Namkumbuka: Dr. Martin Luther King - ''I Have A Dream''

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,267
LINCOLN%2BMEMORIAL.JPG

Mwandishi amesimama Lincoln Memorial aliposimama
Dr. Martin Luther King alipotoa hotuba yake, ''I Have a Dream.''

Siku kama ya leo Martin Luther King aliuliwa Memphis kwa kupigwa risasi na hii leo imetimia miaka 50 toka Martin Luther King auliwe mwaka wa 1968.

Martin Luther King alikuwa mpigania haki za watu weusi Marekani. Kumbukumbu hizi zinanirudisha mimi miaka 50 nyuma nikiwa kijana mdogo na umri wa miaka 18 na mwanafunzi wa St. Joseph’s Convent, Dar es Salaam.

Shule yetu ilikuwa katikati ya mji karibu na Bahari ya Hindi, Bridge Street.

Kutoka shule ilipokuwapo na nyumbani kwetu Libya Street ilikuwa inanichukua kama dakika 20 au zaidi kidogo kufika shule.

Miaka ile ya 1960 Wamarekani walikuwa na ushawishi mkubwa sana kwa sisi vijana na safari ya Mwalimu Nyerere Amerika mwaka wa 1963 wakati wa John Kennedy akiwa rais wa Marekani ilizidisha pia uhusiano mwema katika ya Marekani na Tanganyika.

Miaka hii ya 1960 Waingereza wakiita, ‘’Roaring 60s’’ kwetu vijana katika ‘’teens.’’ hasa wa Dar es Salaam hakika ilikuwa miaka ya wazimu khasa na tukiiga kila kitu cha Kimarekani, kuanzia mavazi hadi muziki wake.

Hizi zilikuwa enzi za ‘’Soul Music’’ na Apollo Theatre, Harlem, New York na Broadway tukizijua kwa kuzisoma na kuangalia picha.

Muziki maalum na makhsusi kwa watu weusi wa Marekani na nje yake.Si rahisi kwa leo kueleza wazimu uliotukumba wakati tukisikiliza nyimbo za James Brown, Wilson Picket, Ray Charles, Stevie Wonder, Ottis Redding kuwataja wachache katika miziki ya vijana, yaani ‘’Pop.’’

Lakini ilikuwa pia enzi za miziki ya jazz ya wapigaji kama Duke Ellington na waimbaji bingwa kama Nat King Cole, Frank Sinatra, Louis Armstrong, ambayo ilikuwa ikipendwa na wenye umri wa kati na hapa sitaki kuwagusa wanamuziki kutoka Uingereza.

Magazeti tuliyokuwa tukipenda kusoma yalikuwa Newsweek, Time na Ebony gazeti la watu weusi Marekani.

Wengi wetu nami nikiwa katika kundi hilo tulikuwa na ndoto kuwa iko siku tutakwenda Marekani kusoma katika moja ya vyuo vikuu vya huko na wako ambao ndoto zao zikaja kuwa kweli na tuko pia ndoto zikabakia ndoto.

Wamarekani walikuwa na kituo chao cha utamaduni mji ambacho ndani mlikuwa na maktaba ya vitabu, muziki na ‘’theatre,’’ sehemu wakionyesha filamu.

Kwa kuwa na vitu hivi Wamarekani walituteka na mimi nilinasa katika dema lile kwani nilikuwa mwanachama wa maktaba ile na nilipofikia makamu ya kuwa naandika katika magazeti ya Uingereza kama Africa Events na New African Mkurugenzi wa United States Information Service alinipa uanachama wa Library of Congress, Washington nikiweza kuazima kitabu au jarida kutoka huko na nikaletewa Dar es Salaam.

Sasa tuje kwa Martin Luther King na mimi.

Mwalimu wangu wa Kiingereza alikuwa mama mmoja wa Kingereza jina lake Mrs. Grant.

Mume wake alikuwa anaitwa Grant na wote walikuja Tanzania katika mpango wa British Council wa kusomesha Kiingereza.
Bwana Grant alikuwa alikuwa akisomesha Chuo Cha Ualimu Chang’ombe.

Mrs. Grant sijui kwa vipi lakini alikuwa mwalimu aliyenipenda labda kwa kuwa nilikuwa na mapenzi makubwa na somo lake lililokuwa linaitwa, ‘’Reading Labaratory,’’ tukifunzwa kusoma kwa haraka, yaani kwa ‘’speed,’’ akiweka, ‘’time clock,’’ kupima unasoma maneno mangapi kwa dakika ngapi kisha kuna maswali unajibu kuonyesha kuwa umeelewa ulichosoma.

Kulikuwa na mashindano ya Elocution Kiingereza na Kiswahili kwa shule zote za Dar es Salam na shule yetu kila mwaka ikishinda katika English Elocution na kuna mwaka tuliwahi kushinda kwa pamoja English na Swahili Elocution.

Mrs. Grant akaniambia kuwa mwaka ule nitafute ''passage,'' yeyote niihifadhi kichwani niingie katika mashindano ya English Elocution.

Mwaka wa 1963 ndiyo mwaka ambao Martin Luther King alitoa hotuba yake maarufu, ‘’I Have a Dream,’’ Lincoln Memorial, Washington DC.

Nilikuwa nimehifadhi mengi kutoka michezo ya William Shakespeare kama ‘’Julius Caesar,’’ ‘’Merchant of Venice,’’ ambayo wala nisingeihitaji kujifunza kwani tayari nilikuwa nimeshahifadhi na ningeweza kusoma wakati wowote hata nikiamshwa usiku wa manane.

Lakini haya yalikuwa mashindano na nilitaka niingie katika mashindano na mtu mashuhuri kama Martin Luther King siyo na Cassius katika ‘’Julius Caesar,’’ au Shylock katika ‘’Merchant of Venice,’’

Niliamua kumsoma Martin Luther King na hotuba yake ‘’I Have a Dream.’’

Nikitoka nyumbani asubuhi nakwenda shule njia nzima naisoma kimya kimya hotuba hiyo na tulikuwa wanafunzi wengi tunawania nafasi hiyo na kila mtu kachukua chake anachotaka kusoma na sote tutasoma mbele ya mwalimu wetu na mbele ya wanafunzi wenzetu na yule aliye bora ndiye atakaewakilisha shule latika mashindano yale.

Nilishindwa kwa hiyo sikuweza kuiwakilisha St. Joseph’s Convent katika English Elocution.

Kwa nini nilishindwa?

Wenzangu walikuwa wanasema Kiingereza kwa ‘’accent,’’ nzuri ya Kiingereza.

Mimi Mswahili wa Kariakoo ‘’accent,’’ yangu ndiyo iliyonifanya nishindwe.

Miaka mingi imepita na leo huwa wakati mwingine nacheka kimoyomoyo nikiwasikia wanangu wanazungumza Kiingereza kwa mbwembwe nyingi na wakati mwingine nashindwa kabisa kuziweka mahali hizo ‘’accent’’ zao au hata kuzitambua.

Lakini kwangu mimi ile kuchagua ile hotuba, ‘’I Have a Dream,’’ hotuba ile na ujumbe uliobebwa mle ndani uliniathiri sana.

Kila nilipokuwa napita katika mistari ya hotuba ile nilikuwa kama vile nawaona Wamarekani Weusi siku zile wakiitwa, ‘’Negroes,’’ wanavyoteswa na Wamarekani Weupe.

Nilikuwa kama vile naisikia moja ya nyimbo maarufu katika ‘’Negro Spirituals,’’ nyimbo ambayo ukiisikiza inakutia huzuni, ‘’Go Down Moses Let My People Go,’’ iliyopigwa na Louis Armstrong.

Ilikuwapo na nyimbo nyingeni ya Sam Cooke, '' A Change is Gonna Come,'' ikiimbwa pia kwa maombolezo na mategemeo kuwa hali za watu weusi itakuja siku zitakuwa bora.

Hotuba ya Martin Luther King na muziki wa Louis Armstrong vilikuwa vikinitoa katika mji wa Dar es Salaam na kunipeleka Marekani ya karne ya 18, Deep South ambako utumwa ulikuwa umeshamiri na Wanegro wakifanyishwa kazi kama watumwa katika mashamba ya pamba.

Wakati mwingine ndoto na mawazo yanayotawala akili huwa kweli ingawa si mara nyingi.

NIlisafiri kwa barabara ndani ya gari ya rafiki yangu James Brennan tukitoka Iowa City akinileta Chicago kupanda ndege kuelekea New York, tulipita Mississippi ambayo mto wenye jina hilo ulinikumbusha Tom Sawyer na Huckleberry Finn, ''characters,'' niliowapenda wakati nikiwa mtoto mdogo nikiwasoma katika kitabu cha Mark Twain - ''Tom Sawyer and Huckleberry Finn.''

Wakati ule wala haikunipitikia kuwa nitakuja kuisoma historia ya America nikiwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam nikisomeshwa na bingwa wa historia Prof, Fredrick Kaijage, mwalimu aliyenifunza mengi na nina deni kubwa kwake, wala haikunipitia kuwa nitakuja kuiona Mississippi River niliyoijua zaidi kwa mikasa ya Tom Sawyer and Huckleberry Finn na pia kwa historia ya ubaguzi ulikuwapo Amerika.

Prof. Kaijage kama walimu wengi katika maisha yangu, alinipenda kiasi siku nilipokuwa kwa sababu yoyote ile sikufika darasani au kwenye semina atajua na ataniulizia kwa wanafunzi wenzangu.

Miaka ya 1960 haikuwa tena miaka ya watumwa kulimishwa pamba bali ilikuwa miaka ya James Meredith aliyekataliwa kuingia Chuo Kikuu Cha Mississipi na Gavana mbaguzi wa Alabama George Wallace kwa kuwa tu alikuwa na ngozi nyeusi.

Sasa mimi ni mtu mzima na wakati mwingine huwa nazungumza na wanangu kuhusu raha na elimu inayopatikana ndani ya kitabu.

Huwa nawaambia kuwa nilipokuwa mtoto nilikuwa nikifika Tanganyika Library siku hizo iko Mtaa wa Mkwepu nilikuwa nikiinamia kitabu kusoma basi huwa naondoka kabisa Dar es Salaam.

Ikiwa ni kitabu cha Spaniards wanaikata Bahari ya Atlantic kwenda Amerika ya Kusini katika nchi ya Aztec mimi nakuwa mmoja wa mabaharia wale nasafiri na wao ndani ya meli yao nafanya yale wanayofanya.

Katika hali hii ya raha nikinyanyua kichwa jua limezama na nje taa zinawaka, Maghrib imeshaingia.

Naondoka maktaba narudi nyumbani, Libya Street mwendo mfupi tu kutoka Mkwepu Street.

Nawaambia wanangu kuwa hawatoweza kuyapata haya hadi wahame kwenye kuangalia DVDs waje kwenye kusoma kitabu.

Huwa nahitimisha nasaha zangu siku zote kwa kuwaambia, ‘’Nothing can replace the book.’’

MIaka ikaenda nikafika Washington DC Lincoln Memorial nikiwa na mwenyeji wangu Dr. Harith Ghassany ambae katika kunionyesha mji akanipeleka Lincoln Memorial.

Mwaka wa 2011 nilisimama pale aliposimama Martin Luther King miaka 48 iliyopita na kutoa hotuba yake maarufu, ‘’I have a Dream,’’ akiwa kijana mbichi wa miaka 34 fikra zangu zikirudi nyuma kwa haraka nikiwa name nimesimama mbele ya darasa nikiwahutubia wanafunzi wenzangu, ‘’I Have a Dream,’’ Mrs. Grant mwalimu wangu wa Kiingereza akinisikiliza.
 
naungana nawewe mkuu, japo sikuwepo lkn napenda audio za martin Luther jr kuchangamsha bongo na kujifunza.
napenda hotuba "the dilema and the challenge".
ntamkumbuka kwa kusikiliza tena leo jioni.
nimejifunza pia mkuu kwa watanzania nyie wa enzi zenu na vijana sisi wa sasa ni kaskazini na mashariki kwa uelewa na vipaumbele.

asante kwa nasaha mkuu
 
naungana nawewe mkuu, japo sikuwepo lkn napenda audio za martin Luther jr kuchangamsha bongo na kujifunza.
napenda hotuba "the dilema and the challenge".
ntamkumbuka kwa kusikiliza tena leo jioni.
nimejifunza pia mkuu kwa watanzania nyie wa enzi zenu na vijana sisi wa sasa ni kaskazini na mashariki kwa uelewa na vipaumbele.

asante kwa nasaha mkuu
Mitale...
Ahsante sana na nakuongezea hotuba yake nyingine maarufu sana:
''I have been to the mountain top.''
 
Nimepoteza hotuba zake nyingi sana.Ikiwamo hii ya "I have a Dream".
Dr Luther Martin Jr is still living in my mind....Ahsante sana Mzee wa Historia, umeichangamsha siku yangu.
Hope to get a lot of him from you.
 
Napenda sana makala zako mzee Mohamed Said. Mara nyingi huwa sitoki kapa kila napozipitia makala hizi. Ahsante sana mkuu!
 
Nimepoteza hotuba zake nyingi sana.Ikiwamo hii ya "I have a Dream".
Dr Luther Martin Jr is still living in my mind....Ahsante sana Mzee wa Historia, umeichangamsha siku yangu.
Hope to get a lot of him from you.
ingia hapa
tutaudio.su au www.tutaudio.ru
search Martin Luther
kuna audio nyingi karibu zote na kuna option ya kudownload.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom