SoC01 Nguvu ya mhimili wa nne kufungua nchi na kuleta maendeleo

Stories of Change - 2021 Competition

Yoda

JF-Expert Member
Jul 22, 2018
37,594
46,197
Vyombo vya habari au kwa jina maarufu la fourth estate katika lugha ya malkia vina mchango mkubwa na wa kipekee katika kuchochea maendeleo, demokrasia na uwajibikaji endapo tu vikiwa huru na kufanya kazi zake bila kutomaswa tomswa na wanasiasa.

Kupitia vyombo huru vya habari ndipo utendaji wa mihimili mitatu ya serikali huweza kufahamika na kufanyiwa tathmini na raia na pia serikali kuendelea kupata au kukosa kibali mbele ya wananchi wengi.

Katika nchi za ulimwengu wa kwanza zilizoendelea ambapo uchaguzi huru hufanywa mara kwa mara maoni ya uma "public opinion" huwa ni kipimo muhimu sana kwa serikali kuendelea kupata uungwaji mkono na mara zote kipimo hichi huwa kinabadilika kulingana na taarifa za kila siku. Kupitia vyombo vya habari huru ndipo mambo ya ufujaji, upendeleo, uvivu, yanaweza kujulikana na kufanyiwa kazi au hata viongozi kuondolewa madarakani.

Kutokana na umuhimu huu mkubwa wa vyombo vya habari, nchi yetu inahitaji kuondoa sheria zote kandamizi ambazo kwa muda mrefu sana zimepelekea taarifa na uchambuzi makini wa mambo muhimu ya siasa kukosekana na kuendelea kushamiri kwa taarifa za udaku, muziki na uchambuzi wa mpira, mambo ambayo yana tija kidogo sana kulifanya taifa hili kuwa kubwa na lenye ushawishi.

Kuufanya mhimili huu wa nne ufanye kazi yake sawa sawa ya kuwa chachu ya maendeleo, sheria za kikoloni za kufungia vyombo vya habari kupitia serikali zinapaswa kufutiliwa mbali. Malalamiko yoyote kwa chombo cha habari yatatuliwe kwa njia ya mahakama na sio dola ambayo mara nyingi huwa ndio mzalishaji na mlengwa wa taarifa hasi zinazofikia katika meza za wanahabari.

Vyombo huru vya habari ndio nguzo kuu ya mabadiliko.

Kama hakuna vyombo huru vya habari demokrasia hufia gizani.
 
Back
Top Bottom