Ndugu wana JF,
Nashukuru sana kwa mchango wenu unaodokezea picha potofu inayojengwa kuhusu chama cha NCCR-Mageuzi.Awali ya yote naomba niweke wazi kwamba mimi ni George Kahangwa, mwanachama wa NCCR-mageuzi, sioni sababu ya kuficha ukweli huo, maana ni vizuri niseme sasa ili hata mnapoendelea kututumia makombora mjue yanafika na tunaendelea kuyatafakari na kuyaona kama changamoto kwetu maana tunaamini ninyi ni watanzania na myasemayo ni sehemu ya ujumbe mlionao kwetu, japo yameghubikwa na hoja zilizojengwa juu ya uongo.
Napenda kutofautiana nanyi katika mambo kadhaa:
Mosi, si kweli kwamba NCCR ni a dead thing, we are alive and well. Kufa kwa chama huthibitishwa na msajiri wa vyama vya siasa kwa kufuata vigezo rasmi. vipo vyama vilivyokwisha kufa na kufutwa, nanyi mnalijua hilo.Aidha kumbukeni nchi yetu kwa sasa ina vyama vya siasa 18, vipo vinavyosikika vikifanya kazi na vipo vilivyosinzia, fanyeni tathmini ya kina ili madai yenu ya ufu wa chama yawe na msingi. chama gani mnathubutu kusema kimekufa wakati mnajua vizuri kinaongoza serikali za vijiji na kina madiwani kadhaa hapa nchini, nk.
Tunajua chanzo cha propaganda hii, tunamjua kiongozi mwandamizi wa chama fulani anayezunguka nchini akiwaaambia watanzania kwamba NCCR imekufa, tulipombaini na kumwuliza kulikoni akatuma ujumbe wa kutuomba radhi, au mwataka nimtaje jamani...
Pili,kumbukeni ujumbe tuliouandika unahusu maslahi ya taifa, someni vizuri ili mtambue kwamba hatudandii hoja bali tunatekeleza wajibu wetu kama chama cha siasa wa kutoa rai kwa jamii nzima ya kitanzania, hatukuiandika serikali tu na hata hivyo serikali isiposikiliza sisi tumetimiza wajibu wetu.
Tatu, suala la Tarime, niwambie wazi kwamba sababu kubwa ya NCCR kutofanya vizuri Tarime ni propaganda ya adui yetu tunayemjua aliyeamua kueneza uongo kwamba sisi tumetumwa na CCM na kwamba ana ushahidi.Mtakeni basi atoe ushahidi, vinginevyo itakuwa ni jambo la kusikitisha kama watanzania mtaendelea kuushabikia uongo ushinde na kutamalaki juu ya ukweli, wanatarime walituhukumu kwa kudhani ni kweli tumetumwa na CCM.
Wakati huo huo mtakumbuka kulikuwa na uchaguzi mwingine mdogo kule Nguruka, NCCR tukaishinda CCM, lakini vyombo vya habari vilivyolishwa sumu ya uongo vikaandika kuwa ni CHADEMA imeshinda Nguruka, tafuteni basi ukweli nani alishinda kule Nguruka.
Vile vile mtakumbuka kuwa chama chetu pamoja na vyama vingine vitatu tuko katika ushirikiano, katika suala la Tarime vyama hivi tulikaa kukubaliana kumsimamisha mgombea mmoja, katika kikao kilichofanyika huko huko Tarime tarehe 11 September, vyama hivi vilimpitisha mgombea wa NCCR, lakini CHADEMA hakikukubaliana na hayo,kikasimamisha nacho mgombea.Huu ukweli msiukimbie, pendeni kujua hasa ni nini kilitokea Tarime.Mkitaka niulizeni ikawaje CHADEMA kikashinda.
Nne, kuhusu mchango wa NCCR katika mageuzi nchini, uko wazi labda kwa wasiojua historia ya mageuzi nchini.Kwa ufupi tu kumbukeni NCCR ilianza kama vuguvugu la wanamageuzi nchini hata kabla ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Kutoka NCCR vilizaliwa vyama vingi sana kikiwemo hicho ambacho baadhi ya wanajf hapa mnaonekena kukishabikia sana.Someni historia hiyo, mtagundua pia kuwa kumbe hata jina la chama kipenzi chenu limetokana na maneno ambayo hadi leo yako katika nembo ya NCCR.
Binafsi mimi ni shuhuda wa jinsi ushirikiano wa vyama ulivyoanzishwa, na nilikuwepo siku tamko la ushirikiano linaandaliwa pale makao makuu ya NCCR, siku chache kabla ya tamko kutangazwa tr.10 May 2007.Ndugu zangu niwashirikishe siri ninayoijua,kabla tamko halijatoka neno ushirikiano lilisomeka muungano, aliyelibadili tunamjua na huyo ndiye mnapaswa kumtupia madongo ya kutokuwa na mchango wa kuviimarisha vyama vya upinzani.
Suala la muungano, NCCR tulilipendekeza kwa wenzetu mara kadhaa (na ushahidi upo) tulilipendekeza baada ya kulifanyia utafiti wa kina nchini (research report ipo), Hamtutendei haki kusema hatuna mchango wowote katika mageuzi ya nchi hii, kusema hivyo ni kupotosha ukweli.
Wana JF, yafaa basi tusimamie ukweli kuliko ushabiki.