*NJIA NYEMBAMBA ---- 29*
ILIPOISHIA
Ulsher alimpa ishara Ras Killer. Mwanaume akatupia bomu la gesi ndani ya chumba. Kama haitoshi, Ulsher naye akatupia la kwake humo ndani.
Wakatoa vinyago vya kuziba hewa wakavivaa.
Punde wakasikia vishindo vya miguu na kisha sauti ya mlango unafunguka. Haraka wakajua Mr. X atakuwa ametoka chumbani. Na ataenda kuongeza nguvu ya mashambulizi dhidi ya Farah na Mou huko chini.
Hivyo basi wakamalizia kubomoa dirisha Ras Killer akitumia nguvuze zisizo na mithili. Wakazama ndani.
ENDELEA
Kutazama huku na huko, hamna mtu! Chumba kilikuwa cheupe pe, basi haraka Ulsher na Ras wakasonga mbele na huku bunduki zao wamezionyeshea mbele. Huko chini, sauti za milio ya risasi zilikuwa zinarindima kwa fujo!
Wakafika chini lakini hawakumkuta Mr. X, na Farah na Mou walikuwa wamajeruhiwa kwa risasi. Mou alikuwa amelala chini akiwa anahema kwa tabu, alikuwa ametobolewa kifua kwa ncha ya risasi, Farah yeye alikuwa amedunguliwa bega lake la kushoto lakini nao pia walikuwa wamewamaliza watu kadhaa wakiwa wamelala wafu kando.
“Mr. X amekimbia!” Alisema Farah akinyooshea kule upande wake wa kushoto. Ulsher akamtaka Ras abaki kuwatazama majeruhi, yeye ataenda kushughulika na Mr. X.
“Hakikisha unaweka presha za kutosha kwenye majeraha. Fanya pia mpango wa kumuwahisha matibabuni.”
Ulsher akakimbia upesi kwenda kule alipoelekezwa. Kwa mbali akamwona Mr. X akiwa anayoyoma na basi akamhifadhi asije mtoka mipangoni. Akakimbia kwa kasi mno akijitahi kubana pumzi. Kadiri alivyokuwa anasonga, akawa anamkaribia mlengwa wake.
Ila hakudumu na hilo, alipokata kona ya pili, ghafla Mr. X akapotea machoni mwake! Hakuonekana wapi alipoelekea. Mtaa ulikuwa kimya na hakukuwa na dalili zozote za mtu kukatiza.
Ulsher akatazama kila pande, akarusha macho yake dirishani na milangoni mwa nyumba wastani zilizopo kwenye mazingira hayo, ila patupu. Taratibu, akiwa ameshika bunduki yake kwa ustadi, akasonga mbele, macho yake yakiangaza kana kwamba duma mawindoni.
Mara akasikia kishindo cha mtu nyuma yake, upesi akageuka kuangaza, kurudisha uso wake mbele akakutana na ngumi nzito ya mwanaume ikambwagia chini! Bunduki ikarukia kando asiweze kuinyaka hata kwa kuunyoosha mkono.
“Habari mrembo?” sauti ya nzito ya kiume ikapaza. Alikuwa ni Mr. X ndani ya kombati nyeusi, kichwa chake kikifunikwa na kofia nzito ya soksi iliyofunika masikio yake. Hakuwa na silaha yoyote pamoja naye.
“Kwahiyo wewe ndiye wamekutuma uje kunimaliza?” akauliza kwa kabehi. “Watakuwa wamenidharau sana. Sasa wamaenitumia mpambanaji ama mke?” akaangua kicheko kilichoishia kwa kikohozi kikavu. Akamnyanyua Ulsher juu kwa mkono wake wa kuume.
“Umeingia uwanja mbovu, mwanamama. Muda huu ulitakiwa kuwa chumbani na mumeo si mitaani.”
Kumaliza kauli yake hiyo, upesi katika kasi ya umeme, Ulsher akadaka mkono wa kuume wa Mr. X kwa kutumia miguu, haraka akitumia uzito wa mwili wake, akambwaga Mr. X kwa njama za judo.
Dharau hizi!
Mr. X akanyanyuka kwa kujifyatua. Akakunja sura yake na kumsogelea Ulsher kwa pupa la hasira. Ulsher akajitutumua kurusha mateke na ngumi, ila hakufua dafu, Mr. X alikuwa mkamilifu kumzidi yeye kwenye uwanja wa mapambano, akamsulubu Ulsher kwa ngumi zake nzito na mateke ya kilo nene, Ulsher akawa hoi! Alilala chini akiwa anamimina damu mdomoni huku akihisi maumivu makali.
“Hakuna wa kunizuia. Sijaona wa kunizuia. Na wewe utakuwa ujumbe mujarabu kwa hao waliokutuma!”
Mr. X akamkandika Ulsher teke la tumbo, Ulsher akatapika damu akilalama kwa maumivu makali. Akataka kumshindilia teke lingine, Ulsher akawa mwerevu. Haraka akaunyaka mguu huo uliotaka kumwadhibu, alafu akafyatua miguu yake yote miwili kuufagia mguu wa Mr. X, akaudondosha mbuyu chini!
Asilaze damu akaruka samasoti na kuinyaka bunduki, akamnyooshea Mr. X akimwamuru anyooshe mikono juu.
“Fuata nitakachokuambia, la sivyo nitatia komo maisha yako!” Ulsher akawaka. Akawasiliana na wenzake na kisha akamtaka Mr. X aweke bayana yale yote atakayomuuliza, akiwa mkaidi atafyatua kitufe cha bunduki akasabahi jehanamu.
“Nani yupo nyuma ya kikundi chako?!” Ulsher akawaka. Uso wake haukuwa na tone la utani. Mikono yake yote ilikuwa imeshikilia bunduki yake ndogo kwa ukakamavu.
“Ni Allah!” akajibu Mr. X. “Ni Allah ndiye anafadhili kila kitu. Yeye ambaye tunamwabudu na kumtumikia.”
Ulsher akapiga risasi mbili za mkupuo pembeni ya Mr. X! Mara mwanaume huyo akaanza kukohoa. Akakohoa mfululizo pasipo kukoma. Akashikilia kifua chake akikohoa mno. Kikohozi chake kilikuwa kikavu kikikwangua kifua. Ulsher akamsogelea akitaka kumjulia hali.
Kufumba na kufumbua, Mr. X akampoka bunduki na kumtupia maili mbele kwa teke la kusinya! Kisha akaendelea kukohoa, huku akihangaika na kucheka, mkono wake wenye bunduki akimnyooshea Ulsher. Alipokoma kukohoa akafuta mdomo wake kwa mgongo wa kiganja, alafu akamwambia Ulsher huku akihangaika kuhema kwa nguvu.
“Ok, muda wa kucheza sasa umeshakwisha tutaonana upande wa pili wa dunia!”
Sauti ya risasi mbili ikavuma tah!-tah! Ulsher akatazama mwili wake akiwa ameachama akikagua ni wapi anavuja damu. Mara akamwona Mr. X akidondoka chini na bunduki yake. Kwa mbali akamwona Ras akiwa amebebelea bunduki, basi akajikuta anatabasamu.
“Upo sawa?” Ras akauliza akiukagua mwili wa Mr. X.
“Nipo sawa,” Ulsher akajibu asiamini anachokiongea.
“Ameshakufa, twende zetu kabla muda haujatutupa mkono.”
“Vipi Mou, anaendeleaje?”
“Twende kwanza. Si salama kukaa hapa!”
Wakaondoka zao wakiwa wameshakamilisha kazi waliyotumwa.
***
Sierra Leone, Freetown. Saa kumi ya jioni.
“Kila kitu tayari!” alisema mwanaume mmoja aliyevalia kanzu na baghalasia akimwambia Amadu aliyekutana naye mlangoni. Amadu akarudi ndani na kuwashtua wenzake: Chui, Farah, Rasta, Fredy, Thomas na Kone, kwa ishara ya kichwa, wote wakatoka ndani kasoro Ulsher na Rose.
Wanawake hao walikuwa wamevalia kidesturi ya kiislamu wakihifadhi vichwa na miili yao. Walikuwa ndani ya nyumba duni yenye sebule ndogo ndaniye kulikuwa kuna vitu kadhaa; viti vilivyochoka, meza kuukuu na picha za kale.
Huko nje watu walikuwa wengi, haswa wanaume, na wengi wao walikuwa wamevalia kanzu haswa nyeupe na za rangi ya kahawia. Watu wao kwa pamoja walijumuika wakashuka chini mpaka makaburini. Wote walikuwa wanaume.
Dua ikasomwa na mwili ukahifadhiwa kule unapostahili, nyumba ya mwisho ya mwili wa binadamu, kisha watu wakatawanyika wakimuacha mfu yule ardhini peke yake.
Baada ya nusu saa, THE GHOSTS, wakakutana nje ya makazi waliyofikia. Wakaketi nje wakiwa wamezunguka meza ndogo iliyokuwa imekaliwa na chupa za maji. Wakawa wanateta juu ya mustakabali wao.
“Mou ametutoka. Mwanajeshi mmoja kaenda chini,” akasema Amadu. “Roho yake haijaenda bure, wala damu yake haijamwagikia mtoni, bali kwenye shamba la haki na uhuru. Hatutaweza kusahau mchango wake kamwe. Tangu mwanzo alikuwa nami, alikuwa nasi. Hakuwahi kuwa na shaka na mipango yetu, wala kusita kuitekeleza, hakika ni pengo kubwa kinywani.
Na kwa kuenzi yale yote aliyoyafanya, hatuna budi kumaliza alichoshiriki kukianzisha. Kumaliza na kutekeleza yale yote yaliyokuwemo ndani ya makubaliano yetu. Bado tuna watu takribani ishirini wa kuwamaliza. Na ratiba ya kufanya hivyo itatolewa muda si mrefu, ikiambatana pia na watu watakaopewa majukumu hayo.”
Baada ya maongezi hayo wakakubaliana pia kujipapasa mifuko na kutoa chochote walichonacho kama rambirambi. Lakini pia wakaazimia kujenga nyumba ya kisasa kwa ajili ya familia ya Mou.
“Tutakutana siku mbili baada ya msiba kukoma,” Amadu akavunja kikao. Lakini kabla hawajatawanyika, wakasikia sauti za wanawake zikipiga yowe! Na mara sauti kali za risasi zikaanza kurururuma kwa fujo!
“Tumevamiwa!” Kone akatamka kwa uhakika.
Na kweli walikuwa wamevamiwa! Jeshi la Talib wakiambatana na magari manne na kifaru kimoja walikuwa wameshafika eneoni. Walikuwa wamebebelea bunduki ndefu zenye mijazo ya risasi za kumwaga. Walishajiandaa kwa vita.
“Hakikisha hakuna anayetoka hai!” sauti ya Talib ikanguruma toka kwenye simu ya redio.
“Ndio, mkuu!” akaitikia kamanda anayesimamia oparasheni. Alikuwa ameketi kando na dereva wa kifaru. Akabadilisha mawimbi na kuwapa maagizo vibaraka wake.
“Zunguka eneo lote sasa, hakuna kumruhusu mtu yeyote kutoka, si mwanamke wala mtoto!”
Magari yakajigawa na kuzunguka eneo lote. Wanajeshi wakashuka na kuamuru watu wote kukusanyika eneo moja wakiwa wamepiga magoti na kunyoosha mikono juu. Hakutakiwa yeyote kuonekana akiwa amesimama ama kutembea, labda kama amechoka pumzi yake!
****
THE GHOSTS watasalimika?
Sent using
Jamii Forums mobile app