*NJIA NYEMBAMBA -- 27*
*MTUNZI: SteveMollel
*MLENGWA NAMBARI MOJA - GUINEA*
Hatari aliyokuwa amebebelea mikononi na mdomoni mwake ndiyo ilimfanya Sisawo awekwe kwenye orodha. Alitakiwa awe mtu wa kwanza kabisa kuuawa kabla ya mtu mwingine yeyote.
Kwanini? Kwa jicho la tatu mtu huyu hakuwa mwenyewe, bali alikuwa kikundi. Nyuma yake alikuwa na jeshi tiifu lenye mafunzo. Anaweza akaleta machafuko muda wowote.
Hivyo basi, kumuangamiza mwanaume huyu, ni kung'oa mbegu hatari ya vita na kupandikiza mazingira mazuri ya amani. Na kuhakikisha hilo linatendeka, Amadu pamoja na Chui wakalivalia njuga.
Yalikuwa ni majira ya jioni tulivu kabisa, na wateja walikuwa wanaingia ndani ya hoteli ndogo ya kitalii inayovutia machoni kwa mpangilio wake.
Hoteli hii, milki halali ya Sisawo, ni miongoni mwa hoteli zifanyazo vizuri sana kibiashara ndani ya Guinea. Japokuwa ni ndogo, ilikuwa inapendeza na ni ya gharama mno.
Majira yakisogea sogea kwenda giza, mara gari mercedes benz nyeusi inaingia ndani ya hoteli hii na kupaki. Ilikaa tuli kwa muda wa kama dakika tano, kisha wakashuka wanaume wawili waliovalia kimaridadi kabisa.
Walikuwa wamevalia suti nyeusi na tai rangi ya samawati. Vichwa vyao vilikuwa vimefunikwa na kofia maridhawa zilizoendana na mavazi.
Wakatazamana kisha wakatikisiana vichwa na kuzama ndani ya hoteli walipokomea mahala mahususi pa mgahawa , sakafu ya chini kabisa.
Walipotua kofia zao na kuziweka mezani, ndipo waonekana kumbe wanaume hawa walikuwa Amadu na Chui. Macho yao yalikuwa tulivu yakiambaa ambaa mazingira.
Kulikuwa tulivu sana mgahawani. Watu kadhaa wenye heshima na nafasi zao walikuwa wakijipatia chakula cha maana. Hawakuwa wengi sana, ila kutokana na udogo wa eneo pakaonekana kama vile pamejaa.
Amadu na Chui walikuwa wamekaa kwenye meza ya peke yao, na bado hawakuwa wamehudumiwa.
"Umemuona?" Akauliza Chui.
"Hawezi kuwa hapa muda huu," akajibu Amadu bado akiendelea kusachi eneo kwa macho. "Pengine yupo huko juu. Inabidi tuhakikishe hilo."
Mhudumu akaja: mwanamke mwenye kimo cha wastani aliyevalia nguo ya tamaduni ya kichina yenye vifungo mpaka kooni.
Alitabasamu akiwatazama watejawe aliowakabidhi orodha ya vyakula na vinywaji.
"Samahani kwa kukawia, naweza nikawahudumia?"
Amadu akatabasamu kabla hajajibu:
"Ndio," na kuongezea: "tungependelea utuletee chakula chako bora kabisa ambacho unachodhani tutakifurahia."
Mhudumu akatabasamu zaidi, kisha akaondoka kwenda jikoni.
"Amadu, umejuaje kama tutakipenda chakula chake?" Chui akauliza.
"Itabidi tuvumilie," Amadu akajibu. "Nia ni kumteka tu, kuna mambo nahitaji kuyafahamu toka kwake."
Haikupita muda mrefu mhudumu akarejea akiwa amebebelea sinia kubwa mbili za chakula zilizofunikwa vema. Akalitua mezani.
"Karibuni."
Chakula kilikuwa ni nyama ya kuku iliyookwa, ndizi za kukaanga na za mchuzi, pamoja pia na tambi zilizokuwa zimechanganywa na mboga za majani.
Harufu yake ilikuwa maridhawa na ilivutia walaji.
"Ahsante sana," akasema Amadu akikamata uma na kisu. "Hiki ndicho chakula wakipenda?"
"Ndio," akajibu mhudumu kwa tabasamu.
"Nimeshaanza kukipenda kabla hata sijala ... unajua mimi na mwenzangu hapa ni wageni. Na huko tulipotoka, hatujazoea kuona huduma hivi kwa namna ya haraka.
Bila shaka meneja atakuwepo hapa hapa mgahawani, sio?"
Mhudumu akatabasamu.
"Hapana, ni nidhamu tu ya kazi," akajibu na kuongezea: "Meneja yupo huko juu ofisini kwake ametulia tu."
Amadu akashukuru, mhudumu akaenda zake.
"Ni muhimu sana kutumia njia ya kuepusha hofu kwa watu kama hawa," akasema Amadu. "Watu hawa tayari wameshafundwa. Pale wanapohisi shaka huwa wanatoa taarifa."
"Kweli, ulichofanya ni chema. Sasa tumeshajua Sisawo yupo wapi. Kwahiyo tunamfuata?"
"Tuvute subra kwanza. Hatuna haraka kiasi hiko. Furahia chakula chako, tumelipia."
Walikula wakiendelea na habari zingine kama kawaida, kama wateja wengine. Wakaagiza na vinywaji vya kusindikizia vilivyozidi kutia hamasa mlo wao.
Wakiwa wanaendelea kula, mara wanamuona Sisawo akiwa anashuka ngazi. Alikuwa amevalia gauni la kitamaduni rangi ya kaki pamoja na kofia yake kichwani.
Punde tu alipotokea, wanaume watatu nao wakatokea hatua kama mbili nyuma. Hawa walikuwa wamevalia suti nyeusi na tai nyekundu.
Walikuwa ni walinzi wa Sisawo. Macho yao yalikuwa yanazunguka huku na kule wakitembea kwa ukakamavu.
Sisawo akaonana na msimamizi wa mgahawa, wakateta mambo kadhaa kisha akaenda zake nje akiongozana na walinzi.
Baada tu ya muda kidogo, Amadu na Chui nao kwa pamoja wakasimama wakiacha sahani zao na mabaki hafifu ya chakula, wakaelekea nje wakitembea kwa mwendo wa wastani usiozaa shaka.
Walipotoka tu langoni, wakaona gari la Sisawo likiwa linapita getini kuacha hoteli. Haraka wakakimbilia usafiri wao na kujipaki na kuanza kulifuatilia gari hilo.
Lakini huku hotelini wakaacha shaka!
Mlinzi wa getini alikuwa mwerevu wa kutosha kuhisi saga lililokuwa linaendelea. Aliwaona Amadu na mwenzake wakikimbilia gari lao pindi walipotazama getini, akili yake ikampigia alarm! Mkuu alikuwa anafuatwa.
Haraka akanyanyua mkonga wake wa simu na kutoa taarifa:
"Kuwa makini, kuna gari inawafuatilia."
Mlinzi huyu ni miongoni mwa wapambanaji wa jeshi la Mandinka. Intelijensia yake ilikuwa juu. Macho na akili yake vilikuwa haraka kwenye kufanya maamuzi. Tena maamuzi sahihi.
Taarifa yake ilipokelewa na dereva wa Sisawo ambaye naye akaipeleka mara moja kwenda kwenye kikosi kazi cha ulinzi.
"Kuna nini?" Sisawo akauliza punde simu ilipokatwa.
"Kuna virusi vinatufuatilia nyuma," akajibu dereva. "Ila usijali mkuu, tushawadhibiti."
Sisawo akatazama nyuma.
"Nani anatufuatilia?"
Walikuwa wameingia kwenye barabara kuu hivyo kidogo ilikuwa ngumu kutambua, magari yalikuwa mengi upande wa kulia, kushoto na nyuma.
"Ni mercedes benz nyeusi. Haina plate number," dereva akatoa maelezo. Sisawo akapekua mpaka alipolitia machoni gari hilo.
"Ni mshenzi gani huyu anathubutu kufuata nyayo zangu!" Alisema kwa majivuni akitazama walinzi wake waliokaa kushoto na kulia yake.
"Hamna wengine zaidi ya wafulani tu!" Akasema mlinzi mmoja. Sisawo akatabasamu.
"Naona wanakiharakia kifo chao!"
Akakunja ngumi akisaga meno.
"Hakikisha mnaua wote! Nyama yao watakula mbwa wangu!"
Gari likazidi kusogea. Kama dakika kumi na tano mbele yakatokea magari mengine mawili nyuma ya gari la wakina Amadu na Chui.
Magari haya yalikuwa ni Ford ranger pick up. Rangize nyeusi. Nyuma yalikuwa yamepakia wanaume watatu watatu kila moja. Wanaume hawa walikuwa wamevalia nguo nyeusi tupu, na kofia za soksi vichwani.
Kwenye sakafu ya gari walikuwa wamelaza bunduki kubwa SMG ambazo huwezi ziona mpaka usogelee gari hizo kwa ukaribu.
Walisogea zaidi na zaidi, tageti yao ikiwa gari walilopo Amadu na Chui. Lakini kabla hawajakamilisha, Chui anagundua huo mchezo. Akamtaarifu Amadu.
"Tazama hizo gari mbili, nahisi zinatufuata."
Macho ya Chui yaliyokuwa yanatazama saiti mira yaliendelea kukodolea hapo kwa umakini. Akaona magari hayo yakijigawa, moja likienda kushoto na lingine kulia.
Akampasha taarifa hiyo Amadu.
"Weka silaha yako karibu," Amadu akasema kisha akakanyaga mafuta. Gari likakimbia zaidi. Huku nyuma napo, magari yale mawili yakachochea mwendo.
"Shikilia vizuri!" Amadu alimwambia Chui. Haraka akaanza kuyakwepa magari mengine kwa mbele akilifuata lile gari lililombebelea Sisawo.
Sasa ukawa ni mfukuzano wa hatari. Magari yalikimbizwa kama wehu.
Kwa ustadi wa hali ya juu, Amadu akayakwepa magari mbele yake pasipo kupunguza mwendokasi. Ni punde tu akawa karibu na tageti yake, Sisawo!
Kufumba na kufumbua wanaume wawili wakachomoza kwenye madirisha ya gari la Sisawo, wakaanza kumiminia risasi kushambulia gari la wakina Amadu. Risasi kama njugu!
Amadu akajitahidi sana kumudu chombo. Alikipeleka kando na kando kukwepa risasi wakiinamisha vichwa vyao chini. Magari yaliyokuwepo nyuma yao yakatwangwa risasi na mara ajali kubwa ikatokea.
Magari takribani nane yaligongana na kuharibika vibaya mno. Ajali hii ikabloku njia kwa wafuasi wa Sisawo waliokuwa wamejipaki kwenye Ford Ranger. Hilo likawapa ahueni wakina Amadu.
"Chui, maliza sasa!" Amadu akapaza sauti. Upesi, Chui akafungua mlango wa gari alafu akachomoza kwa chini akiwa amebebelea bunduki yake ndogo.
Akafyatua risasi tatu tu kisha akajirudisha ndani na kufunga mlango upesi.
Bado gari lilikuwa linayumbayumba, lakini risasi za Chui hazikwenda kombo. Zikapasua vichwa vya wanaume wale waliokuwa wanamimina risasi na kuwaacha wafu.
"Sasa imebaki kazi moja!" Akasema Amadu. Hakukuwa tena na pingamizi mbele yake. Akakanyaga mafuta barabara na kuisogelea kabisa gari la Sisawo.
Magari yote yalikuwa kwenye mwendokasi mkali mno. Lakini Sisawo bado hakuona kama inatosha.
"Kimbiza! Kimbiza!" Akasema akimbamiza dereva makofi.
Moyo wake ulikuwa unaenda mbio akiogopa kifo. Alikuwa anageuza kichwa chake mara kwa mara kutazama wanaomkimbiza. Roho ilikuwa inamuuma kuona anakaribiwa.
Kufumba na kufumbua, kama miujiza, Amadu analifikia gari la Sisawo. Na pasipo kuchelewesha muda, akalipush kwa nyuma ubavuni mwa gari hilo. Gari likapoteza mwelekeo!
Liliserereka na kisha likajasimama mbele ya gari la wakina Amadu, likikaa kiubavu. Sisawo akatoa macho kama dafu akistaajabu namna gari la wakina Amadu linavyowajongea kwa kasi.
Tahamaki, wakasombwa na kupaishwa juu wakibiringita hewani!
Kwa haraka ya upepo, Amadu akachomoza dirishani mwa gari, akalenga uvungu wa gari la Sisawo lililokuwa hewani. Alipiga risasi tatu akilenga tanki la mafuta.
Mara punde, gari likalipuka huko juu kwa juu. Amadu akakwepa mabaki yaliyokuwa yanaanguka wakiwa wanaendelea kutimka.
Misheni ikawa imefanikiwa! Sisawo hakubakia hata jivu, yeye pamoja na dereva wake.
Amadu aliacha njia kuu akashika njia za kuchepukia ambazo alidumu nazo kwa muda mfupi kabla hawajabadili gari kwa kukwapua lingine.
Wakaongoza njia mpaka nje kabisa ya jiji walipoachana na gari na kutembea kwa miguu.
Walitembea kwa ukakamavu wakihakikisha wapo salama na hamna mtu aliyewaona pindi wanatekeleza gari.
Baada ya mwendo mdogo, wakaona magari mawili yanakuja kwenye uelekeo wao. Basi haraka wakajificha kwenye mojawapo ya chaka. Wakatulia kimya wakitazama kwa umakini.
Magari hayo yalipita yakitembea taratibu. Yalikuwa ndiyo yale yale, Ford Ranger ya wafuasi wa Sisawo. Wanaume walikuwa wamebebelea bunduki zao mikononi wakitupa macho yao haswa.
Mara,
"Wale pale!" Akasema mwanaume mmoja akinyooshea kidole kwenye chaka.
***
☆Steve
Sent using
Jamii Forums mobile app