SEHEMU YA 2:
Eliza alikunjua karatasi ndogo tena, akasoma maneno hayo matatu kwa woga:
"MIMI NYUMA YAKO."
Ghafla, hakuweza kupumua. Hii haikuwa hadithi ya kutungwa. Mtu hakuwa nyuma yake tu;
alikuwa ameshafika mlangoni mwake. Mtu huyu alikuwa anatembea nyuma yake, alisimama wakati alipokuwa amesimama, na alikuwa amesubiri hadi alipofunga geti ndipo akaiweka karatasi.
Kwanini aliweka karatasi pindi tu Eliza alipofunga geti? Je aliwezaje kufanya hivyo na kwanini alionesha nia kumtisha zaidi?
Eliza alitupa karatasi hiyo chini kama alikuwa ameshika moto. Alifungua mlango wake kwa kasi, akajirusha ndani, na kufunga mlango kwa
funguo zote mbili alizokuwa nazo. Alivuta pazia zote za dirisha sebuleni.
Nyumba yake ilikuwa tulivu, kimya, ikiwa na giza. Alikimbilia jikoni, akachukua kisu kirefu kutoka kwenye droo, na kurudi sebuleni. Kisu hicho kilitoa mwanga hafifu wa taa za nje.
"Lazima nipige simu polisi," alijisemea, sauti yake ikitetemeka.
Alichukua simu yake, lakini ghafla akahisi ugumu kuipiga namba. Alikuwa akipiga simu kuhusu nini hasa? Karatasi? Polisi wangemwona kama mwanamke mwenye hofu, akiona vivuli.
Eliza alijipiga moyo konde. Alikuwa
salama ndani. Hakuna anayeweza kuingia.
Alikwenda kwenye chumba chake cha kulala, akakiacha kisu chake kwenye meza ya kando ya kitanda. Alijaribu kulala, lakini kila sauti ndogo nje ya nyumba—mbwa akibweka mbali , upepo ukipiga mlango—ilikuwa kama hatua za yule mfuatiliaji.
Alilala kwa shida.
Usiku ulikuwa umeenda mbali. Ilikuwa karibu
Saa Tisa Usiku.
Sauti.
Sauti iliyomtia baridi:
kioo Cha dirisha lake kikasuguliwa taratibu.
Eliza alisimama wima kitandani. Akachukua kisu chake kimyakimya.
Alitembea polepole kuelekea sebuleni. Alisogea hadi kwenye dirisha kuu, ambapo alikuwa amefunga
pazia zito la bluu.
Sauti ilitoka hapo. Mtu alikuwa nje, kama akifanya kitu kwenye
dirisha lake.
Eliza alishikilia kisu kwa mikono miwili, akijibana kwenye ukuta. Alihisi jasho la baridi likimtoka mgongoni.
Akasikia
'mkoromo' mfupi, wa chini, kama mtu akipumua
Kisha, sauti ya mwisho—
'kliki'—ya komeo la dirisha likifunguliwa.
Pazia lilibaki limefungwa, lakini Eliza alijua. Dirisha lilikuwa wazi.
Ghafla, akahisi upepo mdogo. Upepo uliokuwa na harufu ya
dongo jipya la sigara.
Alibana kisu chake. Alifikiria kukimbia, lakini mwili wake ulikuwa umeganda.
Kivuli cheusi, kikubwa, kilianza kuonekana kwenye pazia.
Kivuli cha mkono. Kinaingia.
Kivuli cha Mkono huyo kilishika pazia, na kwa muda mfupi sana, Eliza aliweza kuona kupitia ufa mdogo uliotokea.
Aliona kitu kilichomtia hofu zaidi ya kitu chochote alichowahi kukiona maishani mwake.
Badala ya uso wa mwanadamu, aliona uso uliokuwa umefunikwa kwa
barakoa nyeusi laini, ambayo ilibana na kuonyesha umbo la fuvu. Macho yake mawili tu yaking'aa kwenye giza.
Na kisha, sauti ilikuja,
haikunong'ona, ilikuwa kama pumzi iliyotolewa kwa shida, kutoka nyuma ya pazia, mita chache kutoka kwake:
"Nilikuambia..."
Itaendelea