21--Nayasema haya kutokana na mambo niliyoambiwa na Sabina ambayo yaliufanya moyo wangu utetemeke kwa hofu. Niliamini kauli isemayo cheka nao lakini si wema kwako na adui yako anaweza kuwa rafiki mkubwa. Nimeamini kweli penzi hufungua moyo wa mtu na kuyatoa hata yaliyo chini ya uvungu wa moyo wake na kuwa tayari hata kufa kwa ajili ya kuyalinda mapenzi yake. Japo nilikuwa nakwenda kinyume na maadili yetu ya kujiingiza kwenye uhusiano katika umri mdogo, lakini naweza kusema ilinifungulia nisiyoyajua yaliyokuwa yakinizunguka , ambayo bila kuelezwa na Sabina binti aliyejitoa muhanga ningekufa kifo kibaya.
Siku moja baada ya kutoka shule Sabina alinieleza tusikae sehemu tuliyoizoea, nilimuuliza kwa nini, alinieleza kuna kitu anataka kunieleza ambacho kinatakiwa tuwe mbali na maeneo ya karibu na nyumbani. Tulikubaliana kama kawaida tulipita njia zetu na kukutana eneo tulilopanga kukutana kisha Sabina aliongoza kuelekea ndani zaidi ya pori.
Tulikwenda mpaka tukayaacha mashamba na kuingia kwenye pori ambalo hakukuwa na watu zaidi ya sauti za ndege. Niliamini sehemu zile kunaweza kuwa na wanyama wakali, kutokana na mwendo kuwa mrefu bila kufika nilianza kuingiwa na wasiwasi .
Sabina unanipeleka wapi? woga uliniingia na kuamini huenda kuonesha mapenzi kwangu ilikuwa njia ya kunikomesha. Niliona kama ni kweli alikuwa amenileta kimtego alikuwa amenipatia, kwa eneo lile sikuwa na ujanja wowote .
Shija wasiwasi wako nini?
Mbona tunazidi kwenda ni habari gani za kunileta huku?
Shija ungejua wala usingeniuliza ungeweza kuniambia hata tupande gari tuondoke wilaya hii twende tukazungumze sehemu ya mbali zaidi.
Ni mazungumzo gani hayo?
Utayajua, japo nilionywa nisimwambie mtu yeyote , lakini nimejikuta nikizama kwenye mapenzi yako pia nakupenda sana tusingekuwa wanafunzi ningekueleza unioe,
Sabina alisema kwa sauti ya upole.
Mmh makubwa, maneno ya Sabina yalinifanya nisihoji tena kitu na kumfuata kila alichotaka kukifanya juu yangu.
Niliridhika na maneno yake tukaendelea na safari iliyochukua nusu saa. Sabina alinieleza tukae chini ya mti wa mkalatusi, baada ya kukaa tulitulia kwa muda kila mmoja akivuta pumzi.
Baada ya kupumzika kwa muda Sabina alinitazama kwa muda usoni mpaka nikamuogopa, kilichofuatia kilikuwa machozi.
Sabina unalia nini? alinishtua baada ya kuongea machozi yalimtoka.
Shija dunia hii kweli ina siri kubwa, siamini kijana mzuri kama wewe kuna watu wanautamani uhai wako? Sabina aliniuliza huku michirizi ya machozi ikiwa mashavuni kwake .
Uhai wangu? Niliuliza kwa kushtuka kusikia vile.
Ndiyo Shija.
Mungu wangu, kwa kosa gani?
Si unakumbuka kuna siku ulihudhuria ngoma ya wachawi ?
Swali lile lilinishtua kwani kwa upande wangu nilikuwa naota, na swali lile niliogopa kulijibu kama ningelijibu basi ningekuwa nimevunja amri ya mzee Manoni ya kutomwambia mtu siri ile ya kukaa kimya kwa kila nitachokiona au kukisikia. Lakini niliamini mpaka Sabina kunileta kule basi alikuwa na siri nzito ambayo sikutakiwa kumficha ukweli wa kitu kilichokuwa ndani ya moyo wangu.
Sabina kweli nilihudhuria ngoma ya wachawi , lakini nilikuwa ndotoni, kwa mara ya kwanza nilitoa siri niliyokatazwa na mzee Manoni.
Hapana Shija, kwa watu kama ninyi ambao si wachawi huhudhuria ngoma au jambo la kichawi hupitia kwa njia ya ndoto.
Kwa hiyo kweli nilikuwa kwenye ngoma ya wachawi ?
Kweli kabisa, hata sisi tulipokuona tulishangaa sana na kujua lazima siri yetu itatoka nje. Wachawi walidhamiria wakuue ili siri ile ufe nayo.
Kauli ile ilinitisha sana na kuona kumbe kuna watu wanakufa bila makosa yoyote , sikutaka kuuliza swali nilitulia ili Sabina aendelee kunimwagia siri nzito za wachawi ambazo sikuzijua na nisingezijua. ...Lakini mzee Manoni,
kusikia lile jina nilishtuka na kuficha hofu yangu,
Sabina aliendelea kuzungumza. Lakini mzee Manoni aliwakataza wasikufanye vile kutokana na wewe kuingia bila kujua. Ila alisema atakuonya usimwambie mtu yeyote , kama utakuwa mbishi basi watachukua uamuzi huo wa kukatisha maisha yako.
Kwani mzee Manoni ni nani katika hao unaowaita wachawi ? Nilimuuliza.
Ndiye mkuu wa kanda ya wachawi .
Alaa kumbe, ehe.
Basi wachawi ambao ni wakubwa sisi ni wanafunzi ambao tumeingizwa kwa shinikizo la wazazi. Wachawi wakubwa walikubaliana kukuwekea uangalizi wa karibu pindi utakapotoa siri ile basi lazima habari wangeitapa. Wangeitana na kutoa uamuzi wa awali wa kuyachukua maisha yako.
Pale kwenu wapo watu ambao huwaoni lakini wapo kwa ajili ya kukusikiliza unazungumza nini na wazazi wako juu yetu.
Lakini ilivyoonekana hukutoa siri nje muda wote ambao ulikuwa chini ya uchunguzi mkali. Tatizo kubwa lililowatibua wakuu wa uchawi ni siku ile uliyotuita sisi wachawi kibaya zaidi mbele ya wanafunzi.
Baada ya kuwapelekea taarifa akiwemo mama yangu ambaye na yeye yumo kwenye kamati ya wachawi wa kanda ambao wapo chini ya mzee Manoni.
Ilitolewa amri ya wewe uuawe mara moja, lakini kabla ya hapo siku ulipohudhuria sherehe ya sadaka ya nyama ya mmoja wa wanachama, siku ile ndiyo uliyopitiwa usingizi darasani na ulipoamka watu wa kwanza kutuuliza tulikuwa sisi na kitu kibaya nasi tulikuwa kwenye sherehe hiyo.
Wasiwasi wetu ulikuwa lazima ungetoa siri kuwa ulituona kwenye ngoma ya kula nyama ya watu.
Sabina umeisha kula nyama ya watu? Nilimuuliza...
Itaendelea...