Njia nyembamba (msimu wa pili) -- 01
Mtunzi: SteveMollel
“Ni kuhusu Guinea ama Sierra?” Kone aliuliza.
“Ni kuhusu Sierra!” Akajibu Raisi. Hapo Kone akavutiwa zaidi. Ni kipi hicho Raisi wake alichomtolea Sierra na kumuitia pale haraka vile? Ni kipi hicho tena Raisi wake anachakusema kuhusu Sierra na si nchi yake, Guinea?
Moyo wake ulianza tu kwenda mbio. Hakujua kwanini.
“Kone, hili jambo ni serious sana. Na kama nilivyokuambia, ni siri sana. Hakuna kiongozi mwingine anayelijua hili isipokuwa waziri wa mambo ya nje tu.” Raisi akaweka kituo kwanza. “Kuna nchi huko ughaibuni, wanataka kuwezesha zoezi la kuiondoa Sierra madarakani.”
Kone alihisi hilo jambo haliko sawa hata kabla Raisi hajaendelea.
“Wamekuja na mapendekezo yao kwangu. Wao na sisi kuna mambo tunayoshea: wote kuna kitu tunahitaji ndani ya nchi ya Sierra Leone. Wamesema ya kwamba itakuwa rahisi sana kuiondoa serikali hiyo kwa kutumia mwamvuli wa utawala wa kimabavu ambao upo madarakani kwani halitasababisha maneno wala macho ya ndani kugundua nini ambacho kipo nyuma ya pazia.”
Kukawa kimya kidogo.
“Wewe Kone unaonaje hili kabla sijajitumbukiza mzima?”
“Sisi kama Guinea tutafaidika vipi na huo mpango wao?” Kone aliuliza.
“Wamesema ya kwamba kuna faida nyingi tutazipata mbali na ambazo wamezianisha.” Raisi akajibu. “Uhusiano baina yetu utaimarika, watatusaidia kiuchumi kwa kiasi kikubwa kwa misaada na mikopo yenye riba nafuu. Lakini pia tutapata yale ambayo tuliweka nayo maagano na Assessoko.”
Kone alikuna kidevu chake akiwaza. Kichwa chake kilimpa ala za hatari. Alidadavua jambo hilo kwa sekunde kadhaa, akamtazama Raisi kwa macho ya uhakika.
“Huu unaweza ukawa mtego hatari. Tatizo linakuja hatujui ni nini haswa malengo ya hao watu, hata kama wametuweka wazi baadhi. Endapo itagundulikana kama nasi tulikuwa pamoja nao, wanaweza wakatugeuka tukawa wahanga wakubwa. Lakini vilevile, tuna uhakika gani kama utayapata yale ambayo yalikuwa ndani ya maagano yetu? Hata pale watakapotugeuka, kumbuka hatutakuwa na mahala pa kushitaki.”
Raisi alivuta kwanza pumzi akabinua mdomo wake. Alikuwa anawaza na kuwazua. Uso wake ulijikunja na macho yake ndani ya miwani yenye fremu nzito nyeusi yalikuwa yanazunguka huku na kule. Aliishia tu kushusha pumzi, akauliza:
“Ila Kone ukiachana na hizo hatari, huoni kama hii ni njia nyepesi zaidi?”
“Ila ni hatari zaidi,” akajibu Kone. “Ila kama unataka tu kulipa kisasi kwa Sierra, nakushauri uende na hiyo njia. Lakini kama unataka kupata kitu kutoka huko, nakushauri uende mwenyewe.”
“Sawa. Basi tunakuwa tumebakiwa na chaguzi lako pekee. Natumai utalifanikisha hilo ndani ya juma moja. Endapo kama likishindikana kwa muda huo basi itanilazimu kwenda na chaguzi la nchi ya ughaibuni.”
Walifikia makubaliano hayo. Kone alikabidhiwa pesa zaidi za kufanikisha mipango yake. Hakudumu sana hapo akaenenda nyumbani kwake baada ya kuagana na mke wa Raisi.
Ilimchukua muda mfupi, akawa nyumbani kwake. Alionana na mkewe aliyemkaribisha kwa bashasha za mapenzi na kumkarimu chakula. Napo hakukaa muda mrefu, mwanaye akaja tokea shuleni. Alimkumbatia babaye na kumweleza namna alivyomkumbuka kabla hajaenda kula na kucheza.
“Unakuwa bize sana, mimi na watoto tunakuhitaji pia.” Alilalama Fatma. Uso wake mpana uliokuwa ndani ya hijabu ulikuwa na sononeko. Tangu mumewe alipopewa kazi na Raisi amekuwa adimu sana nyumbani, na hata pale mara chache anapokuwepo basi hatokaa kwa muda kabla hajahepa. Jambo hilo lilimkosesha furaha Fatma, na hata kumpukutisha mwili kwa kukosa mahaba ya mumewe.
“Unajua nini nafanya kwa sasa. Nimekuwa nikikuambia kila siku.” Alisema Kone. Sauti yake ilikuwa na kaukali ndaniye.
“Mume wangu, najua nini unafanya na wala sihitaji kuambiwa tena. Lakini kumbuka kwamba familia ni kitu cha kwanza na si mali: nyumba, gari wala fedha!”
Kone alisimama akavua shati lake. Alivua pia na suruali kisha akajilaza kitandani. Fatma alimjongea akalala pembeni. Hakutaka kumkwaza mumewe, alimpa tabasamu na kuweka kiganja chake mgongoni mwa mwanaume huyo.
“Samahani kama nakukera, nakukosa mno. Natumai leo utakuwa na mimi kwa muda mrefu.”
Macho yake yalionyesha upendo kwa ndani. Na haikumchukua muda mrefu Kone akauona upendo huo alioupokea kwa tabasamu mwanana.
“Nitakuwepo na wewe mpenzi wangu.”
Fatma alitabasamu akasaula nguo na kulala karibu na mumewe. Alimwelezea ni kwa namna gani alivyokuwa anamkosa akawa mpweke. Alimweleza maendeleo ya watoto na biashara zao. Wakati akifanya yote hayo mikono yake milaini ilikuwa inakanda hamu toka kwa mumewe. Kone alikuwa anarembua kwa raha: kwa namna kubwa alikuwa ‘amemisi’ huduma hizo.
Lakini kama vile kitumbua mchangani, umoja huo ukavunjwa na muito ulioingia ndani ya simu ya Kone. Fatma alimtaka mumewe asipokee wala kusumbuka nayo lakini Kone hakuweza kuinyutia simu hiyo kwani alitumai inaweza kuwa ya muhimu sana. Alikuwa ni Rose anamtafuta, na alijikuta anatabasamu baada ya kuona jina hilo kiooni.
“Amenitafuta.” Sauti ya Rose ilisema kwa ufupi.
“Sawa, tutaonana baada ya muda mfupi,” akajibu Kone. Simu ilikatwa ikawekwa kando. Kone alimtazama mkewe akamkuta akiwa amefura, na akiwa anafanya jitihada za kuvaa hijabu yake.
Alijaribu kumwelezea mkewe hali ilivyo lakini mwanamke huyo hakutaka kusikia chochote. Alichosema ni:
“Nenda kwa Rose wako huyo.” Kisha akatoka ndani ya chumba isieleweke anaenda wapi.
Muda wa usiku wa saa nne:
THE GHOSTS wakiwa wamejipakia vema ndani ya gari, wamebebelea mabegi makubwa matupu na wamevalia nguo nyeusi, walishika njia kuelekea Rokel Barracks Ulsher akishikilia usukani. Kwa usiku mzima walikuwa wanapanga nini cha kufanya huko Barracks wakitumia ramani iliyochorwa vema na na Mou Farah. Walianisha mpango A, be na hata che. Walishajipanga wapi pa kuingilia na wapi pa kutokea. Wapi wapite na wapi wasipaguse. Kilichobakia ilikuwa ni kutenda tu.
Baada ya dakika chache walifika karibu na eneo la tukio. Wanaume wote walishuka wakamwacha Ulsher ndani ya gari. Walikuwa wamebebelea bunduki ndogo na migongoni wakiwa na mabegi makubwa meusi. Wanaume hao waliposhuka Ulsher aligeuza chombo, akazima taa na injini kisha akatulia tuli sasa akiwa anangojea kupokea taarifa yoyote toka kwa wenzake.
Amadu na wenzake walijongea karibu zaidi na Barracks. Wanaume hao walijigawa kila mtu akaenenda pande yake. Waliufikia ukuta wakapanda na kuingia ndani kwa uangalifu mkubwa. Kazi kubwa kwa wakati huo ilikuwa ni kukwepa taa kubwa ya mnara. Walifanikiwa kukwepa taa hiyo na kujiweka salama zaidi ndani ya kambi hiyo kubwa, Chui alimuua mwanajeshi aliyekuwa anaendesha taa hiyo kwa kumrushia kisu kilichomuangua na kumtuza chini. Wanajeshi watano nao waliokuwa zamu wakauwawa, mkono wa Amadu, Farah, Ussein na Mou ukihusika.
Mpaka wanakutana mahali walipopanga ndani ya muda waliopanga, walikuwa tayari wameshawateketeza wanajeshi kumi huku kusiwe na kelele zozote. Kuwanyonga watu hao na kuwanyofoa uhai kwa kutumia visu ndiyo ilikuwa namna ya kusonga. Walifanya kwa upesi na yote hayo yalichukua chini ya dakika moja tu!
Farah alitoa ishara kwa kutumia mikono. Wenzake walimtazama kwa umakini. Alipomaliza pasipo hata kutia neno, wakajigawa tena katika vijikundi. Mou alienda na Chui, Amadu alienda na Farah, na Ussein akaenda mwenyewe. Hatukujua wapi walielekea, tulikuja kustaajabu wakiwa mbele ya stoo ya silaha, tena tulijua uwepo wao baada ya kudondoka chini kwa mlinzi wa eneo hilo. Alikuwa tayari anavuja damu, kabla hajapiga kelele akiwa anaenda kuchukua kifo chake, Chui alimziba mdomo mpaka akaenda. Macho yake yalielekea juu akawa kimya.
Wakati Chui akiwa anamalizana na mtu huyo, wenzake walikuwa tayari ndani wakipakuwa silaha. Walichukua za kutosha na kujaza mabegi. Lakini walipotoka ndani wapate kuondoka, mwanajeshi mmoja akawaona. Alikuwa ni mojawapo wa watu wa lindo. Salama yake kuwa hai mpaka muda ule, ilikuwa ni kukaa ndani ya kambi na si nje.
Lakini uhai huo usidumu, ukapokonywa na risasi iliyotoka kwenye bunduki yenye kiwamba cha kumeza sauti. Alikuwa ni Amadu alimlenga. Risasi ilitoboa fuvu la mwanaume huyo na kuzama ndani. Bunduki yake aliyokuwa ameibebelea begani haikumsaidia kitu. Kwa namna tukio hilo lilivyochukua nafasi, hakupewa hata muda wa kusogeza kiungo. Alianguka chini kama mzigo. Sauti ya kishindo chake kilimshitua mwanajeshi mwingine upande mwingine, sasa ikawa wazi kuwa wakina Amadu walikuwa katika hatari ya kugundulikana.
Yaani muda wowote!
Walikwepa kwa kupita njia nyembamba ili wasionekane. Lakini hawakufanikiwa kuufikia ukuta, sauti ya king’ora ikawaka. Wanajeshi walifurumuka toka ndani ya makazi wakaanza kurandaranda huku na kule. Ndani ya muda mfupi waligundua mtu wa roll call alikuwa ameuwawa, mtu wa mnara alikuwa ameuwawa, mlinzi wa stoo alikuwa ameuwawa, na watu wa zamu walikuwa wameuwawa. Haraka wanajeshi walielekea kwenye stoo ya pili kudaka silaha kisha wakasambaa ndani ya kambi.
Ila kama kuna kitu ambacho hawakuwa wanakijua ni kwamba, tayari THE GHOSTS walikuwa wamejiweka kwenye mpango be. Walikuwa wamejificha kwenye stoo hiyo hiyo ya pili wakijua fika hakuna atakayedhani watakuwa hapo. Na kweli, nani angeliwaza? Wanajeshi walifikiri wavamizi watakuwa wanahaha huku na kule kuchoropoka ndani ya kambi hiyo. Na basi huo ukawa mwanya kwa THE GHOSTS kutoka eneo hilo kwa wepesi na kudaka kuta. Walibebana wakarushiana nje. Amadu alimpa taarifa Ulsher juu ya hali hiyo kwa kubinya kitufe pembeni ya begi lake kikasafirisha taarifa mpaka kwa Ulsher kwa kulia tip tip, Ulsher akatia moto chombo na kuyoyoma.
Baada tu ya kutua chini, THE GHOSTS walitoa vikopo vyeupe ndani ya begi lao wakawa wanamwaga mchanga wenye rangi ya njano huku wakikimbia kuelekea kusini mwa kambi. Mbwa wa wanajeshi waliwafuata, lakini baada ya kunusa mchanga ule, walidondoka chini wakafa! Wanajeshi hawakuwa na mwelekeo, sasa wakawa wanakimbia wasijue maadui wameelekea wapi.
THE GHOSTS walifika mtoni, huko walikuwa tayari wamepanga magogo ambayo waliyatupia ndani ya maji ya mto wakaambaa nayo mpaka pale walipotimiza muda wa dakika kumi majini kisha wakatoka na kufuata barabara ambapo huko walimkuta Ulsher. Walikwea kwenye gari na kuondoka upesi.
Baada ya masaa kumi na mawili:
“Amesemaje?” Aliuliza Kone. Alishindwa kuvumilia aketi kwanza ndiyo aongee. Hamu yake ya kuongea na Rose ilikuwa kubwa tangu pale alipopewa muda mchache sana na Raisi apate kutimiza malengo yao.
“Kaa kwanza.” Rose alisema akitabasamu. Kone alivuta kiti akaketi. Macho yake yalikuwa yanamtazama Rose kwa kulowa na matamanio.
“Amesema niende jioni hii. Atakuwa mwenyewe na ameniandalia bonge la party,” alisema Rose kwa tambo za kike.
“Sasa hapo ndio pa kumaliza kazi, Rose,” alisema Kone. “Tusipoteze tena hii nafasi. Raisi ametupa muda mdogo sana.”
“Njia si ile ile?”
“Kama tulivyokubaliana yaani. Ile ile!”
Walipeana habari hizo na sasa matumaini ya kumaliza walichokianzisha yakiwa makubwa zaidi. Waliagiza vinywaji baridi na chakula cha bei kali. Matabasamu yalituama usoni mwao. Wakiwa wanamaliza chakula chao hicho, mara ujumbe ukaingia kwenye simu ya Rose. Ulikuwa unatoka kwa Kessy, na ulisomeka:
‘Samahani, siwezi tena kuonana na wewe kwa leo kuna jambo limetukia’
Rose aliachama mdomo kwa kushangazwa. Alimuonyesha Kone huo ujumbe, Kone akavunjika moyo. Alilalama kweli na hakujua nini kiliharibu tena hiyo sherehe. Ila baada ya muda mfupi kwenye mojawapo ya televisheni iliyokuwepo karibu, akapata kushuhudia taarifa ya habari: kambi ya jeshi imevamiwa na kuibiwa silaha!
Alijikuta anatikisa kichwa chake akasonya.
“Tutakuwa tunafanya kazi ya ubuyu kila siku. Tuwatafute hawa waasi kwanza!”
***
☆Steve