Nikaenda kumzika ibilisi wangu....! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nikaenda kumzika ibilisi wangu....!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Jun 20, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Jun 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Ilikuwa ni ajali kubwa na hata mimi sijui niliweza vipi kupona. Dereva na mke wangu walifia pale pale kwenye eneo la tukio. Tulikuwa tukitokea Chalinze kurudi Dar es salaam baaada ya kukagua shamba ambalo ilikuwa tulinunue katika kijiji cha Msata wilayani Bagamoyo. Mbele kidogo ya mji wa Chalinze ndipo ajali hiyo ilipotokea . Dereva wetu alikuwa akijaribu kulipita lori fulani lakini wakati huo huo gurudumu la mbele la gari letu lilipasuka na kusababisha gari kuyumba ambapo lililivaa lile lori. Kufuatia kuligonga huko, gari letu lilirudishwa katikati ya barabara ambapo liligongana uso kwa uso na gari lingine lililokuwa linakuja mbele yetu. Sikujua kilichotokea hadi baada ya siku mbili Muhimbili.

  Nilipopata fahamu ilinichukua muda kukumbuka kidogo kilichotokea. Nilipouliza kuhusu mke wangu hakuna aliyesema kitu kati ya wale ndugu na jamaa zangu waliokuwa pale kando ya kitanda changu. Pamoja na maumivu yangu nilijua kilichokuwa kimetokea. Nilianza kulia, hata kabla hawajaniambia chochote. Kaka yangu aliponiambia "jikaze ni kazi ya Mungu, shemeji mama Rehema ametutoka." Nilipoteza fahamu. Nilipopata fahanu na kukubali kuipokea taarifa ile, niliambiwa kuwa mke wangu alifia pale kwenye eneo la ajali pamoja na dereva. Mimi nilikuwa nimevunjika mguu wa kushoto, mkono wa kushoto na mbavu mbili na kubanwa kifuani. Hali yangu kwa kweli haikuwa nzuri lakini nililazimika kujikaza. Mke wangu alikuwa amekufa, haikuwa rahisi kukubali.

  Nilikuwa nampenda na yeye pia alikuwa ananipenda. Ukweli ni kwamba tulikuwa tukiaminiana sana na mke wangu ambaye nitamwita Sia {Jina linalokaribiana na jina lake halisi}. Tulikuwa tumeshibana kiasi kwamba, kulikuwa hakuna ambaye alikuwa hajui.
  Nilikumbuka kwamba kwa miaka minane ya ndoa yetu tulikuwa hatujawahi kukorofishana, ukiacha kusigishana kwa hapa na pale. Nilikuwa sijawahi kumsaliti na hata yeye pia. Nilijaribu kukumbuka ahadi zetu kwa kila mmoja na kuhusu watoto wetu wawili mmoja wa kiume na mwingine wa kike. Kwa kweli ilinichukuwa muda wa saa kadhaa kukubali kwamba nilikuwa sina mke, mwili wa yule nimpendaye ulikuwa ukiganda mochuari. Nilijikuta nikiinuka kwa nguvu na kupiga yowe nikitaka kwenda kumfufua mke wangu. Nilikuwa nimechanganyikiwa kwa kweli! Ndugu zangu na jamaa waliokuwepo pale wodini walinishika na kunituliza.

  Ilibidi waombe msaada kwa madaktari ambapo nilichomwa sindano iliyonipa utulivu na usingizi. Nilipoamka jioni sana, nilikuwa na utulivu kidogo, kaka yangu aliniomba nijikaze na kumrudia mungu, Aliniambia nijaribu kuukubali ukweli na hali halisi. Nilijikaza na aliniambia kwamba mazishi ya mke wangu ingebidi yafanyike kesho, kwa mujibu wa makubaliano ya ndugu wa pande zote.
  Aliniambia dereva wangu alikuwa amezikwa tayari na ndugu zake. Nilimwomba kaka wauache mwili wa mke wangu ili niwe nae karibu kwa muda fulani. Kaka alinishawishi sana nikubali kwa sababu, kama mwislamu ninajua inavyokatazwa kuuweka mwili wa marehemu bila kuuzika kwa muda mrefu, bila sababu.

  Hatimaye nilikubaliana naye, lakini nilisema ni lazima nami niende kuzika. Kaka alinimbia kwa hali yangu nisingeruhusiwa na madaktari na wala nisingeweza kumudu kwenda makaburini Kinondoni.
  Nilimwambia kaka katika yote ningemkubalia lakini sio hilo la kutomzika mke wangu. Nilimwambia, habari ya madaktari aachane nayo na kuhusu mimi kumudu ningemudu tu. Nilikataa katakata hata kusikiliza ilibidi kaka aondoke pale bila muafaka. Walikuja ndugu zangu wengine kunishawishi lakini niligoma kabisa, hadi ikabidi wakubaliane nami.

  Lakini walijua ingekuwa ngumu sana kutokana na hali yangu.
  Kesho yake walikuwa tayari wamepata ufumbuzi. Walikubaliana na uongozi wa hospitali kwamba nipelekwe makaburini kwa gari la wagonjwa. Ni kweli nilikwenda kuzika. Pamoja na kuwa waislamu huwa hatutoi heshima za mwisho kwa kuuona mwili wa marehemu, mimi nililazimisha hadi nikaonyeshwa mwili wa mke wangu. Alikuwa hana alama hata moja usoni kwani alikuwa ameumia miguuni hadi kifuani. Nilipomwona nilipoteza fahamu………… Tulimzika mke wangu na nikarudishwa hospitalini.

  Nilitoka hospitalini baada ya mwezi mmoja na kurejea nyumbani. Nyumba yangu mwenyewe ilinitisha na nilihisi simanzi kubwa kuwa mle ndani. Watoto wangu walinisikitisha zaidi. Lakini nilishaamua kuikubali hali halisi. Nilikuwa nimekubali kuanza upya maisha.
  Siku ya Tatu tangu kurejea nyumbani niliamua kupangua ili kuvipanga upya vitu vya marehemu. Nilipanga nguo zake na mapambo mengine ya kike. Halafu ilibidi kupanga vitu vilivyokuwa kwenye droo zake ambazo funguo zake alikuwa nazo mwenyewe marehemu. Kwa sababu sikuwa najua alipokuwa ameweka funguo za droo zile mbili ilibidi nizivunje moja baada ya nyingine.

  Droo ya kwanza ilikuwa na barua na karatasi mbali mbali za mawasiliano na mambo mengine. Hapo nilianza kuzisoma barua. Barua ya kwanza ilikuwa ni kutoka kwa mpenzi wake. Haikuwa ni barua ya zamani, kwani ilikuwa imetumwa kwake miezi minne tu kabla ya kifo chake. Ilitumwa na bwana aliyekuwa ametuuzia ile gari iliyohusika kwenye ajali iliyomuua. Sehemu ya barua ile ilikuwa imeandikwa:

  Kuhusu hilo nisawa mpenzi.
  Wewe mwambie nitawauzia kwa mkopo, tena kwa bei rahisi sana. Lakini hizo fedha utazichukua wewe. Kuhusu kwenda Harare nitakufahamisha, jaribu kwa upande wako kumwambia kwamba utakuwa na semina huko, April. Najua kufika Aprili tutaelekea huko. Nataka tuwe mahali huru na salama ili niufaidi mwili wako na wewe uumiliki wangu.


  Barua hiyo ilijaa upuuzi mwingi……

  Nilipomaliza kuisoma nilihisi kama ninayeota au ambaye nitaugua kichaa. Ni kweli huyu jamaa ndiye aliyetuuzia lile gari iliyochukua maisha ya mke wangu kwa bei ya chini sana. Gari Nissan Pajero kwa shilingi milioni 3.5 nzuri tu, hata kama imetumika! Kumbe ulikuwa ni mpango wake na mke wangu wa kuipatia familia yangu gari. Nilienda kupekua barua na hati kadhaa. Niligundua hati ya nyumba kwa jina la mke wangu.

  Nyumba hii ilikuwa Kijitonyama. Nilipata barua nyingine. Hii ilikuwa ni ya bwana wake wa zamani lakini ilikuwa imeandikwa mwaka mmoja tu nyuma, ilikuwa ikimlaumu mke wangu kwamba hakuwa mkweli Sehemu muhimu katika barua hiyo ilikuwa imeandikwa:

  Ninajua wazi huyo…….ni mwanangu na hata rafiki yangu……. amesema tunafanana sana. kama umeamua kunidanganya , ni sawa, lakini kumbuka hiyo ni damu yangu.
  Sitamchukua wala kumdai lakini kujua ukweli ni muhimu kwangu.

  Nilipomaliza kusoma barua ile nilishikwa na kizunguzungu. Nilitulia hapo kitandani kwa muda. Halafu niliendelea kupekua kwenye karatasi hizo. Niliona barua kadhaa na kadi za mapenzi.

  Kadi mbili zilikuwa zinatoka kwa bosi wake. Barua moja ilikuwa ikitoka uingereza kwa mtu aliyeitwa P Hughes. Huyu ni wazi alikuwa ni mpenzi wa mke wangu kwa muda mfupi, alipokwenda Uingereza miaka miwili nyuma kwa kozi fupi ya miezi sita. Barua yake ilikuwa imejaa sifa nyingi, akimsifia mke wangu kwa kuwa na mwili mzuri na kuwa mtaalamu wa mapenzi na ilisifia shanga zake pia.

  Nilihisi nikibana kifua na mapigo ya moyo wangu yalikuwa kama yamesimama. Bila shaka siku ile ndipo yalipoanzia maradhi yangu ya shinikizo la chini la damu, ambayo ninayo hadi sasa. Nilivunja ile droo ya pili ambayo ilikuwa na picha kadhaa. Zote zilikuwa ni picha za mapenzi. Nilitazama mbili za kwanza, nikatoka chumbani mle nikiyumba.

  Naomba nisiseme sana kuhusu picha hizi, kwa sababu, hata kama mtu sio mke wako, ni mwanamke unayemfahamu tu, ukiona picha zake akiwa kwenye hali kama ile, utatahayari sana. Picha unazoziona kwenye mikanda ya ibilisi au kwenye mtandao wa inteneti ndizo zilizokuwa pale kwenye droo, zikiwa ni za mke wangu na wanaume watatu tofauti.

  Yule aliyejifanya kutuuzia gari na nyingine za wanaume wawili ambao sikuweza kuwafahamu. Baadae mchana baada ya kupata nguvu nilimpigia simu kaka mkubwa wa marehemu na kumwomba apite nyumbani. Huyu ni mtu wa hekima sana na hadi sasa tunaelewana sana.
  Alipofika nyumbani nilimwomba radhi na kumwonyesha barua na picha zile. Alizitazama kidogo na kunirudishia, alikaa kwa muda na kusema, "Huyu sio dada yangu niliyekuwa namfahamu mimi, hii ni aibu kubwa sana shemeji." Hakuweza kusema chochote baada ya hapo, Alipoondoka kwa huzuni kubwa nilichukua nguo zote za mke wangu, barua, picha na vitu vingine vyote ambavyo vingenipa kumbukumbu yake na kwenda kuvichoma moto.

  Nilivichomea moto shambani kwangu, Kiwangwa Bagamoyo na kufukia majivu yake. Tangu siku ile hadi leo sijakanyaga kaburini kwake, watoto wake wanakwenda na huwa nawahimiza kufanya hivyo. Yule mkubwa anajua mengi hivi sasa baada ya kusimuliwa na baadhi ya ndugu. Nilimwambia kwamba maneno yale hayana ukweli.

  Lakini najua anafahamu kuwa yana ukweli, kwani kuna siku aliniiuliza, mbona haoni picha za mama yake ukutani. Nilimwambia, zinanitia uchungu zaidi. Ilibidi niende Afrika Kusini kupima DNA, ili kujua kama yule mtoto mdogo ni wangu kweli.

  Bahati nzuri ilionesha kwamba ni wangu kwa asilimia kubwa sana. Hii ilinipa moyo sana. Kilichonitokea kimenifanya nisiwe na hamu hata ya kuwa karibu na mwanamke, achilia mbali kuoa.

  Mtu ambaye umemuamini kuliko binadamu mwingine, kumbe ndiye anayefanya uasi usio na kipimo gizani. Nasema hivi mnapaswa kuwaamini wapenzi au wake zenu. Kilichonitokea mimi ni bahati mbaya na ninaamini kama marehemu angeendelea kuishi ni lazima ningekuja kumnasa.


  Habari hii iliwahi kuandikwa kwenye gazeti la Jitambue.
   
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  Jun 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Tunaambiwa siku zote tusisemee mioyo ya watu wengine, kwani wao ndio wanaojua hasa nini kinaenda kwenye mawazo yao. Ni hatari kwa mfano, mtu kusema hadharani kwamba mpenzi wake hatoki nje. Anachotakiwa kufanya mtu ni kuamini kwamba mpenzi wake hatoki nje lakini sio kutangaza kwamba mpenzi wake hawezi kutoka nje. Kuna mambo mengi sana ambayo yanaweza kuwa yanafanywa gizani na wapenzi wetu ambayo tukiyafahamu hutokea kutuumiza sana na kutufanya kuchanganyikiwa.

  Hebu fikiria, inakuwaje pale mume anapoamini kwamba mkewe ni mwaminifu sana na hawezi kutoka nje, iwe ni kwa jua au mvua. Bila shaka anapong'amua kwamba hutoka sana nje, kunakuwa na kuchanganyikiwa na kuumia kwa kiwango cha juu sana. Lakini jambo la kujiuliza ni hili.
  Ni kwa sababu zipi hasa mtu anapendwa na kupewa kila kitu na mpenzi wake lakini bado anakwenda nje na kufanya mambo mengi, makubwa na ya aibu kiasi hiki? Kila kitu hatimaye hujifunua wazi hata kama tumefukiwa makaburini tayari! Utu na uadilifu wetu "feki" hutusuta huko mbinguni tuliko………..
   
 3. Graph Theory

  Graph Theory JF-Expert Member

  #3
  Jun 20, 2012
  Joined: Jul 2, 2011
  Messages: 3,803
  Likes Received: 1,116
  Trophy Points: 280
  Nikadhani ni Masaibu yaliyokupata kweli, kumbe stori ya kwenye gazeti la Jitambue. Lakini hayo ndiyo yanayotokea katika ulimwengu wa mapenzi.
  The unseen is illustrated by the seen.
   
 4. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #4
  Jun 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Barnabas Shadrack ni tukio la kweli na sio stori ya kutunga kama unavyofikiria..............
  Katika gazeti la Jitambue tulikuwa tunaandika ushuhuda kutoka kwa wasomaji wa gazeti hilo na watu mbalimbali ambao kwa kupenda kwao wenyewe walikuwa wanatoa ushuhuda wa maisha waliyoyapitia ili wasomaji wa gazeti hilo wapate kujifunza.

  Ninazo simulizi nyingi za ushuhuda kutoka kwa watu mbalimbali ambazo sikubahatika kuziweka katika gazeti hilo la Jitambue kutokana na gazeti hilo kusitishwa kuchapishwa, naahidi nitaziweka hapa siku zijazo........................
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 5. HorsePower

  HorsePower JF-Expert Member

  #5
  Jun 20, 2012
  Joined: Aug 22, 2008
  Messages: 3,617
  Likes Received: 37
  Trophy Points: 145
  Ni hbr ya kuhuzunisha, mahusiano ya ndani ya ndoa na uaminifu wa wanandoa ni kitu kinachozungumziwa sana na jamii baada ya maadili kumong'onyoka kwa miaka ya hivi karibuni. Njia pekee ya kuondokana na hili tatizo ni kuwashauri watu wamche Mungu na Kumuogopa Mungu zaidi ili kuepuka kutenda matendo mabaya kama haya sirini.
  Ukimwogopa binadamu, unaweza kufanya kwa siri lakini ukimuogopa na kumheshimu Mungu, huwezi kutenda mabaya kama haya maana Mungu anatuona popote.
  Mungu atupe neema ya kuwa waaminifu kwa wale wote wenye ndoa na wapenzi. :embarrassed:
   
 6. Graph Theory

  Graph Theory JF-Expert Member

  #6
  Jun 20, 2012
  Joined: Jul 2, 2011
  Messages: 3,803
  Likes Received: 1,116
  Trophy Points: 280
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 7. mimixoxo

  mimixoxo Member

  #7
  Jun 20, 2012
  Joined: Jan 7, 2011
  Messages: 40
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  Ni fundisho kwetu sote, Usiusemee moyo wa mwenzi wako.....muamini and do your part.
   
 8. Katavi

  Katavi Platinum Member

  #8
  Jun 20, 2012
  Joined: Aug 31, 2009
  Messages: 39,469
  Likes Received: 4,128
  Trophy Points: 280
  Asante sana kwa hili bandiko Mtambuzi. Kuna somo la kujifunza hapa.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 9. cacico

  cacico JF-Expert Member

  #9
  Jun 20, 2012
  Joined: Mar 27, 2012
  Messages: 8,392
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  nimejifunza kitu haswaaaaaaa babu Mtambuzi. yaani mmmmhhhhh imenihuzunisha sana!
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 10. piper

  piper JF-Expert Member

  #10
  Jun 20, 2012
  Joined: Jan 17, 2012
  Messages: 3,260
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  Asante as alwayz michapo yako huwa fantastic mkuu, imekaa pouwa
   
 11. E

  Elizabeth Dominic Platinum Member

  #11
  Jun 20, 2012
  Joined: Dec 7, 2007
  Messages: 4,547
  Likes Received: 52
  Trophy Points: 145
  Loh loh loh!........... Mtambuzi nimeisoma hii habari huku nimeshikilia pumzi, sasa najiuliza kuna wa kumwamini kweli duniani? Kama hawapo wa kuwaamini tuishi vipi na wenzetu huku tukiwa hatuna imani...............inachanganya kwakweli
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 12. maishapopote

  maishapopote JF Gold Member

  #12
  Jun 20, 2012
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 2,000
  Likes Received: 957
  Trophy Points: 280
  hawa dada zetu hawa......huwezi kuamini wakati mwingine lakini ndo ukweli inabidi ujikaze kiume....
   
 13. HorsePower

  HorsePower JF-Expert Member

  #13
  Jun 20, 2012
  Joined: Aug 22, 2008
  Messages: 3,617
  Likes Received: 37
  Trophy Points: 145
  Uaminifu ni suala la ndani kabisa la mtu, na ni ngumu sana kuwa na ushahidi wala kipimo cha uaminifu ktk mahusiano. Kikubwa ni kukubabali hali ya mahusiano uliyonayo na kuplay your part-Namaanisha wewe mwenyewe kujitahidi kuwa mwaminifu bila kuusemea moyo wa huyo mpenzi wako, utaumbuka!
   
 14. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #14
  Jun 20, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  HorsePower nakushukuru kwa kusherehesha similizi hii, kwa kweli huwa navutiwa sana na maoni yako pale unapojadili mada mbali mbali humu jamvini.
  Kuna mengi huwa najifunza kutoka kwako..............................
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 15. Zux de

  Zux de JF-Expert Member

  #15
  Jun 20, 2012
  Joined: Apr 29, 2012
  Messages: 227
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Sio mnahuzunika kwa kusema muhuzunike katika mioyo. Ndugu zangu tuwe muwewakwel katika mapenzi.
   
 16. HorsePower

  HorsePower JF-Expert Member

  #16
  Jun 20, 2012
  Joined: Aug 22, 2008
  Messages: 3,617
  Likes Received: 37
  Trophy Points: 145
  Nakushukuru sana kaka kama umeligundua hilo, pamoja sana!
   
 17. y

  yaliyomo yamo Member

  #17
  Jun 20, 2012
  Joined: Apr 26, 2012
  Messages: 40
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  mesej delivad
   
 18. E

  Elizabeth Dominic Platinum Member

  #18
  Jun 20, 2012
  Joined: Dec 7, 2007
  Messages: 4,547
  Likes Received: 52
  Trophy Points: 145
  Sawa kabisa nakubaliana na wewe kwa maneno yako hapo juu hata hapo kwenye bold ni kitu nimejifunza kufanya hivyo kwa maana yalishanikuta yanayoshabihiana na hii habari, tatizo ni kuwa once ukiwa na mtu imani yako kwake ndio mara nyingi uwa ni msingi wa mahusiano yenu sivyo huwezi kuishi na mtu usiye na imani naye hata kama ni kwa kujidanganya, kukishakuwa na mistrust hamuwezi kwenda pamoja. Yes utaweza jitahidi kuplay your part lakini really what keeps you going?
   
 19. Eiyer

  Eiyer JF-Expert Member

  #19
  Jun 20, 2012
  Joined: Apr 17, 2011
  Messages: 28,238
  Likes Received: 3,670
  Trophy Points: 280
  Huwa najisemea mwenyewe kwamba;simezi kuwa mwaminifu kwa sababu nina mke au naogopa maradhi,nitakua mwaminifu kwa sababu ni UBINADAMU,kinyume cha hapo ni unyama!
   
 20. HorsePower

  HorsePower JF-Expert Member

  #20
  Jun 20, 2012
  Joined: Aug 22, 2008
  Messages: 3,617
  Likes Received: 37
  Trophy Points: 145
  What keeps you going? Kwanza kubaliana na mahusiano uliyoyaingia na kuyapenda na pili tambua kuwa huyo uliyenaye anaweza kuwa hana tofauti na hao wengine ambao hauna mahusiano nao, kwa lugha rahisi, tambua kuwa binadamu ana udhaifu na mapungufu; na tatu ni imani kama ulivyosema wewe mwenyewe, lakini imani yako kwake isikufanye ujisahau na kuusemea moyo wake! Ni vizuri kuwa na tahadhari. Kumbuka, chochote chaweza kutokea kwenye hayo mahusiano.
   
Loading...