*NJIA NYEMBAMBA --- 25*
*Mtunzi: SteveMollel*
Iliwachukua lisaa kumaliza kusoma faili la Guinea, ikawachukua tena lisaa limoja kulipitia la Sierra Leone, wakapumzika. Mambo yalikuwa mengi na hatari zaidi. Kila karatasi waliyoifungua ilikuwa na mambo mazito kuliko ya awali. Mambo yaliyowaacha mdomo wazi.
Kama kuna somo kuu walilolipata kwa kupitia nyaraka hizo, basi ni kutoamini yale tu macho yako yanachoona. Ulimwengu ni zaidi ya hapo. Kuna mambo mengi yapo ardhini, kama usiposhika jembe ukalima basi maisha yako yote utaishia kusema dunia ni milima na mabonde.
Walikunywa kahawa nyepesi wakati wakingojea maakuli jikoni yaliyokuwa yanaandaliwa na mkono wa Rose. Walisindikiza subira yao kwa soga za hapa na pale, walipomaliza kula wakaendelea na zoezi.
Simu ya Kone iliita, ila hakuna aliyetambua kwani ilikuwa imewekwa mfumo wa kimya. Si chini ya mara tano simu hiyo iliita. Kone alikuja kulitambua hilo baadae baada ya kumaliza kupitia kila jambo mafailini. Alikuwa ni mkewe amuita.
Alijaribu kumtafuta, salio likawa halijitoshelezi. Njia pekee aliyoiona sahihi ikawa ni kuondoka kwenda nyumbani.
"Inanipasa niende," alimwambia Rose.
"Kwahiyo vipi sasa?" Rose akauliza. "Tunaamua nini juu ya haya?" Alinyooshea mkono wake kwenye mafaili.
"Tutakuja kuongea baadae, Rose."
"Una uhakika tunaweza tukaongea baadae? Muda si rafiki, na sidhani kama Amadu atakuwa na uvumilivu wa kiasi hicho," alisisitizia Rose. Kone akashusha pumzi ndefu.
Pengine angemwambia mwanamke huyo juu ya mkewe, angemuelewa. Ila hakutaka kufanya hivyo, aliweka siri. Alipima hoja ya Rose akaona ina mashiko. Hakukuwa na muda wa kusubiri tena, basi akajikuta anaamua kuketi. Kama moto basi ni moto na si vuguvugu.
"Unaamua hili?" Aliuliza Kone akimtazama Rose machoni.
"Ndiyo, naamua. Kwa akili zangu zote tena nikiwa timamu," Rose akajibu kwa kujiamini.
"Kila mtu anajua kazi hii ni ngumu na hatari, ila hakuna wa kuifanya zaidi yetu," Kone alisema na kuongezea: "Ni sisi tu ndio tunangojewa ili mapambano yaanze. Kwahiyo kama nikimtaarifu Amadu, basi anaweza kutuambia tuanze mapambano mara moja. Hatujajua angelipendekeza iwe nchi gani ila inaweza ikawa yeyote ile, kwahiyo tunahitaji kujiandaa."
"Ni kweli. Ila huoni kama ingekuwa vizuri kumwambia kwanza Amadu ili basi kama kujiandaa tujiandae kwa mujibu wa mpango? Bila shaka mipango haiwezi kufanana, na hata maandalizi yake pia."
"Umeongea la maana," Amadu akaunga mkono hoja. Alifanya mpango akaongeza salio simuni kisha akamtumia ujumbe Amadu;
"Tumeridhia kufanya kazi."
"Kwanini usimpigie?" Rose akauliza.
"Namba yake haipatikani," Kone akamjibu. "Nimejaribu mara kadhaa nikashindwa kumpata. Ni ujumbe tu ndiyo unaenda. Uzuri anajibu haraka."
Kweli, ndani ya muda mfupi ujumbe unaingia kwenye simu ya Kone. Kone anaufungua na kuusoma kwanguvu Rose asikie.
"Leo, majira ya saa tano usiku, kuna kazi ya kufanya ndani ya Sierra Leone. Ni kazi ya mauaji, takribani kilomita sitini na tano toka yalipo makazi yenu. Mtuhumiwa namba tano."
Walirejelea kwenye mafaili yao kumtazama mtuhumiwa namba tano. Alikuwa ni mwanaume mrefu mpana. Mpenzi wa vileo na kuhudhuria kumbi za starehe.
"Nitakuja kukupitia baadae," akasema Kone. Rose akatikisa kichwa.
"Bila shaka ntakukuta umeshajiandaa," Kone akaongezea. Rose akatikisa tena kichwa. Kone akaaga aende sasa.
***
***
"Hatujampata, mkuu," Alisema Rauli ndani ya kijikao kidogo cha dharura alichoketi na Talib. Walikuwa ikulu ndani ya kajichumba kadogo ka mkutano.
"Rauli," Talib aliita. "Hauna ambacho umefanikiwa kufanya?" Akauliza.
Rauli alipepesa macho mdomo ukibanwa na kigugumizi. "Ki ... kip - o, mkuu."
"Kipi?"
"Nimeweka maajenti wangu mtaani, wanafanya skauti ya kuwatafuta waandamanaji."
"Mpaka sasa wamekamata wangapi?"
"Bado, mkuu. Wana ..."
"Wao wameua maajenti wako wangapi?"
"Watano."
Talib akatabasamu.
"Mkuu, hali si nzuri. Waandamanaji hawa wamekuwa wakimshuku mtu yeyote mgeni ndani ya maeneo yao," alijitetea Rauli.
"Kwahiyo kama ni hivyo?" Talib aliuliza. "Rauli, ndio maana nikakupa hiyo kazi. Ukae na utazame namna ya kuwapoteza watu hawa.
Unavyokuja na kuniambia njia yako imefeli, unadhani nina muda wa kusikiliza huo upuuzi wako?"
Rauli akatikisa kichwa.
"Ulitaka nini ulichokiainisha kwenye mipango yako nikakunyima?"
"Hamna, mkuu."
"Sasa unaniletea porojo gani hapa?"
Talib akasimama. Alipiga kofi meza akifoka:
"Toka! Ukirudi hapa pasipo kuniletea cha maana, nitakumaliza mbwa wewe."
Rauli alisimama, akaenda akitazama chini. Alijihisi vibaya, lakini pia alijihisi amekosewa. Aliminya lips akienenda na kujipaki kwenye gari lake, mercedes benz jeupe toleo la zamani, akatoka ikulu.
Baadae ilikuja kuripotiwa mwanaume huyu amejiua kwa kujinyonga. Ilikuwa ni punde baada ya kuonana na wenzake na kuwaambia hawezi tena kazi. Hawakumuelewa, labda kwasababu hakusema sana.
---
Waswahili husema mzaa janga hula na wa kwao. Na hakika hawakukosea. Msiba haukosi ndugu.
Wakati Sierra Leone kukifukuta, Al Saed anafikishiwa habari mbaya kabisa inayomharibia siku. Anahabarishwa watumishi wake wameuawa, ni Rambo pekee ndiye alibaki hai, tena akiwa majeruhi hohehahe.
Taarifa hizo zilimkuta akiwa anakula chakula cha mchana. Hamu ya kula ilikoma punde akaharakisha hospitali kumuona Rambo apate kumuelezea kilichosibu. Isingelikuwa ni mkuu wa nchi, asingeliruhusiwa kumuona mhanga kwa kuambiwa ampe muda wa mapumziko. Zaidi, uso wake uliwaogopesha wauguzi kwani ulikuwa umefura na kughafirika vya kutosha.
Hatua zake alizotupa zingekufanya umpishe njia pasipo kuombwa.
Alijikuta anapigwa ganzi ya mwili alipomuona Rambo akiwa amejilaza kitandani. Alijihisi mwili umepoteza nguvu, magoti yanagongana. Alipata joto la mwili upesi, akaona nguo zinambana. Alitamani hata kuzivua.
Kwake Rambo kulala kitandani halikuwa jambo dogo hata kidogo, ilikuwa ni ishara ya kushindwa. Ishara ya kuzidiwa. Atafanyaje sasa ilhali wanaume aliowategemea wamalize kazi, wamemalizwa kabla ya kazi?
Uso wote wa Rambo ulikuwa mwekundu, jicho moja lilivimba rangi ya zambarau. Mkono wake wa kuume ulikuwa umevunjwa. Kichwa kilikuwa kimezungushwa plasta nzito kana kwamba mti umeungwa usianguke. Mguu wa kushoto haukuwepo, wa kulia ukiwa umevunjika.
Alitia imani. Ungeweza sema amekufa.
Al Saed alimsogelea karibu zaidi, akashika kitanda. Aliita kwa sauti ya chini, mara tatu, mara Rambo akafungua jicho, lile lililokuwa na afadhali, la kushoto. Nalo lilikuwa limevijilia damu. Hakumudu kuliangaza kwa muda, akalifumba.
"Mkuu," aliitika kwa shida.
"Nini kimetokea, Rambo?" Al Saed akauliza. "Nini kimewakumba?"
"Tuli ... va- miwa, mkuu," alijibu Rambo kwa shida. Alikohoa mara mbili kisha akaendelea: "Tulipang - a vizuri tu ... vizuri ... Tulipo,anza kusha ... mbulia, mabomu mata...tu ya -liru - shwa mbele yetu." Rambo akaweka kituo. Alivuta kwanza hewa, mara kwa mara akiugulia maumivu.
"Baa ... da ya ha-po, sikumbuki cho-cho-te zaidi ... zaidi ya make - lele ya wenzangu na make... le, le ya risasi. Nasha ... nga .. aa nimefika ... je hapa hai."
Akaweka kituo kirefu.
Ilikuwa ni habari ya kuwahiwa kabla hujawahi; pale ujanja wako unapokuwa ujinga mbele ya adui. Kikosi cha wanaume hawa, wakina Rambo, walitanguliwa hatua tatu mbele kimaamuzi. Kila walichokuwa wanafanya kilishatarajiwa tayari, na kikapangiwa namna ya kukikomesha.
Wakiwa wamepashwa habari na mateka wao, kiongozi wa kamati ya ulinzi na mjumbe wake, walivamia maeneo yale matatu elekezi. Walipovamia eneo moja, hawakukuta kitu, na la pili pia, hivyo basi wakajua la tatu ndilo lenyewe hivyo nguvu zikatiwa hapo.
Ambacho hawakukijua ni kwamba, maadui zao nao walikuwa wameshalitambua hilo, kwani taarifa za uvamizi wa maeneo mawili ya nyuma walishazipata toka kwa maajenti wao. Hivyo basi, wakajipanga.
Wakina Rambo walikuta eneo kimya kama vile hamna watu. Walikuja eneoni hapo kwa miguu. Walisogelea jengo hilo kwa kunyatia, na kwa uangalifu.
Lilikuwa ni jengo la kisasa kubwa la ghorofa, halikuwa limemaliziwa plasta. Kwa nje kulikuwa kuna bustani kubwa likizingira, pamoja na matofali kadhaa.
Rambo na wenzake wakiwa wanasogea, kuna wanaume wanne waliokuwa wanawatazama, wakiwa wamekaa chumba cha juu. Walipofika eneo la karibu zaidi, wanaume wale wakatazamana, kisha wakapeana ishara. Mmoja akatoa mabomu kwenye kamfuko cheusi kalichokuwepo kando. Akayachomoa pini na kuyarusha kwa mkupuo.
Yakiwa hewani, wengine wakashikilia bunduki zao tayari kwa mashambulizi.
Kufumba na kufumbua, mabomu yakatua miguuni mwa wakina Rambo. Hakika wakatoa macho kwa mshangao. Roho zilikuwa mikononi sasa. Walikutana uso kwa uso na kifo.
"Kimbia!" Mmoja wao alifoka. Kila mtu alijaribu kujiepusha na adha ya kifo kwa kutumia miguuye, ila hawakufika hata hatua mbili, mabomu yakajitusu na kuwarushia mbali.
Kilichomnusuru Rambo, ni kutulia tuli baada mlipuko huo, alikuwa amepoteza fahamu. Wenzake waliokuwa wanagugumia kwa maumivu, walishushiwa mvua ya risasi, na kisha wahusika wakahepa.
Ni baada ya masaa matatu, ndipo wakaja waokozi na kubeba miili ya Rambo na wenzake. Walikuwa ni wanajeshi watano waliobebelea silaha. Walipekua nyumba wakapata maganda lukuki ya risasi.
Walidhani Rambo amekufa pia. Isingekuwa hekima za mfanyakazi wa mochwari, basi alikuwa anatiwa kwenye jokofu kama wenzake waliotiwa humo pasipo kupata huduma yoyote.
***
"Twende basi tukale, mpenzi," Kone alimwambia Fatma aliyekua amejilaza kitandani. Ni majira ya saa mbili usiku sasa na takribani dakika za kutosha.
Macho ya Fatma yalikuwa mekundu. Alilaza kichwa chake juu ya mkono. Alikuwa amegeuzia uso wake ukutani asimwangalie mumewe. Hakutaka kabisa kuongea na mwanaume huyo tokea aliporudi toka kwa Rose.
"Mke wangu, utakaa hivyo mpaka lini? Niambie basi kosa langu ni nini."
"Kone, kama hujui kosa lako, huna haja ya kuomba msamaha," alisema Fatma kwa mara ya kwanza. "We nenda kale, mimi utanikuta hapahapa!"
"Siwezi nikaenda pasipo wewe. Watoto watajisikiaje?"
Kimya.
"Fatma," Kone akaita tena. Aliongea zaidi na zaidi ila Fatma hakusema tena chochote, mwishowe akaamua kwenda kula mwenyewe. Aliwadanganya watoto mama anajisikia vibaya. Watoto walikula wakaenda zao, wakamuacha baba peke yake mezani.
Baada ya muda mfupi, Kone anajipepesa kutafuta simu mfukoni. Hakupata kitu. Alitazama mezani na maeneo ya karibu, napo hakupata kitu. Moja kwa moja akajua atakuwa ameiacha chumbani.
Alijinyanyua akaenda chumbani taratibu. Alimkuta mkewe akiwa anatumia simu hiyo, akipekua ujumbe. Aliishia kumtazama akimngojea amalize. Bado macho ya mwanamke huyo yalikuwa mekundu.
Alimaliza upekuzi, akaiweka simu kando na kugeukia ukutani. Kone hakuichukua simu hiyo, akamtazama mkewe kwa muda wa kama dakika nne pasipo kusema jambo. Alikuwa anatafakari mambo lukuki kichwani.
Alimgusa mkewe bega, akimuita. Fatma hakuitikia.
"Samahani, mke wangu. Nimejua kosa langu. Nilipitiwa, hakika nilisahau kabisa. Ila kesho, naapa, nitakupeleka kwenye ile nyumba ukaione."
"Kesho?" Fatma aliuliza na kisha akaguna. Aligeuza shingo yake akamtazama mumewe. "Unadhani tutakaa hapa mpaka lini? Kila uchwao tuwe tunatoa pesa kulipia nyumba, chakula. Mpaka lini? Uliliona hili halina maana, ukalipuuzia. Umeona ya Guinea na Rose ni ya maana zaidi kuliko familia yako?"
Fatma aliongea kama chiriku. Kone alikaa kimya kusikiliza. Mwanamke huyo alipochoka, akajilalia zake, akimalizia kwa kusema:
"Safari njema ya mauaji."
Kone alishusha pumzi ndefu akiegemeza mgongo wake ukutani. Aliendelea kutafakari mambo kadha wa kadha wakati muda ukisonga. Yalipofika majira ya saa nne, alichukua simu yake akampigia Rose.
"Vipi tayari?"
"Ndio, nakungoja wewe."
"Poa, nakuja."
***
☆Steve