Njia nyembamba - 07
Mtunzi: SteveMollel
****
Usiku ulikuwa umeshaambaa kwenye uso wa ardhi ya Sierra Leone. Mwezi ulitawala anga ukionekana vyema kwa ukubwa huku ukiungwa mkono na nyota zilizozagaa kila kona. Ilikuwa ni saa tano ya usiku ikiitafuta saa sita iwe siku nyingine. Amadu pamoja na Ulsher walikuwa wamesimama wakiegemea kuta ya kibaraza cha nje ya nyumba ya wakina Chui. Nyumba nzima ilikuwa kimya na taa zilikuwa zimezimwa kasoro za nje tu. Huko nje kwenyewe kulikuwa kimya, hakuonekana watu wakikatiza, labda vijibwa na paka.
“Sikuwahi kudhani siku moja nitakuja kufikia hivi kwenye maisha yangu. Kweli hakuna anayeijua kesho yake.” Ulsher alisema huku akitizama nyota zimetazo. Amadu alimtizama akamshika mkono.
“Najua ni jinsi gani kwako ilivyo ngumu; ulizaliwa na kijiko mdomoni. Lakini usihofu, kila kitu kinachotukia maishani kina makusudi yake, na kinatupa fursa ya kufungua mlango mwingine. Historia ya Sierra Leone haitokuja kukusahau kamwe kwa utakachokifanya.”
Ulsher alitabasamu. Akamwambia Amadu;
“Sijawahi kukutana na mtu mwenye moyo kama wewe.”
Amadu akitizama mwezi akasema;
“Mama yangu aliwahi kunambia moyo ndio mafanikio. Chochote kianziacho moyoni lazima kifanikiwe kwakuwa kina dhamira na imani ndani yake.”
“Kweli. Nashukuru sana kukutana na wewe, Amadu. Kila siku unanipa sababu ya kupigania pumzi yangu.”
Ulsher alimkumbatia Amadu akambusu shavuni. Amadu alitabasamu akashukuru, kisha wakarudi kwenye mkao wao wa hapo awali wa kuegemea kuta ya kibaraza. Amadu alirusha macho yake angani akaendelea kuutizama mwezi.
“Kila siku usiku nakuona ukiwa umekaa hapa mwenyewe, unatizama anga kabla ya kwenda kulala. Kwanini unapenda kufanya hivyo?” Ulsher aliuliza. Amadu alitabasamu huku akiendelea kutizama mwezi, akasema;
“Kila ninapotizama mwezi kwa muda, naona uso wa mama yangu. Namuona baba yangu na dada yangu.”
“Pole, Amadu.”
“Ahsante.”
“Naomba nikuache, usingizi umenielemea sasa.”
“Sawa. Usiku mwema.”
“Nawe pia.”
Ulsher aliondoka akabakia Amadu peke yake. Baada ya kupita dakika tano tangu Amadu awe peke yake, kuna sauti ya mtu akiomba msaada ilivuma ikitokea upande wa magharibi. Amadu alirusha macho pande zake zote pasipo kuona kitu. Alitoka kibarazani akawa anafuatilia sauti aisikiayo, akafika eneo alipokuta mtu akimkaba mwenzake huku akimuamuru atoe kila alicho nacho. Amadu akanyata akimsogelea mkabaji, alimpokaribia alimpiga shina la shingo kwa kutumia ncha ya kiganja chake kama mtu akataye gogo na panga. Mkabaji akalegea na kumuachia mkabwaji. Amadu akamkamata mkabaji shati akampokonya kisu alichokuwa amekibebelea kisha akamruhusu mhanga wa kukabwa aende zake.
“Nyie ndio mnaoharibu hili jiji na kufanya lisikalike, mnajifanya majogoo ya mjini, sio?” Amadu aliuliza kwa ukali.
“Hapana, kaka. Ni maisha magumu tu. Hatupendi kufanya hivi.” Mkabaji alieleza huku akiwa ameipinda shingo yake.
“Umekosa kazi za kufanya mpaka ukabe?”
“Hapana, ndugu yangu. Mama yangu anaumwa, amelazwa, inatakiwa pesa kubwa afanyiwe upasuaji maji yatolewe kwenye figo yake. Sina chanzo chochote cha kipato kwa sasa. Kazi niliyokuwa naitegemea imekufa, mwekezaji amefunga kiwanda chake na kurudi kwao baada tu ya utawala mpya kuingia. Sina mbele wala nyuma.” Wakati mkabaji anamalizia kusema hayo maneno, machozi yalikuwa yanamtiririka. Amadu aliacha kushika shati la mkabaji akamwambia;
“Hili unalofanya si suluhisho, linaweza likakuingiza katika matatizo mengine makubwa. Ukikamatwa ukauwawa? … Nenda katafute kazi nyingine umuhudumie mama yako.”
Mkabaji alishukuru. Aliacha hata na kisu chake kwa Amadu akaondoka zake.
Kesho yake mida ya saa tisa ya jioni:
“Hallo, mheshimiwa raisi!” Sauti ya Kone ilisikika ikitokea ndani ya chumba. Punde mlango ulifunguliwa Kone akatoka chumbani akiwa kavalia bukta fupi na shati jepesi, akawa anaelekea sebuleni huku simu ikiwa sikioni.
“Ndio muheshimiwa, kuna taarifa nataka kukupatia … Eeeh toka huku Sierra … Kwa taarifa nilizozipata, keshokutwa kutafanyika sherehe kubwa ikulu ya kuupongeza utawala mpya, wageni kadhaa wamealikwa toka nchi mbalimbali kuja kuhudhuria … ndio, mheshimiwa … Ndio, fursa inaweza ikapatikana … Sumu? … Mi nadhani tukitumia mwanamke itakuwa vyema zaidi, huyo mwanamke ndio atamuwekea sumu mfano kwenye kinywaji … Ndio muheshimiwa … Usihofu, mkuu nitalisimamia hilo vyema … sawa, baadae.” Simu ikakata.
Baadae mida ya saa kumi na moja:
“Nadhani hii ni fursa nzuri ya kufanya tukio letu.” Amadu aliwaambia wenzake, “Hiyo sherehe ya ikulu itakapokuwa inafanyika nina imani ulinzi hautokuwa vyema maeneo ya benki kuu, wafanyakazi wakubwa watakuwa wamehudhuria kwenye sherehe hiyo, hata ambao watakuwepo watakuwa wametekwa na hilo tukio. Vile vile wananchi wengi watakuwepo videoni na maredioni kusikiliza na kutizama yanayojiri huko ikulu, hii ndio fursa nzuri, mnaonaje?”
“Kwangu, naona sawa.” Ussein alijibu na kuongezea, “Ila mipango yetu je?”
“Kuhusu mipango, hakuna shaka. Tayari nimepata ramani yote toka kwa mjomba, inaonyesha kuanzia juu mpaka chini ya jiji, mitaro na njia zake zote za chini. Cha kufanya ni kesho twende na kupitia maeneo hayo ili tuelekezane kwa ufasaha zaidi.” Amadu alifafanua. Wenzake wakaafiki.
Saa nane ya mchana siku iliyofuata:
Magari manne makubwa aina ya Scania yaliyobebelea vifaa mbalimbali vya upambaji yalikuwa yametuama mbele ya ikulu. Walikuwepo watu kadhaa wakitoa vifaa ndani ya magari hayo na kuhamishia chini, watu hao walikuwa wamevalia sare zenye maandishi yaliyosomeka ‘The tight black ceremonial masters’: shati jeupe na suruali nyeusi. Walikuwa bize kweli wakitua matambara, vishikio vya taa, maua makubwa, mabango yenye ukubwa wa kati, maspika makubwa, mafagio, makapeti na kadhalika. Baada ya masaa mawili ikulu ikawa imebadilika na kuwa ya kuvutia zaidi. Kitu pekee ambacho kingemfanya mtu atambue kwamba hapo ni ikulu labda ni uwingi wa walinzi waliotapakaa kila hatua wakiwa wamekumbatia bunduki zao kama vile wapo eneo la vita.
Mwanaume mmoja mrefu aliyekuwa anawasimamia wenzake kupamba na kuremba alimfuata mojawapo ya walinzi akamuambia:
“Naomba utuitie meneja.”
Mlinzi akafanya alichoagizwa.
“Meneja, tayari tumemaliza.”
Meneja akapekua eneo na macho yake makubwa kisha akaguna.
“Una uhakika?”
“Ndio, meneja.”
Meneja akatupa tena jicho lake kutizama.
“Sitaki ile rangi ya mapazia uliyopambia pale jukwaani. Nani kakuambia utumie kijani, bluu na nyeupe?”
“Kwasababu ni rangi ya bendera ya taifa.”
“We huoni haijapendeza?”
“Kwahiyo nibadilishe, mkuu?”
“Aaaahmmm … Embu weka na nyekundu kidogo, nyeusi na nyeupe.”
“He! … Meneja, hiyo si itakuwa rangi ya MDR?”
“Kuna shida kwani?”
Meneja akaondoka. Mpambaji akawarudia wenzake na kuwataka wafanye mabadiliko kwenye mapazia waliyoyatandaza jukwaani. Kazi ikafanyika na kwisha, meneja akaitwa tena kutizama, ngekewa mabadiliko yakampendeza machoni.
“Safi sana. Sasa ujira wenu mtaupata.”
Wapambaji wakaonesha meno yao kwa tabasamu. Meneja akaondoka kwenda ndani. Mlango wa chumba alichokuwemo General ulifunguliwa akaingia meneja akiwa anatabasamu.
“Kila kitu sasa kipo sawa sasa, mkuu.”
General akatabasamu na kutengenezea kola ya shati lake la jeshi. Alikuwa ameketi juu ya kitanda kikubwa chenye shuka jeupe kama usufi na mito mikubwa kadhaa. Chumba kilikuwa kikubwa mno na chenye kila mahitaji. Sakafu yake ilikuwa imefunikwa na zulia la manyoya, ukutani kulikuwa kumepachikwa kioo kikubwa chenye fremu rangi ya dhahabu.
“Safi sana, Thomas.” General akasema, “Kuna cha ziada?”
“Ndio, kipo, mkuu.”
“Kipi hiko?”
“Naomba uniruhusu …”
Meneja akaufuata mlango akaugonga mara tatu, mlango ukafunguliwa na mlinzi wakaingia wanawake hamsini, wote wakajipanga mstari. Meneja huku akiwa ametabasamu akamtizama General.
“Haya ni maua yatakayopendezesha shughuli yetu.”
Alisema Meneja kisha akawatizama wale wanawake na kupandisha kichwa. Wanawake wote wakavua nguo zao na kubakia uchi wa mnyama. General akaonyesha tabasamu. Alinyanyuka akaanza kuwakagua wanawake kwa kuwashika-shika maungo yao. Alipomaliza alimpa mkono Meneja.
“Safi sana! Hakika hivi viatu vimekutosha.”
“Nashukuru sana, mkuu.”
“Shughuli yote hii ipo mikononi mwako.”
“Bila shaka nitaitendea haki.”
“Sawa. Waweza kwenda sasa.”
Meneja na wanawake wake wakatoka nje ya chumba. Meneja akawakusanya wanawake nje ya jengo la ikulu akawaambia:
“Naomba mhakikishe mnakuwa vema mbele ya wageni. Mnalipwa pesa nzuri na nategemea huduma nzuri kutoka kwenu.”
Mwanamke mmoja akamjibu Meneja.
“Hii ndio kazi yetu, hatuna desturi ya kulipua. Tunajua nini cha kufanya bwana Meneja.”
Siku hazigandi, siku ya tafrija ikatimba. Wakati kukiwa ni jioni muziki laini wenye mahadhi ya kiafrika ukawa unapigwa taratibu. Sauti za wasanii mashuhuri wa bara la Afrika kama Yvone Chakachaka, Kanda Bongoman na Youssour Ndou zilikuwa zinavuma. Watu wa rangi mbalimbali walikuwa wamejazana kwenye uwanja wa ikulu. Kila mtu alikuwa ameshikilia kinywaji chake huku wahudumu wakihakikisha kila ambaye glasi yake imekaukiwa anahudumiwa haraka iwezekanavyo. Hakukuwa na viti, watu wote walikuwa wamesimama. Walinzi walikuwa wametawanyika kila upande wakihakikisha usalama unakuwepo. General Kessy alikuwa akisalimiana na wageni wake mbalimbali wakipeana mikono na wengine wakikumbatiana. Alikuwa tofauti na wengine kwa kuvalia nguo ya jeshi yenye vyeo vya kila rangi kwenye mabega yake na kifuani mwake.
Baada ya dakika kadhaa za kusalimiana na wageni General Kessy akaenda kwenye kihutubio kilichokuwa kimeketi kwa juu kidogo kiasi cha kuonekana na kila mtu aliyekuwepo lile eneo. Juu ya kihutubio hiko kulikuwepo na kipaza sauti chembamba pamoja na chupa ya maji ya kunywa. General alisafisha koo lake kwanza alafu akaanza kutema maneno:
“Nashukuru sana kwa uwepo wenu hapa, mabibi na mabwana. Ni faraja kwangu kuona kuna watu ambao bado wanaitakia mema Sierra Leone.”
Wakati hayo maongezi yanaendelea upande mwingine wa nchi THE GHOSTS walikuwa wanajiandaa kwa ajili ya tukio lao la ukwapuzi wa pesa benki kuu wakivalia nguo za kazi na kupaki vifaa vyao vya kazi mabegini. Nyenzo kama nyundo, vifaa vya utobozi, gloves ngumu, kamba, mtungi wa gesi, kurunzi, ngazi ya kufunga na kufungua, baruti na ramani vilibebwa. Kila mtu alikuwa amevalia kofia nyeusi aina ya boshori pamoja na gambuti. Walijiweka kwenye gari dogo jeusi wakaondoka eneo la nyumbani kwa mwendo wa kawaida usiopalilia mashaka.
“Nitahakikisha nchi inakuwa salama kwa nguvu zangu zote.” General aliendelea kuhutubia wageni. “Alikunywa maji kidogo alafu akaendelea.
“Sitokuwa na huruma na wale wote watakaodiriki kwa njia yoyote ile kuhatarisha usalama wa nchi yangu. Nitakuwa rafiki kwa marafiki zangu na adui kwa maadui zangu. Tumeichukua hii nchi kwa lengo la kuifanya isimame tena kwa miguu miwili, na tunaamini itasimama. Hao wazungu wanaonitishia kukata mahusiano na mimi na hata baadhi ya vi-nchi vioga vya Afrika, hainisumbui wala kuninyima usingizi kamwe. Nitakuwa wa kwanza kuonyesha ulimwengu kwamba nchi za Afrika zaweza kujitegemea.”
Wageni wakapiga makofi kupongeza. Kone akiongozana na mwadada mrembo mwenye shepu ya kujaa wakaingia eneoni. Kone alikuwa amevalia suti ‘taxido’ nyeusi ikiwa imemkaa vizuri mno. Mwanamke aliyeongozana naye alikuwa amevaa gauni refu jekundu la kung’aa, shingo yake nyembamba ilikuwa imebebelea mkufu wa silva ukifanana na bangili yake mkononi.
Kone alishusha pumzi ndefu akamwambia mwanamke aliyekuja naye.
“Yule unayemuona pale juu anaongea, ndiye tageti yako. Hakikisha unamtia mkononi na unatimiza adhma. Natumai hautoniangusha. Najua hawezi kuzuia mihemko yake kwa mwanamke mrembo kama wewe.”
“Nitajitahi kwa akili na nguvu zangu zote.” Mwanamke akajiapiza.
Umbali wa hatua zisizozidi hamsini toka uzio mkubwa wa benki kuu palikuwepo na mfuniko wa chuma juu ya barabara ya sakafu. THE GHOSTS walisogelea mfuniko huo kwa tahadhari, Amadu akachoropoa nyundo na bisibisi ngumu akaanza kutawanya na kuvunjavunja saruji iliyokuwa imekamata kingo za mfuniko. Alipomaliza alipenyeza bisibisi chini ya mfuniko alafu akapiga na nyundo, mfuniko ukapanda juu, akaudaka na kuuvutia pembeni, likaonekana shimo jeusi lisilojulikana wapi laishia.
“Hii ndio njia!” Amadu akawaambia wenzake. Akachomoa kurunzi na kumulika ndani pakaonekana mtaro washuka chini lakini mbele bado kukiwa ni giza nene.
“Una uhakika ndio hapa tulikuja mchana, Amadu?” Ulsher aliuliza. Amadu akatikisa kichwa.
“Ndio hapa. Tufanye haraka kabla hatujaonekana.”
Wote wakadumbukia ndani ya shimo na kurudishia mfuniko. Walitua sehemu yenye maji machafu kimo cha magotini, kila mtu alimulika na kurunzi yake wakasonga mbele kama ramani isemavyo. Kulikuwa na mende na panya wa kutosha humo ndani pia joto la makadirio ya nyuzi joto arobaini na tano lililofanya wajae jasho ndani ya muda mfupi tu. Baada ya mwendo wa dakika kama tatu na nusu wakafika sehemu ambapo mtaro wa maji umegawanyika na kutengeneza njia panda. Hapo Amadu akasimama na kunyooshea kidole dari.
“Ni hapo juu. Inabidi tupasue hapo juu!”
Farah akatoa ngazi na kuifungua akaibananisha ukutani. Akapanda mpaka juu akaanza kutoboa dari na mashine tobozi. Kwa muda wa dakika, hakuna kilichofanikiwa. Palikuwa pagumu mno kupenyeka.
“Haiwezekani!” Farah akawaambia wenzake.
“Tumia njia ya pili.” Amadu akashauri. Farah akapachika baruti kisha akashuka wakasogea kando.
Puuuuh! Baruti likalipuka na kutawanya ikabakia tabaka jepesi sasa. Farah akapanda tena juu na kifaa tobozi chake akapenyeza chuma mpaka juu. Mtungi wa gesi ukatobolewa na kupenyezwa mrija, mrija ukapitishwa kwenye tundu lililotobolewa kisha gesi ikafunguliwa, taratibu ikaanza kuingia na kusambaa ndani ya benki. Gesi ilipokwisha, mrija ukachomolewa na kupachikwa kwenye mtungi mwingine uliotoka kwenye begi la Ussein, kazi ya kusambaza gesi ikaendelea.
General alimaliza kuhutubia, wageni wakapiga makofi mazito. Alimiminiwa glasi ya mvinyo akainyanyua juu.
“Kwa wale wanaoitakia mema Sierra Leone!”
“Kwa wale wanaoitakia mema Sierra Leone!” Wageni wakaitikia huku wakiwa wamenyanyua vinywaji vyao juu kisha wakavipeleka vinywani.
Ndani ya benki wafanyakazi walianza kupata mawenge na kupoteza uwezo wa kuona vema. Punde wote walilala, ikiwemo na walinzi wa ndani. THE GHOSTS waliingia ndani ya jengo wakiwa wamefunika nyuso zao na vinyago vya kujikinga na gesi. Wakavunja kamera na zingine kuzipulizia spray. Walichukua funguo za milango toka kwenye kwenye ubao wa ofisi, wakafungua milango kadhaa. Kwenye milango iliyohitaji alama za vidole wakawachukua walinzi na kuwawekesha viganja vyao kwenye kioo. Walipofika kwenye makabati magumu ya kuhifadhia pesa hapo kukaleta kidogo mushkeli.
“Tutumia baruti?” Mou akauliza.
“Hapana!” Ulsher akajibu, “Kama tukitumia baruti na hapa, tutazalisha sauti kubwa sana na kudaka mishangao toka pande mbalimbali. Polisi wanaweza kuja muda si mrefu.”
“Sasa tunafanyeje?” Mou akauliza tena.
“Nina wazo,” Ulsher akasema. “Inabidi tujue kilipo chumba cha ulinzi, huko kutakuwa na video zote zinazoonyesha kila kamera iliyo humu ndani.”
“Alafu?” Mou akadakia.
“Alafu tutatafuta kamera inayotizama hili eneo. Tutarudisha nyuma mkanda na kutizama pale namba za siri zinapoekwa. Tutaivuta picha kwa karibu na kunakili namba hizo.” Ulsher alifafanua. Amadu akamkumbatia kwanguvu.
“Una akili sana! … Wote tufanye kama Ulsher alivyosema. Tufanye haraka, ndani ya dakika tatu tu.”
General alishuka kwenye kihutubio akaungana na nyomi la wageni wake. Hiyo ikawa fursa kwa Kone na mrembo wake ambao walijisogeza taratibu mpaka eneo alilopo General, wakamsalimia.
“Naitwa Kone, mwakilishi wa serikali ya Guinea.”
General akatabasamu kwa kejeli.
“Ajabu. Raisi wako ni jirani yangu, ina mana ameshindwa kuja mpaka atume mwakilishi?”
“Hapana, mheshimiwa, amebanwa na kazi. Ila pia hakuweza kukaa kimya wakati nyumba ya pili kuna tafrija, ndio mana akatuma mwakilishi angalau uwepo wake utambulike.”
General akatabasamu kisha akamtizama mwanamke wa pembeni.
“Na huyu ni nani?”
“Anaitwa Rose: rafiki yangu wa Sierra Leone.”
“Ni mpenzi wako?”
“Hapana, mheshimiwa. Rafiki yangu tu.”
General akamtizama mwanamke kuanzia juu mpaka chini, aliporudisha macho yake juu akakutana na tabasamu mwanana la mwanamke likishikana na macho legevu.
“Naweza nikatembea hatua kadhaa na rafiki yako?”
“Unaweza tu, mheshimiwa. Hakuna tatizo.”
Mwanamke akapenyeza mkono wake kwenye kwapa la General wakaondoka baada ya kukonyezana na Kone. Walitembea hatua kadhaa huku General akisifu uzuri wa mwanamke aliyeambatana naye. Baada ya kuuliza kama ana mwanaume na mwanamke kujibu hana, General akapenyeza rupia:
“Naweza nikawa nawe usiku wa leo?”
Mwanamke akatabasamu.
“Sidhani kama nitakuwa na muda, mheshimiwa.”
“Kwanini?”
“Mimi ni mfanyabiashara, nakuwa bize.”
“Kwahiyo siwezi kuwa nawe kabisa? … Tafadhali, nitarepea hasara utakayopata kwa kutozingatia biashara yako kwa dakika utakazokuwepo hapa nami.”
“Kweli?”
“Unadhani mkuu wa nchi anaweza danganya?”
Mwanamke akatabasamu tabasamu pana. Wakaongozana na General kwenda ndani ya ikulu. Walipoingia ndani ya chumba, General akaanza kumpapasa na kumtomasa mwanamke kwa pupa. Mwanamke akamsukumizia General kitandani kisha akavua nguo zake zote na kuanza kucheza kwa madaha mbele ya macho ya General yaliyojaa uchu. General alishindwa kuvumilia, alinyanyuka akamfuata mwanamke kwa hamu. Mwanamke akamnong’oneza sikioni:
“Kalete vinywaji kwanza.”
Haraka General akafungua mlango na kumuagiza mlinzi alete vinywaji. Vilipoletwa vilipokelewa na Mwanamke akiwa amevalia taulo, General alikuwa yu bafuni anaoga. Huo ukawa upenyo kwa Mwanamke kutia sumu kwenye kinywaji cha General kisha akakichanganya vema. General akatoka bafuni na kumkuta mwanamke uchi wa mnyama, mkononi mwake akiwa kabebelea glasi ya kinywaji.
“Karibu.”
General akasogea na kutwaa kinywaji chake. Kabla hajanywa fundo, hodi ikagongwa mlangoni. General akaweka kinywaji chake chini akauendea mlango.
“Samahani mheshimiwa kuna tatizo limetokea.” Aliongea mlinzi kwa sauti nyenyekevu lakini yenye tahadhari ndani yake. Macho yake yalionyesha hofu kana kwamba anaogopa kusema kilichomleta.
“Tatizo gani?” General aliuliza hali akitizama tizama usalama na macho yake makavu.
“Kuna taarifa zimetufikia hivi punde. Benki kuu imevamiwa. Pesa nyingi mno zimeibiwa.”
Kabla ya kutia neno General akitoa kwanza macho kwa hasira. Alijua fika pesa iliyopo benki kuu ndiyo ambayo anategemea na inampa kiburi. Sasa imekombwa! Alikabwa na kigugumizi.
“Saa … sa … saa ngapi! Saa ngapi tukio hilo limefanyika? … Umesema ni ndani ya muda mfupi.” Alijijibu mwenyewe.
“Ndio mheshimiwa.” Mlinzi alijikuta akijibu kwa hofu.
“Hakikisha mnabana njia zote kuu, asitoke mtu yeyote nje ya jiji. Nataka watuhumiwa wakamatwe ndani ya masaa ishirini na nne na pesa yote irudi! Haraka!” General aliamuru kwa ukali. Uso wake ulieleza jinsi alivyogadhabika. Mlinzi alifungua miguu yake upesi kutoka eneo hilo, kabla hajafika mbali aliitwa na General kwa ukali akageuza shingo yake.
“Mwambie Talib aje haraka iwezekanavyo!”
“Sawa mkuu!” Mlinzi aliitikia kisha akatokomea akikimbia kama vile hataki kuitwa tena. General aliingia ndani akavaa nguo zake haraka. Alimtaka na mwanamke avae nguo zake kwani wanaondoka wataonana siku nyingine atakampopigia simu akimuhitaji. Baada ya mwanamke kujibaraguza kimahaba ya uongo kwa General kama vile mtu anayempenda kumbe ana hila nyuma yake, General alimuaga kwa kumpa mabusu motomoto na kusogeza ahadi ya kuonana karibu zaidi. Kwa muda kidogo akasahau matatizo yake mpaka pale alipokutana na Talib uso kwa uso, hapo akawa kifaru aliyejeruhiwa.
“Talib, umewapata?”
Aliuliza kama vile ametoa amri mwezi au juma lililopita.
“Hapana mkuu. Ila nimeshatoa agizo njia zote zibanwe, na makachero wangu wanafuatilia kwa ukaribu mno!”
General akasonya. “Sitaki hadithi, Talib.” Alifoka, “Nakupa masaa machache tu, niwaone wahusika wote wakiwa kitanzini.”
“Sawa, mkuu. Nitafanya juu chini. Lakini kwa mujibu wa kamera za nje na za ndani kabla hazijaathiriwa zinaonyesha wahusika ni Amadu pamoja na wenzake aliotoroka nao.”
Taarifa hiyo ikamgutua Kessy. Ni kama vile alikuwa amewasahau watu hao ambao kwa sasa wanaonekana kumuadhibu. Alikunja ngumi kwanguvu akisaga meno. Macho yake yalikuwa mekundu kana kwamba amekula pilipili. Alipanda gari lake akiongozana na msafara kwenda eneo la tukio – benki kuu. Huko alitazama mazingira yote yaliyoonyesha namna tukio lilivyotekelezwa na kuambiwa kiasi halisi cha pesa kilichokuwa kimeibwa, taslimu dola za kimarekani laki moja, ambayo ni sawa na kiasi cha Leone milioni mia tano sitini nne na laki tano! Kwa namna uchumi wa nchi hiyo ulivyokuwa umeyumba, hiyo pesa ilikuwa kubwa sana. Pesa ilikuwa imefujwa sana na serikali kiasi kama hicho kuibiwa, lilikuwa ni pengo kubwa sana.
“Talib, nataka hawa watu haraka!” Kessy aliropoka. “Nataka wanyongwe!”
“Ndio, mkuu!”
“Nakupa juma moja tu!” Alisisitiza. “Juma moja tu!”
Usiku huo uligeuka ukawa mchungu mno kwa Kessy. Alilala kitandani kwake mawazo yakimtinda mno ni kwa namna gani atawapata wadhalimu wake na kurejesha pesa yake. Aliamka mara kwa mara akampigia simu Talib akimpa maelezo. Hakutaka kabisa mtu yeyote atoke nje ya jiji la Freetown kwa kutumia njia yoyote ile: angani, majini wala ardhini. Alitaka vyombo vyote vya habari vitangaze jambo hilo na sura za watuhumiwa zikiwekwa wazi huku donge nono la zawadi likiwa limeongezwa maradufu.
Tofauti na siku zingine, siku hiyo Kessy alikuwa mwenyewe ndani ya chumba chake. Hakuwepo mwanamke yoyote wa ‘kumfariji’, kama vile asemavyo kila uchwao. Tena siku zingine huwa na wanawake zaidi ya wawili japokuwa mara kwa mara wanawake hao huwa wanaishia kupigwa, kuingiliwa kimabavu ama kinyume na maumbile. Yote yakiwa ni kwasababu Kessy hakuzoea raha za kupewa taratibu ama madaha. Kuishi kwake misituni kwa jina la waasi kulimharibu akili kwa namna moja ama nyingine.
Masaa matano mbele:
Rose, mwanamke mrembo alikuwa amevalia gauni jekundu lililomkaa vema, alikuwa amekaa na Kone ndani ya mgahawa ulio karibu na bahari. Uso wake ulikuwa umerembwa vizuri na kukupa kila sababu ya wewe kumtazama. Kone yeye alikuwa amevalia suti nyeusi, kama anavyopenda mara nyingi. Ukimwona kwa mwili wake na muonekano basi ungepata kusema ni afisa wa serikali ama mtu mweye nafasi kubwa sehemu nyeti za serikali. Ukiachana na utofauti wao huo, wote walikuwa na utulivu usoni ila pia usiri. Walikuwa wanaongea taratibu wakiwa wamejitenga na umati wa watu. Walikuwa waangalifu na wenye kubeba tahadhari.
“Kama isingelikuwa hilo jambo la benki, ningelikuwa nishammaliza,” alitamba Rose akiongea kwa pozi. “Tayari kinywaji chake nilishatia sumu. Nilikuwa namngojea anywe tu, kazi iwe imekwisha.”
Kone alikunywa kwanza juisi yake alafu akatazama baharini.
“Mungu wake bado kijana,” alisema. “Ila muda wake utawadia tu. Lazima afe kwa namna yoyote ile.”
“Sasa hivi umepangaje sasa?” Aliuliza Rose akimtazama Kone na macho malegevu.
“Mpango wetu unategemea na wewe,” Kone alijibu.
“Kivipi?”
“Inategemea siku atakayokuita na wapi atakapokuitia,” alieleza Kone. “Kama akikuita uende Ikulu, itakuwa rahisi zaidi. Na sidhani kama kutakuwa kuna njia nyingine nzuri zaidi ya kummaliza na sumu.”
Kuka kimya kidogo upepo wa bahari ukipuliza.
“Unajua nataka nikuweke mahala salama,” Kone alisema. “Ukitumia sumu niliyokupa, hatakufa kwa haraka. Inaweza ikamchukua hata siku mbili tofauti na kama ukitumia njia zingine amabazo zitakuweka matatani kiusalama.”
Rose akatikisa kichwa kuridhia.
“Ila ni wakina nani hao walioiba benki kuu?” Aliuliza. Alijikuta amepata hamu ya kutaka kujua aliyeharibu mpango wao.
Kone alisonya akakuna kidevu. Alitazama upande wake wa kushoto, mbali akawaona wanajeshi wawili wakiwa wanabandika makaratasi kwenye kuta za nyumba, mistimu na miti. Alitazama kwa umakini akagundua neno moja kubwa jeusi kwenye tangazo hilo: WANTED. Pasipo kujiuliza mara mbili, Kone akawa amegundua ni wakina nani wanaotafutwa.
“Adui wa adui yako ni rafiki.” Alisema Kone kisha akamtazama Rose. “Watu walioiba benki kuu ni mojawapo ya watu waliokuwa pamoja na Kessy kwenye kundi lao la waasi kabla hawajapata madaraka.
“Wapo wangapi?”
“Watano.”
“Tu?”
“Ndio, ila bila shaka umeona madhara yao. Inabidi tuwatafute hao watu. Tukiwapata kazi itakuwa rahisi sana na iliyojaa matumaini.”
“Utawapataje?”
“Penye nia pana njia. Nitawapata karibuni kuliko unavyodhani.”
“Vipi kama ukiwapata nikiwa tayari nimeshamuua Kessy?”
“Bado itakuwa bora zaidi. Nina matumaini wao ndio watakaimu nafasi ya Kessy. Na kama tutakuwa tumewasaidia kwa njia moja ama nyingine basi tunatumai makubaliano yaliyowekwa kati ya Assessoko na rasi wetu yatatimia.”
“Naweza nami nikapata nafasi ya kushiriki?”
“Bila shaka, Rose,” alijibu Kone kisha wakagongesha glasi zao za juisi wakiziambatanisha na tabasamu.
***
☆Steve