Mwanasiasa Mdomo Tupu ni Sawa na Mchawi Mnafiki!

Mwanasiasa Mdomo Tupu ni Sawa na Mchawi Mnafiki!

Alloyce PR

JF-Expert Member
Joined
Nov 15, 2020
Posts
811
Reaction score
877
Katika jamii nyingi za Kiafrika, mchawi huogopwa kwa sababu ya hulka yake ya unafiki, mwenye uso wa tabasamu mchana, lakini usiku huwaza maangamizi kwa wengine. Ni mtu anayeishi kwa kutegemea uongo, siri, na usaliti ili kufanikisha malengo yake binafsi. Hali hii inazidi kuakisiwa kwenye taswira ya mwanasiasa wa kisasa ambaye hana nia ya dhati kwa watu wake bali ni mwepesi wa kutoa ahadi zisizo na mizizi wala tija. Mwanasiasa wa namna hii ni “mdomo tupu” anayepayuka kwa maneno matamu yasiyoambatana na vitendo. Na hivyo, kwa hakika, ni sawa kabisa na mchawi mnafiki.

Katika kila msimu wa uchaguzi, tunashuhudia mavazi ya suti, maneno ya kisiasa yaliyojaa matumaini, nyuso za huruma, na ahadi za kimapinduzi. Lakini mara tu baada ya kushika hatamu, maneno hayo hubadilika kuwa mihemko ya kimaslahi binafsi. Kwa lugha nyingine, mdomo wa mwanasiasa huyu ni jukwaa la maigizo, na si kielelezo cha dhamira ya kweli ya kulinda maslahi ya wananchi.​

Siasa Bila Maadili ni Kivuli cha Uchawi wa Kisasa

Siasa ni chombo muhimu cha ujenzi wa jamii. Inapokosa maadili, hulka yake hubadilika na kuwa kama ya uchawi, chombo cha kuumiza, kuficha nia, na kuvuruga matumaini ya wengi. Mwanasiasa mdomo tupu huzungumza kwa sauti kubwa lakini hana jibu kwa changamoto za wananchi. Ni mtu anayepiga kelele jukwaani, lakini kimya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hutoa hotuba za huruma, lakini anaishi kwa anasa zinazodhalilisha maisha ya masikini anaodai kuwatetea.

Unafiki na Uwepo wa Mdomo Bila Moyo

Kwa nini tuseme mwanasiasa wa aina hii ni mchawi mnafiki? Ni kwa sababu maneno yake huahidi nuru lakini matendo yake huzalisha giza. Ni mtu wa maneno mengi, ahadi kemkem, lakini hana mpango wa kuzitimiza. Kama ilivyo kwa mchawi anayecheka nawe mchana na kukutafuta usiku kwa uovu, mwanasiasa mdomo tupu anawachekea wananchi wakati wa kampeni, kisha huwageuka akishashinda. Hii ni aina ya unafiki unaoumiza roho ya taifa na kufifisha ndoto ya maendeleo.

Wananchi Wanapaswa Kuzima Uchawi huu wa Kisiasa

Ni wakati wa wananchi kuwa macho. Maendeleo hayaji kwa kishindo cha maneno, bali kwa uthibitisho wa vitendo. Tunapaswa kuwakataa wanasiasa wanaotegemea mdomo badala ya mikono ya kazi. Tunahitaji viongozi wenye imani ya kweli, ambao hawatoi ahadi kama tamthilia za maigizo bali wanaweka mikataba ya uwajibikaji na wanaishi ndani ya misingi ya ukweli, uwazi, na huduma kwa watu.

WITO KWA WANANCHI NA KWA VYAMA VYA SIASA.

Mwanasiasa mdomo tupu ni hatari kama mchawi mnafiki. Maneno yake ni sumu inayopakwa asali. Katika zama hizi tunazohitaji matumaini, mwelekeo, na mshikamano wa kitaifa, tuache kabisa siasa za kejeli, uongo, na usanii. Ni wakati wa kujenga taifa kwa msingi wa ukweli, si kwa mdomo wa kishetani wa miviga ya kisiasa.

Kumbuka: mdomo wa mwanasiasa usiokuwa na dhamira ni mdomo wa uchawi wa kisasa, ukiona mwanasiasa anayeahidi sana lakini hatendi, yule anayeshindwa kutekeleza ahadi zake na kisha kuibuka na ajenda za kutaka huruma tofauti na yale aliyoyaahidi kwa wananchi, mkimbie kama mchawi wa usiku!
 
Back
Top Bottom