*NJIA NYEMBAMBA -- 30*
ILIPOISHIA
Na kweli walikuwa wamevamiwa! Jeshi la Talib wakiambatana na magari manne na kifaru kimoja walikuwa wameshafika eneoni. Walikuwa wamebebelea bunduki ndefu zenye mijazo ya risasi za kumwaga. Walishajiandaa kwa vita.
“Hakikisha hakuna anayetoka hai!” sauti ya Talib ikanguruma toka kwenye simu ya redio.
“Ndio, mkuu!” akaitikia kamanda anayesimamia oparasheni. Alikuwa ameketi kando na dereva wa kifaru. Akabadilisha mawimbi na kuwapa maagizo vibaraka wake.
“Zunguka eneo lote sasa, hakuna kumruhusu mtu yeyote kutoka, si mwanamke wala mtoto!”
Magari yakajigawa na kuzunguka eneo lote. Wanajeshi wakashuka na kuamuru watu wote kukusanyika eneo moja wakiwa wamepiga magoti na kunyoosha mikono juu. Hakutakiwa yeyote kuonekana akiwa amesimama ama kutembea, labda kama amechoka pumzi yake!
ENDELEA...
"Vipi? Umewaona?" Akauliza kamanda wa oparesheni.
"Hapana, mkuu!" Akajibu mwanajeshi aliyetokea ubavu wa kulia wa nyumba akiwa amebebelea bunduki aina ya SMG.
"Tafuteni! Tafuteni kote!" Kamanda akaamuru. Macho yake yalibeba ujumbe aliokuwa anaumaamisha. Basi watu watano wakajimega upesi na kusambaa kuangazaa, wakazama kwenye nyumba za karibu na wengine wakayatupa macho yao umbali mrefu kama wataona chochote kitu. Lakini mwisho wa siku wakarejea mikono mitupu!
"Hawa lazima watakuwa wanafahamu!" Akasema Kamanda. Akamnyaka mwanamke mmoja na kumtupia mbele, akiwa amemnyooshea bunduki, akamkaripia:
"Wenzenu wapo wapi?!"
Mwanamke yule akiwa analia, akasema hajui. Hata akaapa. Machozi yalikuwa yanamtiririka na uso wake ulikuwa unatia huruma.
"Sijui! Kweli sijui!"
Kamanda yule akatishia kumshindilia risasi mwanamke huyo. Akawatazama na wale wananchi wengine akiwatishia wasipo sema basi atammaliza mwanamke yule mbele ya macho yao, lakini hakukuwa na kitu! Watu walikuwa wameinamisha nyuso zao chini kwa hofu. Wengine walikuwa wanamwaga machozi.
Kamanda akaona zoezi lake halizai matunda, basi akawanyaka na watoto watatu akawaongezea pale mbele, akawalaza chini na kukoki bunduki yake na kisha akapaza sauti kuu akinyooshea mdomo wa bunduki kwenye kichwa cha mtoto mmoja wa kike, kwa makadirio mwenye miaka mitano.
"Nitafunua ubongo wa mtoto huyu punde itakapofika namba tatu tu!"
Mtoto huyu asiye na kosa alikuwa anamwaga machozi na makamasi. Hakuwa anajua kinachoendelea hapa lakini macho yake yalimjuza hali ni mbaya na inatisha! Kuona watu wazima wakilia na hata kuhofia, haikuwa kitu cha mazoea. Mkono mpana wa Kamanda ulikuwa umeminya mkono wake mwembamba kwa nguvu!
Hata wenzake waliokuwa wamesimama kando, wakiwa wameshikiliwa na wanajeshi, nao walikuwa wanalia wakiita wazazi wao wawasaidie dhidi ya kikombe kile. Wakiwa ndani ya nguo zao kuukuu, wakatia huruma ambayo haikufua dafu kwa wanajeshi waliotumwa hapo kutenda kazi.
"Moja!" Kamanda akahesabu. "Mbili! ... Tat ..."
"Usimuue tafadhali!" Akasimama mwanaume mmoja mweusi aliyevalia shati la njano. Akaamriwa apige magoti chini upesi!
"Ni wakina nani mnawataka?" Akaropoka mwanaume huyo. " ... mie nilikutana na watu fulani wakiwa wanakimbilia kusini. Sijui kama ndiyo hao mwawataka! Tunaomba msituue!"
Kamanda akamuuliza mwanaume huyo juu ya idadi ya watu hao. Baada ya hapo akawaamuru watu wake waelekee huko upesi! Basi magari matatu yaliyopakia wanajeshi , nane kwa idadi, yakaanza safari haraka kwenda kusini.
Wakatembea kwa umbali wa nusu na robo kilometa kabla hawajamuuliza mkulima mmoja juu ya watuhumiwa wao. Wakapata taarifa kuwa walionekana wakielekea magharibi mwa shamba lake.
"Watakuwa wanaelekea kuikuta barabara ya lami!" Akasema mwanajeshi mmoja.
Lakini hawataweza kuwasaka watu wao kwa kutumia magari kwani iliwalazimu wazame ndani ya msitu kama walivyofanya watu wanaowasaka. Huenda pia watu hao wakawa wamejificha msituni humo.
Wakashuka na kuanza kukimbia wakizama ndani ya msitu, wakitumia taarifa za watu waliokuwa wanawauliza njiani. Lakini kadiri walivyokuwa wakizama ndani ya msitu, watu wakawa hawaonekani tena. Sasa wakawa wanafanya kufuatilia alama za viatu, na ishara za kulala kwa majani.
Baada ya muda mchache wakafika karibia na mtoni.
"Itabidi tuvuke!" Akasema mmoja.
"Hapana, ngoja kwanza ..." akatahadharisha mwingine. "Hawa watu hawajavuka mto!"
"Umejuaje?"
"Mbona hapa karibia na mto hatujaona tena alama zao za viatu na wakati ndiyo sehemu mbichi?"
"Vipi kama zitakuwa zimefutwa na maji ya mto?"
"Tokea kule?" Akanyooshea kidole kwenye kingo ya mbali ya mto.
"Sasa?"
"Ni aidha kushoto ama kulia kwetu ndipo wameelekea."
Mara ghafla, umbali wa kama hatua thelathini kule ng'ambo ya mto, wakaona kitu kikubwa kama gogo kikitumbukia mtoni! Haraka wakanyooshea bunduki zao huko.
Akili na macho yao yakakazia eneo hilo. Haikupita muda mrefu, kwa mbele kidogo, jiwe kubwa nalo likatumbukia mtoni! Sasa wanajeshi hawa wakawa wamekubaliana kuwa kutakuwa kuna jambo kule.
Wakiwa kwenye buwazo hilo, kufumba na kumbua, mara wakashangaa wamevamiwa tokea nyuma na watu waliovalia majani.
Hawakuwa na nafasi yoyote ya kupambana. Bunduki zikaangukia chini!
***
"Mkuu, ni muda sasa umepita, wamekuambia kitu?" Akauliza mwanajeshi mmoja aliyemfuata Kamanda kwenye gari.
Kamanda akafanya jitihada za mawasiliano na wanaume wake aliowatuma akitumia simu ya redio.
"Tumekaa kwa muda mrefu sasa na hawa watu wasio na matumizi! Mpo wapi? Mmefanikisha? Ova!"
"Tumefanikiwa, kamanda. Sasa tunarejea, ova!"
Sauti ikamjibu na mara mawasiliano yakakatwa. Kamanda akatabasamu.
"Hatimaye mambo yamekwisha!" Akaangua kicheko kikubwa akionyesha mpaka magego.
***
"Kama ulivyosema, bado wapo ndani ya kijiji."
"Nilijua hilo, sasa hatuwezi tukaondoka tukawaacha wananchi katika hali ile. Ni lazima tufanye kitu."
"Yah! Inabidi tukawaokoe, na kuwamaliza wale mbwa waTalib!"
"Ndio! Lakini inabidi tuwe na mpango, la sivyo tutaharibu kila kitu. Lazima wananchi wawe salama kwenye oparesheni hii!"
"Ndio! Ni lazima tuhakikishe hilo."
***
Ikapita robo saa.
Kamanda ndani ya gari alikuwa tayari amesinzia. Mdomo wake alikuwa ameuachama kama shimo la mdako. Ndani ya gari alikuwa mwenyewe wakati wafuasi wake wakiwa wamesimama huko na wananchi wasio na hatia.
"Piga magoti!" Mwanajeshi alimkaripia bibi mateka aliyekuwa anayumba kwa kuchoka miguu.
"Tafadhali naomba nilale, miguu inaniuma sana mwanangu," akajitetea bibi yule akitazama kwa sura ya huruma. Macho yake yalikuwa mekundu, akionyesha ni mdhaifu.
"Hakuna kulala!" Akakaripia mwanajeshi. "Nimesema piga magoti!"
Bibi akajitahidi kupiga magoti akiwa anahangaika kwa kushindwa kuhimili. Mwanajeshi akakasirika, akapiga hatua zake kubwa kumfuata bibi huyo, lakini kabla hajamfanya kitu, akasikia sauti ikimuamuru:
"Weka bunduki chini, nyosha mikono juu!"
Kutazama, akamwona Amadu akiwa amemkaba Kamanda na kumminyia mdomo wa bunduki kichwani.
"Wote weka silaha chini kabla sijatoboa kichwa cha bosi wenu!" Amadu akanguruma. Wanajeshi wale wakatazamana. Pengine walikuwa wanafikiria kufanya jambo. Lakini mara wenzake na Amadu wakatokea wakiwa wamewazingira na huku wakiwanyooshea bunduki. Basi hapo wakawa hawana namna bali kusalimu amri!
Wakaweka silaha chini na kunyoosha makwapa.
THE GHOSTS wakawaruhusu mateka kuondoka. Haraka watu hao wakapotea kana kwamba wanakimbizwa na chatu! THE GHOSTS wakawafunga kamba mateka wao na kuwapaki nyuma ya magari, wakaondoka nao!
"Pengine mpango wetu wa kummaliza Talib unaweza ukawa mrahisi zaidi ya tulivyowaza," akasema Amadu.
Ni nini alikuwa anawaza? Ni wapi wanaelekea?
****
Sent using
Jamii Forums mobile app