SEHEMU YA 29
"Mama! mama! mamaaaaaaa!" Nilipayuka na kulia kama mtoto punde nilipougundua ukweli. Mbali ya kutulizwa kwa kupewa nasaha na watu wa Mungu kwa maneno ya hekima na imani lakini bado fahamu zangu ziliziba. Nilichanganyikiwa sana na kulia kwa uchungu wa hali ya juu. Kwa muda mfupi yalikuja matukio mengi ya wema wa mamaangu kwa muda wote. Kwenye tabu na dhiki tulizopita, mama mcheshi asiyekaukiwa maneno ya kutia nguvu na faraja kwa wanae. Furaha yake ilikuwa ndoa yangu. Laiti ningejua kama ndoa yangu inaweza kuwa chanzo cha kifo chake basi nisingeoa kamwe. Aaaah! alikuwa bega kwa bega kwa kila idara. Leo hii binti aliyeamini awali ndiye pumziko la faraja yangu anasababisha aiache dunia ingali bado tunamuhitaji? Ooooh! Hasira! hasira kila ilipokuja taswira ya Atuganile na mamaake nilizidi kuvimba kifua. Nilitamani niyeyuke nikawakatekate kwa mapnga wafe kinyama kwa mikono yangu. Lakini kizunguzungu kilinivaa zaidi na fahamu zikazima vuup!.
Hakuna nilichoweza kukumbuka tena zaidi ya hapo.
Nilikata moto na kuzima kabisa safari hii ikiwa si utani tena wala makusudi kama pale kanisani. Hali ilikuwa mbaya kwa walioniona kizaazaa kipya kikaibuka. Ilikuwa kidogo niumeze ulimi kama isingekuwa jitihada za mchungaji mmoja ambae pia alikuwa na taaluma ya utabibu hospitali kuu ya moyo. Zilifanyika jitihada hima za kunusuru uhai wangu nilipopoteza fahamu kabla ya kukimbizwa hospitali na kubaki katika hali hiyo kwa siku tatu nikiwa wodi ya wagonjwa mahututi. Nyuma yangu taratibu za kumuhifadhi mamaangu katika nyumba yake ya milele ziliendelea pia. Sikufanikiwa kuliona walau jeneza lililobeba mwili wa mamaangu. Niliyakosa mazishi yake nikiwa hoi nisiye fahamu hospitali.
Kwa siku hizo tatu ambazo sikuwa nafahamu za ulimwengu wa kimwili lakini katika hali ya ajabu kwenye ulimwengu sijui niuite wa kiroho ama nafsi ama sijajua hata nastahili kuuitaje ulimwengu huo ambao ulianza kunifunulia kila kitu kuhusu Atuganile. Huenda Mungu aliamua kunitendea muujiza ama fahamu zangu ndizo zilitengeneza matukio hayo kipindi nikiwa nimelazwa wodi ya wagonjwa mahututi huku wengi wakiamini inaweza kuwa huo ukawa mwisho wangu rasmi wa kuishi duniani. Ilikuwa kama niko katikati ya ndoto yenye muendelezo ya matukio yote yaliyopita ambayo sikuwahi kuyajua kuhusu mke wangu Atuganile. Ndio, ndio hivyo ilivyokuwa. Nilimuona Atuganile katika kila hatua na kila jambo ambalo kikawaida alinificha wala sikugundua awali. Nilimuona katika siku tatu zile nikiwa sina fahamu za kimwili lakini fahamu za kiroho zilikuwa wazi. Nilimuona na niliuona uchafu wa Atuganile Mwakyusa. Hakika Niliyaona mengi ndani ya weweseko ambalo lilinisahaulisha kama niko mahututi na mamaangu hayuko tena duniani. Nilimuona na nilielekezwa kila hatua na mtu ambae sikuwahi kuiona sura yake wala sikuwahi kupata wazo la kumuuliza walau jina lake zaidi ya kuitika na kutazama kila alichonionesha na kunielekeza.
*******
||ATUGANILE MWAKYUSA||
"Hilo ndilo jina lake halisi, binti aliyeukwaa uyatima angali mtoto sana kwa tamaa za mamaake ili awe mkuu wa washirika wilaya ya Kyela." Sauti ilinambia tukiwa tumekaa kwenye benchi la mgahawa mmoja nje ya shule ya sekondali Kyela.
"Tamaa za cheo gani? na ushirika upi unaomaanisha?" Niliuliza huku nikiwa nimeinamisha kichwa bila hata kumtazama mtu niliyekuwa nasema nae.
"Mama Atuganile ni mshirika wa chama cha uchawi akitwaa koba alilorithi kwa bibi yake mzaa baba. Alishafanya mengi hadi akapanda ngazi tofauti lakini ilipofika kupata cheo kikubwa ilibidi amtoe kafara mtu aliyempenda kweli ambae hakuwa mwengine zaidi ya mumewe. Alimtoa na walimla nyama katika ulimwengu wa kishetani na kichawi. Na hapo ndipo alipotawazwa cheo cha ukuu wa wachawi ngazi ya wilaya ya Kyela ingawa kwa sasa yeye anahusika kimkoa na mwanae Atuganile tayari ni mkubwa kiwilaya ya Kyela." Aliendelea kunambia bwana yule na kunifanya nishangae kusikia mama Atuganile ni mchawi tena mkubwa na zaidi nilistuka kusikia kuwa na Atuganile naye mchawi? tena mkubwa kiwilaya? kwa umri ule! Lakini nikiwa nimetaharuki kabla sijamuuliza swali aliendelea kunichambulia kile kilichokuwa nafsini mwangu huku safari hii mazingira tuliyokuwepo yakawa kule kijijini kwa kina Atu tena siku ile nikiwa nazungumza na Atuganile.
"Nyumba yao si ya nyasi wala hawana maisha magumu kama waonavyo watu wa kawaida. Sasa tazama kwa makini alichokuwa anakifanya Atuganile pale na uitazame nyumba yao pasipo kupepesa."
Aliponiamrisha nami nilikodoa. La haula! Nilishangaa kuona Atuganile kwanza si mzuri wa kutisha kama nilivyokuwa naamini ingawa pia alikuwa mzuri. Tena pale alipokuwa nazungumza nae kumbe alizungukwa na vijakazi zaidi ya sita wakiosha vyombo huku wengine wakimpepea wakati yeye ameketi juu ya migongo ya wengine waliopiga magoti na kuwafanya kama viti. Hakuwa anaosha vyombo yeye kama ambavyo nilikuwa naona pale nilipokuwa nazungumza naye huku nikimshangaa uzuri wake. Nilijiona na nilisikia kila nilichokuwa nasema na Atu. Nilibaki nimeachama midomo zaidi baada ya kumuona mama Atu kumbe alikuja muda ule kwa mazingara akiwa uchi wa mnyama na kunipaka kitu usoni mwangu huku Atuganile akinicheka kwa kicheko ambacho siku ile sikukisikia wala kukihisi.
"Sasa pale ndipo ulipofifishwa macho yako na kuanza kumuona binti yule hakuna afananae duniani." sauti ilinielekeza huku nikitembea hadi pale nilipokuwa nimesimama nikisema na Atu nikitamani kumshika na kumfuta mtu ambae ndiye alikuwa mimi siku ile lakini mikono yangu ilibaki kupita na kugusa hewa. Niligeuka kumtazama Atuganile machoni mwake alikuwa na macho kama ya paka kila alipokuwa ananitazama ambapo ingawa siku ile nilimuona kama malaika. Nilishangaa na kujishangaa mwenyewe kwanini nilikuwa mjinga vile.
"Hakuna ambacho alikuwa hakijui Atuganile kuhusu wewe zaidi ya mambo matatu. Kwanza wapi kilifukiwa kitovu chako pili lini siku yako ya kufa na cha tatu kuhusu binti Suyrashfatina. Lakini mbali na hayo matatu kila kitu kuhusu nyota na mengineyo alijitahidi kuyajua siku baada ya siku. Tazama hapa nini ulikuwa unakula." Sauti iliniambia na mara mazingira yalibadilika na kutokea siku ile usiku nikiwa kwa kina Atuganile mkekani tukila pamoja huku nikiongea kwa ucheshi na kuwachekesha. Daaah! nilipotazama kumbe nilikuwa nimetengewa chakula na lile jitu la kutisha ambalo liliwahi kuja nivamia siku ile niliyodondoka na kupoteza fahamu kazini kijiji cha Mtakuja. Jitu chafu, nywele timutimu, pande la jitu lenye kutisha likila kilafi pamoja nami chakula kile tofauti na walichokuwa wanakula Atuganile na mamaake. Sisi tulitengewa kwenye chungu kichafu nyama zenye kuoza sambamba na mchuzi wa funza funza ambao lile jitu alionesha kuupenda haswa akila haraka haraka sambamba na unga ambao machoni niliona ni ugali mzuri wa moto sambamba na nyama ya kuku na mboga za majani.
Nikiwa nimetaharuki nikitamani nimsukume mtu ambae ndiye alikuwa mimi ili asile kile chakula lakini mara alitokea binti mwengine mzuri sana na kuketi mbele yangu karibu yangu kabisaaa! tena kumbe kila nilivyochota kile chakula ambacho niliona nikipeleka mdomoni mwangu na kutafuna kumbe haikuwa hivyo. Kiliishia mdomoni mwa yule binti ingawa kilichotwa kwa mikono yangu. Alivyokuwa anatafuna na kumeza ndivyo nilivyokuwa nafanya mimi ingawa nilikuwa natafuna hewa na kumeza hewa. Ajabu zaidi kilichonishangaza nilibaini kwamba binti yule aliyezuka ghafla pale siku ile kumbe hata kina Atuganile achilia mbali lile jitu pia hawakuwa wakimuona.
"Nani tena huyu? Ina maana nao hawakumuona?"
"Huyo ndiye SUYRASHFATINA hawakumuona wala hawajawahi kugundua uwepo wake. Na kupitia binti huyu kwa mapenzi ya Mungu wako uliyakwepa mengi mno mazito uliyokusudiwa."
Sauti ilisema pasipo kunifafanulia zaidi yule binti mzuri vile aliyeitwa Suyrashfatina ni nani haswa na kwanini alikuwa pale upande wangu. Lakini kabla sijauliza kutaka kujua mengi kwa mwenyeji wangu niliyekuwa nasema naye muda wote pasipo kupata wazo la walau kumgeukia kumuona yupoje ama hata kumuuliza jina tu! mara nikiwa katikati ya fikra ya swali langu, mazingira yalibadilika tena na kutokea siku ile tukiwa tunatembea na wenzangu eneo lile la shamba la mahindi asubuhi kulielekea transfoma. Ilikuwa siku ile ya kizaazaa cha kudondoka na kuingia kwenye ulimwengu wa ajabu kwa mara ya kwanza na kuyaona mambo ya ajabu. Aaaaah! dunia ina mambo. Tunaishi kwenye dunia ya ajabu sana. Oooooooh! Hakika nilichokiona hapa ni zaidi ya maajabu yote yaliyopita. Kuna mengi yanatokea nyuma ya viini vya macho yetu hapa duniani. Kama hujui moja ya sababu za wazee wa zamani kuwatafutia wake/waume wa kuoa/kuolewa watoto zao ni kuwaepusha na matatizo tofauti na moja wapo kama ambalo nililikwaa katika ndoa yangu.
Aaaaaaaaaah! lakini chozi langu..........litalipwa!
ITAENDELEA