73--Tulitembea kwa mwendo wa dakika kama kumi na kutokea kwenye barabara kuu itokayo Musoma kwenda Mwanza. Baada ya kuiona barabara, akili yangu kidogo ilianza kupata mwanga japo bado sikuelewa ile ni sehemu gani pamoja na kuelezwa kuwa ni Kahangara
Muda ulionesha kuwa kunazidi kupambazuka kutokana na mwanga kuongezeka. Pia watu waliongezeka, kila mmoja akiwa na lake. Wakulima walielekea mashambani na wanafunzi mashuleni, pia kituoni tulipokuwa tumesimama watu wachache waliongezeka.
Kijua nacho kilianza kuchomoza kuonesha kumepambazuka. Tulisimama kituoni nikiamini kabisa watu walijua sisi sote ni wanawake . Baada ya muda, basi la kutoka Magu liliwasili. Tulipanda na kusimama kutokana na siti zote kuwa na watu.
Helena aliniuma sikio kwa sauti ya chini. Usizungumze kitu, mambo yote niachie mimi. Sawa, nilimjibu kwa sauti ya chini. Basi lilielekea Mwanza huku nikiwa bado siamini kama kweli nimetolewa kwenye umsukule japo ilikuwa tofauti na siku za nyuma Helena alipojaribu kunitoa kwenye himaya ya wachawi na kukutana na matukio ya ajabu yaliyonikwamisha .
Japo gari lilikuwa likienda, bado sikuamini kama tutavuka salama. Basi lilipofika maeneo ya Kisesa, wingu zito lilitanda mbele na upepo mkali ukaanza kuvuma na kusababisha tufunge madirisha. Wasiwasi uliniingia nikajua mambo yameiva , nilijiuliza kama nikikamatwa tena na wachawi watanifanya nini?
Haukupita muda mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilishuka. Kutokana na upepo mkali, nusura gari tulilokuwa tumepanda lianguke baada ya kuyumba na kuteleza mpaka pembeni ya barabara. Wakati huo mbele kulikuwa hakuonekani vizuri kutokana na mvua kuwa kubwa.
Moyo ulinienda mbio kwa hofu na kuamini kabisa wachawi tayari wameshatuzingira. Pamoja na kuwa na baridi kali kutokana na mvua ile ya asubuhi, mimi kijasho kilikuwa kikinitoka. Helena aliugundua wasiwasi wangu na kuniuliza:
Shija vipi? Naona mambo yameharibika. Mambo gani? We huoni mvua.
Sasa mvua imeharibu nini?
Naona kama tumefuatwa. Na nani? Si wachawi ! Shija hebu acha hofu, kwani mvua yote ni ya wachawi Lakini si unaona jinsi hali ilivyo , bado kidogo gari lianguke.
Ni hali ya mvua tu, inaonekana upepo umemfanya dereva asione vizuri mbele. Wazo la kusubiri mvua ipungue ni zuri, la sivyo anaweza kutuangusha. Barabara inateleza sana kwa muda huu. Helena ni kweli usemayo si hila za wachawi ? Walaa, niamini mimi.
Hakuna kitu chochote kibaya kitakachokutokea , kama kikitokea ni amri ya Mungu wala si wachawi . Basi niliogopa sana, nilijua ni yale yale ya siku zote. Shija usiwe na wasi, mpango huu hakuna anayeujua mpaka mama arudi kwenye mkutano, muda huo utakuwa umeshafika kwa mjomba.
Ooh, afadhali maana kwa upande wangu hali ilikuwa mbaya. Tulisubiri mpaka mvua ilipokatika ndipo tulipoendelea na safari.
Nilimshukuru Mungu baada ya kuingia Mwanza salama. Tulipanda daladala hadi Pasiansi kwa mjomba. Tulipokaribia, kutokana na maelezo ya Helena kuwa hataki kufika pale, aliomba nimuoneshe nyumba kisha tuagane. Helena, tumekaribia kwa mjomba.
Ni wapi? Nyumba hiyo hapo yenye rangi ya maziwa, nje kuna nguzo ya umeme. Sasa Shija, nafikiri kazi yangu imekwisha. Nakuomba uende salama na Mungu akulinde kwa kila jambo. Asante Helena, nawe Mungu akulinde japo najua nimekuachia mtihani mzito na mama yako.
Shija hilo lisikutie hofu, hakuna chochote kitakachotokea. Muhimu katika ahadi yangu ilikuwa ni kukulinda. Niliposhindwa niliapa kukutoa kwenye dunia ya wafu, namshukuru Mungu ahadi yangu kwako imetimia. Nashukuru sana Helena, sijui nikulipe nini?
Hakuna cha kunilipa, Shija umenifundisha vitu vingi maishani mwangu ambavyo sikutegemea kuvipata kwa kijana mdogo kama wewe . Helena busara si umri bali uwezo wa kuchambua baya na zuri na kufikisha maneno yenye kumfanya mtu apate kitu kupitia wewe bila kujali umri wako.
Shija nakuomba tena usikubali kurudi kijijini. Kwa muda huu baki kwa mjomba, pia siri hii ibakie moyoni mwako. Nitafanya hivyo Helena. Mwisho Shija nakutakia maisha marefu yenye furaha, kwa vile nimepajua nitakuja siku moja, kwa heri! Msalimie mjomba, mkewe na wadogo zako.
Helena alisema kwa sauti ya majonzi huku machozi yakimtoka , kitu kilichofanya nami nitokwe na machozi.
Asante Helena, nawe nakutakia harusi njema na Mungu akuepushe na nguvu za kichawi. Asante Shija. Tulikumbatiana kabla ya kuagana, tulishikana kwa muda huku kila mmoja akilia kilio cha kweli.
Baada ya kuachiana, Helena alisema kwa sauti ya mafua kutokana na kutokwa na kamasi nyembamba.
Shija nakupenda sana, hata sijui moyo wangu umeuwekea kitu gani.
Nimekubali kuolewa kwa vile nauchukia uchawi lakini bila hivyo nisingeolewa kamwe, ningekusubiri.
Asante Helena kwa kunipenda, hata mimi nakupenda na nitaendelea kukupenda siku zote za maisha yangu. Nakuona ni zaidi ya pumzi ninazovuta. Helena olewa ukijua Shija anakupenda sana.
Na Sabina? Helena aliniuliza swali la uchokozi.
Wote nitaendelea kuwapenda kama tulivyokuwa tukipendana tukiwa shule ya msingi. Asante Shija, kwa heri, Helena aligeuka na kuondoka huku akilia kilio cha kwikwi , kitu kilichoniacha njia panda. Nilitaka kumwita lakini mdomo ulikuwa mzito.
Nilimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea machoni mwangu. Nilisimama kwa muda nikijiuliza Helena kanifikisha mpaka jirani kwa mjomba, sawa lakini swali kubwa ni mjomba atakaponiona atanipokea vipi? Niliamua niende tu, mengine yangejulikana huko huko.
Nini kitaendelea, mtu aliyekufa akionekana mzima itakuwaje, fuatilia mwisho ya simulizi hii