Ni tamaduni na mazoea au asili? Maana kuna sababu za kibailojia ulizitaja awali.
Asili hujenga tamaduni na mazoea.Mazoea na tamaduni ya kujengwa na asili yaweza kuanza kwa kutumia maarifa madogo tu, kwa sababu jamii hutoka kwenye maarifa madogo na kwenda kwenye maarifa makubwa kadiri muda unavyozidi.
Kadiri jamii zinavyotoka kwenye maarifa madogo na kuzidi kuelekea kwenye maarifa makubwa, ndivyo wanajamii wanavyotakiwa kumulika mapokeo yote ya tamaduni na mazoea.
Maarifa madogo yalifanya atu waamini kwamba dunia ni bapa, kwa kuiangalia kwa macho yenye kuona masafa mafupi kwa ukungu wa asili, baada ya kuendelea watu walipata kujua kwamba dunia ni tufe, si ubapa.
Habari ya kufikiri kwamba dunia ni ubapa ni ya asili zaidi ukiangalia kwa masafa mafupi, ni habari rahisi zaidi. Inajibu maswali rahisi kirahisi zaidi. Lakini ukweli ni kwamba asili ina asili ya kutoa na muonekano uliojaa hadaa. Kinachoonekana bapa kumbe ki mviringo, kinachoonekana kidete kikawa kitupu (solids matter is 90% empty space - see atomic theory) kinachoonekana kitupu kikawa kidete (a "vacuum" can spring virtual subatomic particles out of nowhere).
Kwa hivyo basi, tukiiangalia asili, tusiidhalilishe kwa kufikiri tunaielewa vilivyo. Kwa sababu tumeshaona kwamba ina tabia ya kutushangaza kwa kile Waingereza wanachokiita kuwa "counterintuitive". Unaona ndivyo kumbe sivyo, na sivyo kumbe ndivyo, kama Alice katika "Alice in Wonderland" na "Through the Looking Glass".
Bado naendelea kuisoma asili, nafurahishwa sana na quantum physics kama umeona natoa mifano mingi inayohusiana nayo. Inaweza kutoa mafunzo mengi sana kuhusu jinsi gani asili - au tunachofikiri kuwa asili- inavyoweza kutuhadaa.
Uzuri wa sayansi unatokana na utamaduni wa kubishana mpaka pumba zinawekwa pembeni na watu wanaona mchele ni upi.
Mpaka kesho nasoma watu wanafanya majaribio ya kuongezea nadharia za relativity za Albert Einstein, ingawa zimesimikwa kwa majaribio yaliyofuatana katika miaka 100 iliyopita.
Kwa hivyo siwezi kuona ugumu kuchambua umakini wa kufanya mambo kwa kile tunachofikiri ni asili tu.
Hata uwezo wa kufikiria mambo haya na kuyaparaganya ni asili pia.