SoC03 Nitafurahi kuona uboreshaji wa mfumo na muongozo wa utoaji wa taarifa za Kiserikali nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Hamza Nsiha

JF-Expert Member
Jul 25, 2022
208
191
Uboreshaji wa Mfumo na Muongozo wa Utoaji wa Taarifa za Serikali nchini Tanzania.

Utangulizi.
Habari ndugu wana JamiiForums! Karibuni tujumuike katika chapisho hili lenye lengo la kuchunguza na kutoa mapendekezo kwa nia njema juu ya taifa letu, hususani katika sekta inayohusika na utoaji wa taarifa za serikali kama kipengele muhimu kinachoathiri uwajibikaji na utawala bora wa viongozi kwa ujumla.​

Mfumo wa Utoaji Taarifa.
Mfumo wa utoaji taarifa katika taifa ni moja ya nguzo muhimu inayosaidia kuunganisha serikali na watu wake katika namna mbalimbali. Kila taifa huru lina mfumo maalumu ambao ni mahususi kwa ajili ya kuhakikisha taarifa muhimu kuhusiana na masuala mbalimbali zinawafikia wananchi wake kwa wakati sahihi. Hivyo, Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine, hutumia njia mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wake wanapata taarifa mbalimbali ambazo ni muhimu katika kuimarisha shughuli za utendaji baina ya viongozi na watu wake.​

Kiu ya Kuona Mfumo Madhubuti.
Kwa ajili ya taifa langu, ninatamani kuona mfumo au muongozo madhubuti wenye kasi ya kupenyeza taarifa muhimu kwa wananchi wake. Binafsi, ninaweza kutoa shukrani zangu za dhati kwa sekta ya habari na mawasiliano juu ya jitihada zinazofanyika, lakini nitafurahi pia endapo nikishiriki katika kuinua sekta yetu nyeti kwa kuainisha baadhi ya changamoto ambazo ni dhahiri zinaathiri sekta yetu.​

Je! Kumekuwa na changamoto gani katika mfumo wetu wa utoaji wa Taarifa nchini?.
  • Kumekuwa na sauti nyingi zinazoibua taarifa tofauti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiserikali. Ni ukweli usiopingika kuwa mfumo wetu wa utoaji wa taarifa za serikali bado haujafanikiwa kwa kina katika kufikisha taarifa zake kwa wakati, hivyo huibua taarifa zingine kutoka kwa watu ambao baadhi yao huwa ni wapotoshaji.​
  • Uwajibikaji na Uelewa wa Wananchi. Baadhi ya wananchi hususia taarifa muhimu za kiserikali kabla hata ya kutafakari na kuchanganua taarifa hizo kutokana na ukosekanaji wa uwajibikaji wa baadhi ya masuala yanayohitaji kufanyiwa kazi. Hii inaleta changamoto ya kutoa majibu sahihi kwa maswali yanayosalia na hivyo kuacha mkanganyiko kuhusu taarifa hizo.​
  • Uwazi na Mfumo Sahihi wa Utoaji Taarifa.Ukweli ni kuwa, mfumo wetu bado haujaainisha mtiririko sahihi wa ufikishaji wa taarifa kwa wananchi wake. Licha ya kuwepo kwa msemaji mkuu, baadhi ya taarifa nyeti za serikali hupitia mlolongo mrefu mpaka kuwekwa wazi, na hii inaweza kuwafanya wananchi kuhisi kama njia mojawapo za kufichwa kwa taarifa.​
  • Lugha Ngumu na Uelewa. Baadhi ya taarifa huhuchukua muda mrefu kung'amuliwa na baadhi ya wananchi kutokana na matumizi ya lugha ngumu ambayo inawafanya washindwe kufahamu taarifa hizo. Mfano, wananchi wengi hupenda kuzungumzia taarifa ambazo hawajazielewa kiundani zaidi.​

Athari za Mfumo Hafifu wa Utoaji Taarifa za Serikali.
Mfumo hafifu wa utoaji taarifa za serikali unaweza kuwa na athari kadhaa katika nchi, kama vile:

Upungufu wa Uwazi: Mfumo hafifu wa utoaji taarifa unaweza kuathiri uwazi wa taarifa na uwezekano wa umma kupata habari muhimu kuhusu shughuli za serikali, miradi ya maendeleo, na matumizi ya rasilimali za umma. Hii inaweza kusababisha ukosefu wa imani kutoka kwa umma na kuongeza tuhuma za ufisadi na ubadhirifu.

Ucheleweshaji wa Taarifa: Mfumo usio na ufanisi unaweza kusababisha ucheleweshaji wa taarifa muhimu kufikia walengwa wake kwa wakati unaofaa. Hii inaweza kuathiri maamuzi na mipango ya kitaifa na kikanda.

Kupungua kwa Uwajibikaji: Mfumo hafifu unaweza kusababisha kupungua kwa uwajibikaji kwa maafisa wa umma na taasisi za serikali. Wakati taarifa muhimu zinapofichwa au kucheleweshwa, inakuwa vigumu kuwawajibisha wale ambao wameshindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Kukwamisha Maendeleo: Mfumo wa utoaji taarifa usio na ufanisi unaweza kusababisha kukwamisha kwa maendeleo ya kitaifa. Bila taarifa sahihi na za kutosha, ni vigumu kufanya maamuzi sahihi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.

Hivyo, nina matumaini kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha na kuinua mfumo wa utoaji wa taarifa za serikali kwani ndio nguzo kuu ya kujenga Tanzania yenye amani, upendo na maendeleo kwa watu wake.

Mapendekezo katika mfumo wa utoaji taarifa.
  1. Kuongeza jitihada katika uchakataji na utoaji wa haraka wa taarifa mbalimbali ili kupunguza sintofahamu kwa wananchi pia kuwaziba midomo wananchi wenye taarifa za upotoshaji.​
  2. Kuimarisha Mifumo ya Kusikiliza Umma kwa kuanzisha mifumo madhubuti ya kusikiliza maoni na malalamiko ya wananchi kuhusu masuala mbalimbali ili kuboresha uwajibikaji na kutatua changamoto za kijamii.​
  3. Kuongeza jitihada katika uwazi wa shughuli mbalimbali za serikali ili kuondoa baadhi ya maswali kwa wananchi. Serikali inaweza kuweka viwango vya juu vya uwazi katika taasisi zake na kuhakikisha taarifa zinazohusiana na matumizi ya rasilimali za umma, miradi ya maendeleo, na sera zinapatikana kwa umma bila kuchelewa, hii itasaidia pia kuongeza imani kwa wananchi dhidi ya taifa lao.​
  4. Kukuza Vyombo vya Habari Visivyokuwa vya Kiserikali kwani taarifa nyingi zimekuwa zikiwafikia wananchi kupitia vyombo hivyo. Hii ni pamoja na kutoa nafasi kwa vyombo vya habari huru na visivyokuwa vya kiserikali kushiriki katika utoaji taarifa ili kukuza uhuru wa vyombo vya habari na kuleta mitazamo mbalimbali katika jamii.​
  5. Pia, kuna umuhimu wa kudumisha mtazamo chanya na kutumia maneno sanifu katika kupokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wananchi. Mfano, kuna baadhi ya viongozi hutumia maneno makali kuwashambulia baadhi ya watu wenye nia ya kuelewa kiundani baadhi ya taarifa. Mfano, kutumia maneno kama ma-mbumbu, wajinga au wasiojitambua.​
Hitimisho.
Nikiwa kama kijana mzalendo wa taifa langu, ninao wajibu wa kushirikiana na wananchi wenzangu kwa nia njema ya kushikamana na serikali yangu kwa minajili ya kujenga nchi yangu.

Sambamba na yote, chapisho langu halina maana kuwa linakosoa mfumo wetu wa utoaji taarifa za kiserikali. La hasha! Chapisho langu linalenga hasa katika baadhi ya maeneo ambayo ninaimani endapo tukishirikiana kwa pamoja basi tunaweza jenga na kuikuza zaidi Tanzania yetu. Kwani, Mawasiliano ndio nguzo kuu inayounganisha watu pamoja na serikali yao hivyo kuongeza uwajibikaji sambamba na utawala bora.

Ni kiu yangu kuona taifa langu lenye amani na upendo, likisonga mbele kupitia ushirikiano bora baina ya taifa na watu wake. Tuzidi kuungana na kuchangia katika kuboresha mfumo wa utoaji taarifa za serikali ili kufikia malengo yetu ya maendeleo na utawala bora. Asanteni sana!
 
Andiko zuri sana, lakini ningefurahi endapo ungewataja kwa majina hao wanaokuwa wakali pindi watu wanapoulizia taarifa fulani......😂
 
Andiko zuri sana, lakini ningefurahi endapo ungewataja kwa majina hao wanaokuwa wakali pindi watu wanapoulizia taarifa fulani......😂
Asante sana! Lakini tushirikiane kujenga taifa letu ndugu, sio vema kutaja majina lakini ni suala la kukumbushana tu mkuu.
 
Kiukweli kuna haja ya kuboresha mfumo huu, maana wananchi wengi huwa tunatamani kupata taarifa lkn zinachelewa sana kutufikia mpaka waone tumelalamika sana. Hongera ndugu yangu
 
Kiukweli kuna haja ya kuboresha mfumo huu, maana wananchi wengi huwa tunatamani kupata taarifa lkn zinachelewa sana kutufikia mpaka waone tumelalamika sana. Hongera ndugu yangu
Asante kaka, Tanzania ni yetu sote hivyo manufaa ni kwetu sote pia
 
Back
Top Bottom