*Njia nyembamba 08*
*Mtunzi: SteveMollel
Masaa mawili mbele:
Tayari Amadu na wenzake walikuwa wamemhamishia makazi mama yake Chui kwa kumtafuta nyumba bora zaidi tofauti na pale pa awali. Walimuachia pesa za kujikimu na kisha wao wakatafuta mahala pengine pa kupanga mambo yao wakiwa mkononi na pesa za kutosha.
Walikuwa ndani ya gari Toyota Landcruiser yenye vioo vyeusi. Walijongea na gari lao hilo mpaka kwenye fukwe ya bahari ya Atlantiki, huko wakaona ndio salama zaidi wakashuka wakipunga upepo huku wakipanga ya kupanga. Ni wapi watapata silaha, alafu mengine yafuate: wapi waanze napo kuijeruhi serikali dhalimu iliyopo madarakani, hayo ndiyo yalikuwa ya kujadili. Kulikuwa ni patulivu na watu kadhaa wakiwa wanaoga kwenye maji ya bahari walikuwa wanaonekana mbali na uwepo wa THE GHOSTS. Hakukuwa na kitu cha kuhofia kwa muda huo.
“Ni Liberia pekee ndipo tutapata bunduki kwa urahisi,” alishauri Mou. Vita kati ya kundi la waasi la Le tueurs na serikali ya Liberia ambayo ilikuwa inapumulia mashine kwa sasa, ilimfanya Mou aamini silaha zitapatikana huko kwa wepesi. Kutokana na mahusiano waliyokuwa nayo kati ya wao na Le tueurs, basi watapata kile wanachokitaka haswa ukitazamia wana pesa za kutosha. Ila Amadu akatilia hilo jambo walakini:
“Sidhani kama itakuwa rahisi kiasi hiko,” alifungua kauli. “Hakuna anayejua kama Kessy atakuwa ameshawasiliana na hilo kundi juu yetu. Kwenda huko ni hatari zaidi, wanaweza wakatushambulia badala ya kutusadia.”
Ilikuwa ni vema kuchukua tahadhari, na Amadu alikuwa mwepesi mno kwenye hilo.
“Kundi la Le tueurs wanajuana na Kessy. Unakumbuka ile barua niliyokabidhiwa na yule mtu wao kwenda kwa Kessy? – ile barua ya siri? – kwanini ilikuwa ya siri. Kessy hakuwahi kumuonyesha Assessoko maudhui ya ile barua na mwishowe alimuua pia. Kundi la Le tueurs na Kessy wanajuana, na dhamira zao ni moja.”
Maelezo hayo yalimridhisha kila mtu lakini pia yalifungua uwanja mpana zaidi wa kuendelea kujadili ili wapate jibu. Ni wazi hawawezi wakafanya lolote kama wasipokuwa na silaha. Hata kipindi MDR inatafuta madaraka, wadhamini toka nje pamoja pia na majirani walihusika kwa namna moja kuwasambazia silaha za kukamilisha malengo yao.
“Tukavamie kambi ya jeshi.” Alishauri Ulsher. Wanaume wote wakamtazama. Ni kama vile ahwakutegemea kwa shauri kama hlo kutoka kwenye kinywa cha mwanamke.
“Kwanini umeona hilo ni sahihi?” Aliuliza Ussein.
“Kama malengo yetu ni kuidhoofisha na kuiondoa serikali,” alianza kuelezea Ulsher. “basi kuishambulia kambi ya jeshi itakuwa njia nzuri sana ya kurahisisha hilo zoezi. Kwa pamoja tukifanya hivyo, tutakuwa tumepoka silaha zao, tumepunguza wapambanaji wao, na kitawagharimu fedha pia.”
“Ni kweli, ila linahitaji uangalifu sana.” Alitahadharisha Farah.
“Kila tunachofanya kinahitaji uangalifu sana.” Alisisitiza Amadu. “Kuvamia kambi ya jeshi, haswa kipindi hiki ambacho si muda mrefu tumevamia benki, lahitaji uangalifu wa hali ya juu.”
Wenzake walimuunga mkono. Ni kweli lilikuwa na hatari kubwa, ila lazima walitakiwa walifanye hilo kama kweli wamelenga kupindua nchi. Na kufanya hivyo maana yake kunahitaji mipango, hivyo wakaridhia kwanza kutembea eneo hilo kabla hawajafanya lolote. Kazi hiyo alipewa Farah na Mou. Na tena ilitakiwa itekelezwe usiku wa siku hiyo!
Masaa saba mbele:
Gari la THE GHOSTS, Toyota Landcruiser lilisimama umbali wa kilomita tano tokea ilipo kambi ya jeshi ya Murray Town Barracks. Halikuwa limewashwa taa na lilikuwa likitembea taratibu mno mpaka hapo penye kificho cha miti lilipokomea. Dereva Mou alitumia tu macho yake na mwanga wa mwezi kuliongoza gari. Yeye pamoja na Farah walishuka toka kwenye gari hilo, wakashika njia kufuata kambi. Walitembea kwa tahadhari wakihakikisha hawasikiki wala kuonekana. Kila mtu alikuwa na bunduki ndogo ameishikilia mkononi.
Baada ya kutembea kama mwendo wa kilomita moja, walianza kusikia sauti za watu na vishughuli vya hapa na pale. Walizidi kujongea karibu zaidi, na hivyo sauti zikawa zinazidi kuwa kubwa. Walifika mahali penye ukuta mkubwa mrefu uliokuwa unafumba kambi hiyo, juu ya ukuta huo kulikuwa kuna vyupa vikiwa vimesimamishwa dede. Hapo sasa ikabidi mbadala ufanyike kwani ilikuwa lazima waingie humo ndani wapate kusoma ramani.
Mou aliinama, Farah akakanyaga mgongo wa mwanaume huyo, akasimama kuchungulia ndani.
“Hapa si pazuri. Twende upande wa kusini!” Alisema Farah. Aliona hatari zaidi kuingilia pale kwani ndani yake umbali mfupi walikuwapo wanaume waliovalia gwanda za jeshi wakiwa wamebebelea bunduki ‘SMG’. Walifika upande huo wa kusini wakarudia mtindo walioufanya hapo awali. Farah alipanda na kuvunja vyupa kabla hajakwea ukuta na kumvuta mwenzake kuzama ndani.
Lengo kubwa lilikuwa ni kujua mahala lilipo ghala la silaha, eneo analokaa mkuu wa kambi na hadhi ya usalama.
Ndani ya dakika nane katika kambi hiyo, Mou na Farah walitimiza yote hayo. Kazi ilibakia kwenye kutoka ndani ya kambi hiyo ambayo iliwalazimu mara kwa mara kujificha kukwepa wanadoria na taa kubwa iliyokuwa mnarani ikizunguka muda wote kwenda kulia, kushoto, kati na juu.
Waliufikia ukuta Farah sasa hivi akakamata ukuta wakati Mou akikwea mgongo wake na kumvuta mwenzake kutoka nje. Walitua na kuondoka eneo hilo upesi kufuata gari lao. Walifika wakamkuta mwanajeshi mmoja akiwa hapo na mbwa wake. Alikuwa amefika muda si mrefu na bado hakuwa ametoa taarifa yoyote kwa wenzake.
Sasa ilibidi Farah na Mou wafanye upesi. Si tu kwamba wawahi taarifa kabla haijatolewa, bali pia wawahi kabla pua ya mbwa haijatia nongwa. Walijigawa haraka kwa ukimya kwenda pande tofauti. Baada ya muda mfupi tu, mbwa akaanza kubweka upande alipo Farah. Mwanajeshi alitazama pande hiyo akiinyoshea mdomo wa bunduki. Ghafla akajikuta akisulubiwa na teke kali toka kwa Mou aliyetokea nyuma. Farah naye alichomoza akadaka bunduki ya mwanajeshi huyo kisha amkakandikia nayo mbwa kwa kutumia kitako, mbwa akazirai.
“Amekufa?” Farah aliuliza wakimtazama mwanajeshi aliyekuwa amelala akiachama mdomo. Mou aliweka mgongo wa kiganja chake kifuani mwa mwanajeshi huyo kisha akabinua mdomo wake.
“Sis’kii mapigo ya moyo.”
“Sasa tunafanyaje?”
“Itabidi tumchukue.” Mou alishauri. “Kama tukimuacha hapa, ataonekana mapema na kusababisha tensheni kubwa kambini. Inaweza ikawa tatizo.”
Wasipoteze muda zaidi, walimchukua mwanajeshi huyo na mbwa wake wakayoyoma toka eneo hilo. Walitembea umbali wa kilomita kama tano ama sita, wakamtua mwanajeshi yule kumtupia huko. Walimbeba mbwa tu waliyefika naye mpaka mahali pa siri wanapoishi.
Wakaeleza yale yote waliyopata kuyaona.
Masaa sita baadae: Ikulu ya Guinea.
“Haloo!” Raisi alizungumza. Alikuwa amevalia kanzu ndefu nyeupe pamoja na kofia yake. Alikuwa ameketi mezani alipokuwa anakunywa chai kufukuza kabaridi cha asubuhi. Alipomaliza tu kunywa chai hiyo, hakuwa na subira, akampigia simu Kone kuulizia ni wapi alipofikia kwenye mchakato wake wa kumtia adabu Kessy aliyekiuka makubaliano aliyoyatia na marehemu Assessoko.
“Mbona kimya, Kone?” Raisi aliuliza. Uso wake ulikuwa mkavu na alikuwa ana hamu na majibu. Bahati mbaya kwake, majibu ya Kone hayakumkuna. Bado Kessy alikuwa hai akiokolewa na tukio la benki kuu kukombwa.
“Sasa inakuaje Kone?”
Kone akamuelezea raisi wake huyo yale aliyoyapanga na Rose, lakini pia juhudi zake za kuwatafuta Amadu na wenzake ili wasaidiane kutimiza adhma.
“Sawa, nimekuelewa. Ila pia kuna jambo ningependa kukushirikisha,” alisema Raisi kisha akavuta pumzi. “Jambo hili ni nyeti na kubwa, Kone. Nisingependa kuliongelea simuni. Panda ndege uje Guinea sasa hivi.”
Kone alitii agizo la raisi wake, alikata tiketi upesi aende Guinea. Kwenye uwanja wa ndege kulikuwa kuna ukaguzi mkubwa sana huku picha za wakina Amadu zikiwa zimebandikwa kila hapa na pale. Ila mwishowe baada ya ukaguzi mwingi, Kone alipanda ndege na baada tu ya muda usiozidi masaa matano akawa amefika Guinea, ikulu, kuonana na Raisi.
Mke wa Raisi aliwapa faragha, wakiwa wamekaa kwenye kibaraza wakiwatazama wanajeshi wanaozungukazunguka na bunduki zao, Raisi alisafisha koo lake akasema:
“Kone kuna jambo limenifikia mezani jana jioni. Mpaka sasa nimekosa kujua ni uamuzi upi niufanye?”
“Ni kuhusu Guinea ama Sierra?” Kone aliuliza.
“Ni kuhusu Sierra!” Akajibu Raisi. Hapo Kone akavutiwa zaidi. Ni kipi hicho Raisi wake alichomtolea Sierra na kumuitia pale haraka vile? Ni kipi hicho tena Raisi wake anachakusema kuhusu Sierra na si nchi yake, Guinea?
Moyo wake ulianza tu kwenda mbio. Hakujua kwanini.
***
☆Steve