Mzimu wa ‘Bunge Live’ watikisa, wananchi watinga mahakamani

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
HATUA ya serikali kuzuia kurusha moja kwa moja mjadala wa vikao vya Bunge kama ilivyokuwa awali, bado inaumiza wananchi

Safari hii wananchi wametinga mahakamani na kwamba leo wamefika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufungua kesi ya kuitaka mahakama hiyo kutengua agizo la serikali la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Januari mwaka huu, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Michezo na Sanaa alilieleza Bunge hatua ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya chombo hicho kama ilivyokuwa awali.

Miongoni mwa sababu alizotoa ni kwamba, serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa gharama katika kuendesha matangazo hayo pia watumishi wa umma kutumia muda mwingi kuangalia Bunge badala ya kufanya kazi.

Hatua ya serikali kuzuia kurusha matangazo hayo ya moja kwa moja imeibua mjadala mkubwa kitaifa ambapo kada mbalimbali nchini zimekuwa zikipinga hatua hiyo.

Katika kesi iliyofunguliwa leo, ina walalamikaji 10 ambao ni Azizi Himbuka, Perfect Mwasililwa, Rose Moshi, Penina Nkiya, Andrew Mandari, Hilda Sigara, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane.

Kesi hiyo imesikilizwa na Profesa Ferdinand Wambari, Jaji Kiongozi katika mahakama hiyo, na jaji mwengine katika kesi hiyo Sakieti Kihiyo, hata hivyo hakuwepo mahakamani leo.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni Nape pamoja na George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo Abubakari Mrisho, ndio wakili wa upande wa walalamikiwa.

Kwa upande wa walalamikaji unasimamiwa na Peter Kibatala na Omari Msemo ambao ni mawakili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kesi ya msingi iliyofunguliwa ni kuitaka mahakama kutengua uamuzi uliotolewa na Nape ambaye aliwasilisha kauli ya serikali bungeni.

Walalamikaji wanaitaka mahakama itangaze kuwa, Raia wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wana haki ya kikatiba ya kujua majadiliano yanayoendelea bungeni kwa mujibu wa ibara ya 18(B), (d) na 29 (1).

Pili walalamikaji wamedai kuwa, serikali imekiuka haki ya kikatiba kwa kuzuia bila kuwa na sababu za msingi haki ya wananchi kusikia majadiliano ya Bunge kwa kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja.

Tatu, walalamikaji wameitaka mahakama kuilekeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurejesha haki ya kikatiba ya wananchi kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Nne, walalamikaji wamedai kuwa, matokeo ya kuzuia matangazo hayo ni kunyimwa kwa haki za Watanzania kutokana na kushindwa kuwasimamia pia kuwafuatilia wabunge na mwenendo wao bungeni.

Tano, walalamikaji hao wamedai kuwa, sababu za kuzuia matangazo hayo hazijitoshelezi hivyo Watanzania na walalamikaji wanayo haki ya kupata taarifa ya vikao vya Bunge kwa maslahi ya taifa.

Hata hivyo upande wa utetezi ulidai kuwa, walichelewa kupata taarifa ya mashtaka hayo hivyo hawakupata muda wa kutosha wa kuaandaa majibu. Kutokana na hivyo, mahakama iliuambia upande wa walalamikiwa kwamba, watajibu mashtaka hayo 15 Julai siku ambayo kesi hiyo itatajwa.
 
Wataangukia pua kama ilivyokuwa kwenye mita 200....Bunge live halijapigwa marufuku...sijui wanachotafuta mahakamani ni kipi au labda kuna maslahi flani ya kuendesha hizi kesi zisizo na kichwa wala miguu
 
mtoa mada ungesema tu specific kuwa ni wana chadema na wana ukwa kwa pamoja wamefungua kesi kuliko kutumia neno wananchi,maana huo mzimu hauwatesi wananchi bali wanaukawa na wanachadema kwa umoja wao...
 
Hivi ninyi mnaopingana na hoja ya kufunguliwa shtaka LA kudai haki ya MTU kupata habari iliyopo kikatiba mpo timamu? Ingezuiliwa mitandao mingine ya kijamii Kama huu tunaoutumia msingepiga kelele? Ondoeni uumini wa vyama muone ukweli juu ya ukanyagaji wa katiba yetu. Leo wanalo LA kuminya Uhuru wa habari na demokrasia. Mnajua kesho watakuja na lipi lingine lenye maumivu makali kuliko haya? Tafakarini kwa makini kwani wanasiasa wanaona poa tu na hawajali mateso yenu. Kuna siku yatazidi Haya na mengine yasiyobagua itikadi zenu yanakuja. Tutalia wote isipokuwa wao walio juu ya sheria. Msisahau kuwa haki hudaiwa na kupiganiwa. Yale ya misri juu ya Uhuru wa habari hayatoshi kutupa somo?
 
Wataangukia pua kama ilivyokuwa kwenye mita 200....Bunge live halijapigwa marufuku...sijui wanachotafuta mahakamani ni kipi au labda kuna maslahi flani ya kuendesha hizi kesi zisizo na kichwa wala miguu
Hicho ndicho kitawafanya wawe masikioni mwa umma wa Watanzania. Hawana hoja za msingi nao wanajua hilo. Haki za kupata taarifa sawa namna gani mnapata taarifa ni jukumu la mtoa taarifa
 
Back
Top Bottom