Njia nyembamba -- (msimu wa pili) 02
Mtunzi: SteveMollel
‘Samahani, siwezi tena kuonana na wewe kwa leo kuna jambo limetukia’
Rose aliachama mdomo kwa kushangazwa. Alimuonyesha Kone huo ujumbe, Kone akavunjika moyo. Alilalama kweli na hakujua nini kiliharibu tena hiyo sherehe. Ila baada ya muda mfupi kwenye mojawapo ya televisheni iliyokuwepo karibu, akapata kushuhudia taarifa ya habari: kambi ya jeshi imevamiwa na kuibiwa silaha!
Alijikuta anatikisa kichwa chake akasonya.
“Tutakuwa tunafanya kazi ya ubuyu kila siku. Tuwatafute hawa waasi kwanza!”
Hilo ndilo lilikuwa amuzi la busara kwa muda huo, kuwatafuta THE GHOSTS. Kone alishindwa kabisa kula wala kunywa akiwa hapo. Hakudumu tena muda mrefu kabla hajaagana na Rose kwa kumpatia kiasi fulani cha pesa kisha akaondoka zake kwenda kuweka mipango thabiti ya kuwapata watu anaowataka.
Kichwa chake kiliamini ya kwamba akiwapata hao watu itakuwa njia rahisi na fupi kwenye kutimiza malengo huku ikiacha mikono yao safi toka kwenye umwagaji wa damu.
Kazi yao wao itakuwa ni kuwapa THE GHOSTS silaha na pesa wauawane wana Sierra wenyewe kwa wenyewe, huku wao wakikaa pembeni na kutazama.
Kuna kazi gani nyepesi kama hiyo kwenye kuteka nchi?
Mawazo yake hayo yalimnyima kabisa fursa ya kumuwaza mkewe wala familia yake. Kila taswira ya familia yake ilipokuja kichwani alijipa ahueni ya kwamba amewaachia pesa ya kutosha, hivyo hakuna cha kuhofia. Yeye kama baba tayari ameshatimiza majukumu yake kwahiyo hana lawama za kutupiwa.
Pasipo kufanya hivyo angelikosa usingizi kwasababu nafsi yake ilikuwa inamshutumu kila mara.
***
Rockel Barracks, wasaa wa alasiri.
Umati wa wanajeshi wa Sierra Leone ulikuwa umekusanyika mbele ya kiongozi wao mkuu, bwana Kessy. Kulikuwa ni tulivu mno na wanajeshi walikuwa wamejipanga kwenye mistari iliyonyooka huku wakiwa wamesimama kwa ukakamavu wa hali ya juu.
Kessy alikuwa anatembea kwenda mbele na kurudi nyuma akiwa ameshikilia bunduki ndogo mkono wake wa kulia. Sura yake ilikuwa nyeusi zaidi na iliyokunjamana.
Alikuwa amevalia gwanda za kijeshi yenye kila aina ya cheo. Japokuwa jua lilikuwa limepoteza nguvu yake, lakini bado lilitosha kufanya vyeo hivyo ving’ae na kumetameta kwenye nguo hiyo maridadi.
Kila mtu hapo kiwanjani alikuwa anafahamu ya kwamba Kessy alikuwa amekasirika. Hata kwa mtoto mdogo angelijua hilo. Hakutaka mtu yeyote amsogelee wala kumuongelesha.
Hakutaka mtu yeyote asimame hata mbele yake. Alikuwa anatazama chini akisaga meno, akienda mbele tu na kurudi nyuma, tendo ambalo alikuwa amelifanya kwa muda wa dakika kumi na tano sasa pasipo kukoma.
“Naona mmeshindwa kazi na hamna umuhimu wowote kwangu wala kwa taifa,” alisema kana kwamba hakutaka mtu yeyote amsikie, ila ghafla aligeukia umati wa wanajeshi akapaza sauti:
“Nataka wote waliokuwa zamu ya ulinzi waje hapa mbele!”
Walijongea mbele watu wanne tu, wengine wote walikuwa marehemu kwa kuuwawa siku ya tukio la uvamizi.
Kessy aliwatazama watu hao akibinua mdomo wake. Macho yake yalionyesha hasira iliyochemka ndani yake.
Hakuchukua hata muda wa kufikiria akanyanyua mkono wake uliobebelea silaha na kuwaua wote hao wanne kwa kupasua vichwa vyao na risasi.
“Hii ndiyo dawa ya wazembe!” Alifoka. “Inawezekanaje watu ambao hawafiki hata kumi kwa idadi, wanaingia eneo lenye wanajeshi kiasi hiki wanaiba silaha na kutoka salama?”
Hakuna aliyejibu, na pengine walidhani jibu halikuhitajika.
Kessy alimuita mbele meja wa kambi, akamuuliza swali hilo akitaka majibu ndani ya dakika moja.
“Nataka unielezee, ni kwa namna gani watu wanaingia humu ndani na kuiba silaha pasipo kukamatwa.”
Meja hakuwa na majibu. Mwili wake ulikuwa unatetemeka kwakuwa alifahamu fika kifo kipo karibu naye. Na kweli hakuchukua muda mrefu akatobolewa fuvu la kichwa na risasi moto.
“Si unaona?” Kessy alifyumu. “Ni ushenzi na uzembe!”
Hakuishia hapo kwa meja na waliohusika na zamu, akaendelea kuua na kuua akihusisha wale walio chini ya meja, wasaidizi wake na wasaidizi wake.
Alitengeneza dimbwi la damu akijaza maiti. Zoezi hilo la mauaji lilikuja kukoma pale tu Talib alipomtaka Kessy asifanye zaidi.
“Isingelikuwa nimewaua hawa washenzi, ningelianza na wewe!” Kessy alimwambia Talib akiwa amekunja uso.
“Nikisikia hao washenzi wamefanya tukio lingine tena kabla hujawakamata, kifo chako kitakuwa malipo!”
Aliposema hayo alijiweka ndani ya gari lake, akaondoka akisindikizwa na msafara wenye magari ya kifahari.
Alichomoa simu yake toka mfukoni akampigia mwanaume mmoja aliyemuagiza amletee wanawake wa kutosha Ikulu usiku huo. Baada ya hayo maagizo akaweka simu pembeni akiendelea kuwaza na kuwazua.
Usiku wake ulijaa anasa kwa kunywa na kufanya mapenzi na wanawake zaidi ya watatu kwa lengo la kutafuta pumziko toka kwenye msongo wa mawazo na hasira alizokuwa nazo.
Harufu ya pombe ilitapakaa ndani ya chumba chake kikubwa chenye samani za kila aina. Pombe ghali zilinyweka na nyama za kuokwa zililiwa mpaka basi.
Alichoka mno, kichwa chake kilichojaa pombe na tumbo lake lililojaa nyama vilimfanya alale kama mfu. Hakuamka mpaka pale alipokuja kuamshwa apokee simu yake toka Liberia.
Alikuwa ni kiongozi wa kundi la Le tueurs, Al Saed, akiwa anamtafuta. Alianza kumtafuta tokea jana usiku lakini hakuwa anapatikana.
Kuna habari nzuri alikuwa anataka kumfikishia, habari ambayo hakuweza kuvumilia kukaa nayo kwa muda mrefu.
“Umetazama televisheni yako?” Al Saed aliuliza.
“Hapana.” Kessy akajibu kiuchovu akijaribu kuketi. Alikuwa yu mwenyewe chumbani wanawake wakiwa tayari wameondoka.
Yalikuwa yamebakia mabaki ya chupa za vileo na foili za nyama ambayo muda si mrefu yangekuja kuondolewa na mfanyakazi wa ndani.
“Unasubiri nini? Tizama televisheni yako.”
Kessy aliwasha televisheni yake akaona taarifa ya habari ikionyesha yale yaliyotukia Liberia. Kundi la Le tueurs lilikuwa limeshinda vita na limetwaa dola ya nchi hiyo.
Japokuwa watu wengi mno walikuwa wamekufa, Kessy hakuliona hilo zaidi ya ushindi wa kundi rafiki kwake. Alijikuta anatabasamu kwa kuanza siku na habari njema kama hiyo.
“Muda si mrefu nitakutafuta,” alisema Al Saed, “Unafahamu hatuna uzoefu na mambo haya ya utawala. Tunatumai utatusaidia kwa namna kubwa.”
Kessy aliwakubalia na aliona hiyo ni fursa nzuri ya kufanya muungano wao uwe imara. Lakini zaidi muungano huo utawafanya waweze kusaidiana kutatua matatizo yao.
Alipokata simu, aliipatia supu kali kabla hajajiweka kwenye kibaraza cha Ikulu ambapo hapo aliendelea kutafakari juu ya tukio la kuvamiwa kwa kambi na kuibwa kwa silaha.
Alimpigia simu Talib aje Ikulu, baada ya mfupi waziri huyo akawasili. Aliletwa na gari jeusi Lamborghini.
“Kuna kitu wanataka kukifanya,” alisema Kessy. “Ni wazi hizo silaha walizoiba zitaenda kutumika kuunda kikundi, na mawazo yangu yananambia watakuwa wana kambi msituni ndio maana hatuwapati tuwatafutapo.”
Walikubaliana kwenye hilo wazo. Silaha zilizokombwa zitakuwa kwenye matumizi muda si mrefu, na hao wezi watakuwa wanajiimarisha kidogokidogo huko misituni wakilenga kuipindua serikali. Hivyo hatua za haraka inabidi zichukuliwe.
“Tuma na usambaze vikosi vya jeshi kwenye misitu yote. Wahakikishe hakuna watu huko wakiwa wanafanya lolote!” Aliamuru Kessy, “Kama tukipata uhakika hakuna watu huko basi itakuwa rahisi kuwapata kwenye makazi ya watu.”
Talib alichukua amri hizo tayari kwenda kuzitekeleza. Lakini kabla hajaondoka, Kessy alimkumbusha alichomwambia jana:
“Kama watu hao wakifanya tukio lolote kabla hujawakamata, basi uhai wako ndio utakuwa malipo.”
Talib alitikisa kichwa na kuondoka.
Ndani ya siku tatu vikosi mbalimbali vya wanajeshi vilisambazwa misituni kwa siri. Kazi yao kubwa ilikuwa ni kutafuta watu na kuwamaliza.
Waliambatana na silaha nzito na nyepesi. Walitembea huku na huko wakihakikisha hakuna wanachokiacha.
Laiti kama wangelijua THE GHOSTS walishafahamu hayo mawazo basi wasingelihangaika. Watuhumiwa wenyewe walikuwa wametulia ndani ya nyumba yao kubwa yenye uzio mrefu wakiwa wamerilaksi.
Walikuwa wamelenga kutofanya lolote kwa muda wa majuma kadhaa kuhakikisha kwanza usalama umetulia ndipo watayafichua makucha yao.
Hivyo basi, wanajeshi wa Sierra walizunguka misitu yote kwa majuma matatu pasipo kupata chochote kitu.
Jambo hilo likamnyima raha Kessy, lakini zaidi Talib ambaye roho yake ilikuwa mkononi akiomba lisitokee lolote ili aendelee kuwa na pumzi yake.
Siku moja ndani ya juma la mwisho la tatu tangu oparesheni ya kutafuta misituni ianze, Kessy alipokea ugeni toka Liberia.
Alikuwa ni Al Saed akija kuomba ushauri na muongozo toka kwa mwenzake huyo. Tafrija kubwa iliandaliwa kumkarimu huyo kiongozi, watu wakanywa na kula.
Baada ya tafrija hiyo fupi, viongozi hao, Kessy na Al Saed, walikaa faragha kupeana mawili matatu.
Ni mambo matatu makubwa ambayo Kessy alimshauri mwenzake: kwanza kutoruhusu demokrasia nchini kwake maana inachochea chuki kwenye mioyo na wananchi; pili, kuminya wizara na kupunguza uwingi wa viongozi ili pesa zisitapanywe; tatu, awe mkali ili kuwatisha na kujiweka salama dhidi ya maadui wake.
“Kama ukiwa lelemama, litatokea kundi lingine kama lako kudai madaraka.”
Hilo lilikuwa nyeti sana. Hakuna aliyetaka kupoteza madaraka ilhali ameyasotea kwa muda mrefu hivyo. Lakini pia Kessy hakusita kumweleza mwenzake juu ya yale yanayoendelea ndani ya nchi yake. Jinsi gani anavyosumbuliwa na vijana aliowalelea.
“Kama unataka msaada wa aina yoyote, tupo tayari,” alisema Al Saed. “Muda wowote siku yoyote nipo tayari kukusaidia.”
Hilo likampa faraja Kessy. Alitabasamu akatikisa kichwa na kusema:
“Bado hawajanishinda kabisa. Natumai nitawamudu, lakini wakinipanda kichwani basi sitajiuliza mara mbili kukuomba msaada.”
Wakaendelea na kuganga yajayo.
“Nadhani itakuwa vema na baadae tutakapokuja kukaa vizuri, tufikirie kujipanua zaidi,” alishauri Kessy. Kwa Al Saed hilo likawa na ukakasi.
“Unadhani itakuwa rahisi?” Aliuliza.
“Hakuna linaloshindikana. Tukiwa pamoja hakuna atakayetuzuia,” aliamini Kessy. “Na tena tutaanza na Guinea.” Akaongezea.
Lakini hala hala chunga jicho na kidole, walishasema washenga na wahenga.
***
Wakati majuma hayo matatu yakiwa yanayoyoma wanajeshi wakiwa msituni, Kwa Kone yaliyoyoma akiwa mtaani kuwatafuta THE GHOSTS. Hakulala usingizi ukaja; alizunguka kila kona ya jiji la Freetown; aliulizia karibia kila mtu akigawa pesa kwa yeyote aliyemsaidia.
Mchana akiwa mtaani, usiku alikuwa kwenye maklabu na madisko bado kusaka.
Majuma matatu yalimuishia akisaka na huku akimuomba Raisi wake aendelee kumpatia muda zaidi. Wakati juma lijalo la nne likiwa katikati, juhudi zake zikazaa matunda.
Ukiwa ni muda wa mchana, gari lake lilisimama mbele ya nyumba yenye ukuta mrefu rangi ya krimu. Alikaa hapo kwa muda wa masaa pasipo kuona dalili yoyote ya mtu. Alichoka kungoja akaamua atoke kwenye gari na kuendea geti kugonga.
Mlinzi alifungua kidirisha cha geti akamuuliza shida yake. Aliposema ni kuonana na wenyeji, hakuruhusiwa kuingia ndani kwa madai kwamba anaowatafuta hawaishi hapo.
Aliendelea kusubiria nje ya geti kama atamuona mtu yeyote akitoka nje, lakini hakuona kitu!
Hali hiyo iliendelea kutokea kwa takribani siku nne asione yoyote kutoka nje ya geti. Alipoenda tena kugonga geti siku hiyo ya nne, aliruhusiwa kuingia ndani.
Kwa siku zote hizo alizokuwa maeneo hayo ya karibu alikuwa anaonekana pasipo kujua. Kamera zilizokuwa getini zilimsoma kwanzia alipokuwa anakuja mpaka anaondoka. Mpaka anakaribishwa ndani, tayari THE GHOSTS walikuwa wamejidhihirishia usalama.
Kone aliketi sebuleni pasipo kuona mtu yeyote. Baada ya dakika kama tatu ndio THE GHOSTS wakatoka ndani na kuungana naye sebuleni. Kone alijitambulisha kwa watu hao na kisha akaeleza namna alivyohangaika kuwatafuta kwa muda mrefu.
Alieleza adhma yake iliyomleta pale, ya kwamba anahitaji kuwasaidia watu hao kushika madaraka ya Sierra Leone.
Kwa kupitia nchi yake, Guinea, atawapatia silaha wanazohitaji, wanajeshi na pesa pia. Lakini yote hayo yakiwa kwenye makubaliano.
“Makubaliano yapi?” Aliuliza Amadu.
Kone akaeleza juu ya makubaliano yaliyowekwa baina ya marehemu Assessoko na Raisi wa Guinea hapo awali, ambayo mwishowe yalikuja kuvunjwa na Kessy.
Amadu na wenzake wakamsikiliza kwa umakini. Alipomaliza kunena, wakamtaka mguinea huyo awape muda wa kufikiria zaidi.
“Tutakutafuta baada ya kujadiliana.”
Kone akaondoka. Alimpasha taarifa Raisi wake juu ya maongezi yake na THE GHOSTS, na namna alivyojawa na matumaini.
Alitumai kabisa atazishinda nyoyo za wanakikundi kile na alimfanya Raisi wake aamini vivyo, lakini ikawa kinyume kwa namna moja ama nyingine.
Ilipita juma moja pasipo majibu. Alirudi nyumbani kwa THE GHOSTS lakini hakuwakuta tena pale, THE GHOSTS walikuwa wameshapotea! Na hakuwa na njia yoyote ya kuwapata tena.
Alichoka pale alipokumbuka ni kwa ugumu gani alivyowapata watu hao na kwa wepesi gani walivyopotea mbele ya macho yake.
Aliamua kurudi Guinea kupumzika kwanza na familia yake. Mkewe, Fatma, akafurahi sana kumuona baada ya majuma kedekede. Hasira za mwanamke huyo zilikoma japokuwa zilimtesa kwa muda mrefu.
Alimkubatia mumewe na kumkaribisha ndani. Kone alivua nguo akala na kujiweka kitandani.
Ikiwa ni usiku, na Fatma anataka kukata kiu yake ya mwili kwa shoka, simu ya Kone inaita. Ilikuwa ni namba mpya. Kone alipokea simu hiyo akaiweka sikioni.
“Tumejadili, na tumeafikiana kutoungana na upande wowote.” Sauti nzito ya Amadu ilivuma simuni kisha simu ikakata.
Kone alishusha pumzi ndefu akatikisa kichwa chake. Mood yote ya tendo ya kula apple la Adamu ilikata.
Kichwa chake kilitingwa na mawazo mzito juu ya THE GHOSTS na Raisi wake. Aliona sasa mambo yanazidi kuwa magumu na yu njia panda ndefu. Ingawa mkewe alijitahidi kwa udi na vumba kupandisha hisia zake, jogoo alikuwa likizo na aligoma kabisa kurudi kibaruani
***
☆Steve