Hizi ni propaganda za CHADEMA tu ili waonewe huruma........ kwani wameanza kushinda majimbo mwaka huu?? mbona wabunge wao wote wapo hai??? suala la kuuawa kiongozi wa chama, hata CCM aliuliwa mwenyekiti wa wilaya kule mbeya hivi karibuni, je? CHADEMA ndio walimuua?? suala la kuuana arusha halijaanza leo
Ndugu yangu Mizizi, hebu zanisha mizizi uone haya kwa kina. Napenda nikupe mifano miwili moja ni hadithi za kale na moja ni kutoka katika kitabu kitakatifu yaani Biblia.
Naanza na hadithi, hii ilisomeka MTEGO WA PANYA KUINGIA WALIOKUWEMO NA WASIOKUWEMO. Katika hadithi hii mtu moja alikuwa amekusudia kutega panya maana walimsumbua sana nyumbani mwake, alipoutega ule mtego panya akauona kuwa ni hatari kwake lakini hakuwa na wezo wa kuutegua, mara akapita jogoo, panya akamwambia, tafadhali saidia kutegua huu mtego maana naona umekaa vibaya unaweza kuingai waliokuwemo na wasiokuwemo, jogoo akamjibu 'mimi wanihusu nini, umetegwa wewe unayeiba chakula ghalani mie napewa' akaondoka zake. Mara akapita mbuzi, panya akaomba vile vile na majibu yakawa yale yale, akaja ng'ombe akaombwa kwa kuwa wewe ni mkubwa hebu saidia kutegua hiki kitu ni hatari kwetu wote majibu yakawa yale yale. Panya akaamua kukaa mbali na mtego ule maana alijua hakuna msaada. Mara akapita nyoka juu ya mtego nao ukafyatuka na kumbana. Mwenye nyumba kwa kudhani aliyekamatwa ni panya akaenda kwenye giza akipapasa ili amtoe huyo panya labda kwa makusudi ya kuutega tena. La haula! kumbe nyoka yule akamgonga yule baba na baada ya muda mfupi akafariki na ndipo shida ilianza. Usiku huo watu wacahche walikuja kulala msibani na ili wale usiku huo jogoo alifanyika kitoweo. Kesho yake watu waliongezeka ikaonekana anayefaa kwa mboga ni mbuzi, akachinjwa na siku ya kuanua tanga watu wengi walifika ikaonekana kitoweo anayefaa ni Ng'ombe akachinjwa. Mtego wa panya ukaingia walookuwemo na wasiokuwemo. Panya akawa anaangalia yote yale na alibaki salama. Mtega panya na wapambe wote walikumbwa na kifo.
Katika BIBLIA: Nakupeleka katika Kitabu cha Esta. Hapa tuna mkuta Mfalme Ahasuero ambaye alimiliki toka Bara Hindi mpaka Kushi, juu ya majimbo mia ishirini na saba. Mfalme huyu alikuwa na Mkuu wa maakida wote aliyeitwa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi. Mfalme Ahasuero alikuwa na mke wa kwa Kiyaudi aliyeitwa Esta. Hamani alitaka aheshimiwe sana kwa cheo chake, alipoona kuwa kuna mtu anayeitwa Modekai mjomba wake Esta hamweshimu kwa kumwinamia akafanya njama za kuliangamiza taifa la wayahudi. Mordekai alipopata taarifa hizi akamtaarifu mpwa wake Esta juu ya mambo mabaya yaliyopangwa juu yao. Esta kwa kuona kuwa yeye yumo katika nyumba ya Mfalme aliona yuko salama. Ndipo mjomba wake akamtumia ujumbe huu nanukuu kwenye Biblia
Esta: 4:13-14 Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijudhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine, ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuuijia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? (Mwisho wa kunukuu)
Ndugu yangu Esta alipata somo na kuchukua hatua na matokeo yake Hamani ndiye alitundikwa kwenye mti ulioandaliwa kwa ajili ya wengine na kuwa chakula cha ndege. Unaweza kujisomea mwenyewe sura yote ya 5 na 6 kwa ujumbe kamili.
Sasa ujumbe wangu kwako na wanaodhania kuwa wako salama ni huu
Tusifanye dharau kwa taarifa mbaya zinazolenga wengine, vinginevyo kibao kinaweza kugeuka wakaingia
waliokuwemo na wasiokuwemo. Mnadhani wanaokusudiwa ni viongozi wa CHADEMA, sawa lakini jua viongozi wa CHADEMA si viongozi wa chama ni viongozi wa watu, je watu watakubali hayo?
Hii fahamuni ni hatari sana kuliko unavyoweza kudhania, Viongozi wa CCM, Selikali na Vyombo vyake vyote vya usalama mnayonafasi ya kuzuia hili la sivyo ikitokea mjue mauaji yatakayofuata yatakuwa ya kutisha hakuna atakayebaki salama. Na hili siyo Arusha tu au Arumeru, ni kwa nchi nzima. Hebu tuzuie ufa kabla ya kafuta kujenga ukuta. Naongea hili kwa uchungu na ninawaomba CCM tusifurahie hili ni hatari kwetu kuliko mtu yeyote. Wewe angalia kwa sasa kupita mtaani na shati au Kanga ya CCM ni shida kwa kuzomewa, itakapokuwa kuchinjana tutaponea wapi?
Henyi makamanda, yaliyomkuta Hamani yanaweza kuwakuta ninyi pia, chukua tahadhali, najua kuwa ninyi mnafanya kazi kwa maelekezo ya chama sawa ila jua kuwa unaweza kufika wakati mkazikimbia kambi au mkatupa magwanda kwa hofu.
OMBI: Kila mtu kwa nafasi yake aliyopewa achukue hatua kuhakikisha kuwa haya hayatokei.