ukibakia kujilaza tu kama mfu), dogo ameenda umbali mkubwa sana kiasi kwamba amepotelea mahali ambapo ni mahususi kwa kutesea nafsi za waliokufa – mahali ambapo hawatakiwi waliohai kufika. Hivyo basi nafsi hizo ambazo zinapitia shurba huko zinachangamkia fursa ya kurudi kwenye ulimwengu wa binadamu kwa kutumia mwili wa Dalton ambao upo kwenye hali ya kutojitambua!

Maneno hayo ya wataalamu ndo’ yanawafungua wazazi macho juu ya yale ambayo mtoto wao, Dalton, alikuwa akiyaandika na kuyachora ukutani, kuanzia watu wa ajabu mpaka maneno kadhaa.

Sasa watamwokoaje mtoto wao arudi kwenye ulimwengu wa binadamu tena? Kwanini picha za Josh, baba wa familia, akiwa mtoto zinafichwa? Nini matokeo ya yote haya? Tafuta muda wako mzuri nyakati za usiku, zima taa, tazama filamu hii ukiwa na maji ya kunywa pembeni.

Screenshot_20200403-004612.jpg

PAPILLON ya 2017.

Hii filamu ni maana halisi ya pene nia pana njia. Inatufundisha namna gani ambavyo kila kitu kinaanzia kichwani na kila penye haja ya dhati hakuna lolote la kuzuia. Ni story ya kweli kabisa ya bwana aliyewahi kutiwa ndani kwa kosa la kusingiwa kuua hivyo anatia nadhiri ya kutolipia kifungo ambacho hakimhusu. Kwa namna yoyote ile, juu ama chini, hatokaa gerezani.

MAMBO YAPO HIVI: Henri (almaarufu Papillon – kipepeo) ni mshirika wa magenge ya wizi katika jiji la Paris lakini punde kidogo bwana huyo anasingiziwa kesi ya mauaji na moja ya genge kisha anahukumiwa kifungo cha maisha kwenye gereza moja iliyopo Guinea (French Guinea). Gereza hilo lina sifa moja kubwa, hakuna mtu aliyewahi kutoroka akafanikiwa.

Wakiwa kwenye chombo cha maji kuelekea huko gerezani, Henri anakutana na bwana anayeitwa Louis Dega. Bwana huyo moja ya watu maarufu na wenye pesa. Alikamatwa sababu ya ughushi (forgery). Na inasemekana bwana huyo ana pesa tumboni mwake, amezimeza. Basi Bwana Henri ananuwia kuunda urafiki na bwana huyo ili awe anamsaidia kifedha kurahisisha utorokaji wake kwa malipo ya kumlinda Dega akiwa gerezani dhidi ya mashababi na manyampara.

Mwanzoni Bwana Dega anakuwa mkaidi lakini baada ya kushuhudia kwa macho yake mtu mmoja akichanwa utumbo ili anyofolewe pesa, akakiri kumhitaji bwana Henri. Basi wanaweka maagano kwamba Henri amlinde mpaka pale mke wake aliyepo uraiani atakapokata rufaa atoke gerezani.

Walipoingia tu gerezani, mkuu wa gereza anawaambia kwamba anajua kuna baadhi wanawazia kutoroka lakini anawahakikishia hawataweza kwani mbali na walinzi wa gereza, huko nje kuna walinzi wawili wawili walio zamu pasi na kuchoka. Mmoja, ni msitu wa vichaka ambapo mtu ni ngumu kukatiza pasipo kufa na njaa na pili kuna njia ya bahari ambapo papa wana njaa kali kila saa!

Kitu kilichokuwa kinanifurahisha katika hii filamu ni namna Henri alivyokuwa anahangaika kuwa karibu na Dega kumlinda na huku Dega akiwa analazimika kwenda chooni ndo’ ajisaidie pesa ya kumpatia Henri. Kuwa kwao karibu hivi kunawafanya wahuni wengine wahisi hawa wanaume ni wapenzi.

Henri anahangaika sana kufanya majaribio ya kutoroka huku akiishia kufeli, kukamatwa, kuadhibiwa na hata kuhamishwa magereza pamoja na mwenzake. Kuna kipindi alipitia mateso makali kiasi kwamba mkuu wa gereza akamuuliza “What are you living for, Pappi?” – maana alishawahi kuona watu wakipitia adhabu zile mwishowe wakavunjika moyo ila haikuwa hivyo kwa Henri.

Kilichoniumiza zaidi ni namna ambavyo baadae Henri anafanikiwa kupata upenyo wa kutoroka lakini Dega aliyepitia naye misukosuko mingi anagoma kuondoka tena gerezani. Anaamua tu kubaki akimsihi Henri aende zake mwenyewe. Alishakata tamaa na hakuona tena sababu ya kutoka humo gerezani baada ya kubaini mke wake kipenzi alimsaliti na kufunga ndoa na mwanasheria wake. INAUMA.

Tofauti na filamu zingine za kutoroka gerezani, katika Papillon mtorokaji si ‘genious’ wa kutumia akili nyingi mno kama wakina Scofield wa Prison Break, bali alikuwa na dhamira. Na hili lilikuwa fundisho haswa ya kwamba kufanikiwa si lazima uwe na akili sana kupita kiasi, bali uwe na nia na dhamira ya kweli.

Screenshot_20200403-004229.jpg

Katafute filamu hizo ufurahie weekend yako!

Imeandaliwa na Steve B.M,
A freelance journalist
A literary scholar and Movie critic.
0685 758 123 (Whatsapp Only)

Karibuni, innocent dependent elly obedy rejea kajojo ekomu1 Vladimir Lenin Ignas lyamuya Yna aika Penison Neylu ndukulusudicho IMERN Amorbwoy fofre kemisho chaliifrancisco jooohs Manlax Braibrizy Zoë kathago Tit 4 Tat kipozi Leonard Robert free lander TELLO kiwaki

na wengineo wapenda movies... toeni nanyi mapendekezo juu ya movies mnazoona na wengine wanatakiwa kuzitazama...
 

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
5,793
2,000
MCHANGANUO No: 2


DEVIL ya 2010.


Ushawahi kupitia siku fulani ambayo uliona kila kitu hakiendi poa? Yani upoupo tu, unajihisi mzito, mvivu au unajihisi hauna bahati kabisa siku hiyo? … kheri wewe ndugu. Hiyo tunaita siku mbaya tu, na inaweza ikawa ni kurasa moja tu katika wiki yako ama mwezi au hata mwaka kabisa, lakini ushawahi kusikia SIKU YA SHETANI?

Siku ambayo sio tu mbaya kama unavyosema zile zingine, la hasha! Bali siku ambayo unapigania uhai wako. Siku ambayo unakutana na shetani uso kwa uso akiwa amekubana kwenye kona mbaya haswa. Kona ambayo machaguzi ni mawili tu … kufa ama kupona!

IPO HIVI: Kwa namna siku hii inavyoanza inaonekana ni ya kawaida tu kama jana na juzi ila kiuhalisia ilikuwa ni siku ya shetani kujivinjari. Mwanzoni kabisa bwana mmoja anasikika akisema kuwa mama yake alishawahi kumsimulia kumhusu shetani. Muda mwingine shetani hutembea ndani ya miili ya watu na huwaadhibu mwenyewe wale walio wadhalimu kwa kuwafungia eneo moja kisha kumuua mmoja baada ya mwingine. Na siku ambayo shetani atakuwa katika uzuru wake mahali fulani ishara yake ni mtu kujiua katika eneo hilo.

Ingali jamaa huyo akiendelea kusimulia, ghafla kuna mtu anajiua kwa kujirusha toka kwenye ghorofa ya thelathini na tano ya jengo refu la ofisi ya Philadelphia. Mtu huyo anaangukia juu ya gari na kufa papohapo.

Baadae kidogo katika jengo hilo watu watano wasiofahamiana wanaingia ndani ya lifti na punde lifti inagoma katikati ya sakafu (floors) mbili ya juu na chini hivyo kufanya uwezekano wa kujinusuru kuwa finyu. Wakiwa wamepaniki na kukwazika, security aliyekuwa ndani ya lifti pia anawatoa hofu kuwa si muda mrefu mambo yatakuwa sawa.

Ndani ya lifti hiyo kuna namna za mawasiliano na eneo la kuongozea chombo hicho lakini siku hiyo katika namna ya ajabu, mawasiliano yaliyokuwepo yalikuwa ni ya video tu pasi na sauti. Yani maana yake ni kwamba kilichokuwa kinaendelea ndani ya lifti kilikuwa kinaweza kuonekana lakini sio kusikika!

Sasa kutokana na kile kisa cha mtu kujiua kwa kujitupa toka juu ya ghorofa, kuna mpelelezi mmoja aitwaye Bwana Bowden alipewa kesi hiyo aifanyie kazi. Na kutokana na kwamba mauaji hayo yalitoke katika hili eneo, basi mpelelezi huyo anajikuta akihusika na hili swala la hawa watu waliokwama ndani ya lifti kwa namna moja ama nyingine.

Lakini shida ni kwamba mpelelezi huyu, Bwana Bowden, hakuwa sawa kisaiokolojia. Si muda mrefu sana alikuwa ametoka kumpoteza mke na mtoto wake kwenye ajali. Kutokana na hilo alijikuta akijiingiza kwenye ulevi ulopindukia.

Sasa kwenye macho ya kila mtu, ikiwemo hata mpelelezi mwenyewe, kesi hii ya lifti haikuonekana kubwa sana ya kusumbua akili. Ni ‘system’ tu. Ndivyo walikuwa wanajidanganya. Lakini baada ya mtu mmoja baada ya mwingine kufa ndipo mambo yanapogeuka na kuonekana si utani hata kidogo!

Anayeua hajulikani ni nani lakini ni bayana yupo ndani ya lifti. Kila mtu anamhisi mwenzie. Haijulikani ni nani ni salama kuwa naye pembeni. Hofu inatawala anga. Lakini zaidi kila mtu aliyepo ndani ya lifti siri yake ya uovu inaanza kubainika.

Mpelelezi, Bwana Bowden, ana kazi kubwa ya kuwaokoa watu kabla wote hawajaisha. Ana kazi kubwa ya kumtambua muuaji. Na ana kazi kubwa ya kubeba na kung’amua zile toba za uovu wa wale waliopo ndani ya lifti.

Moja ikiwa inahusiana na kifo cha mtoto na mke wake.

NI KISANGA NA NUSU!
 

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
5,793
2,000
Upo vizuri kijana hila Hiyo triangle sikuielewa kabisa kuona matukio yanajirudiarudia
Nimekupa hint hapo mkuu, ungefanya ka-udadisi kidogo ungefungua fumbo lako. Jina la Meli, AEOLUS, ndo lina habari kuhusu hiyo movie ambapo mtoto wa AEOLUS, aitwaye Sisyphus, alikuwa mtawala katili na mdanganyifu hivyo kupelekea kupewa adhabu ya kupandisha jiwe kubwa mlimani, kisha jiwe linarudi chini na kuanza tena upya pasipo kumaliza.

Kwenye movie ya TRIANGLE tunamwona Jess akimwakilisha Sisyphus kwa kuwa mama katili kwa mtoto wake lakini pia mdanganyifu (unaweza ona hili kwa ile ahadi alompatia dereva taksi kwamba anarudi ingali hakufanya hivyo), na yule dereva taksi ni kama kiashiria cha kifo kwani alimbeba Jess baada ya kupata ajali na mwanaye na pengine wote kufa lakini tunaona Jess akiwa anakataa kifo, anataka kurekebisha makosa yake kwa mtoto.

Hapati hiyo nafasi. Anatumikia adhabu yake kwa kurudia palepale mpaka atakapokata shauri ya kuondoka na 'dereva taksi' yakwishe.

Sent using Jamii Forums mobile app
 

elly obedy

JF-Expert Member
Jan 12, 2015
470
500
Ahsante mkuu umeelezea vizuri sana , na mimi ngoja niitafute hiyo Papillon, movie zinazo fanana kama series ya Prison Break huwa napenda sana kuzifuatilia👏🏻
 

Hziyech22

JF-Expert Member
Jun 8, 2019
6,302
2,000
Mchanganuo wa movies zingine nitaendelea kwenye comments ...
Umechambua vizuri Sana katika hizo zote hapo nimeona moja tu ambayo ni Triangle kwa maelezo ulizotoa kwa movie zilizobaki nimevutiwa nazo Sana nitazicheki Kuna wengine humu wanataja horror movie za ovyo mradi tu ziwe horror tu hazina mvuto Wala ubunifu wowote.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom