Njia nyembamba -- 06
Mtunzi: Stevie Mollel
Ndani ya nyumba kubwa ya saruji yenye ukubwa wa kati, bati chakavu lenye kutu na madirisha yasiyo na pazia, walikuwemo wamekaa Amadu, Chui, Ussein, Farah, Mou na Ulsher juu ya mkeka wenye michoro hafifu na majeraha kadhaa. Walikuwa wamekaa wakitengeneza mtindo wa duara, na katikati yao ilikuwa imeketi sinia kubwa la bati limejaa wali pomoni. Kila mtu alikuwa anajishughulisha na kula akitumia mkono wake kama kijiko. Baada ya maudhui ya sinia kupungua kwa kiasi cha nusu, Chui alifungua jamvi la maongezi akiuliza;
“Mnakumbuka siku ile MDR walivyotapakaa mitaa ya Freetown baada ya kuvamia ikulu?”
Kabla hajajibu mtu yeyote, Chui aliendelea kumwaga maneno kama vile kajibiwa na kuruhusiwa aendelee;
“Kuna mzee jirani yetu kila siku analalamika, duka lake lilivamiwa na kukombwa karibia duka zima, si pesa, si bidhaa. Yani amekuwa ombaomba ghafula!”
Amadu alitikisa kichwa chake huku akitafuna. Mou kabla hajameza alichokuwa anatafuna alidaka mada;
“Washenzi sana wale. Sasa walikuwa wanaonyesha picha gani kwa wananchi wanaoenda kuwatawala?”
Ulsher akajiweka madani kwa kuuliza,
“Nani kasema MDR ni kundi la ukombozi?” Kabla wengine hawajafungua midomo, aliendelea kulonga, “Ni genge tu la wahuni waliojivika ngozi ya kudai ukombozi lakini nyuma ya mapazia wanaendeshwa na uroho wa madaraka. Makundi mengi ya waasi Afrika yanatumia mifadhaiko ya wananchi na ukosefu wao wa matumaini kwa serikali yao kama ngazi ya kutimiza adhma yao. Wanabaka wanawake, wanaua watoto, wengine wanawaingiza watoto kwenye uwanja wa vita huku wakiwapumbaza na madawa ya kulevya, vile vile wanaua watu wasio na hatia, unategemea mtu au kikundi cha namna hiyo kibadilike kitakaposhika madaraka?”
“Sawa mwanafalsafa.” Chui alidakia, wote wakacheka, “Sasa nini kifanyike? Je tuuache utawala wa General Kessy?”
“Hapana.” Ulsher alijibu, “Kuuacha utawala wa kidhalimu na kimabavu wa General Kessy ni jambo lisilofichika kwamba litawagharimu sana wana Sierra Leone, hatuna budi kuuondoa kwa gharama yoyote ile.”
“Lakini unapinga kundi la waasi, sasa tunafanyeje?” Chui aliuliza.
“Kweli napinga makundi ya waasi,” Ulsher alijibu, “lakini hili la kwetu si la waasi. Hatutaasi misingi ya haki za binadamu wala amani ya wananchi. Hatutajificha kwenye kibanzi cha ukombozi wa uongo, bali ukweli.”
“Upo sahihi.” Amadu naye akatia neno, “Kumuacha mtu msaliti kama General Kessy ni dhambi tutakayoshindwa kuitolea ufafanuzi mbele ya Mungu. Kama aliweza kumsaliti mtu aliyemfikisha pale kwa gharama kubwa mwishowe akamtoa sadaka ili apate uongozi, huyo ni mtu hatari. Hawezi kushindwa kuwasaliti wana Sierra kwa mlengo wake binafsi. Ila kuna jambo sasa naanza kulipatia mashaka. Mnakumbuka siku ile tulienda kuchukua silaha Liberia?”
“Ndio.”
“Ile siku nilikabidhiwa barua nipeleke kwa General Kessy. Nilikatazwa kabisa nisiifungue huko njiani na nisimpe mtu yeyote bali General. Kwa utaratibu wetu nilitegemea ule ujumbe ambao upo kwenye barua ungekuja kuanishwa mbele yetu, lakini mpaka tunaondoka ule ujumbe ulibakia kuwa siri, sijui ulibeba ajenda gani ambao hatukutakiwa kuufahamu?”
“Mmmh … kutakuwa na jambo.” Ussein alipata shaka, “Nadhani tutajua kinachoendelea baada ya kuona ni maamuzi gani atakayochukua General Kessy kwenye hili vuguvugu la Liberia.”
“Kweli.” Wote walikubali kilichosemwa. Mara mlango wa sebule ulifunguliwa akaingia mama mmoja mzee, alikuwa kajivika baibui na kuacha uso pekee ambao ulikuwa unafanana na uso wa Chui mno, kwa mtu anayemfahamu Chui hawezi akapata shida kubashiri kwamba yule alikuwa mamaye.
“Amir!” Mama aliita jina halisi la mwanae, Chui akamtizama mama na kuitikia,
“Naam.”
“Picha zenu zimebandikwa jiji zima la Freetown, mnatafutwa na serikali! … Mungu wangu, mwanangu unaenda kunyongwa!” mama alilia. Chui alitizamana na wenzake pasipo kusema kitu. Mama akaendelea kunena;
“Sasa utaendaje kutafuta pesa kwa ajili ya familia na unatafutwa hivyo? Je majirani hawatosema kama upo hapa ili wapate pesa?”
Chui alinyanyuka akamtoa mama yake kuelekea ndani. Baada ya dakika kadhaa, alirudi mwenyewe, alishika kiuno akashusha pumzi ndefu.
“Sasa tunafanyeje?”
“Kaa chini kwanza.” Amadu alimtaka Chui. Chui alikaa akamtizama Amadu.
“Kitu ambacho mama yako amekuambia ni kitu ambacho tulikuwa tunakitegemea, hakuna haja ya kuogofya. Ni dhahiri MDR wangetutafuta kwa njia yoyote ile. Hapa cha kufanya ni kupanga tujue tunakabili vipi hii hali. Tujue wapi tunatoa pesa, na tufanye uwezekano wa kutoka hili eneo haraka. Kuna yeyote mwenye wazo?” Amadu aliuliza kisha akapepesa macho yake kutizama wenzake, hakuna yeyote aliyesema kitu. Basi Amadu akaendelea kunena;
“Mimi nina wazo nini tufanye. Na hilo wazo langu litakuwa ni kupiga ndege wawili kwa wakati mmoja, ila lataka utayari.”
“Amadu, unatuuliza tena kuhusu utayari?” Mou alishangaa. “Sidhani kama kuna ambaye hayupo tayari mpaka saa hii. Yupo?” Mou alitizama wenzake, wote wakajibu;
“Hayupo!”
Amadu akaendelea kutema maneno;
“Wazo langu ni kwenda kuvamia benki kuu ya Sierra Leone. Tunaenda na kubeba pesa za kutosha kukimu mahitaji ya mama yako, na pia kununulia silaha za kufanya mambo yetu. Tutalenga ndege wawili kivipi? Kwanza tutalenga ndege wa kutimiza mahitaji yetu, pili tutalenga ndege wa kudhoofisha serikali ya General Kessy kwa kuiachia hasara kubwa. Mnaonaje?”
Walitizama kwa sekunde kadhaa chini ya tano, Chui akawa wa kwanza kujibu;
“Naunga mkono.”
Wengine wakafuatia; “Tunaunga mkono.”
Waligusanisha ngumi zao, wakatabasamu.
“Sasa inabidi tuwe na mipango madhubuti ya kufanya hilo jambo, maana si dogo ni kubwa.”
“Kweli, Amadu.” Farah alisema, “Inatakiwa tupange kuanzia kutoka hapa mpaka tutakapotoka ndani ya benki. Kila kitu kiwe kimepangwa na si kuendeshwa kwa bahati.”
“Ni kweli.” Amadu alikubali, “Naomba nifanye hiyo kazi ya kupanga kila kitu. Kuna mjomba wangu anaishi hapa Freetown, ni mhandisi na amehusika sana kwenye kazi ya kuujenga hili jiji tokea kitambo, waziri wa ujenzi alikuwa anampa fursa sana kwakuwa alikuwa ni jamaa yake. Anajua majengo na kila barabara ya huu mji kuanzia barabara za juu mpaka za chini. Atatusaidia sana katika hili.”
“Sawa, basi utatutaarifu. Au mnaonaje?” Ussein aliuliza wengine, hakuna ambaye alipinga, wakawa wamepeana makubaliano katika hilo. Chakula kilikuwa kimekwisha, Ulsher alinyanyuka akatoa sinia kulipeleka jikoni, akiwa huko anaosha sinia, alisikia redio ikiruruma. Ilikuwa ni redio ya taifa maana ndiyo pekee iliyobakizwa wakati zingine zikiwa zimezuiwa kutangaza. Ulsher aliacha kukosha chombo akatega sikio apate kusikia. Sauti ya mtangazaji ilisema;
“Muda si mrefu tutajiunga kwa matangazo ya moja kwa moja toka kwa mheshimiwa mkuu wa nchi, amiri jeshi mkuu. Leo hii atatangaza wizara zake na mgawanyo wa majukumu. Hakikisha hukosi tukio hili la kihistoria.” Baada ya hiyo kauli ilifuatia wimbo wa taifa. Ulsher alikosha chombo haraka akabeba redio na kuipeleka sebuleni walipo wenzake. Wote wakatega masikio kusikiliza. Baada ya punde sauti ya General Kessy ilisikika kwenye spika za redio ikisalima wananchi, baada ya hiyo salamu akasema dhamira ya maongezi yake kwa wananchi kuwa ni kutangaza wizara zake na watu watakaozisimamia. Alianisha wizara mbili tu: ulinzi na maliasili, sekta zingine akasema zitaingizwa humo humo ndani ya hizo mbili. Mkuu wa wizara ya ulinzi, akatajwa ni General Talib Awadh na wa Maliasili akatajwa General Mohammed Emmo.
Bada ya hotuba ya mkuu wa nchi kumalizika, mjadala ukazuka miongoni mwa wakina Amadu.
“Ana akili kweli huyu mzee, yani anampa wizara Talib? Talib kweli? Hata kusoma na kuandika hajui!” Farah alisema kwa tambo za utani.
“Cha kushangaza wizara zipo mbili tu, uliona wapi? Na wizara zenyewe, moja ya kumlinda yeye, ulinzi, na nyingine ya kunyonya maliasili za nchi. Hajataja vipaumbele vyake kama serikali, hajatuambia ni kivipi wizara kama ya elimu, fedha, mambo ya nje vinaingiaje kwenye hizo alizotaja.” Ulsher alitanabahi. Amadu naye akatupia yake;
“Utakuwa ulifanya makosa sana kama ulitegemea mtu ambaye aliacha shule mapema sana tokea utoto wake awe na akili kama hiyo. General Kessy hana ufahamu wowote kwenye mambo ya utawala. Anachojua yeye ni kushika mitutu. Yani ameshindwa hata kutafuta wataalamu, wasomi na wabobezi wamshauri?”
Amadu aliweka kituo. Kisha akaendelea,
“Ila kwetu ni faraja. Kuwaweka watu hao kama watu wake wa utawala kunazidi kutupanulia na kutuwekea wazi udhaifu wa serikali hii, itatusaidia kutimiza malengo yetu.”
“Kweli.” Mou aliwajibia wenzake.
********
Raisi wa Guinea alikuwa amekaa kwenye bustani ya ikulu pamoja na mwanaume mmoja mweusi aliyenyoa mtindo wa panki. Raisi alikuwa amevalia gauni kubwa jeupe la kitamaduni wakati mwenzake akiwa ameficha uchi wake na suti nyeusi. Mbele yao kulikuwepo na ka-meza kadogo ka-mbao kakiwa kamekaliwa na chupa ya maji ya kunywa ikiwa na glasi mbili pembeni. Nyuma yao hatua tano, alikuwepo amesimama mwanajeshi akiwa kabebelea bunduki kubwa, kazi yake ilikuwa kutizama huku na kule uso akiwa kaukunja kama vile amekosana na mtu.
“Rafiki yangu Kone, nimeumia sana.” Raisi alisema huku akitikisa kichwa, “Nimepata hasara sana juu ya Sierra Leone lakini mwishowe nimeambulia patupu. Wanajeshi wangu wamekufa, baadhi ya vifaa vyangu havijarudi, aisee!”
“Pole sana, mheshimiwa raisi. Unaonaje kama ukianzisha vita naye, najua hana msaada wowote, ni sisi ndio alikuwa anatutegemea.”
“Hapana, Kone. Siwezi kuanzisha vita kwa sasa.”
“Kwanini?”
“Kumbuka imebakia miezi michache kabla hatujaanza mchakato wa uchaguzi mkuu. Endapo nikianzisha vita nitakuwa najipalia makaa ya kupoteza uchaguzi kwa jambo ambalo halitakuwa na mantiki mbele ya macho ya wananchi. Nitamaliza pesa yote ya uchaguzi. Inabidi niwe na njia mbadala mbali na hiyo.”
“Nimekuelewa mheshimiwa. Unaonaje kama tukichochea vita ya wenyewe kwa wenyewe alafu sisi tukautumia huo mwanya kufanya yetu?”
“Tunachocheaje sasa kitu kama hiko na kundi lenyewe la waasi ndilo hilo limeshika dola?”
“Mheshishimiwa, kuna njia.”
Kone alisema kwa kujiamini. Alikunywa maji yaliyokuwepo kwenye glasi yake kisha akamtizama raisi.
“Kuna wafuasi watano wa MDR walioasi kundi lao. Picha zao zimebandikwa maeneo mbalimbali ya jiji la Freetown wanatafutwa kwa hali na mali. Unaonaje kama tukiwekeza kwao?”
“Kone, unaamini vipi kama hao watu wanaweza kazi mpaka kufikia hatua ya kuwekeza kwao?”
“Mheshimiwa raisi, nisingependa nikupe jibu la kukurupuka, wacha nikafanye utafiti kwanza. Ila niliguswa nao sana, juhudi kubwa ya kuwatafuta watu hao ilinipa taswira ya kwamba ni watu hatari. Na najua pia hao watu watakuwa wana hamu ya kulipiza kisasi kwa njia moja ama nyingine kutokana na chochote kile kilichowafanya waasi kundi lao.”
“Sawa, Kone, lakini unajua hili jambo ni sensitive sana. Ningependa ufanye utafiti juu yake kwanza.”
“Sawa, mheshimiwa. Nitalifanya kadiri ya uwezo wangu.”
*******
☆Steve