Nusu siku ndani ya jeneza

Nusu siku ndani ya jeneza

Mungu akuamshe salaama kesho utupe zaidi. . Nimejifunza vingi ambavyo sijui angetokea nani kunifundisha. Thanks
 
NUSU SIKU NDANI YA JENEZA - 8-

ILIPOISHIA :
Mfano, kile chumba cha kondoo, ndani yake kuna wanaoshughulikia wanadamu wenye tabia ya kondooo.
“Unajua iko hivi, kila binadamu aliyezaliwa ana tabia inayofanana na mnyama mmoja aliyopo duniani.”
“Ha! Kweli?” nilishtuka sana. SASA ENDELEA…

“
Ni kweli. Na mle mwenye vyumba ndimo mnamokuwa na wanowaongoza binadamu hao. Wapo binadamu wapole sana, hao wamefanana na kondoo, kuna binadamu hawajatulia muda wote, wala hawawezi kukaa mahali pamoja muda mwingi hao ni mbuzi.
“Mfano mwingine, hakuna binadamu ana tabu kama atafanana na mbwa. Binadamu anayefanana na mbwa ana tabia ya ukali na kusema kila wakati, mnaita gubu. Akiwa mwanamke lazima ataangukia kwenye vitendo vya kuuza mwili, mnaita ukahaba.
“Unajua ni kwa nini?” aliniuliza.
“Sijui.”
“Lazima usijue, lakini pia nikikusimulia hutaelewa lolote. Ila kikubwa ninachotaka utambue ni kwamba kila binadamu mmoja lazima atakuwa amefanana tabia na mnyama fulani wa mwituni au wa majumbani. We hapo ulipo unaweza kuikumbuka tabia yako na utagundua imefanana na mnyama mmoja, ndiyo maana watoto wanaweza kuwa wa baba mmoja mama mmoja lakini wakawa na tabia tofauti. Lakini tabia za wanyama hutokea wakati fulani zikawanufaisha wanadamu, mfano kumkuta mtu anafanana na mnyama swala, huyu kama atajijua akaamua kuwa mwanariadha anaweza kufika mbali sana.
“Kama binadamu atajua anafanana tabia na mnyama simba halafu akaamua kuwa mpiganaji, naye atafaidika sana. Mtu anayefanana na simba mara nyingi pia akiamua kuanzisha kampuni na kuajiri watu anakuwa na sauti sana ya utawala.
“Mtu anayefanana tabia na kobe, akiwa mwanamke atakuwa wa kuzaa kwa muda mrefu katika maisha yake. Yaani mara nyingi atakuwa akionekana kubeba watoto.
“Mtu akifanana tabia na mnyama kama paka, katika maisha yake iko siku moja lazima atafumaniwa na mke wa mtu au mume wa mtu.
“Mtu akifanana tabia na tembo, siku zote katika maisha yake atakuwa mtu mwenye kupenda kuwa juu kwa wenzake na atafanikiwa kwa hilo. Watu wa aina hii kwenye makampuni ndiyo wana tabia ya kushawishi migomo, wakiwa kwenye mkutano au kundi akisema jambo yeye linawavutia wengi kuliko wakisema wenzake wasiokuwa na tabia ya tembo.
“Lakini pia mtu huyu atafanikiwa zaidi kama ataamua kufanya kazi za kubomoa majumba yaliyojengwa kinyume cha sheria kwa kutumia tingatinga.
“Mtu akifanana tabia na twiga ana bahati ya kuonekana yeye tu hata akiwa kwenye kundi la watu mia moja. Mara zote yeye huwa kinara kwa kuonekana. Ila hatari yake ni kwamba endapo atakuwa mwizi au jambazi wakafanya tukio sehemu na kukimbia yeye lazima atakuwa wa kwanza kukamatwa.
“Faida yake ni kwamba kama ni mfanyabiashara, akataka mkopo kwenye benki fulani halafu kuna wengine wanaotaka mikopo na wameandika barua yeye atakuwa wa kwanza kujibiwa kuliko wenzake.
“Kama ni mwanafunzi, mwalimu akiuliza swali halafu wanafunzi wote wakainua mikono kujibu, yeye atakuwa wa kwanza kuchaguliwa kujibu.
Alipofika hapo yule kiumbe akaniuliza swali:
“Hivi unamjua mtu mwenye tabia inayofanana na mnyama fisi?”
“Simjui.”
“Sawa huwezi kumjua. Mtu mwenye tabia ya mnyama huyo mara nyingi hukwepwa na wenzake. Umewahi kusimama kwenye kituo cha basi kwa kutawanyika halafu kila basi likija linasimama kwa wenzako?”
“Nimewahi sana.”
“Je, umewahi kuona kwamba ukiamua kusogea eneo ambalo mabasi yanasimama, mengine yakija yanapita kwenda kusimamia pale ulipokuwa umesimama awali?”
“Ndiyo imeshanitokea sana tu.”
“Je, umewahi kubaini kwamba upo ndani ya basi, umekaa siti ya watu wawili lakini hapo umekaa peke yako halafu kila abiria akiingia anakupita kwenda kukaa na abiria wengine mpaka basi linajaa ndiyo mtu anakuja kukaa na wewe?”
“Mara nyingi sana, hivi ni kwa nini?”
“Basi wewe una tabia za fisi, ndiyo maana nimechukua muda mrefu sana kukujulisha kwanza mambo ambayo una uhakika nayo.”
“Da! Kwa hiyo mimi maisha yangu yangekuwa bure duniani, ningekuwa mtu wa kusumbuka au kutegemea wengine watafute ili mimi nile kama alivyo fisi?”
“Ndiyo! Kama una kumbukumbu nzuri, vitu vyako vingi ulivyonavyo umekuwa ukiachiwa na watu, uongo?”
“Kweli kabisa.”
“Je, utakubaliana na mimi hata mke uliyenaye alishaolewa akaachika ndiyo ukamuoa wewe?”
“Ni kweli kabisa. Sasa ili kuendelea ingebidi nifanye nini?”
“Ulitakiwa kufanya biashara ya kuuza vitu vikuukuu, mfano nguo za mitumba. Magari yaliyokwishatumika, kununua vitu vya zamani na kwenda kuviuza mahali pengine au hata kuwa dalali wa kuuza nyumba zilizokwisha jengwa na kukaliwa, lakini si dalali wa kuuza viwanja au kupangisha nyumba.”
“Nilichoka kabisa, niliamini aliyoyasema yote kwani yalinitokea. Pia niliamini kuhusu vitu, hata kitanda cha kwanza katika kuanza maisha niliachiwa, godoro na shuka pia. Baadhi ya ndugu zangu walipokuwa wanakuja nyumbani walipenda kuniachia mavazi, viatu hata saa au simu.
“Mke niliyemuoa alikuwa ameshaolewa na jamaa mmoja anaitwa Mdoe, alipoachana naye ndiyo nikaibuka mimi na kuoa. Nikakumbuka kuna mzee mmoja jirani yetu aliwahi kuangaika sana kuuza baiskeli yake kwa sababu alikuwa na dharura lakini siku moja nilipoamua kumsaidia niliiuza ndani ya saa moja tu tena kwa mtu ambaye alikataa kuinunua kwa mzee huyo.”
Nilibaki nimemtumbulia macho kiumbe yule kwani sasa tulikuwa kama marafiki tu na wala sikuwa nawaza lolote kuhusu maisha yangu ya baadaye wala yaliyopo.
Kuna swali nilikuwa nalo nje kabisa na hayo, nikamuuliza:
“Eti, kuna viumbe wanaweza kupenya kuingia ndani ya nyumba hata kama imefungwa?”
“Wapo, hata mimi naweza.”
“Inakuwaje?”
“Sisi tuna miili ya moto, hatuna mifupa kama unavyodhani.”
“Kama ungekuwa hauna mfupa ungekuwa hai?”
“Uwezo wetu na wenu ni tofauti sana.”

Ili kujua zaidi usikose kusoma baadae....
 
Back
Top Bottom