Wakubwa heshima kwenu!
Nimelazimika kuingia mapema kujaribu kuweka mambo sawa ili mjadala uwe na manufaa.
1.kwa aliyeangalia vizuri taarifa ile wakati mimi nazungumza nilichokisema ni kuwa, MCHANGO WA VIONGOZI WA DINI KATIKA AMANI NA UTULIVU WA NCHI YETU NI MKUBWA MNO NA WANASIASA WAUHESHIMU. LAKINI PIA NIKASISITIZA KIZAZI HICHI CHETU KUKABILIWA NA KANSA MBAYA YA UFISADI NA RUSHWA NA KUWAOMBA VIONGOZI WA DINI WASAIDIE SERIKALI KATIKA VITA YA KUKIOKOA KIZAZI NA KANSA HII.
2. KAMWE KATU HAKUNA BEI YA UTU WANGU,NA KWAKWELI KUSEMA NAPE KANUNULIWA KWANGU NI ÑATUSI MAKUBWA.NACHUKIA UFISADI LEO KULIKO JANA..NA GRAFU ITAENDELEA KUPANDA YA KUCHUKIA UFISADI NA KUUPIGA VITA.
3. NAAMINI KATIKA UZALENDO KWA NCHI KWANZA CHAMA BAADAE,NIMEKUWA NIKIYASEMA HAYA NA KUYAAMINI HADHARANI,HIVYO SI SAHIHI KUSEMA ETI KWA NAPE CCM NDIO BABA NA MAMA YAKE. KUMBUKENI NILIKUWA TAYARI KUFUKUZWA CCM KWA KUSIMAMIA HAKI LEO KUTUMIA MANENO YA KEJELI KAMA HAYA SI SAWASAWA NADHANI.
4. NAAMINI YAPO MAMBO HAYAWEZEKANI KWA NGUVU YA SIASA PEKEYAKE INAHITAJIKA NGUVU YA DINI/MUNGU,NA KWAKWELI KATIKA HILI NIMESOMA WARAKA WA MAASKOFU TOKA MWANZO MPAKA MWISHO SIJAONA KASORO NATAMANI TUUCHUKUE UWE SEHEMU YA ILANI YA CHAMA. NAWAPONGEZA MAASKOFU.
Sasa tujadili.
Nape Nnauye
Kaka, unauzungumziaje waraka huu wa Padri Karugendo?
WAKATI wa uchaguzi mkuu wa 2005 nilikuwa mratibu wa Mkoa wa Mtwara, wa waangalizi wa uchaguzi kupitia TEMCO. Pia nilikuwa nimepatiwa kazi ya kuandika mada juu ya upinzani mkali ndani ya vyama wakati wa kura za maoni, na upinzani mkali baina ya vyama vyama vya siasa wakati wa uchaguzi mkuu.
Baada ya uchaguzi, mwaka 2006, Redet iliandaa mkutano wa hali ya kisiasa Tanzania, uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mimi na wenzangu tuliokuwa tumepewa kazi ya kuandaa mada mbalimbali juu ya uchaguzi mkuu wa 2005, tulipewa nafasi ya kuwasilisha mada zetu. Na baadaye mada hizi zilijadiliwa na wadau mbalimbali waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.
Mada yangu ilijikita sana juu ya matumizi ya fedha kwenye kura za maoni ndani ya CCM. Kwamba ushindani mkali uliojitokeza ndani ya CCM kule Mtwara Mjini na Vijijini uliongozwa na nguvu ya fedha kuliko kuangalia sifa na uwezo wa mtu.
Wasomi wengi waliojitokeza kugombea ubunge wa kiti cha Mtwara Mjini, walitupwa nje na kumpitisha mtu aliyekuwa na kisomo cha kawaida, lakini alikuwa mtu mwenye fedha. Alitembeza bahasha wakati wa kura za maoni. Pia nilionyesha jinsi ushindani mkali uliojitokeza kati ya CCM na NCCR-Mageuzi Mtwara Mjini uliongozwa na nguvu ya fedha.
Ushindani ulikuwa mkali kiasi kwamba viongozi wa juu ndani ya CCM, walikuwa wakipigana vikumbo kuja Mtwara kuokoa jahazi. Misafara ya magari ilikuwa mingi, na ni wazi kulikuwa na matumizi makubwa ya mafuta. Dalili kwamba fedha nyingi zilitumika wakati wa kampeni.
Vitu kama khanga, sukari na sabuni vilikuwa vikigawiwa nyumba hadi nyumba. Kule Mtwara Vijijini ambako mwanzoni walimkataa mgombea mbele ya Rais Jakaya Kikwete, walilainishwa na nguvu ya fedha na kusahau kabisa malalamiko yao juu ya mgombea. Kampeni zilipopamba moto walianza kuimba nyimbo za kumsifia huyo mgombea.
Nakumbuka vizuri swali nililokuwa ninarudia mara kwa mara wakati nikiwasilisha mada yangu lilikuwa fedha hizi zinatoka wapi. Kusema kweli nilishuhudia fedha nyingi zikitumika wakati wa kampeni. Nilishindwa kuelewa kama zilikuwa zikitoka kwa watu binafsi au zilikuwa ni za chama.
Na kama zilikuwa zinatoka kwa mtu, alikuwa na biashara za namna gain. Na kama zilikuwa ni za chama, mbona nilikuwa nimeshuhudia sehemu mbalimbali za Tanzania, watendaji wa CCM, wanaishi muda mrefu bila mshahara?
Wakati ule nilikuwa ninashindwa kuelewa ni wapi fedha hizo zilizokuwa zikitumia kwenye kampeni zinatoka. Leo nina jibu! Baada ya kashfa ya EPA, swali langu lina jibu!
Katika mada yangu, nilionyesha wasiwasi wangu wa chama kutawaliwa na fedha, badala ya kutawaliwa na fikra na sera. Pia nilihoji mambo ya kushangaza yaliyojitokeza kwenye kampeni za CCM; mfano mgombea wa CCM alikuwa anajigamba kwamba ana uraia wa nchi mbili - Tanzania na Msumbiji.
Hakupata shida! Maofisa Uhamiajia waliendelea kumsikiliza na kumshangilia. Tanzania, nchi inayowafukuza watu ambao ni wahamiaji haramu, inamkumbatia mtu mwenye uraia wa nchi mbili kwa vile ni mgombea wa CCM, ni jambo ambalo sikulielewa wakati ule na hadi leo hii silielewi, maana nina imani jamaa huyu bado ana uraia wa nchi mbili.
Pia, nilielezea jinsi viongozi wa serikali Mtwara, walivyokuwa wakimpigia kampeni na kumuunga mkono jamaa huyo kwa vile walikuwa wakifanya biashara pamoja. Kwa ujasiri na kwa kujiamini nilifafanua hali ya ufisadi iliyokuwa inaishambulia CCM na kudhoofisha demokrasia nchini. Na kama kuna kitu ambacho ni adui wa demokrasia, basi ni nguvu ya fedha.
Hoja kubwa katika mada zetu ilikuwa ni kama uchaguzi unaimarisha au unadhoofisha demokrasia. Baada ya kuwasilisha mada yangu, Nape Nnauye, alinyanyuka na kunitukana. Siwezi kusahau wakati ule katika maisha yangu.
Ingawa sikutarajia kuungwa mkono asilimia mia moja kwenye mada yangu, lakini sikutarajia matusi. Nilitegemea nguvu ya hoja badala ya hoja ya nguvu.
Kusema ukweli wakati Nape anachambua mada yangu, hakutoa hoja, bali alitoa matusi. Alinitukana kwa kusema uongo na kukisingizia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia fedha nyingi wakati wa uchaguzi mMkuu.
Kwamba siku za nyuma alikuwa akiniheshimu sana kwa makala zangu nilizokuwa nikiandika, lakini siku hiyo kwa vile nilisema uongo na uzushi dhidi ya CCM alinidharau. Aliwashambulia watu wote wanaoichafua CCM na kuipaka matope.
Alisema CCM ni chama safi chenye watu safi. Na kwamba ushindi unatokana na mapenzi ya watu.
Nakumbuka sikujibizana naye kwa kuogopa sote wawili tusionekane hamnazo. Tunashauriwa katika maandiko matakatifu kwamba tusirudishie tukano kwa tukano. Baadhi ya wachangiaji walijaribu kumrudi Nape, lakini yeye kwa jeuri na kiburi cha chama, aliendelea na matusi yake.
Wakati wa kunywa chai, nilimfuata na kumpatia ushauri wa bure. Kama ni mtu anayetunza kumbukumbu, atakuwa anakumbuka vizuri ushauri wangu kwake. Sikumsikia tena baada ya siku ile aliponitukana hadi juzi alipojitosa kwenye vyombo vya habari na kushutumu ufisadi ndani ya chama chake kisafi na chenye watu wasafi.
Sasa wakati yeye mwenyewe, Nape Mnauye, anawashutumu baadhi ya wana-CCM kuwa mafisadi, ninachoweza kumwambia ni Nape Nnauye kuwa uyaone.
Waswahili wanasema kuishi kwingi ni kuona mengi. Mimi niliposema ufisadi ndani ya CCM nilitukanwa. Yeye naye ameuona ufisadi ndani ya chama chake na kusema! Nina imani atashangiliwa kama itakuwa kinyume, huko ndiko kukua na kuyaona mengi!
Nape alifikiri mimi ni msaliti, alifikiri mimi siipendi Tanzania. Kwa maneno yake alinitaja kama mpinzani na kama nilivyoona, wapinzani kwake ni wasaliti.
Ingawa kweli sina chama na wala mimi si mwanasiasa. Je, yeye leo hii ni msaliti? Au ni mzalendo anayekerwa na ufisadi? Ni miongoni mwa watu wanaokerwa kuona nchi inatawaliwa na fedha badala ya kuongozwa na fikra pevu? Imekuwaje watu aliowashangilia kuwa wasafi jana, leo anawatuhumu kwa ufisadi? Au ana lake jambo?
Nina shaka kama ataweza kuwa mwenyekiti wa vijana wa CCM. Mwaka ule alinitukana mimi kwa kuwalalamikia CCM, kukubali kuongozwa na fedha badala ya kuongozwa na fikra pevu na sera. Leo hii yeye analalamika kwamba kuna mafisadi ndani ya CCM, na kwamba mafisadi hawa wanaweza kuingilia uchaguzi.
Tumejenga utamaduni wa kuongozwa na fedha badala ya fikra. Hivyo kwa vile Nape anapigana vita na mafisadi, hawezi kufanikiwa kuwa mwenyekiti. Atakayechaguliwa ni yule aliye upande wa vizito, ni yule anayekubali kuongozwa na fedha. Mwenyekiti wa vijana ni muhimu sana kwa uchaguzi mkuu wa 2005. Hivyo makosa hayawezi kufanyika.
Ni bahati mbaya kwamba Nape amechelewa kuona ufisadi uliotanda ndani ya chama cheke cha CCM. Ninasema ni bahati mbaya kwa maana amefumbua macho amechelewa, kama angelifuata ushauri wangu, akafumbua macho mapema, labda angefanikisha matumaini yake.
Hata hivyo, yeye bado ni kijana, bado ana wakati wa kusahihisha makosa aliyoyafanya, bado ana muda wa kujiunga na wale wanaoamini kwamba ili chama kiwe kizuri, kiwe cha Watanzania maskini na wanyonge, ni lazima kiongozwe kwa fikra. Sasa awapishe wenye fedha wachukue nafasi zao!