Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Sehemu ya Kumi na Tano (Extended):

Msiba wa Zai uliniletea polisi malangoni mwangu.

Polisi wale walikuja kunihoji kuhusu namna ninavyomjua mwanamke yule na pia kuhusu makazi yake pale nyumbani kwangu.

Niliulizwa maswali kadhaa, na Amiri pia, walipomaliza walijiendea wakaja kuniita tena siku nyingine baada ya kumalizika kwa msiba wa Zai.

Polisi wale, kwa maelezo waliyokusanya kwa majirani, ndugu yake Zai na pia mimi, walihitimisha kuwa Zai alianguka akajiumiza vibaya nyuma ya kichwa chake, kuhusu kuoza mapema kwa mwili wa marehemu, kwakweli sikupata kusikia maelezo yao yenye maana.

Siku ya mazishi ya Zai, nami nilihudhuria kama sehemu ya mfiwa, tena mfiwa wa karibu, nilivalia nguo zangu za msiba, gauni jeusi na kichwa nilichokifunga na kiremba cheupe.

Nililia na kugugumia kadiri nilivyoweza, na kwa mujibu wa imani ya Zai, msiba ule haukuchukua muda mrefu Zai akaenda kuzikwa, sikupata hata kumwona kwa mara ya mwisho, sikupata hata kuhudhuria mazishi yake.

Ni baada ya kuzikwa kwake ndipo nilipata kuja na kuweka shada yangu juu ya kaburi lake, shada ya maua, shada iliyoandikwa RAFIKI kumuaga mwanamke yule alokuwa amevaa ngozi ya rafiki kwangu.

Sikuwa najua nilie kumwomboleza ama nilie kwa furaha ya kumpoteza ... kumpoteza mtu alokuwa ananichoma gizani.

Niliona nitimize tu sheria, mbele ya macho ya watu mimi ni rafiki wa Zai, sikutaka kukaa visogoni mwao, nisipofanya haya si n'taonekama nilitaka mwanamke yule afe?

Watu hawatadhani kuwa mimi nimemuua?

Acha nipendezeshe mboni za macho yao, moyo wa mtu kichaka cheusi, kwani itanigharimu kiasi gani?

Nikimaliza hapa maisha yangu yataendelea kama kawaida, niliwaza na kutumai.

Nilitegemea maisha yangu sasa yatakuwa kama ya watu wengine, nami narejea kuishi kama binadamu wa kawaida, lakini kumbe nalikuwa najidanganya, bado kazi ilikuwa kubwa sana mbele ya paji langu la uso.

Mengine yalikuwa yakiningoja kwa hamu ya kwamba hilo likiisha basi na sisi tupate nafasi.

Baada ya msiba huo, niliendelea na maisha yangu kama ada, kama tujuavyo maisha hayasimamishwi na kitu chochote kile, baada ya kama juma moja hivi nikapata kuonana na mama yake Anwari, mama huyo alikuwa anaendelea kunisumbua kwenye simu na mimi nikaona ni vema nikakutana naye kwaajili ya kuweka mambo kadhaa sawa.

Mama huyo aliniambia amefurahi sana kuonana na mimi kwani baada ya kifo cha Zai hakutarajia kama makutano yale yangefanyika tena.

Alisikitishwa sana na kifo cha Zai na alinambia wazi kuna baadhi ya makubaliano baina yake na mwanamke huyo hayakupata kutimia mpaka kifo chake, kifo kilimnyakua kwa kasi sana, kasi ambayo hakuitarajia, na sasa basi jambo hilo limemwachia funzo kubwa, kufanya yale yote yanayowezekana upesi sana.

Mojawapo ni lile lililomfanya akaniita hapo.

Alinambia Anwari alimweleza vema kuwa ana mtoto, mtoto wa kiume, na mtoto huyo amezaa na mimi, hivyo angependa kumwona mjukuu wake kabla hajafungasha kwenda zake Marekani ambako ndipo alipokuwa anaishi kimakazi.

Aliniahidi atamhudumia mtoto huyo kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake, muhimu amwone na watambuane, anaomba sana sana, hana mtu mwingine isipokuwa mtoto huyo kwani Anwari ambaye alikuwa ni mwana wake wa pekee, sasa hayupo tena duniani.

Familia pekee ni huyo mtoto wangu.

Alisema, "Magreth, najua wewe na Anwari hamkuwa katika maelewano bora, alinambia hilo, mlihitilafiana kila mmoja akashika ya kwake lakini kiukweli kabisa, tangu nimfahamu Anwari hamna mwanamke aliyewahi kumpenda kama wewe.

Siku zake za mwisho juu ya uso wa dunia alikuwa akinishuhudia sana jambo hilo, namna anavyoumia kukukosa, na ninaamini kabisa kama bado mngalikuwa wote basi asingelipatwa na maswahibu kama yale."

Mwishowe akanieleza tofauti zetu mimi na Anwari zisiingilie na kuharibu maisha ya mtoto kwani yeye hana hatia, baada ya hapo sasa akanipatia wasaa wa mimi kuongea, kwani muda wote huo nilikuwa namskiza tu kama mbwa bwege mbele ya bwana wake.

Nilianza kwa kumuuliza, tena nikiwa nautazama uso wake, ya kwamba ana hakika gani kama mtoto yule nilonae ni mtoto wa mwanae?

Nilimwambia kwa kukaza sauti yangu kwa msisitizo, mimi ni mke wa mtu kwa muda sasa na Anwari nilishaachana naye kitambo ya reli ya mjerumani, mtoto wangu nimempata ndani ya ndoa na hivyo ni halali ya bwana Mgaya pekee.

Sitaki kuharibu ndoa na familia yangu niliyoijenga kwa damu na jasho jingi, mambo ya Anwari nishayazika kule Kinondoni, sitaki kuyasikia wala kuyaona.

Na siku hiyo tuloonana basi ndo' iwe mwanzo wa mwisho wetu kwenye makutano, sina haja ya kuonana naye tena labda kama ni msiba, huo siwezi kuukwepa ni wajibu wetu kuuhani, lakini mengineyo basi aniwie radhi.

Mwanamke huyo alijaribu kuongea lakini sikutaka tena kumsikia, masikio niliyafunga, nilimuaga naenda zangu nyumbani kwani nina mambo mengi yananingoja, muda wa kuketi na vikao ushaniisha.

Kwasababu hiyo, mama yake na Anwari alinikabidhi 'business card' yake akanambia pale nitakapopatwa na haja ya kuwasiliana naye basi nisisite kumtafuta.

Yeye anasafiri, atakaporejea panapo majaliwa basi atafanya jitihada zingine za kuonana na mimi.

Nikasema 'haya', haya ya kinafki, alimradi mwanamke huyo hapajui ninapoishi na mawasiliano yetu ni ya simu tu, hakuna cha kuhofia, nikisham-block tu basi pepo yangu hii hapa.

Nilirejea nyumbani nikiwa na mwili mzito kweli, uzito wa uchovu, hivyo nilipofika niliongoza moja kwa moja bafuni ili nipate kuoga nipate akili mpya.

Nikiwa naoga, nikawa nayatafakari yale ya mama Anwari na kikao chake, nikajikuta natabasamu mwenyewe, tabasamu la dhihaka.

Niliona pambano hilo kama mbegu ya haradali katika kiganja cha binadamu mtu mzima, ni kitu kidogo mno, nikifumba tu vidole vyangu basi na yote yanakuwa yamekwisha.

Nikiwa naendelea kuoga na kuwaza huku najipapasa huku na kule kujisafisha mwili wangu, mara nilihisi jambo nyuma ya kiuno changu.

Nilijipapasa hapo na vidole kujikaguakagua nikabaini kuna kama alama mbili ama tatu za michubuko, michubuko midogo midogo ambayo sikuelewa nimeitolea wapi.

Michubuko hiyo haikuwa na maumivu bali alama zake zilikuwa dhahiri.

Nilimalizia kuoga nikatoka bafuni, moja kwa moja mpaka kwenye kioo kikubwa cha kabati la chumbani kwaajili ya kujikagua.

Nilijitazama mwili wangu taratibu nikabaini alama zile ni chale, si kingine.

Nikajiuliza nimezipatia wapi?

Kweli nifikiri kama nitakumbuka kitu lakini hamna nilichoambulia, sikukumbuka mahali wala mtu alonichanja chale zile.

Ajabu tena wakati najipaka mafuta mwilini, nikagundua nina chale zingine chini ya kiganja changu cha mkono wa kushoto, hapa kwenye maungo ya mkono, nikahamaki kwa namna hiyo ya ajabu.

Mambo gani haya?

Nilikagua karibia kila eneo la mwili wangu kwa mara nyingine tena, kwa umakini zaidi, hatua kwa hatua, nikaona hamna kitu kingine zaidi ya zile alama mbili.

Niliamini alama zile nimezipata usiku wa nyuma yake, kama isingelikuwa hivyo basi ningeshaligundua mapema.

Nilijivesha nguo nikatoka kwenda zangu sebuleni, kabla ya kufanya kitu kingine nikaona nimtafute kwanza mtoto ili nipate kumsalimu maana sikuonana naye tangu nilipofika.

Nilimtafuta kule nje sikumwona, kule mabandani pia sikumwona, lakini sio mwenyewe, Amiri pia hakuwapo machoni pangu, hivyo basi nikaamini watakuwa wako pamoja.

Kilichonifanya niamini hivyo ni jinsi watu hao wawili walivyokuwa wamejenga mahusiano yao kwa muda ule.

Mwanangu alikuwa akitumia muda wake mwingi kuwa na Amiri, wakicheza na kuzurura, kiasi hakuwa na muda na mimi kabisa.

Hata kumtwaa kwenye mikono ya Amiri ilikuwa inaniwia ugumu, na kwasababu haikuwa inaniathiri kitu, basi sikuona ubaya wa jambo lile.

Nikaendelea ma shughuli zangu nikingoja,

Nikingoja wawili hao watakaporejea.

Nilishika hiki nikashika kile, sikutaka kukaa kivivu, nilojitumikisha na mambo kadhaa lakini bado nilihisi mwili wangu hauko sawa.

Mwanzo nilidhani ni uchovu na ndo' maana nilioga upesi kuanza upya lakini sasa nikabaini mawazo yale hayakuwa sawa, haikuwa uchovu, ilikuwa ni kitu kingine kinasumbua mwili wangu.

Na nilihofia kitu hiko kisije kikawa na mahusiano na chale zile nilizopachikwa mwilini.

Niliogopa kiasi kwamba nikaanza kusali kumwomba Mungu aniepushe na kadhia yoyote ya walozi, mipango yao ikome na isifanikiwe kabisa katika mwili wangu.

Baadae, kama nilivyokuwa natarajia, Amiri alirejea nyumbani akiwa ameongozana na mtoto kando yake.

Walikuja wakanisalimu na Amiri akanieleza kule walipotoka, alinambia wametoka machungani kisha wakapitia dukani kununua peremende anazopenda mtoto.

Nilimuuliza mwanangu juu ya hali yake, akanambia yuko vema, nami niliona hivyo, alikuwa mwenye furaha kiasi cha kunifurahisha na mimi pia.

Nilimshukuru Amiri kwa kukaa vizuri na mwanangu, naye hakujali sana, akanambia anapenda sana kukaa na kucheza na watoto, hivyo akibaki naye hufurahia sana.

Baada ya maongezi hayo mafupi, Amiri alienda zake akaniacha na mtoto.

Baadae, wakati wa kulala, punde tu baada ya kuoga, mtoto alidai kwenda chumba cha Amiri kulala huko.

Mwanzo nilidhani utani tu, utoto unasumbua, lakini ajabu mtoto hakuacha kusisitiza kuwa anataka kwenda kule.

Alipoona hatuelewi kwa maneno ya kawaida, alianza kulia kwanguvu akitaka ombi lake likubaliwe, nilipuuzia kilio chake nikidhani atanyamaza kisha alale lakini sikufanikiwa, aliendelea kulia na kulia, akibadili tu mitindo lakini hanyamazi.

Mwishowe bwana Mgaya alinitaka nimpeleke mtoto huko anapopataka, yeye amechoka na kazi, anataka kupumzika na atapumzikaje ingali mtoto analia muda wote?

Nikafanya kama atakavyo.

Nilienda kugonga mlango wa chumba cha Amiri kwa mara kadhaa, Amiri hakuitika, kumbe hakuwamo ndani.

Nilipogonga vya kutosha pasipo majibu, nilienda kumtafuta nje ili nimpe taarifa ya ugeni wa mtoto, napo huko nje sikumwona.

Niliita kwa sauti ya usiku, Amiri Amiri, hakuitikia, si uwanjani wala kule mabandani.

Nilisimama nikatazama mabanda, natamani kwenda huko lakini kiza chake kinanitisha, nikawaza mtu anaweza kuwamo humo kweli? Sidhani, kama angalikuwapo basi angalisikia sauti yangu inayoita.

Lakini kabla sijaondoka, nikasikia sauti kali ya kuku wakilia - KWAA - KWAA- KWAAAAH! Nikashtuka kweli.

Kulikuwa ni kimya sana, kimya cha usiku, na sauti ile ililia kwa ghafla sana tena nikiwa natafuta utulivu wa kujua Amiri alipo.

Mapigo yangu ya moyo yaliruka sababu ya woga, woga kweli, nikaona sasa ya kule nje yanatosha acha nirudi zangu ndani.

"Mama," sauti iliniita, kutazama mlangoni nikamwona mwanangu akiwa amesimama hapo, urefu wake umemfanya aguse kitasa cha mlango, macho yake makubwa ameyarusha kwangu, kwangu nikiwa narejea kuendea mlango niingie ndani.

"Unafanya nini huku nje?" Nilimuuliza, akanambia kwa sauti yake ya kitoto, Amiri yuko ndani.

Nikaongozana naye mpaka chumbani, kweli nikamkuta Amiri akiwapo huko, alinisalimu akaniuliza kama nilimtafuta kisha akanambia yeye alikuwamo ndani muda wote, ningegonga vizuri angesikia.

Sikutaka maongezi mengi, nikamwelekeza aketi na mtoto wangu usiku huo kwani haachi kulialia, kesho asubuhi nitakuwa naye kumsaidia, pasi na tabu akaridhia na usiku huo ukapita hivyo.

Sikusikia tena sauti ya kuku wala ya mtoto akilia.

Kulikuwa kimya.

Ukimya wa usiku.

Nami sikuchukua muda nikapitiwa na usingizi mkali kweli, sijui kama nilijigeuza usiku huo, nikajikuta asubuhi tena ya saa tatu, tayari bwana Mgaya ameshaenda kazini na tayari Amiri ameshaamka na kushika kazi zake.

Hamna nilichoandaa, wala hamna nilichoshika mpaka muda huo.

Nilijikokota kwenda jikoni kuandaa angalau chai, nilipoweka sufuria jikoni nilijilaza kwenye kochi kungoja chai yangu iwe tayari, ajabu nilipitiwa na usingizi papohapo, Amiri anakuja kuniamsha tayari chai imekaukia jikoni, sina hili wala lile!

Jiko zima limeparwa na harufu, harufu kali ya viungo vya chai, harufu hiyo ikanitibua kichefuchefu nikakimbilia nje upesi kwenda kutapika.

Hapo ndo' nikafahamu sikuwa sawa, kuna kitu mwilini mwangu, nilidhani ningekuwa sawa baada ya kulala na kuamka lakini haikuwa hivyo.

Nilifanya jitihada za kujikagua mwili, nikabaini tayari nina ujauzito, ujauzito ambao bila kipingamizi ulikuwa ni wa bwana Anwari.

Nikalegea kwa kukosa nguvu.

Sasa nafanyaje?

Sikujua.

Akili yangu iligoma kufanya maamuzi.

Baadae ndo' nikawazua niitoe mimba ile, niitoe kabla haijamea na kuanza kunisumbua, lakini, nikajiuliza, nikiitoa na bwana Mgaya akabaini hilo haitaniweka matatani?

Nilisita.

Niliogopa kuzua mambo mapya hapa, nikaona ni vema nitulie kwanza kuwazua na kuyasoma mazingira, nichague jambo sahihi.

Niliendelea na kazi zangu, japo kwa kujivutavuta. Hamna kitu kinaboa kama mimba changa, hukupelekesha na kukutumikisha.

Nilijitahidi nisionenyeshe dalili zozote mbele za macho ya watu lakini kwa Amiri nilifeli, tena nilifeli siku ileile nisiuvute hata muda zaidi.

Nakumbuka kijana huyo aliniuliza, kama kawaida yake, uko sawa? Mbona unaonekana kama unaumwa? Nikamwambia niko sawa, lakini akaniuliza tena mbona natapika?

Kumbe aliniona nikiwa natapika?

Nilishangaa.

Nikajitetea ni tumbo tu lilinivuruga ila kwa sasa niko sawa, hamna taabu, baada ya maelezo hayo akaondoka zake.

Baadae bwana Mgaya alirejea nyumbani, kama kawaida na majira yake, kwenye gari akiwa amenibebelea zawadi na vitu kadhaa kwaajili ya mifugo, kama sijakosea mifuko kadhaa ya multi-vitamins ambayo Amiri aliipakua na kuipeleka bandani.

Siku hiyo, bwana Mgaya alinishangaza kidogo, si kwamba alibadili ratiba yake, la hasha, kama ilivyo kawaida alienda kule bandani kwa muda mfupi kisha akarejea ndani kujumuika na familia.

Baada ya kupata chakula cha usiku, tulielekea chumbani na huko ndo' alinianzisha maongezi ambayo kwa namna fulani yalinitikisa akili yangu.

Sikuelewa alikuwa anawaza nini lakini maswali yake yalinionyesha kuna jambo fulani anafahamu, jambo ambalo halikumkaa vema na yeye.

Aliniuliza kuhusu mazishi ya Zai, nikastaajabu kidogo, kwani mazishi hayo yalishapita na hakuna kitu aliwahi kunigusia, imekuaje leo?

Nilijitahidi kuhimili mshtuko wangu, nikamjibu kawaida kadiri nilivyoweza.

Baada ya hapo aliniuliza kuhusu utata wa kifo kile cha Zai akinitaka nimweleze hatma ya kifo kile kwenye marejeleo ya mpelelezi, napo nikastaajabu tena, kunani hii mada?

Nilianza kujiuliza maswali mengi kichwani mwangu nisipate majibu yake.

Nilijitahidi kumeza taharuki yangu, kwa hali yote, nikamjibu kwa vile nilivyokuwa nafahamu, namna ileile ambayo polisi walisema.

Baada ya hapo bwana Mgaya akaniuliza akiwa ananitazama na macho ya njia panda kama nilikuwa nafahamu chochote kuhusu kifo cha Zai kabla ya kutokea kwake, swali hilo likanifanya nishindwe kujihimili tena, nikaonyesha taharuki yangu mbele ya uso wake.

Nilimuuliza, "kwanini unaniuliza hivyo?"

Hakutaka kusema wazi.

Alisema anataka tu kufahamu kama kuna lolote au lah.

Nilipomjibu sikufahamu kitu, akaniuliza na vipi kuhusu kifo cha mama yake? Je, nilikuwa nafahamu chochote kabla ya kutokea kwake?

Hapo 'alarm' ikaita kichwani mwangu, maswali haya si bure, ni wazi kabisa kuna kitu.

Ila ni kitu gani?

Kitu gani kilichomfanya aniulize kuhusu vifo vya wale watu wawili? Kitu ga ...

Haraka akili yangu ikanirejesha kwenye kitu kimoja kilichojiri kabla ya vifo hivyo viwili kupata kutokea.

Nacho si kingine bali zile ndoto!

Kumbe bwana Mgaya hakuishia kuyasikia yale nilozungumza kwenye ndoto ya Zai tu, aliyasikia pia na yale niloyasema kwenye ndoto ya kifo cha mama yake?

Nilijiuliza kichwani mwangu, nikajipa jibu ndio, kama hapana basi asingeniuliza lile swali, angeanzia wapi?

Aliyasikia nilozungumza ndotoni na pengine akapuuza lakini hili la Zai limemrejesha tena kule, kule kwenye kaburi la mama yake, sasa nitasema nini?

Atanihisi vipi?

Nilihisi kinywa kimenikauka mate.

Nilitazama uso wa bwana Mgaya nikijaribu kung'amua kilichomo kichwani mwake, nini anachowaza, lakini sijui kama nilifanikiwa.

Hofu nilokuwa nayo haikunipa utulivu wa akili.

Nikiwa bado najitafuta, tafaruku ya mawazo kichwani mwangu, mlango wa chumbani ulilia - ngo-ngo-ngo kisha sauti niliyoitambua kuwa ya Amiri ikasema, "hodi hodi."

Nilinyanyuka nikauendea mlango kutazama, hapo nikamkuta Amiri akiwa amesimama na mtoto, mikono yake kamwekea begani, akanambia mtoto anataka kuja kulala na mimi hivyo amemleta.

Nikampokea mtoto na kumshukuru, kabla hajaondoka akaniuliza tena lile swali.

Swali aliloniuliza saa ile.

Swali lake la siku zote.

"Uko sawa?"

Aliniuliza akinitazama usoni. Sijui alikuwa anaona nini.

*****
Uwahi kuleta muendelezo mkuu
 
Japo hatulipii chochote ila inakera sana yaani
Sana yani
Soma hii hapa n nzuri sana huyu anatuma kila siku na imefika mbali
 
Back
Top Bottom