SEHEMU YA 50
AZRA Malama, alibaki ameganda, akishindwa achukue uamuzi gani, hata hivyo kadiri alivyochelewa kufanya uamuzi ndivyo kundi lile lilivyozidi kumzunguka.
Kijana huyo akajikuta katikati, hakuwa tena na nafasi ya kufanya uamuzi wowote wala kupambana. Walikuwa ni wengi sana.
Alipiga magoti na kuinama chini.
Akaingia mikononi mwa Waswadege, watu ambao walikuwa na hasira naye kwelikweli kutokana na maafa aliyokuwa ameyasababisha.
Kundi hilo la wapambanaji lilimfunga Azra kamba, kisha wakamuunganisha kwenye farasi na kuanza kumburuza huku wanaelekea sehemu maalumu ya kutesea, ili wakampe mateso makali kijana huyo. ***
Wakati kijana huyo akikamatwa, upande wa pili vilio vilikuwa vimetawala katika kisiwa cha Swadege ya Rwadege.
Madhara aliyokuwa ameyasababisha Azra Malama, kwenye mapambano kati ya kundi la Shebo lililomfuata Uwandani likiongozwa na Kalega, yalikuwa ni makubwa. Watu wengi walikuwa wamepoteza maisha.
Zaidi ya watu ishirini!
Hiyo ilikuwa ni idadi kubwa mno ya watu kupoteza maisha kwenye pambano la mtu mmoja, ambalo kwa Swadege lilihesabika ni pambano dogo na la kihistoria.
Kutokana na hali hiyo watu wa Swadege walitokea kumchukia mno kijana huyo Azra Malama.
Walimchukia kuliko njaa, jua kali linaloharibu mazao au mafuriko.
Hata hivyo chuki haikuishia kwa Azra, peke yake. Ilikwenda mpaka kwa mama Cecilia na binti yake Jemima, waliyomleta kijana huyo Swadege.
Ndugu waliyopoteza watu wao waliamini kama si mama Cecilia na Jemima, maafa hayo yasingetokea, jambo lililowafanya ndugu hao kushika mapanga, mikuki na vijiti vya moto, wakiwa kwenye farasi na kwenda mpaka nyumbani kwa mama Cecilia kwa ajili ya kuchoma makazi hayo kwa moto.
Walipofika walimkuta Kalega, mama Cecilia na binti yake Jemima, wakiwa ndani. Baada ya kusikia fukuto la farasi, Kelega alitoka ndnai na kusimama uwanjani kwao, mama na dada yake wakiwa nyuma yake, kulisikiliza kundi hilo lilitaka nini, baada ya kufika.
“Hatuwezi kukubaliana na alichokifanya mama yako,” mmoja wa watu wale aliyeitwa Bonza, alimwambia Kalega.
“Hakuna aliyekuwa anamhitaji Azra,” Kalega alijibu.
“Lakini mama na dada yako ndio waliomleta!” Bonza aliongeza kwa msisitizo.