JE MUNGU ALIRUHUSU MATALA(MITAALA) AU TUMEJIAMULIA?
Sehemu ya Kwanza
Bwana asifiwe mwana wa Mungu. Karibu katika somo lingine kuweza kuangazia baadhi ya mambo ndani ya jamaii
Matala au (‘mitaala’ kama ilivyozoeleka na wengi) ni ndoa zinahusisha mwanamume mmoja kuoa wanawake zaidi ya mmoja, yaani ndoa ya wake wengi. Kuna baadhi ya jamii hasa bara la Afrika, matala ni jambo la kawaida namakabila mengi Tanzania, na baadhi ya dini zimeruhusu matala lakini kwa maelekezo au vigezo kadhaa vya kutimiza.
Kwa sababu matala imekuwepo kwenye jamii yetu kwa muda mrefu basi watu wengi wanadhani ni sawa na kwamba hakuna shida. Hii sio sawa kabisa mwana wa Mungu, hatuwezi kukubali vitu kwa sababu tu eti vilikuwepo tangu zamani za mababu, na ukumbuke kabla hao mababu hawajakuwepo, Mungu alikuwepo. Ili jambo likubalike lazima Mungu alikubali,yaani lazima iwe sawa na neno, na usije kwangu eti ooooh David,mimi nimefunuliwa kuwa na matala(mitaala), nitakukemea na kibao kama kikikufikia basi Mungu atanipongeza.
Mbaya zaidi siku hizi hata wanawake wana ndoa za wanaume wengi, ajabu kabisa!Mungu atusamehe sana.
Mtazamo wa Mungu(Neno) ni upi sasa kuhusu matala? Ndoa ni taasisi iliyoasisiwa na Mungu hapa duniani. Mungu alimfanya mwanadamu wa kwanza, Adamu, ambapo neno linasema:-
“Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu….” Mwanzo 1:26
Mungu akaona sio vyema Adamu awe peke yake(Mwanzo 2:18), akamfanyia ‘Mke’ msaidizi. Mungu hakumfanyia Adamu “Wake” yaani “wives” kwa kiingereza.
Na kama Mungu angetaka Adamu awe na mke zaidi ya mmoja basi Mungu angemfanyia mke zaidi ya mmoja. Kwahiyo mmoja tu na Mungu akaona inatosha. Mungu anajua zaidi kuliko mimi na wewe mwanamke mwenye mume zaidi ya mmoja au wewe mwanamume mwenye mke zaidi ya mmoja.
Kwa sababu ya tamaduni zetu tunazoishi na makabila yetu tumejikuta tumeleta mawazo mengi sana duniani kuhusu ndoa tofauti kabisa na Mungu alivyowaza juu yetu.
Tumekuja kuibomoa hii taasisi. Kuna baadhi ya mawazo yetu yanakubaliana na mipango ya Mungu na mawazo mengi tuliyojiletea yanapinga mipango ya Mungu juu yetu. Na hii ndio kweli kuhusu matala au mitaala. Kwahiyo suala la matala au mitaala ni moja ya mawazo yetu sisi wanadamu tuliyojiletea kwenye ndoa zetu kwa sababu ya tamaduni zetu jambo linalokinzana na neno la Mungu.
Kwahiyo itoshe kusema kwamba matala sio makubaliano yetu na Mungu juu ya ndoa. Kumbuka kila jambo ambalo haliendani na kile Mungu alifanya, alichosema Yeye basi ni dhambi. Mpango wa Mungu ni mume mmoja na mke mmoja. No more No less(Soma mwanzo 2)
Hebu tuangaliebaadhi ya mifano ya matala au mitaala ndani ya biblia.
>Mtu wa kwanza kupotoka na kuingia kwenye matala alikuwa ni Lameki, alikuwa na wake wawili, Ada na Sila(Mwanzo 4:19-24) na biblia inamsema kabisa kuwa alikuwa ni muuaji.
>Ibrahimu alikuwa na matala pia(Mwanzo 16:1-5). Mkewe Sarai hakuwa na uwezo wa kuzaa, akaamua kumpa kijakazi wake kwa mumewe. Hajiri alizaa motto kwa Ibrahimu. Biblia inasema Sarah akawa na wivu juu ya Hajiri. Ndoa hii ilikuwa ndoano haswaaa.
>Matala nyingine ilikuwa kwa Esau. Alikuwa ni mtoto wa Kwanza wa Isaka na Rebeka. Esau alioa wanawake wawili wahiti (Soma mwanzo 26:33-34). Wakasababisha mateso kwa Isaka na Rebeka. Kwahiyo matala madhara yake sio kwa mume na mke peke yake kwani tunaona hapa matatizo yalienda hadi kwa Isaka na Rebeka, Baba na Mama wa Esau, au Baba mkwe na mama mkwe wa wake wa Esau.
>Gidioni alikuwa shujaa na kiongozi hodari. Alikuwa na watoto wa kiume 70 kwa wanawake tofauti (Waamuzi 8:30-31). Unadhani angekuwa baba wa aina gani kwa watoto wa kiume tu 70, hapo hatujaambiwa idadi ya watoto wa kike? Je ndio ambavyo Mungu anataka sisi akina baba tuwe?
>Mfalme Sulemani alikwa na wanawake 700, na Masuria 300. Huyu alivunja rekodi!! Biblia inasema wake zake wakaugeuza moyo wake usimwelekee Mungu (1 Wafalme 11:3). Anguko lake kubwa lilisababishwa na matala, alikiuka kanuni ya Mungu, Neno linasema “Wala asijizidishie wake ili moyo wake usikengeuke…” Kumbukumbu la Torati 17:17
Hakuna sehemu kwenye biblia ambapo matala imefanya vyema, au wamemaliza vyema mbele za Mungu. Kila tulichoona hapo juu kilisababisha matatizo, na hiyo haijabadili kitu. Hata sasa hilo halijabadilika,matala hadi sasa imesababisha matatizo makubwa kwenye ndoa za leo. Naandika haya ikiwa tayari wapo wanaolia na waliojela kwa sababu ya matala. Kuna yatima wengi kwa sababu ya matala. Kuna biashara nyingi zimekufa kwa sababu ya matala. Familia nyingi zimesambaratika kwa sababu ya matala, na kwenye hili la matala kuna wengine ni siri lakini siri hii ni kwao na sio kwa Mungu.
Tutaendelea na sehemu ya pili............
Mungu akubariki
Davidi Chacha
August 24, 2017